Kiungo Kilichojificha: Jini Shaytwaan Na Mchawi
Kiungo Kilichojificha
Imekusanywa Na:
Muhammad Faraj Saalim (Rahimahu Allaah)
Imepitiwa Na:
Naaswir Haamid
Utangulizi
Tawhiyd
Maana Ya Tawhiyd?
‘Ibaadah
Aina Mbali Mbali Za Shirki
Jinni
Jina Lake
Imani Juu Ya Ghayb
Ushahidi Ndani Ya Qur-aan Tukufu
Ushahidi Ndani Ya Sunnah
Wameumbwa Kwa Moto Dalili Katika Qur-aan
Dalili Katika Sunnah
Majini Wanazaliana
Wameumbwa Kabla Ya Binadamu
Uhusiano Baina Ya Jinni Na Shaytwaan
Ibilisi Ni Katika Malaika?
Aina Za Majini
Mahali Wanapoishi
Wanakula Na Kunywa
Wanaweza Kujigeuza
Wamo Wanawake Na Wanaume
Wanaowa?
Wanakufa?
Wamo Waislamu Na Makafiri
Waislamu Majini Wataingia Jannah?
Wanawaogopa Wanadamu
Wanasikia Habari Za Mbinguni
Uchawi
Nini Maana Ya Uchawi?
Utawezaje Kumjua Mchawi
Uchawi Upo - Dalili Ndani Ya Qur-aan Na Sunnah
Soma Bahati Yako (Lucky Stars)
Uchawi
Umeanza Zama Za Nabii Sulaymaan ('Alayhis-salaam)?
Uchawi Ni Kufru
Hukumu Ya Uchawi Katika Diyn Ya Kiislamu
Kujikinga Na Shari Zao
Du’a Zinawakumba
Dhikru Llaah
Usiviingize Ndani Ya Nyumba Yako
Utangulizi
Shukrani zote ni zake Allaah, msaada wote tunamuomba Yeye tu, tunamtegemea Yeye tu, kwa sababu kila kisichokuwa Yeye ni dhaifu na nguvu zote na ufalme wote ni wake Yeye peke yake, milango Yake iko wazi siku zote.
Kawaida ya mwanadamu ni kuwa kila unapotaka msaada kutoka kwake, basi yeye hukasirika. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), anaghadhibika usipomuomba Yeye msaada wake.
Katika Hadiyth Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
“Yule asiyemuomba msaada Allaah basi hughadhibika naye.”
Tunashuhudia kwamba hakuna Rabb Anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Rasuli wake na kipenzi chake, ameufikisha ujumbe na ameituwa amana aliyopewa, amewatoa watu kutoka katika kiza cha kufru na ushirikina na kuwaingiza katika Nuru ya Uislamu kwa idhini ya Rabb wake (Subhaanahu wa Ta’aalaa), amepigana jihaad kama alivyopaswa, basi tunakuomba Rabb wetu Umsalie na kumsalimu Rasuli wako huyu mtukufu pamoja na ‘Aali yake na Swahaba wake wakarimu.
Amma Ba’ad,
Nimeona ni vizuri niandike risaalah hii ili niwatahadharishe ndugu zangu Waislamu juu ya ubaya wa kuwaendea wachawi, wapiga ramli na watabiri, nikizingatia juu ya uhusiano huo nilioutaja hapo juu, baina ya Jinni na Mchawi.
Baada ya kumaliza kuisoma darsi hii Insha Allaah, tutakuwa tumekwisha ufahamu uhusiano uliopo baina ya Jinni na wachawi pamoja na wapiga ramli na watabiri ili tuweze kuepukana na shari zao.
Tunamuomba Allaah Atufungue vifua vyetu tuifahamu darsi hii na aijaalie kazi hii iwe halisi kwa ajili Yake tu - Aamin.
Tawhiyd
Atakayechunguza hali za Waislamu ataona kwamba haziridhishi hata kidogo. Waislamu wanategemea mataifa yasiyokuwa ya Kiislamu katika kila jambo lao. Iymaan zimekuwa dhaifu, Waislamu wameipoteza hata Swalah yao. Wako Waislamu wasioswali, na hata wale wanaoswali, basi wengi wao hawaswali kama inavyopaswa. Ujinga katika mambo ya diyn umeenea, uzushi (bid’aa) umezidi, ushirikina umekuwa ndiyo njia ya kupatia riziki.
Kutokana na hayo, umoja baina ya Waislamu ukaanza kutoweka na mapenzi yakageuka kuwa bughudha na heba yao ikaanza kupotea. Haya yote ni kwa sababu ya kutofuata itikadi iliyo sahihi aliyokuja nayo Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nayo ni itikadi ya Tawhiyd.
Maana Ya Tawhiyd?
Kwa ufupi, maana ya Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa kuzielekeza ‘ibaadah zote kwake Yeye tu (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
‘Ulamaa wameigawa ‘ilmu hii yaTawhiyd katika mafungu matatu:
1 – Tawhiydur-Rubuubiyyah
Nayo ni kuamini kwamba aliyeumba kila kitu, anayeruzuku na kuendesha mambo yote ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Asiye na mshirika na pia kuamini kwamba Ufalme wote ni wake:
Allaah Anasema:
قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ
Sema: Ni nani Rabb wa mbingu na ardhi? Sema: Ni Allaah. [Ar-Ra’d: 16]
Na Akasema:
قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾
Sema: Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)? Watasema: Ni Allaah; basi sema: Je, basi hamuwi na taqwa? [Yuwnus: 31]
1 - Shirk ya Ar-Rubuubiyyah
Mwenye kuamini kwamba yupo mwengine mwenye uwezo wa kumruzuku kwa njia za ghayb au wa kumtengenezea mambo yake asiyekuwa Allaah, huyo anakuwa ametenda kitendo cha Shirk Ar-Rubuubiyyah.
Anayewaendea wachawi au watabiri huwa anawategemea wamtengenezee mambo yake na kumwekea vizuri kwa njia za ghayb au kwa nguvu zisizoonekana, na kwa ajili hii anaingia katika shirk hii ya Ar-Rubuubiyyah.
2 -Tawhiydul-Uluuhiyyah
Maana yake ni kuzielekeza ‘ibaadah zote kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Allaah Anasema:
قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ﴿١٦٣﴾
Sema: Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza. [Al-An ‘aam: 162-163]
Shirk Al-Uluuhiyyah
Mwenye kuelekeza ‘ibaadah zake kwa mwengine asiyekuwa Allaah, kwa kuswali penye kaburi lake, kuapa kwa jina lake, kuchinja kwa ajili yake, kuomba msaada wake, kumuogopa kuliko Rabb wake au kufuata sheria zake zinazokwenda kinyume na sheria za Rabb wake, n.k, huyo anakuwa amefanya kitendo cha Shirk Al-Uluuhiyyah.
Anayemwendea mchawi, hutakiwa kuchinja mnyama kwa ajili ya kuwaridhisha majini, hupewa herizi ambazo yareti kama angeweza kuzifungua na kusoma yaliyomo, basi angeona na kutambua kuwa yaliyoandikwa humo na wachawi hao ni mazungumzo baina yao na majini ya kuwataka wamlinde mtu huyo.
Hofu za watu wa aina hii kwa wachawi huwa ni kubwa sana kuliko hofu yao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na kuwategemea kwao wachawi hao katika kutengeneza mambo yao ni kwingi kuliko wanavyomtegemea Allaah.
Kwa hivyo anayemwendea mchawi au mtabiri anakuwa ametenda kitendo cha Shirik Ar-Rubuubiyyah.
3 -Tawhiydul-Asmaa was-Swifaat
Allaah Amejipa majina mazuri mazuri na sifa nzuri nzuri na akawataka waja wake wamuombe na kumtukuza kwa majina na sifa hizo.
Allaah Anasema:
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿١٨٠﴾
Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanamili katika kukadhibisha Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf: 180]
Shirk fiyl Asmaa was-Swifaat
Mwenye kuomba kwa majina ya wengine wasiokuwa Allaah, kama vile kuomba kwa majina ya Manabii, majina ya Mawalii n.k. na akayaacha majina hayo matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), (kwa mfano badala ya kusema "Yaa Qawiyy, = Ee Mwenye Nguvu, Yaa Maalik, = Ee Mfalme, Yaa Qaadir = Ee Mwenye Uwezo - hayo ni katika majina mazuri mazuri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), akayaacha majina hayo. Akasema kwa mfano "Ee Nabiy fulani, Ee Waliy Fulani, Ee Swahaba fulani au Ee Jinni fulani" n.k.), huyo atakuwa ametenda kitendo cha Shirki ya Al-Asmaa was-Swifaat.
