03-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Baada Ya Kufariki Dunia

 

Baada Ya Kufariki Dunia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki dunia: macho yalibubujika machozi, mioyo ilihuzunika, ulimwengu uliingia kiza, na waumini wakijilaumu wenyewe kwa mabadiliko yatakayotokea baadaye. Mwalimu aliyekuwa kipenzi cha waumini wote na aliyekuwa rehema kwao, alifariki dunia. Mtu anapompoteza aliyekuwa kipenzi na anayeheshimiwa sana, moyo wake unajaa kumbukumbu; alikuwa akikaa pale; alikuwa akisimama pale; alikuwa akisema na kufanya kadha, na kadha.

 

Watu wanapompoteza wampendaye, kwa kawaida hutafakari na kukumbukia maneno na misemo aliyoitamka. Na kama aliyekufa alichukuliwa kama kiigizo, wanakumbuka nasaha zake, hususa nasaha za mwisho, wakikazana kwa moyo wao wote kuzitekeleza. Wanarejea maneno yake na kuyapa uhai mpya kwa utendaji.

 

Kama mioyo yenu ilijeruhiwa na kifo cha Mtume wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi jibidiisheni kutekeleza nasaha zake za mwisho. Irbaad bin Saariyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia;

 

“Mjumbe wa Alah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa khutbah yenye umbuji na hekima, khutbah ambayo ilisababisha macho kububujika machozi na mioyo kutetema. Tulisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah! Inakuwa kama kkhutbah ya kuaga! Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Muogopeni Allaah, na lazima msikilize na muwatii (walio katika mamlaka), hata kama mtumwa wa Kihabeshi atafanywa kiongozi wenu. Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migogoro; hivyo kilichopo juu yenu ni Sunnah zangu na Sunnah za Khalifah walioongozwa baada yangu; zuiweni (yaani Sunnah zangu….) kwa magego yenu.[1] Na jihadharini na muwe mbali na mambo yaliyo zaliwa, kwani kila uzushi ni upotevu”.[2]

 

Tulisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah! Hii ni kama khutbah ya kuaga! (ya mwisho)  sasa unatuagiza nini?

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Nimewaachieni ushahidi uliowazi, ambao usiku wake ni sawa na mchana wake. Hapana aendaye kombo baada yangu isipokuwa yule aliyekhasirika.

 

Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migongano mingi; na juu yenu ni yale myajuayo kutokana na Sunnah yangu na Sunnah ya Khalifah waongofu: Iumeni (yaani Sunnah yangu….) kwa magego yenu. Mnawajibika kumtii mtumwa wa Kihabeshi. Kwa hakika, muumini ni sawa na ngamia Anif (ngamia aliyewekewa mbao katika pua yake, kutokana na kuhisi maumivu, anamtii mpandaji) popote anapoelekezwa, anakwenda.”[3]

 



[1] Maana yake: Shikamana na Sunnah yangu na ning’inia kwayo, kama vile mtu anayening’inia katika kitu kwa meno yake hufanya kwa magego, alichelea kitu kile kitamponyoka.

[2] Ilisimuliwa na Abu Daawuud ndani ya Swahiyh Abu Daawuud (3851), na At-Tirmidhiy ndani ya Swahiyh Sunnan At-Tirmidhiy (2157); na Ibn Maajah ndani ya Swahiyh Sunnah Bin-Majah (40) vile vile wengine. Rejea Swahiyh At-Targhiyb Wat-Tarhiyb (Uk.24) na Kitaab As-Sunnah (54) cha Bin Abu Asim, kilichopitiwa upya na Shaykh Al-Albaaniy-Allaah Amrehemu.  Katika masimulizi ya An-Nasaaiy na Al-Bayhaqiy katika Al-Asma Was-Swifaat kuna yafuatayo: ‘Na kila upotevu ni Motoni.” Na nyongeza hiyo imo katika Silsilah Swahiyhah, kama katika Al-Ajwibah An-Nafi’ah (Uk.545) na Iswlahul-Masaajid (Uk. 11.)

[3] Swahiyh Sunan Bin Maajah (41).

 

 

Share