Suratul ‘Aswr Ina Siri Yoyote Kubwa?
Suwratul ‘Aswr Ina Siri Yoyote Kubwa?
SWALI:
Assalam Aleykum. Sifa Njema Anastahiki Rabb Wa Viumbe Vyote Allaah Tabaraka Wataa'alaa. Nimepata Kusikia Kuwa Suwrah Al-asr Ni Suwhra Ambayo Haina Kafu Pia Suwrah Hii Ina Siri Kubwa Ndani Yake. Je Naweza Kufafanuliwa Siri Hiyo.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika si Suwrah ‘Aswr peke yake ambayo haina Kaaf bali na Suwrah Al-Falaq pia haina kaaf. Na Suwrah yoyote ile haiwi kubwa au kuwa na siri kwa kuwa haina herufi moja au nyengine.
Siri ambayo inaweza kuonekana iliyomo katika Suwrah hiyo ni kugusia mambo ya mwana Aadam kwa muhtasari. Na kwa ufupi wake imekusanya mambo yafuatayo:
1. Maisha ya mwana Aadam hapa duniani.
2. Iymaan.
3. Matendo mema.
4. Da‘wah.
5. Subira (na maadili mema) kwa ujumla.
Kwa kujumlisha maudhui hayo yote kwa muhtasari ndipo Imaam Ash-Shaafi‘iy akawa ni mwenye kusema: “Lau kama Allaah hakuteremsha Suwrah nyengine ila hii ingewatosha.”
Anakusudia ingewatosha kwa sababu ya maudhui muhimu zilizotajwa ndani ya Suwrah hiyo ambazo zimetanda kila upande wa binaadamu katika maisha yake ya kila siku.
Lakini hiyo kauli ya: “kuna siri kubwa” ni maneno ambayo hayakuthibiti dalili zake. Ni maneno yanayotumiwa na baadhi ya wahadhiri wasio na ‘ilmu kuwaambia watu kwa kutaka kutukuza jambo kupita kiasi au kulipa hali ambayo haipo.
Qur-aan haifichi kitu na hakuna usirisiri wowote katika mambo ya Uislamu.
Na Allaah Anajua zaidi