03-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya 1: Utangulizi

 

03-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya 1: Utangulizi

 

Alhidaaya.com

 

 

Sura Ya 1: Utangulizi

 

Hakuna shaka yoyote kwamba, hakika shukrani zote zinamstahikia Allaah. Tunamhimidi, tunaomba msaada Kwake, na tunaomba maghfirah. Tunaomba hifadhi kwake Allaah kutokana na maovu ya nafsi zetu, na makosa ya matendo yetu. Yeyote Allaah Anayemuongoza, hakuna wa kumpotosha, na yeyote Allaah Anayempotosha, hakuna wa kumuongoa. Ninashuhudia pia kwamba hakuna yeyote anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah, na ninashuhudia kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mjumbe na Nabiy Wake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٢﴾

Enyi mlioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekwishakuwa Waislamu kamili[Aal 'Imraan: 102]

 

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١﴾

Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwachunga daima. [ An-Nisaa: 1]

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli nyofu ya haki.Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu. [Al-Ahzaab: 70-71]

 

Kwa hakika, maneno bora ya kweli ni Maneno ya Allaah, na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mambo maovu kabisa ni yale ya kuzusha, na kwa kila jambo jipya lililoanzishwa ni uzushi, na kwa kila uzushi ni upotofu, na upotofu unapelekea Motoni.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Kwa hakika, Wanachuoni ni warithi wa Rusuli, na Manabiy hawakuacha nyuma dinaar wala dirham kurithiwa. Isipokuwa, wameacha nyuma elimu ili kuweza kurithiwa, na yeyote anayechukua kutoka humo amepata fungu kubwa mno.” [1]

 

"Ilmu hii (Diyn) itabebwa na watu wenye kuaminika katika kila kizazi. Wakizikataa tahriyf (madai ya kizushi) ya wale wanaovuka mipaka, madai ya uongo ya waongo, na ta-awiyl (upinduaji tafsiri) za wajinga." [2]

 

"Allaah Atamuinua katika jamii hii mwishoni mwa kila miaka mia moja mtu ambaye ataihuisha Diyn yake." [3]

 

Historia ya Uislamu inasimama kama ni shahidi wa Wanachuoni wengi wakubwa wakubwa, watengenezaji na waitaji wa njia ya Allaah; wale ambao wamefuata nyayo za Salafus-Swaalih (wema waliotangulia) katika iymaan na matendo, katika kumuitikia Allaah na kuweka vipaumbele kwenye maisha; katika ushujaa na ujasiri, katika hatari na jitihada na katika kujitoa muhanga wa maisha yao yote kwa moyo wote kwa ajili ya shughuli ambazo ni faida kwa ajili ya siku ya Qiyaamah. Miongoni mwa wenye sifa hizi bora na walio juu ni al-Allaamah, Al-Imaam, Shaykh Al-Islam Taqiyud-Diyn Ahmad Ibn Taymiyyah – ambaye kumbukumbu za maisha yake zinaweza kufikia kurasa nyingi za historia ya Kiislamu zikiwa na mafanikio ya milele na hamasa zisizo na mpaka.

 

Ibn Taymiyyah alikuwa ni Mwanachuoni mkubwa ambaye alikuwa mweledi kwenye nyanja nyingi za elimu ya Kiislamu na aliyeishi ndani ya kipindi kiovu cha kisiasa, kijamii na kidini. Ndani ya kipindi chake, taifa la Waislamu lilikabiliana na vitisho vingi; vikiwemo vya ndani na nje – vitisho vilivyo vibaya zaidi ni:

 

·

·    Uvamizi wa jeshi la msalaba kutoka magharibi.

 

·   Uhaini wa Fwaatimiyah (Mashia) katika kusuhubiana na jeshi la msalaba dhidi ya taifa la Kiislamu.

 

·    Unyanyasaji wa Tartar kutoka mashariki, na mauaji yao na ufisadi usio na hisia yoyote.

 

·    Ufisadi wa wafalme na watawala, na kujiweka mbali kwao na Uislamu.

 

·    Ueneaji wa upofu katika kufuata Madh-hab uliosababisha ugawaji wa matabaka makubwa.

 

·   Ueneaji wa imani za kishirikina miongoni mwa Waislamu uliotokana na jitihada za wazushi na wanaojinufaisha nafsi zao kutoka miongoni mwa Mashia (Raafidhwah), Masufi na Mabaatwini.

 

Ilikuwa ndani ya kipindi hichi cha mashaka mengi ambapo Allaah alimpeleka Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu) kusuguana na changamoto hizi na kwa ajili ya kuihami Diyn safi dhidi ya mawimbi makubwa ya makosa yasiyoeleweka, ukafiri, uzushi na mafundisho yasiyopatikana ndani ya Diyn.

 

Jumuiya nyingi zinazotaka mabadiliko na wale wenye fikra njema waliathiriwa na Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah, na walimshukuru na kwa wazi wazi walieleza hisia zao za shukrani kwa kazi zake. Wengi wao kwa namna moja ama nyengine wamechangia elimu zao au misimamo ya mienendo yao kwa hoja za mabadiliko zilizotolewa na Ibn Taymiyyah. Hata hivyo, hawawezi kuwa sahihi kudai kwamba walikuwa sawa sawa na Shaykh al-Islaam kwa sababu hata kwamba, mienendo hii ama wafikiriaji hawa wataona sababu ya msingi pamoja na Shaykh al-Islaam ndani ya baadhi ya mwenendo wa maisha na tabia zake, wataenda nae kinyume katika njia zake za msingi.