Atakayejaribu kuzigeuza sifa zake (Subhaanahu wa Ta’aalaa), au maana yake, au kufananisha sifa hizo ziwe sawa na sifa za binadamu au za kiumbe chochote kile, huyo pia atakuwa ametenda kitendo cha Shirkul-Asmaa was-Swifaat.
Anayemwendea mchawi au mpiga ramli, huyo anampa sifa hizo mchawi huyo pamoja na majini wake wanaomtumikia kwa kuamini kwake kwamba wao (majini na wachawi) wana uwezo wa kutengeneza, kudhuru, kubadilisha au kuijua ‘ilmu ya ghayb n.k. Na badala ya kuomba kwa majina mazuri mazuri ya Rabb wake anakwenda kuomba kwa majina ya majini hao na mizimu yao n.k. Kwa ajili hivyo anakuwa ametenda kitendo cha kufru ya Al-Asmaa was-Swifaat.
‘Ibaadah
‘Ibaadah katika Uislamu, inakusanya matendo yote anayoyapenda Allaah na kuridhika nayo.
‘Ibaadah ziko aina nne:
1. |
‘Ibaadah za kimwili kama vile kuswali, kufunga, kuhijji, kutufu n.k. |
2. |
‘Ibaadah za mali, kama vile kutoa zakkah, kuchinja, kutoa swadaqah n.k. |
3. |
‘Ibaadah za Moyo kama vile khushuu katika Swala, kumnyenyekea Allaah, kumtegemea, kumuogopa, kumpenda, kumtukuza n.k. . |
4. |
‘Ibaadah za kutamka kama vile kuomba du’aa, kuapa, kumdhukuru Allaah, n.k. |
Tawhiyd ndiyo Moyo wa diyn ya Kiislamu, na hakuna diyn yoyote duniani inayohubiri Tawhiyd isipokuwa diyn hii tukufu. Lakini kinachosikitisha ni kwamba wapo wajinga wengi wasioijua Tawhiyd wameingiza mambo katika diyn hii hata ikaonekana kwa baadhi ya wasiokuwa Waislamu kama ni diyn ya ushirikina.
Wachawi, waganga na watabiri, wote hawa wanajinasibisha na diyn hii kwa kujiita Shaykh Fulani, Alhajj Fulani au Maalim Fulani na hawa wote Uislamu uko mbali kabisa nao.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuja, aliwakuta makuhani na watabiri waliokuwa wakiitwa "Arrafiyn", wakiwa wamejaa penye Al-Ka’abah na kazi zao zilikuwa ni kutabiri, kutisha na kuwadanganya watu kwamba eti wao wanaijua ‘ilmu ya ghayb na kwamba wana uwezo wa kudhuru na kunufaisha.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa na kazi kubwa ya kuwapiga vita waongo hao na kuwabainishia watu kwamba uwezo huo ni wa Allaah Peke Yake, na kwamba atakayewaendea waongo hao kuwauliza jambo, atakuwa amekwisha kufuru.
Hii ni kwa sababu Uislamu umekuja kuyapiga vita mambo hayo na umekuja kuwafahamisha watu kwamba hakuna aijuwae ghayb isipokuwa Allaah peke yake.
Allaah Anasema:
قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ﴿٦٥﴾
Sema: Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye ghayb isipokuwa Allaah. [An-Naml: 65]
Kwa hivyo Malaika hawaijuwi ghayb, wala Manabii, wala hata Majini na watabiri pamoja na wachawi wao. Na mtu anapokutwa na shida au dhiki yoyote ile akawaendea watu wa aina hiyo na kumuacha yule ambaye kwake tu inapatikana faraji na kwake tu inaondoshwa dhiki, basi mtu huyo anakuwa amepotea upotofu mkubwa kabisa na anakuwa ameingia katika shirki itakayomfanya Jannah iwe haramu kwake na Moto uwe ni makaazi yake. Tunamuomba Allaah Atuingize katika Jannah Yake na kutuepusha na Moto Wake - Aamiyn.
Aina Mbali Mbali Za Shirk
Shirk ziko aina nyingi na katika sura mbali mbali, na siyo katika sura ya uchawi tu.
· - Miongoni mwa shirk ni kwenda katika makaburi ya mawalii na
kutafuta baraka au kuomba shida zako ziondolewe hapo na kwa uwezo wao.
· - Kuchinja kila mwaka au wakati maalum kwa ajili ya kuilinda nyumba na majini au Shaytwaan.
· - Kuchinja kwa ajili ya Bwana Arusi na Bibi Arusi ili wairuke damu ya mnyama huyo eti Jinni atashughulika na damu hiyo na wasiwadhuru maarusi.
· - Kuvunja yai au kuchinja kwa ajili ya kununua gari jipya na kumwaga damu katika magurudumu.
Hayo yote ni baadhi tu za aina mbali mbali za shirk.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Amelaaniwa na Allaah atakayechinja kwa (ajili ya mwengine) asiyekuwa Allaah.”
Kutokana na haya nikaona ni bora nikamate kalamu na kuwatahadharisha ndugu zangu Waislamu kwa kadiri ya uwezo wangu ili wajiepushe na mambo haya ya shirk kwa njia ya kuwadhihirishia uhusiano uliopo baina ya Majini, Watabiri na Wachawi. Kwa sababu kuwaendea watu hawa ni kitendo cha shirk, na hapana kitendo kibaya Allaah Anachokichukia kuliko kitendo hicho.
Pia nimeona ni bora niwafafanulie ndugu zangu ili wakijue Kiungo Baina Ya Majini, Wachawi na Watabiri na jinsi gani watu hawa wanavyojikurubisha na shaytwaan kwa njia za kukufuru ili wapate kutumikiwa nao.
Allaah Anasema:
إِنَّمَا صَنَعُوا كَيْدُ سَاحِرٍ ۖ وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ﴿٦٩﴾
Hakika walivyoviunda ni hila za mchawi, na wala mchawi hafaulu popote ajapo. [Twaahaa: 69]
Wanafuata hayo, na kumwacha Allaah ambaye Anasema:
أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ وَيُخَوِّفُونَكَ بِالَّذِينَ مِن دُونِهِ﴿٣٦﴾
Je, kwani Allaah si Mwenye kumtosheleza mja Wake? Na wanakutisha na wale wasiokuwa Yeye? [Az-Zumar: 36]
Kila asiyekuwa Allaah ni dhaifu. Hata hao watu wa Ahlil-Badri waliopigana vita vya Badar idadi yao wakiwa watu mia tatu na kidogo tu dhidi ya makafiri elfu na kuwashinda makafiri, basi Allaah anawataja kuwa ni madhaifu.
Allaah Anasema:
وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ
Kwa yakini Alikunusuruni Allaah katika Badr na hali nyinyi mlikuwa (kikosi) dhaifu. [Aal-‘Imraan: 123]
Sasa kwa nini mtu anaacha kumtegemea Allaah Mwenye nguvu na kuwategemea madhaifu? Kwa nini anaiacha haki na kufuata batili? Kuna nini baada ya kuiacha haki isipokuwa kufuata upotovu tu?
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ ۖ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ﴿٣٢﴾
Basi Huyo Ndiye Allaah, Rabb wenu wa haki. Na kuna nini baada ya haki ila upotofu? Basi wapi mnageuzwa? [Yuwnus: 32]
Jinn
Jina Lake
Ameitwa Jinn kwa sababu ya kutokuonekana kwake na watu, na hii ni kwa sababu kila kisichoonekana kwa jicho la binadamu katika lugha ya Kiarabu jina lake hutokana (hutoholewa) na herufi mbili hizi; (Jiym) na (Nuun).
Kwa mfano; 'Bustani' huitwa 'janna' kwa sababu ya kuzungukwa kwake na majani kila upande pasiweze kuonekana ndani. Elimu ya uzazi huitwa 'Ilmul ajinna', kwa sababu ya kutokuonekana kwa kile kilichokuwemo tumboni mwa mzazi. Hata mwendawazimu naye huitwa 'majinun' kwa sababu ya kutoweka kwa akili yake. Na Majinni nao wamepewa jina hilo kwa sababu ya kutokuonekana kwao kwa macho ya binadamu.
Ukichunguza utaona kuwa maneno yote hayo; 'Janna, ajinna, majinun, jinni', yana herufi ya 'Jiym na Nuun' ndani yake.
