Nini Afanye Aweze Kudumisha Swalah Ya Alfajiri Na Kuweza Kukuza Iymaan Yake?

SWALI:

Asalama aleykum.

Napenda kuwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya.swali langu nini nifanye ili niweze kudumisha sala ya fajar. Nashindwa kuamka ktk swala hio. Pia imani yangu ni very weak nifanyaje? jazakalahu khairan


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kutoweza kuamka katika Swalaah ya Alfajiri.

Jambo lolote mtu yeyote akiwa na hima nalo basi hufanikiwa kulifanya na akapata usaidizi kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

Hivyo, kuinuka kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri bila shaka zipo njia nyingi zinazoweza kumsaidia mtu kuamka. Miongoni mwazo ni:

 

  1. Ni kutegesha saa kwa wakati unaohitajia kuamka.

 

  1. Ikiwa umeoa saidianeni na mkeo katika kuamshana na ujira wake ni mkubwa wa kufanya hilo.

 

  1. Ikiwa katika nyumba wapo watu wengine kama wazazi, ndugu na watoto mnaweza kusaidiana. Na huko ndiko kusaidiana kwenye ujira mkubwa.

 

  1. Ikiwa una jirani Muislamu basi aganeni muwe mnasaidiana ili muweze kuswali kwa wakati.

 

  1. Ikiwa una rafiki au jamaa walio mbali wanaweza kuwa ni wenye kukupigia simu ili kukuamsha katika usingizi.

 

Hivyo zipo njia nyingi za kumwezesha mtu kuamka; nasi ni kutaka na kutotaka kuamka kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri.

 

Ama Imani kudhoofika ni katika maumbile ya mwanaadamu kwani Iymaan hupanda na kushuka. Hupanda kwa utiifu na hushuka kwa maasiya. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aayah Zake huwazidisha Iymaan, na wakamtegemea Mola wao. Hao ambao wanasimamisha Swalaah na wanatoa katika yale Tunayowaruzuku” (al-Anfaal 8: 2 – 3).

 

Hivyo, ili kuongeza Iymaan yako ufanye mambo yafuatayo:

 

  1. Uwe na Iymaan yenye nguvu ya Allaah Aliyetukuka kwa kuwa na khofu Yake na matarajio. Ukifanya hivyo utaweza kumtii kwa kutekeleza maagizo Yake na kuacha makatazo Yake.

 

  1. Kuisoma Qur-aan kwa kuilewa, kuizingatia na kutekeleza yaliyo ndani.

 

  1. Kusoma Sunnah na Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa lengo la kutaka kufuata aliyokuja nayo.

 

  1. Kusoma visa vya watu wema na jinsi walivyofanya katika kukuza Iymaan zao.

 

  1. Kufanya urafiki na watu wema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share