 

Lengo la Da’wah na jitihada za Ibn Taymiyyah lilielekezwa kwa kuanzisha Tawhiyd na kukana 'ibaadah yoyote isiyokuwa ya Allaah. Ingawa aliandika kwa mapana kwenye mada kubwa mbali mbali, zote hizi zilikuwa ni ndogo tu katika kuanzisha 'ibaadah ya Allaah. Hivyo, jumuiya za kisiasa za leo ambazo zinafanya kwamba uanzishwaji wa dhana ya ‘Taifa la Kiislamu’ kama kwamba ndio fanikio lao kuu, hali ya kuwa wanaamini kwamba wito wa kuanzisha 'ibaadah safi kwa ajili ya Allaah kuwa ni kikwazo, hawawezi abadan kuwa na usulubu wa mwenendo wa Ibn Taymiyyah.

 

Ibn Taymiyyah kwa hakika aliwaita watu kwa uwazi katika kupitia nafasi za Madhaahib mbali mbali na usahihi wa kutegemea Ijtihaad inapohitajiwa. Hili lilikuwa na lengo kwamba ufuataji upofu wa Madhahebu hautakuwa ndio kikwazo cha kurejea nyuma katika hali ya awali na ufuataji ambao utakuwa karibu na ushahidi. Da’wah yake ilipigana kurejea nyuma katika elimu ya Salaf, Waislamu waongofu siku ambazo Uislamu ulikuwa huru na ushirikina na uzushi.

 

Iwapo mfikiriaji mpya wa enzi za leo ataona sababu kuu za Ibn Taymiyyah kukana maamuzi ya upofu dhidi ya Madhehebu mbali mbali, lakini tu akaamua kulirudisha hili kwa kitu kiovu zaidi kama vile tafsiri zake binafsi au dhana za kisasa au mfano wa hizo; basi hatoweza kudai usulubu katika mwenendo wa Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah ambaye wito wake mkuu ulikuwa ni kuwarudisha watu nyuma kuelewa (misimamo ya) Salaf.

 

Vivyo hivyo, Shaykh al-Islaam alifuata njia ya Salaf katika kuwalingania viongozi Waislamu hata kama ni watendaji dhambi. Pale Wa-Tartar walipovamia Shaam,[4] Ibn Taymiyyah aliwaita watawala wa enzi zake na Waislamu kwa ujumla kusimama dhidi ya tukio hilo na kupigana nao. Ingawa hata hivyo Wa-Tartar ki-nje nje walitamka shahada, Ibn Taymiyyah aliwatambua kama ni watu wasioamini kwa sababu ya ufuataji wao wa moja kwa moja kwenye sheria za Genghis Khan Al-Yasiq, na pia kutoipa thamani kwa vyote – Shari’ah na heshima ya maisha ya Kiislamu.

 

Iwapo mtu hivi leo ataunganisha miambaano (mapengo) baina ya Wa-Tartar na baadhi ya watawala Waislamu wa wakati wa leo bila ya kutilia maanani sababu kuu, masharti na kutenda matendo ambayo yanasababisha ufisadi ndani ya ardhi na kumwagika damu; basi mtu huyo anatenda kinyume na mafundisho ya Shaykh Al-Islaam wala hawezi kujifakharisha mwenendo wake katika njia ya Ibn Taymiyyah.

 

Shaykh al-Islaam aliisimamisha bendera ya imani na elimu ya Ahlus-Sunnah ndani ya maisha yake, kipindi ambacho ndani yake kilikuwa kimejaa uzushi, upotofu, ufisadi uliotapakaa na bado alikuwa na hamasa. Jitihada zake mbele ya uso wa mashaka, msimamo wake mbele ya ukweli, subra zake chini ya mitihani na matumaini yake kwa mwisho mwema; kuna mafunzo mengi ndani yake kwa mwanafunzi wa maarifa ya uswuwl (jurisprudence) na mlinganiaji katika njia ya Allaah.

 


[1] Kipande cha sehemu refu ya Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Daawuwd (3641 & 3642), at-Tirmidhiy (2682), Ibn Maajah (223), na Ibn Hibbaan (88), na al-Albaaniy akaithibitisha kwamba ni sahihi ndani ya kitabu chake cha Sahihy at-Targhiyb wa-Tarhiyb (70).

[2] Imesimuliwa na al-Bayhaqiy na kusahihishwa na Shaykh al-Albaaniy ndani ya Mishkaati, namba 248.

[3] Abu Daawuwd (3/4278), al-Haakim, at-Twabaraaniy ndani ya al-Awsatw. Imesahihishwa na al-Albaaniy ndani ya as-Swahiyhah (2/150)] 

[4] Jina la kale linalowakilisha maeneo ya Syria, Jordan, Palestina na Lebanon.

 

Share