‘Imaan Juu Ya Ghayb
Kuamini juu ya ghayb (yasiyoonekana) ni katika misingi ya itikadi ya Diyn.
Allaah Anasema:
الم ﴿١﴾ ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٢﴾ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾
Alif Laam Miym. Hiki ni Kitabu kisicho na shaka ndani yake, ni mwongozo kwa wenye
taqwa. Ambao huamini ya ghayb na husimamisha Swalaah na katika vile Tulivyowaruzuku hutoa. [Al-Baqarah: 1-3]
Katika aya hizi, Allaah Ametaja baadhi ya sifa za wacha Mungu ikiwemo sifa hii ya kuamini ghayb.
Na maana ya neno 'ghayb', ni yale tusiyoweza kuyaona lakini ametueleza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) au Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ushahidi Wa Kuwepo Majini Katika Qur-aan Tukufu
Katika Qur-aan Allaah Anasema:
وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِّنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنصِتُوا
Na pale Tulipowaelekeza kwako (ee Muhammadصلى الله عليه وآله وسلم ) kundi miongoni mwa majini wakisikiliza kwa makini Qur-aan; [Al-Ahqaaf: 29]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي
Enyi hadhara ya majini na wana Aadam! Je hawajakufikieni Rusuli miongoni mwenu wanakusimulieni Aayaat Zangu.. [Al-An’-aam: 130]
Ushahidi Wa Kuwepo Kwa Majini Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Aalihi wa Sallam) 'Sunnah'
Katika 'Sunnah', (mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wameelezea Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim katika vitabu vyao vilivyo sahihi kwamba Ibni Abbas amesema:
“Majinni waliposhindwa kupata siri kutoka mbinguni na wakawa wanafukuzwa kwa vimondo kila wanapojaribu kuzisogelea mbingu, wakarudi makwao. Na jamii zao walipotaka kujua sababu ya kurudi kwao huko na kushindwa kwao kupata siri za mbinguni, maana kabla ya hapo walikuwa wakiweza kupata baadhi ya habari za huko, wakawajibu: "Pamewekewa vizuizi baina yetu na baina ya (kupata) habari za mbinguni". Wenziwao wakasema: "Bila shaka pana jambo kubwa lililotokea, tembeeni ardhi yote Mashariki na Magharibi mtafute ni kitu gani kilichokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni”.
Walipofika mahali paitwapo; “Soko la Akadha”, Waislamu walikuwa wakiswali Swalah ya Alfajiri, na majini hao wakaisikia Qur-aan ikisomwa, ndipo waliposema: "Hii (Qur-aan) WaLlaah, ndiyo iliyokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni".
Wakarudi kwa watu wao na kuwaambia: “Enyi jamii yetu! “Hakika sisi tumesikia Qur-aan ya ajabu" Allaah amesema katika Suwrah-Jinn aayah ya mwanzo:( Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nimefunuliwa Wahy kwamba kundi miongoni mwa majini lilisikiliza; wakasema: ‘Hakika sisi tumeisikia Qur-aan ya ajabu) [Al-Jinn: 1]”.
Hizi ni dalili zilizo wazi za kuwepo kwa viumbe hawa, na kukanusha kuwepo kwao kwa sababu ya kutokuonekana kwao si hoja, maana vitu vingi hatuvioni na tunakubali kwamba vipo kutokana na athari zake. Kwa mfano, joto, baridi, umeme n.k. Hivi vyote hatuvioni lakini tunakubali kuwepo kwake baada ya kuona athari zake.
Dalili Katika Qur-aan Kuwa Jinn Ameumbwa Kwa Moto
Ndani ya Qur-aan mna dalili nyingi zinazotujuulisha kuwa Jinni ameumbwa kwa moto, na tutazitaja baadhi ya dalili hizo:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ﴿١٢﴾
(Ibliys) Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’araf: 12]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ﴿١٥﴾
Na Akaumba majini kutokana na mwako wa moto. [Ar-Rahmaan: 15]
Dalili Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Aalihi wa Sallam) Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametujuulisha pia kuwa Majinni wameumbwa kwa moto, na tutataja baadhi ya kauli zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Wameumbwa Malaika kwa nuru na Majinni kwa ndimi za moto na Adam ameumbwa kwa mliyokwisha elezewa (Udongo).” [Imepokewa na Muslim].
Majini Wanazaliana
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا
Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu. [Al-Kahf: 50]
Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika aya hii pale aliposema 'na kizazi chake' inamaanisha kwamba majinni wanazaliana.
Wameumbwa Kabla Ya Binadamu
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia Anasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٦﴾ وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ﴿٢٧﴾
Na kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari. Na majini Tuliwaumba kabla kutokana na moto ulio mkali mno. [Al-Hijr: 26-27]
Kwa hivyo majini waliumbwa kabla yetu na waliishi katika ardhi hii hata kabla ya kuumbwa kwa Adam (‘Alayhis-salaam). Na hii ndiyo maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) alipowaarifu Malaika kuwa anataka kuumba viumbe katika ardhi wakasema:
أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ
Utaweka humo atakayefanya ufisadi humo na kumwaga damu, [Al-Baqarah: 30]
Malaika waliuliza suala hili si kwa ajili ya kupinga amri ya Allaah au kwa kumuonea wivu mwanadamu, bali waliuliza kwa ajili ya kutaka kuijua hikmah ya kuumbwa viumbe hawa, na hii ni kwa sababu walielewa kutokana na viumbe vilivyotangulia vilivyoishi ardhini, kwamba vina sifa ya ufisadi na umwagaji wa damu.
Anasema Ibni Kathiyr (huyu ni katika ‘ulamaa na mfasiri mkubwa wa Qur-aan) kwamba kabla ya kuumbwa kwa wanadamu, Majinni na viumbe wasiokuwa wanadamu walikuwa wakiishi ardhini na kwamba walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa pamoja na umwagaji wa damu.
Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
Majinni waliishi ardhini kabla ya wanaadamu na walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akawaondoa na kuwaleta wanadamu.
Maneno kama haya pia yalisemwa na Hassan Al-Basry (Rahimahu Allaah), na akaongeza kusema: Hii ndiyo maana Malaika wakamuuliza Rabb wao suali hilo.
Uhusiano Baina Ya Jinni Na Shaytwaan
Shaytwaan na Jinni asili yao ni moja, hapana hitilafu baina ya maulamaa kuhusu jambo hili, isipokuwa wamekhitalafiana katika suala: “Je Ibilisi ndiye baba wa Majinni (asili yao) mfano wa Adam ambaye ni baba yetu na asili yetu ?)”.
Majibu:
Iblisi si asili yao, bali yeye ni miongoni mwao.
Allaah Anasema:
فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ
Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini.. [Al-Kahf: 50]
Kwa vile Allaah amemtaja Iblisi kuwa ni ‘miongoni’ mwa majinni, kwa hivyo yeye ni mmoja wao na si asili yao kama mfano wa Adam (‘Alayhis-salaam) alivyokuwa asili ya wanadamu.
Tulisema kuwa wameitwa 'Majinni ' kwa sababu ya kutokuonekana kwao na sisi tumeitwa 'Insaan' kwa sababu ya kusahau kwetu, kwani neno 'Insaan', asili yake linatokana na neno 'Nisiyan', na maana yake ni kusahau.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Adam alisahau na vizazi vyake vikasahau.”
Ama neno 'Shaytwaan', katika lugha ya Kiarabu maana yake ni 'kila anayeasi na kupinga au kuzuwia au kushawishi viumbe wasiifuate njia ya Allaah', awe Jinni au Mwanadamu.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ۚ
Na hivyo ndivyo Tulivyojaalia kwa kila Nabiy maadui - mashaytwaan katika wana Aadam na majini wakidokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba na ya ghururi. [Al-An’aam: 112]
Iblisi Ni Katika Malaika?
Iblisi si katika Malaika, bali ni miongoni mwa Majinni kutokana na dalili zifuatazo:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema katika Qur-aan Tukuf:
فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ
Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini..[Al-Kahf: 50]
Na Anasema pia:
لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ
Hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]
Kutokana na aayah hii, tunapata ushahidi mwingine kuwa; Malaika hawamuasi Allaah. Kwa hivyo Iblisi angelikuwa Malaika, asingemuasi Rabb wake bali angetenda kama alivyoamrishwa. Lakini yeye alitenda kinyume na hivyo. Alimuasi Allaah pale alipokataa kumsujudia baba yetu Adam (‘Alayhis-salaam), akasema:
قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ﴿١٢﴾
(Ibliys) Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’raaf: 12]
Na hapa pia tunapata ushahidi mwingi pia kuwa Iblisi si miongoni mwa Malaika, kwani Malaika wameumbwa kwa Nuru na MaShaytwaan wameumbwa kwa moto.
