Kumuita Mtoto Nuur Muhammad Inafaa?

SWALI:

Asalam Alaykum Warahamatullah Wabarakatu

Shukran sana ndugu zetu wa Al hidaaya mwenyezi mungu awazidishie kila la kheri na afya njema na muzidi kutuelimisha kwani tuna nufaika sana na tovuti hii Insha allah Allah Azidi kuwawezesha.

Je kumuita mtoto NOOrmohamed inafaa au anatakiwa kuitwa Mohamed peke yake? Kama kutakua na category ya majina mazuri ya maswahaba au watu wema waliotangulia tupate kuchagua inshaallah.

Jazakallah khair


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kufaa au kutofaa kumuita mtoto jina la Noormuhammad.

Ni vyema kumuita mtoto ima Muhammad peke yake au Nuur peke yake na wala usichanganye hayo majina mawili. Kuyacanganya kunaleta maana ya ‘Nuru ya Muhammad’ na ni jina ambalo linaweza kutafsirika tafsiri nyingi na pia hakujawahi kufundishwa jina kama hilo katika majina mazuri.

Kadhalika tumekatazwa kujiita majina ya kujinasibisha na sifa Fulani kubwa na huenda akawa mtoto hana sifa hiyo atakapokuwa mkubwa, au kuwa ni mwenye sifa adui au dhidi ya ile aliyopewa. Mfano yale majina yenye kutoa sifa njema kama ‘Taqiyud Diyn’ ‘Mcha Mungu wa Dini’ au ‘Muhyud Diyn’ (watu wanatamka muhidini) yaani ‘Mwenye kuihuisha Dini’, na tumeona baadhi ya wenye majina kama hayo ima ni walevi, wahuni na sifa nyingi ovu. Kwa hiyo Muislamu anatakiwa ajiepushe na majina kama hayo na achukue na kutumia majina yale ambayo wameitwa nayo wema waliotangulia kama Mitume, Maswahaba na Matabi’iyn. Na majina mazuri ni mengi kupita kiasi.

Ama kuhusu majina, yapo mengi yaliyo mazuri kwa wanaume na wanawake.

Ikiwa ni ya wanaume basi tuna majina yale 25 ya Manabii na Mitume, pia majina yaliyofungamana na jina la Allaah kama ‘Abdullaah, ‘Abdur-Rahmaan, Abdur-Rahiym na kadhalika. Na pia majina ya Maswahaba. Ama ikiwa ni ya wanawake basi utapata lile lililotajwa katika Qur-aan la Maryam, majina ya wanawake wema waliotangulia, wakeze Mtume wa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Khadiyjah, Sawdah, ‘Aaishah, Hafswah, Swafiyyah, Maymuunah, Zaynab, Hind, Ramlah, na kadhalika na pia majina ya Swahaabiyaat kama Rumayswaa’, Humayswaa’, Zunayrah, Faatwimah, Sumayyah, Nusaybah, Barakah, Asmaa’, Khansaa’ na kadhalika.

Pia unaweza kusoma zaidi katika kiungo kifuatacho:

Majina Ya Watoto Na Maana Yake

Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto

Kumwita Mtu Muhammad, Kuliandika Na Kutamka Kama Linavyoandikwa

Hukmu Ya Kuwapa Watoto Majina Ya Allaah Au 'Abdur-Rasuul, 'Abdul-Husayn

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share