Katika aayah iliyotangulia Iblisi alisema: 'Mimi ni bora kuliko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto". Angelikuwa yeye ni miongoni mwa Malaika angelisema: ‘Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa Nuru’. Kwa sababu Malaika wameumbwa kwa nuru kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia:
“Malaika wameumbwa kwa nuru na Majinni kwa ndimi za moto na Adam (ameumbwa) kwa mliyokwisha elezewa (Udongo).” [Imepokewa na Muslim na Ahmad bin Hanbal].
Aina Za Majini
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Majinni (wako) namna tatu; namna moja wana mbawa wanaruka na namna (nyengine) majoka na n’ge na namna nyengine hawaishi mahala pamoja na hupenda kuhama.” [Imepokewa At-Twabaraniy na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaniy ambaye ni mmoja katika ‘ulamaa wakubwa wa ‘ilmu ya tahakiki za Hadiyth.]
Mahali Wanapoishi
Majini wanaishi katika majangwa na katika sehemu za kutupa taka, kwa sababu wao wanakula mabaki ya vyakula vya binadamu.
Zimepokelewa Hadiyth nyingi pia kwa njia ya Ibni Abbas na Ibni Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akienda jangwani na kuwasemesha Majinni na kuwalingania katika diyn ya Kiislamu na kuwataka wamuabudu Allaah mmoja wa kweli.
Majinni wanapenda pia kuishi vyooni, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha du’aa ya kusoma kabla ya mtu kuigia chooni; akasema: “Mmoja wenu anapoingia chooni basi aseme: "ALlahumma inniy a’udhu bika minal khubuthi wal khabaaith.” Na maana yake: “Allaah najikinga kwako kutokana na majinni wanaume na majinni wanawake.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
Majini pia wanaishi katika mashimo:
Kutoka kwa Qataadah kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mmoja wenu asikojowe ndani ya shimo.” Na alipoulizwa kuna ubaya gani mtu kukojoa ndani ya shimo akasema: “Inasemekana kuwa Majinni wanapenda kuishi humo.” [Imepokewa na An-Nasaaiy]
Wanakula Na Kunywa
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mmoja wenu anapokula, basi ale kwa (mkono wa) kulia na anapokunywa anywe kwa (mkono wa) kulia, kwa sababu Shaytwaan anakula kwa kushoto na kunywa kwa kushoto.” [Imepokwa na Muslim].
Na akasema:
“Mtu anapoingia nyumbani akasema: 'BismiLlah', na anapokula (akasema BismiLlah), Shaytwaan husema: 'Hatuna makaazi humu (ndani ya nyumba hii), na hatuna chakula cha usiku'. Ama anapoingia asiseme: 'Bismillah', Shaytwaan husema: 'Tumepata makaazi humu', na asiposema BismiLlaah pale anapokula, basi (Shaytwaan) husema: 'Tumepata makaazi na chakula’.” [Imepokewa na Muslim]
Wana Uwezo Wa Kujigeuza
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda (chakula cha) Zakkah ya Ramadhwaan, akaja mtu akawa anaiba katika chakula kile, nikamkamata na kumuambia kwamba nitampeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akasema: 'Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi na shida nyingi.”
Anasema Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: “Ee Abu Hurayrah umefanya nini na mfungwa wako jana?”
"Akasema: "Nikamwambia: "Ee Rasuli wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aa.lihi wa sallam) akasema: “Ama huyu amekudanganya na atarudi”
Nikajuwa kwamba atarudi kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema hivyo. Nikamtegea, akaja tena siku ya pili kuiba chakula, nikamkamata, nikamuambia nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaniambia: “Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi sitorudia tena”. Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ee Abu Hurayrah umefanya nini na mfungwa wako jana?”
Nikamuambia: "Ee Rasuli wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ama huyu amekudanganya na atarudi”.
Nikamkamata mara ya tatu akiwa anaiba (tena) chakula, nikamuambia: "Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hii ni mara ya tatu na kila mara unasema hutorudia kisha unarudia." Akasema: "Niache nikufundishe maneno Allaah atakufaa nayo". Nikamuuliza: “Maneno gani hayo?" Akasema: “Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Aayatul-Kursy - Allahu Laa Ilaaha Illa Huwal Hayyul Qayuum - mpaka mwisho na itaendelea kukuhifadhi aayah hii na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka”. Nikamuacha aende zake.
Asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: “Amefanyaje mfungwa wako jana?” Nikamuambia: “Ee Rasuli wa Allaah amejidai eti amenifundisha maneno ambayo Allaah atanifaa nayo, basi nikamuacha huru". Akaniuliza: “Ni maneno gani hayo?” Nikasema: "Ameniambia: ‘Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Aayatul-Kursiy mpaka mwisho na Allaah Ataendelea kukuhifadhi nayo na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka’.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ama yeye amesema kweli ingawaje ni muongo.” Unamjua nani uliyekuwa ukizungumza naye siku tatu hizi ee Abaa Hurayrah?” Akajibu: "La simjuwi". Akasema: “Yule ni Shaytwaan.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
Kwa vile Shaytwaan huyu aliyekuwa akiiba alikuwa akimjia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa sura ya binadamu, basi hii ni dalili kwamba majini wana uwezo wa kujibadilisha umbile lao.
Wamo Miongoni Mwao Wanawake Na Wanaume
Katika Hadiyth niliyoitaja hapo juu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Anapoingia mmoja wenu chooni, basi aseme: “(Kwa jina la Allaah) Ee Allaah najikinga kwako kutokana na mashaytwaan ya kiume na ya kike” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Majini wanaoana na kuzaliana, na ushahidi umo ndani Qur-aan katika kauli Yake Subhanahu wa Ta’aalaa Aliposema:
أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا
Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu. [Al-Kahf: 50]
Hata hivyo ‘Ulamaa wengi hawakubali majini waowane na wanadamu. Pana kisa cha mwanamke mmoja kutoka Yemen alikuwa akidai kwamba anajiwa na jinni na kwamba jinni huyo anataka kumuowa. Alipoulizwa Imaam Maalik kuhusu jambo hili akasema:
‘Sioni kifungu chochote cha shari’ah kinachoharamisha, isipokuwa nakuogopeeni fitnah (Mitihani).’
‘Ulamaa wamesema kuwa kauli ya Imaam Maalik hii inatujulisha juu ya hofu yake. Kwani mwanamke yeyote anaweza kujipatia mimba kwa njia zisizo za halali, kisha akasema kwamba ameolewa na jinni na kwa njia hii uhuni utazidi na fitnah zitaenea.
‘Ulamaa wengine wamekataa kabisa fikra ya kuoana baina ya majini na wanadamu wakiegemea kauli ya Allaah isemayo:
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً
Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni kwamba Amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao; [Ar-Ruwm: 21]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً
Na Allaah Amekufanyieni wake katika jinsi yenu; na Amekufanyieni katika wake zenu wana na wajukuu; [An-Nahl: 72]
Katika aayah hizi Allaah Anatufahamisha kwamba ametuumbia wake zetu katika jinsi yetu, wakati Majinni si katika Jinsi yetu.
Na Akasema: “Ili mupate utulivu kwao", wakati mwanadamu hawezi kupata utulivu kwa jinni, maana siku zote mtu hupata utulivu kwa kiumbe aliye mfano wake na majini si mfano wetu.
Majini Wanakufa?
Allaah Anasema:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ
Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. [Ar-Rahmaan: 26]
Na Akasema:
وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ
Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. [Al-Qaswasw: 88]
Inavyojulikana ni kwamba Iblisi yuhai mpaka siku ya Qiyaamah. Allaah Amesema:
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾ قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ﴿٣٧﴾ إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ﴿٣٨﴾
Akasema: Rabb wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa.Akasema (Allaah): (Allaah) Akasema: Basi hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula. Mpaka siku ya wakati maalumu. [Al-Hijr: 36-38]
Kwa hivyo Ibilisi ataishi mpaka siku maalum anayoijua Allaah peke yake kisha atakufa, na majini nao pia wanazaliana na watakufa kama sisi.
Wamo Miongoni Mwao Waislamu Na Makafiri
Allaah Anasema:
وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَـٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا﴿١٤﴾
Na kwamba miongoni mwetu ni Waislamu, na miongoni mwetu wakengeukaji haki; hivyo atakayesilimu, hao ndio waliofuata uongofu. [Al-Jinn: 14]
وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا﴿١١﴾
Na kwamba miongoni mwetu ni wema, na miongoni mwetu kinyume chake; tumekuwa makundi ya njia mbali mbali. [Al-Jinn: 11]
Katika kuifasiri aayah hii, anasema Ibni Abbas (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
“Kauli ya Allaah: “Tumekuwa njia mbali mbali”, maana yake ni “Makafiri na Waislamu”.
Baadhi ya ‘ulamaa wanasema:
“Diyn mbali mbali na madhehebu mbali mbali.”
Waislamu Katika Majini Wataingia Jannah?
Katika tafsiri yake Ibni Kathyir amesema:
“Waislamu miongoni mwa Majini wataingia Jannah kama Waislamu katika wanadamu.”
Na dalili yake pamoja na dalili za maulamaa wengine ni kauli ya Allaah akitujuulisha juu ya hali ya wanawake wa Jannah aliposema:
لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ﴿٧٤﴾
Hajawabikiri binadamu kabla yao wala jini. [Ar-Rahmaan: 74]
Na Aliposema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ ﴿٤٦﴾ فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ﴿٤٧﴾
Na kwa mwenye kukhofu kisimamo mbele ya Rabb wake atapata bustani mbili. Basi ni zipi neema za Rabb wenu mnazikadhibisha? [Ar-Rahmaan: 46-47]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amejaalia jazaa ya majini na binadamu wema kuwa ni Jannah, na majini waliijibu aayah hii kwa kumshukuru Allaah wakasema:
‘Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako.’
Hii ni Hadiyth iliyosimuliwa na Imaam Attirmidhiy kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba amesema:
“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliisoma Suwrah Al-Rahmaan mpaka mwisho kisha akasema: ‘Mbona mumenyamaza kimya, Majini wamekuwa bora kuliko nyinyi kwa kujibu kila ninapowasomea aayah hii: "Basi ipi katika neema za Rabb wenu mnayoikanusha (kuwa si neema yake)?" Wao huijibu kwa kusema: "Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako”. [Imesimuliwa na Attirmidhiy na Al-Bazaar na Al-Haakim na pia Ibni Jariyr na Shaykh Al-Albaaniy amesema kwamba Hadiyth hii ni njema.]
Dalili inayopatikana kutoka katika aayah hizi ni kwamba; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwapa Majini mafundisho ya Diyn, na kuwafahamisha kwamba pana jaza ya Jannah kwa Mwenye kuogopa.
Kama Majini hawatoingia Jannah hapangekuwa na haja ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwatokea na kuwapa mafunzo ya Diyn na kuwajuulisha juu ya Jannah inayowangoja wale wanaomuogopa Allaah.
Majini Wanawaogopa Wanadamu
Ameeleze Ibn Abi Ad-Dunya kwamba Mujaahid amesema:
“Usiku mmoja nilikuwa nikiswali akanitokea mfano wa mtoto mdogo mbele yangu nikamshika kwa nguvu zangu zote akainuka na kuuruka ukuta hata nilisikia kishindo cha kuanguka kwake.”
Akaendela kusema: ‘Wao (majini) wanakuogopeni kama nyinyi mnavyowaogopa.’
Imepokewa kutoka kwa Mujaahid kuwa alisema:
‘Shaytwaan anakuogopeni kuliko nyinyi mnavyomuogopa akikukaribia usimregezee akakupanda, bali shindana naye na hatimae ataondoka.’
Kuweza Kwa Majini Kusikia Habari Za Mbinguni
Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba alisema:
“Amenihadithia mmoja katika Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa; usiku mmoja walipokuwa wamekaa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nyota moja ikaanguka na kun’gara. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza: “Mlikuwa mkisemaje wakati wa ujahilia (kabla ya kuja Uislamu?” Wakajibu: “Tulikuwa tukisema: Usiku wa leo amezaliwa mtu mtukufu na amekufa mtu mtukufu.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: “Bali haiangushwi nyota kwa ajili ya kifo cha mtu wala kwa kuzaliwa kwa mtu, lakini Rabb wetu aliyetukuka anapotoa amri, Malaika wabebao ‘Arsh husabbih (husema Subhana Llaah), na viumbe vya mbinguni vyote humsabbih Allaah pia. Kisha husabbih viumbe wa mbingu za chini mpaka habari inapofika katika mbingu ya dunia. Majini huzipata habari hizo na huwatupia mabwana zao nazo ni habari za kweli, lakini wao huongeza habari za uongo juu yake.”
Kutokana na Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha), amesema:
“Niliuliza: "Ee Rasuli wa Allaah, makuhani walikuwa wakituelezea baadhi ya mambo na yalikuwa ni ya kweli." Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hiyo ni habari ya kweli ameipokea jini akamtupia bwana wake na kuongezea uongo mara mia.” [Imetolewa na Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim na Ahmad na Al-Bayhaqiy]
Uchawi
Nini Maana Ya Uchawi?
Ibn Mandhwuur ambaye ni mtungaji wa kamusi maarafu ya Kiarabu iitwayo “Lisaanul-‘Arabiy” amesema:
“Neno “Uchawi”, kwa Kiarabu “As-Sihru”, maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na Shaytwaan na kwa msaada wake (Shaytwaan)”, na akasema pia kuwa: “Uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli”.
Ama Swahaabah Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Uchawi ni kuidhirisha batili katika sura ya haki.”
Hayo ni katika kamusi za lugha. Amma katika kamusi ya Diyn, maana ya neno ‘uchawi’ (Aa-Sihru), kama alivyofasiri Mwanachuoni mkubwa Fakhruddin Ar-Razi kuwa:
"Ni kila jambo lililofichika sababu zake, linalotokeza kwa sababu zisizo za kawaida na ndani yake mna hadaa (khidaa)".
Amma Shaykh Wahiyd ‘Abdus-Salaam Baaliy, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho 'As-Swaarim Al-Bataar Fiy Muhaarabat As-Saharatil Ashraar', na kitabu kiitwacho ‘Al Wiqaayah Minal Jinni Wa Shaytwaan’. Ambaye pia ni mtaalamu maarufu katika ‘ilmu ya majini na maShaytwaan na uchawi na ambaye pia ni katika maulamaa maarufu wanaotoa majini kwa njia ya kusoma Qur-aan, yeye anasema:
"Uchawi ni makubaliano baina ya mchawi na Jinni akishurutishwa mchawi kufanya mambo ya haramu au ya shirki, na baada ya kufanya hayo, Jinni anashurutishwa kumsaidia na kumtii mchawi huyo kila anachotaka".
Baadhi ya yale ambayo mchawi anatakiwa na Shaytwaan ayatende ili ajikurubishe naye ni:
o Mchawi anatakiwa auvae msahafu miguuni na aingie nao chooni |
o Aandike baadhi ya aya za Qur-aan kwa damu ya hedhi |
o Miongoni mwao wanashurutishwa kuandika aayah za Qur-aan penye nyayo za miguu |
o Au aiandike Suuratul-Faatihah kinyume nyume |
o Awsali bila ya Wudhuu |
o Wengine hutakiwa kuchinja mnyama bila ya kulitaja jina la Allaah kisha amtupe mnyama huyo mahali maalum anapoamrishwa na Shaytwaan |
o Wamo miongoni mwao wanaozungumza na nyota au kuzisujudia |
o Au hutakiwa kuandika herizi kwa maneno yenye kufru ndani yake |
Imeelezwa kwamba katika nchi ya Sham kulikuwa na mtu ambaye watu walikuwa wakimpenda na kumheshimu sana wakimdhania kuwa ni mtu mwenye makarama. Mtu huyu alikuwa kila mwaka katika msimu wa Hajji akiwatumikia watu wa mji wake kwa kuchukua barua zao na vitu vyao na kuwapelekea watu wao waliokwenda Saudia kuhijji.
Alikuwa akipeleka na kurudi kwa muda wa siku moja au mbili tu, na watu walimpenda sana na kuamini kwamba alikuwa ni Waliy. Siku moja mtu huyo aliumwa sana, akamuita mwanawe na kumwambia kuwa kama atakufa, basi aende mahali fulani wakati wa usiku na atamkuta ngamia wa aina fulani na ampande na kufuata amri zote atakazopewa na ngamia huyo.
Alipofariki dunia, mwanawe alifanya kama alivyoambiwa na baba yake, akaondoka peke yake wakati wa usiku na kuelekea jangwani kule alikoambiwa na baba yake kuwa atamkuta ngamia. Akamkuta ngamia kama alivyoambiwa, akampanda na alipokuwa anaenda, ngamia akaanza kusema na kumtaka kijana yule ashuke na amsujudie.
Yule kijana alishtuka sana kusikia ngamia akisema na pia akashangazwa na amri zake, akamwambia: "Vipi nikusujudie, kweni wewe ni nani?" Ngamia akajibu: "Ikiwa unataka nifuate amri zako kama nilivyokuwa kwa baba yako, na nikupeleke popote utakapo duniani, basi unisujudie kama alivyokuwa akinisujudia baba yako."
Yule kijana akajibu: "Mimi ninamsujudia Allaah peke yake, amma wewe la, siwezi kukusujudia". Yule ngamia akamrusha kijana yule kutoka juu ya mgongo wake na kumwangusha chini, na kijana yule akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama yake na kumuelezea yote aliyoyaona na kwamba baba yake alikuwa akimsujudia Jinni ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kusafiri kila anapotaka kwenda kwa kupaishwa na jinni yule.
Kwa haya inatubainikia kuwa Jinni hamsaidii wala hamhudumii mchawi wala mtu yeyote isipokuwa naye kwa mkabala wake anatumikiwa kwa kutendewa matendo ya kufru, na Maulamaa wanasema kuwa:
"Kila mchawi anapokufuru zaidi, basi Shaytwaan humtumikia kwa nguvu zaidi, na mchawi akitaka apate huduma ya hali ya juu kabisa kutoka kwa masultani wa majinni au kwa Kiarabu wanaitwa "Maradatul-Jinni", basi inambidi afanye kufuru kubwa zaidi. Kwa ajili hiyo, mchawi anapotaka nguvu juu ya wenzake inamlazimikia akufuru zaidi".
Kutokana na haya tunafahamu kwamba mchawi na Shaytwaan ni marafiki na washirika katika kumuasi Allaah.
Allaah Anasema:
وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ قَدِ اسْتَكْثَرْتُم مِّنَ الْإِنسِ ۖ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُم مِّنَ الْإِنسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا ۚ قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ﴿١٢٨﴾
Na Siku Atakapowakusanya wote (Allaah Atasema): Enyi hadhara ya majini! Kwa yakini mmetafuta kwa wingi (kuwapotoa) katika wana Aadam. Na watasema marafiki wao wandani katika wana Aadam: Rabb wetu! Tulinufaishana baadhi yetu na wengineo, na tumefikia muda wetu ambao Umetupangia. (Allaah) Atasema: Moto ndio makazi yenu, ni wenye kudumu humo, isipokuwa Atakavyo Allaah. Hakika Rabb wako ni Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Al-An’aam: 128]
Vipi Utaweza Kumjua Mchawi?
Zifuatazo ni dalili zitazokuwezesha kutofautisha baina ya mganga na mchawi. Utakapoona mojawapo ya dalili zufuatazo utambuwe kuwa huyo ni mchawi bila shaka yeyote na wala si Shaykh au mganga (daktari).
Dalili hizo ni:
·- Mchawi huuliza jina la mgonjwa na jina la mamake |
·- Huchukua baadhi ya vitu vya mgonjwa kama vile nguo za nje au za ndani au kitambaa cha kufutia jasho n.k. |
·-Hutaka mnyama mwenye sifa maalum au rangi maalum ili achinjwe na hapigiwi BismiLlaah anapochinjwa |
·-Huandika hirizi |
·-Husema maneno yasiyojulikana |
·-Humtaka mgonjwa aepukane na watu muda maalum na akae katika chumba kisichofikiwa na jua |
·-Mara nyengine humtaka mgonjwa asiguse maji muda wa siku arubaini hivi (anasema Shaykh Wahiyd Abdus-Salaam Bali kwamba akikutaka ufanye hivyo ujue kwamba Jinni anayemtumikia mchawi huyo ni mkiristo) |
·-Humpa mgonjwa vitu ili avifukie ardhini |
·-Humpa mgonjwa karatasi aziunguze kisha ajifukize na moshi wake |
·-Mara nyengine humwambia mgonjwa jina lake na mji anaoishi |
·-Huandika maneno katika karatasi na kumwambia mgonjwa azichemshe na kunywa maji yake |
Ukiona Dalili Hizi Kwa Mganga Umjue Hapo Hapo Kuwa Ni Mchawi Na Uepukane Naye |
Anasema Shaykh Wahiyd ‘Abdus-Salaam Baliy:
"Ukiutizama uso wa mchawi utakiona kiza cha kufru kilivyotanda katika uso huo mfano wa mawingu meusi”.
Anaendelea kusema Shaykh huyo:
“Kwa wale wanaowajua wachawi, wanawaona siku zote wakiwa katika dhiki, shida, matatizo katika siha zao, matatizo na wake zao au watoto wao na siku zote hawana raha wala utulivu”.
Allaah Anasema:
وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا﴿٦﴾
Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu. [Al-Jinn: 6]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا
Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, [Twaahaa: 124]
Dalili Kuwa Uchawi Upo, Katika Qurani Na Katika Sunnah - Mafundisho Ya Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Katika Suwrah Yuwnus aayah ya 77 Allaah Anasema:
قَالَ مُوسَىٰ أَتَقُولُونَ لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَكُمْ ۖ أَسِحْرٌ هَـٰذَا وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُونَ﴿٧٧﴾
Muwsaa akasema: Je, mnasema kuhusu haki ilipokujeni? Hii ni sihiri? Na wachawi hawafaulu. [Yuwnus: 77]
Hii ni dalili kwamba uchawi upo na Allaah anatufundisha katika aayah hii kwamba uchawi haufaulu.
Na katika Suwrah Al-Falaq Akasema:
وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ﴿٤﴾
Na kutokana na shari ya wanaopuliza mafundoni. [Al-Falaq: 4]
Katika kuifasiri aayah hii, mmoja katika maulamaa wakubwa wa tafsiri ya Qur-aan Imaam Al-Qurtubiy amesema:
"Maana ya neno "Naffaathaat", ni wachawi wanapopuliza katika nyuzi huku wakizipiga fundo.
Na Ibni Kathiyr katika tafsiri yake akinukuu kutoka kwa Ikrimah na Mujaahid na Al-Hassan Al-Basry (Rahimahuma Allaah) amesema:
"Hawa wanaopuliza mafundoni ni wachawi, na Allaah anatuamrisha tujiepushe na shari zao.
Amma Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinazotufahamisha kwamba uchawi upo na kwamba uchawi ni katika madhambi makubwa sana, ni hizi zifuatazo:
Kutoka kwa Abi Hurayra (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Jieupusheni na (mambo) saba yaangamizayo. Wakasema: 'Ni yepi hayo ewe Rasuli wa Allaah?" Akasema: "Kumshirikisha Allaah, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharimishwa na Allaah ila kwa haki yake, kula riba, kula mali ya yatima, kurudi nyuma (kukimbia) katika vita vya Jihaad (huku ukiwaacha wenzio wanapigana), na kuwasingizia uwongo wanawake wema wasio na makosa". [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ndugu yangu Muislamu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema kuwa mambo hayo 'yanayomuangamiza', maana yake ni kuwa yanamuangamiza mtu katika moto wa Jahannam.
Ukirudia kuisoma tena Hadiyth hiyo utaona kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameutanguliza uchawi kabla ya dhambi ya kuuwa, ingawaje kuuwa ni dhambi kubwa sana, na Allaah Anasema katika Suwrah -Nisaai aayah ya 93:
وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا﴿٩٣﴾
Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam, ni mwenye kudumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu. [An-Nisaa: 93]
Juu ya ukubwa wa dhambi hiyo ya kuuwa, lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameipa uzito zaidi dhambi ya uchawi kwa kuiweka nafasi ya pili baada ya shirki na kabla ya dhambi ya kuuwa.
Soma Bahati Yako (nyota Yako) Lucky Stars
Katika Hadiyth ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Dawuud na Ibni Maajah, Hadiyth ambayo Shaykh Al-Albaaniy ameitaja kuwa ni "Hadiyth njema", na Hadiyth hii pia ni dalili kwamba ‘ilmu ya kutabiri kwa nyota ambayo huandikwa katika magazeti na watu hupenda kusoma kwa kutaka kujua bahati zao, kitendo hiki ni haramu na yeyote atakayesoma nyota yake, basi Swalah zake hazikubaliwi kwa muda wa siku arobaini. Hii ikiwa anasoma na huku haziamini, amma akisoma na huku anaziamini, basi anaingia katika hukumu ya aliyemuendea mtabiri na kumuuliza jambo, na anakuwa amekwisha kufuru yote yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Atakayejifunza sehemu ya ‘ilmu ya nyota (utabiri) amejifunza sehemu ya uchawi, akiongeza atakachoongeza (katika uchawi au nyota).”
Na hii ni kwa sababu wanaosoma ‘ilmu ya nyota (utabiri) wanaamini kwamba katika nyota wanaishi majini ambao ni masultani na wakuu, na wanaitakidi kuwa mambo yetu yote husababishwa na harakati za nyota hizo kila zinapotaharaki kutoka mahali kuelekea pengine. Kwa ajili hiyo wao huzingoja nyota hizo masaa mengi ya usiku ili wapate kuandika talasimu zao, na huku ni sawa na kuziabudu nyota hizo.
(Pana tofauti baina ya ‘ilmu ya anga za juu (Astronomy) ambayo haina ubaya wowote ndani yake, na ‘ilmu ya nyota (Astrology) - utabiri - ambayo ni haramu).
Ushahidi mwengine unapatikana katika Hadiyth iliyosimuliwa na ‘Umraan bin Hussaiyn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Hayuko pamoja nasi mwenye kuamini juu ya nukhsi (ukorofi) [Waarabu walikuwa wanapotaka kusafiri humrusha ndege na akielekea upande wa kulia basi husafiri, amma akielekea upande wa kushoto huamini ni ukorofi na kuivunja safari yake], na pia hayuko pamoja nasi mwenye kupiga ramli au mwenye kupigiwa, na atakayemuendea mtabiri na akamsadiki asemayo basi kesha kufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam”. [Imepokewa na Al-Bazaar]
Katika Hadiyth hizi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatukataza tusiwaendee wachawi wala watabiri wa aina yoyote ile kwa kuwauliza juu ya jambo lolote lile, hata kama atajibadilisha na kujiita Al-Hajj Fulani au Shaykh Fulani au Maalim Fulani au Mganga Fulani na hii ni kutokana na kufru zao wanazozifanya kwa kuwasujudia majini na kuridhishana nao ili wawatumikie.
Na hii ni dalili kwamba uchawi upo, maana kama haupo, basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asingetukataza kufanya kisichokuwepo.
Pia Hadiyth hizi zinatufahamisha kwamba mambo haya ni haramu na atakayeyatenda anakuwa amekwishayakanusha yale aliyokuja nayo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwamba hapana aijuwae ghaibu isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Hadiythi ziko nyingi sana, lakini hizi pamoja na aya zilizotangulia zinatosha kuwa ni dalili kwamba yote hayo yametajwa katika Qur-aan na katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Uchawi Umeanza Zama Za Nabii Suleiman ('Alayhis-salaam)?
Wachawi wanaposoma talasimu zao huwadanganya watu kwa kuanza kusoma baadhi ya aayah au sura ndogo ndogo za Qur-aan na kulitajataja jina la Nabii Sulaymaan na utawasikia daima wanamnasibisha Nabiy huyu (‘Alayhis-salaam) na kufru zao hizo ili wajinga wanaowafuata wadhani kwamba hayo yamo katika diyn.
Uchawi haujaanza zama za Nabii Sulaymaan kama wachawi wanavyozuwa na kumsingizia Nabii huyu wa Allaah. Bali ulikuwepo kabla yake kwa miaka elfu nyingi.
Uchawi ulikuwepo tokea zama za Nabiy Swaalih (‘Alayhis-salaam) aliyekuja kabla ya Nabiy Sulaymaan kwa miaka elfu nyingi.
Allaah Anasema:
قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ﴿١٥٣﴾
Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa. [Ash-Shu’araa: 153]
Uchawi Ni Kufru
Wachawi na wafuasi wao hupenda kumsingizia Nabiy Sulaymaan kwa kuinasibisha na kufru yao hiyo na Nabiy huyu mtukufu ambaye Allaah Alimpa ufalme ambao hajaupata mwengine baada yake, kwa sababu alimpa uwezo wa kuwatiisha majini, upepo, na alipewa uwezo wa kujua lugha za wanyama n.k.
Allaah Anasema:
فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ رُخَاءً حَيْثُ أَصَابَ ﴿٣٦﴾وَالشَّيَاطِينَ كُلَّ بَنَّاءٍ وَغَوَّاصٍ ﴿٣٧﴾وَآخَرِينَ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ ﴿٣٨﴾
Basi Tukamtiishia upepo unaokwenda kwa amri yake polepole popote anapotaka kufika. Na mashaytwaan, kila ajengaye na mpiga mbizi. Na wengineo, wafungwao minyororoni. [Swaad: 36-38]
Katika tasfiri yake, Ibni Kathiyr amenukuu kauli ya Ibni Abbas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
"Asif - alikuwa mwandishi wa Nabiy Sulaymaan na alikuwa akilijuwa jina tukufu la Allaah (Al-Ismul-a’adham), na alikuwa akiandika kila kitu katika daftari kwa amri ya Nabii Sulaymaan na kulificha daftari hilo chini ya kiti cha Nabii Sulaymaan. Alipofariki Nabiy Sulaymaan, majini wakayatoa maandishi hayo wakachanganya na kuandika baina ya kila mistari miwili uchawi na kufru yao, kisha wakawaambia watu wao kuwa hayo ndiyo maandishi ya Nabii Sulaymaan na ndiyo aliyokuwa akiyatenda, na Mayahudi wakayasadiki maneno hayo, wakawa wanamtangazia Nabii huyu kuwa ni mchawi.“
Mpaka alipokuja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuteremshiwa aayah ya 102 katika Suwrah Al- Baqarah:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ﴿١٠٢﴾
Na wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan juu ya ufalme wa Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru. Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua. [Al-Baqarah: 106]
Anasema Shaykh ‘AbduLlaah Swaalih Al-Faarsiy katika tafsiri yake kwamba aayah hii inaonesha wazi kuwa:
a. - Uchawi ni amali ya ukafiri |
b. - Mchawi hawezi kumdhuru mtu ila kwa idhini ya Allaah |
c. - Mchawi mwenyewe anadhurika kwa uchawi wake |
Katika aya hii Allaah anatufahamisha pia kuwa uchawi ulikuwepo kabla ya Nabii Sulaymaan kwa miaka mingi. Tokea zama za ustaarabu wa Babiloni walipoteremshwa Malaika wawili, Haruta na Maruta ili kuwaonyesha watu na kuwafahamisha nini uchawi, wapate kuujuwa mara watakapouona na wasiufuate, na hii ni kwa sababu uchawi ni kufru.
Watu waliacha kufuata nasaha za Malaika hao na wakajifunza yale ambayo yatawadhuru na wala hayatawafaa, ingawaje walikuwa wakijuwa kuwa aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera. Wachawi mpaka hivi sasa wanajaribu kuunasibisha uchawi wao na Nabiy Sulaymaan pamoja na Malaika hawa wawili.
Tatizo kubwa hupatikana pale wachawi wanapofanya uganga wao pale wanaposema maneno yao ya kichawi. Wao huchanganya maneno hayo na baadhi ya aayah za Qur-aan na wanaofanyiwa uganga hudhania kwamba Qur-aan ndiyo inayosomwa na kwa ajili hiyo na kutokana na ujinga wao, huhadaika na kujiingiza nao katika shirki.
Hukumu Ya Uchawi Katika Diyn Ya Kiislamu
Anasema Imaam Maalik (Rahimahu Llaah) katika kitabu chake Al-Muwattaa kwamba:
“Mchawi anayefanya uchawi mwenyewe, hukumu yake ni kuuwawa, ama yule anayemuendea mchawi, huyo hauwawi.”
Ibni Qudaamah naye anasema: "Hukumu ya mchawi ni kuuawa."
Hukmu kama hizi pia zimepokelewa kutoka Swahaba mbali mbali kama vile ‘Umar, ‘Uthmaan, Ibni ‘Umar na wengineo (Radhwiya Allaahu ‘anhum).
Hukmu hii ya kuuwawa kwa mchawi pia ameitamka Imaam Ahmad bin Hambal (Rahimahu Llaah).
Na imepokelewa kutoka kwa Swahaba mbali mbali kwamba ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwaandikia Swahaba kuwaamrisha wamuuwe kila mchawi mwanamke au mwanamume.
Anasema mmoja katika swahaba kwamba baada ya kupata maandishi hayo waliwakamata na kuwaua wachawi watatu.
Amma Imaam Shaafi’iy (Rahimahu Llaah), yeye anaona kuwa mchawi asiuliwe isipokuwa akikiri mwenyewe kwamba ameuwa kwa uchawi wake.
Kutokana na yaliyotangulia infahamika kwamba Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) pamoja na maulamaa wengi wanaona kwamba hukumu ya mchawi ni kuuliwa. Isipokuwa Imaam Shaafi’iy (Rahimahu Llaah), yeye anaona kuwa auliwe tu ikiwa mchawi huyo atakiri kwamba ameuwa kwa uchawi wake.
Kujikinga Na Shari Za Wachawi Na Majini Wao
Zifuatazo ni baadhi ya njia za kujikinga na waovu hao:
Kusafisha Niyah
Iblisi alipohukumiwa kupotea kwa sababu ya kuasi kwake, aliahidi kuwapoteza viumbe wote isipokuwa wale waliosafika kikweli.
Iblisi akasema kumwambia Allaah: "Isipokuwa wale waja wako waliosafika kweli kweli".
Kusafisha nia (Al-Ikhlaasw), maana yake ni kuzihusisha ‘Ibaadah zote kwa moyo wote kwa ajili ya Allaah peke yake. Sio kujionesha mbele za watu kuwa ni Mcha wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na unapokuwa peke yako unamuasi.
Al-Junaid, mmoja katika maulamaa wakubwa wa wakati wake amesema:
"Allaah ana waja wake wenye akili, walipopata akili wakaifanyia kazi, walipofanya kazi wakaitakasa kazi hiyo na kule kuitakasa kwao kukawaingiza katika milango ya kheri yote".
Kutia Wudhuu:
Katika Hadiyth nyingi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha juu ya umuhimu wa kubaki na Wudhuu kila mtu anapoweza kwa ajili ya kupata thawabu na kwa ajili ya kujikinga na kila shari.
Swalah Katika Jama’ah:
Kuswali Swalah za jamaa msikitini, maana Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kwamba mbwa mwitu (Shaytwaan) huwala kondoo wanaotembea mbali na wenzao.
Swalah Za Sunnah:
Swalah za Sunnah uzisali nyumbani, usiiache nyumba yako ikawa kama kaburi, na unaposali nyumbani Shaytwaan hulia na kutoka nje ya nyumba yako huku akisema: "Sina pa kulala humu, wala sina pa kula humu".
Kumuomba Allaah:
Kumuomba Allaah kila mara Shaytwaan anapotaka kukuchezea na kila unapoingia mahali pachafu.
Kwa mfano:
Unapoingia chooni uisome dua hii: "Allahumma inniy a’udhu bika minal khubuthi wal khabaaith”. Na maana yake: (Allaah mimi najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake).
Kabla ya kulala usome Suwrah Al-Ikhlaasw, Suwrah Al-Falaq na Suwrah An- Naas pamoja na Aayatul-Kursiy. Maana Hadiyth sahihi tuliyoitaja mwanzo wa darsi hii inasema kuwa anayeisoma aayah hii, Allaah Anaendelea kumhifadhi mpaka asubuhi anapoamka.
Ni vizuri pia kuzisoma aayah tano za mwanzo za Suwrah Al-Baqarah kisha Aayatul-Kursiy. Kisha kuzisoma aayah tatu za mwisho za Suwrah Al-Baqarah na Allaah atakulinda na majini pamoja na uchawi katika siku nzima.
Kuzisoma dua mbali mbali kama vile:
“A’uwdhu bikalimaati Llaahi ttaammaati min kulli shaytwaani wa haammah wa min kulli ‘aynin laammah”. Na maana yake ni: "Najikinga kwa Allaah kutokana na kila Shaytwaan na (kila) mdudu anayesota (kama vile nge na nyoka n.k. na kwa kila jicho linalodhuru).
“Bismillahi lladhiy laa yadhuru ma-‘a smihiy shay un fil ardhi walaa fiy ssamaa wahuwa ssamiy’ul ‘aliym”.
Unapotoka nje ya nyumba usome: “BismiLlaah tawakkaltu ‘ala Llaah walaa haula walaa quwwata illa biLlaah.”
Kusoma Qur-aan
Qur-aan ni kinga kubwa sana, na Muislamu anatakiwa daima awe anaisoma nyumbani kwake. Hapana kitukufu anachokiogopa Shaytwaan kuliko Qur-aan, du’aa, pamoja na ‘Ibaadah zinazokusogeza karibu na Rabb wako. Na kila mtu anapokuwa mbali na Rabb wake katika kumuasi, basi atambuwe kuwa anajiweka mbali na Rabb wake na kwa ajili hiyo anampa Shaytwaan fursa ya kumsogelea na kumtawala.
Kwa kupiga mfano: Mtu anapita njiani akakumbana na mbwa mkali anayebweka huku akiwa amemzuwilia njia. Bila shaka mtu huyo atashindwa na hila ya kumuondosha ili apite na zake; bali ataogopa asitafunwe na mbwa huyo. Lakini mtu huyo mara atakapotambua kuwa mwenye mbwa huyo yupo karibu, na kwamba akimuomba amwondoe njiani basi kwa ukelele wake mmoja tu, mbwa huyo ataondoka taratibu na kumpisha apite, bila shaka atamuomba msaada wake.
Mfano huu ni mfano wako wewe binadamu unapomuomba Rabb wako akukinge na mashaytwaan.
Du’aa Zinamkumba Shaytwaan
Kama vile Shaytwaan anavyoweza kuwakumba wanadamu walioghafilika na kumdhukuru Allaah, Shaytwaan naye pia hukumbwa na du’aa za wanaomdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
Imeelezwa na maulamaa kuwa, Shaytwaan anapojaribu kumsogelea Mcha wa Allaah mwenye kumdhukuru Rabb wake kila wakati kwa ajili ya kumkumbuka, basi du’aa zake humkumba Shaytwaan huyo na kumuangusha chini. Kisha mashaytwaan wenzake hukusanyika na kuulizana: "Amepatwa na nini huyu?" Wenzao huwajibu: "Amekumbwa na binadamu".
Dhikru Llaah
Kwa kumaliza napenda kujikumbusha nafsi yangu kwanza na pia kuwakumbusha ndugu zangu Waislamu pia kwamba, hakuna kinga kubwa inayomkinga mtu na kila balaa baada ya Qur-aan kama kumdhukuru Allaah.
Kumdhukuru unapolala, unapoamka, unapotoka nyumbani, unapositushwa na jambo, unapofurashishwa. Katika kila jambo lako jema au lisilo jema, bali hata katika kumuasi Rabb wako unapomkumbuka Allaah na kukumbuka uwezo Wake juu yako na neema Zake juu yako mara utayaacha maasi hayo.
Na ukumbuke kwamba kwa msaada wake Yeye tu (Subhaanahu wa Ta’aalaa) utaweza kujikinga na kila balaa.
Usiingize Ndani Ya Nyumba Yako Vifuatavyo:
Mwisho kabisa ningependa kukumbusha kuwa ndani ya nyuma yako usije ukaingiza yafuatayo:
· Usitundike picha [ya viumbe hai] yeyote ile.
· Usisikilize nyimbo.
· Usiweke baraza za kusema watu au kutukana watu.
· Usitizame filam za sinema n.k.
Hayo yote yanakaribisha mashaytwaan katika nyumba yako na yanafukuza Malaika.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾ إِنَّ الَّذِينَ اتَّقَوْا إِذَا مَسَّهُمْ طَائِفٌ مِّنَ الشَّيْطَانِ تَذَكَّرُوا فَإِذَا هُم مُّبْصِرُونَ ﴿٢٠٢﴾
Na pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan; basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. Hakika wale waliokuwa na taqwa inapowagusa pepesi za shaytwaan hukumbuka, basi mara wao huwa wenye kuona kwa utambuzi. [Al-A’raaf: 200-202]
Hivi ndivyo ilivyo, wale wanaoasi daima hawapendi kuona wenziwao wanaokoka na wanajaribu kila njia kuwavutia katika maasi. Lakini mwenye kuomba msaada wa Allaah basi Rabb wake