05-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): "Nawaamuru Kumcha Allaah"

 

“Nawaamuru  Kumcha Allaah”

 

Tiini amri za Allaah na mjiepushe na makatazo yake. Jueni ya kuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajua yote myatendayo, yote ya dhahiri na mliyofanya kwa siri.

Msiruhusu utashi uwaongoze, kwani ni sababu ya uovu na kuingizwa katika moto wa Jahanamu. Jitakaseni. Jiepusheni na Moto wa Jahanamu kwa kufanya amali njema.

 

Kama dunia ina kushawishi na uzuri na vivutio vilivyo haramishwa, na dhahabu yake inayomeremeta, au na starehe zinazopotosha, kumbuka maneno ya Mtume, “Nawaamuru mumche Allaah.” Iwapo unataka kuokolewa na mitihani na misiba, na kama unataka uruzukiwe na riziki ya halali, mche Allaah.

 

“….Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea.   

Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia. ….” (65: 2-3).

 

Kama unataka kuokolewa kutokana na shida na kama unataka mambo yako yawe sahali, mche Allaah:

“… Na anayemcha Allaah, Allaah Humfanyia mambo yake kuwa mepesi.” (65: 4).

 

Kama unataka kujifunza njia ya ufanisi na uchaji, mche Allaah.

“… Na mcheni Allaah. Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu. (2: 282).

 

Enyi Waislamu, kama mnatamani kutawala na kuongoza, na kama mnataka kuwa vinara katika nyanja zote na utawala, “mcheni Allaah”.

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao Aliyowapendelea, na Atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu. (24: 55).

 

Kama unatamani kuwa mtu anayeheshimiwa sana na watu, basi mche Allaah:

“…Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi...” (49: 13).

 

Sio ya kuchosha na ufukara na makosa ya jinai yanayotishia mfumo wa jamii kutokana na matokeo ya kiwango cha chini cha Taqwa (uchaji, wema, na kumcha Allaah)?

 

Kumcha Allaah kuna kuhitajia kuuridhia ukweli, hata kama utatoka kwa mtu aliye chini yako kiukoo, jinsia, hadhi au umri.

“Nikuamuru kumcha Allaah” ni maneno yaliyotimia ambayo ni mwafaka kwa kila zama na mahali; mwafaka kwa wanaume na wanawake, kwa matajiri na masikini, kwa weupe na weusi; mwafaka kwa wote, mchungaji na wachungwao.

 

Kwa maneno haya – “Nakuamuru kumcha Allaah” –mtu binafsi, jamii na taifa lote linaweza kufikia ufanifu, lakini wanapotenda kwa mujibu wa kidokezi.

 

“Mche Allaah, na lazima uwasikilize na kuwatii (walio madarakani)  hata kama ni mtumwa kwa Kihebeshi anafanywa kiongozi wako.” Haya ni sawa na kauli,

 

“Sikiliza  na utii, hata kama ni mtumwa wa Kihabeshi, kichwa chake ni kama zabibu kavu, anakuwa mtawala wako.”[1].

 

Katika Hadiyth nyingine,

 

“Yeyote atakayeona kiongozi wake anafanya jambo asilolipenda, basi awe na subira kwani yeyote anayeacha jama’ah kwa pima au shubiri kisha akafa, anakufa kifo cha jahiliya.”[2].

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alisema,

 

“Kusikiliza na kutii ni wajibu kwa Muislamu, kwa avipendavyo na avichukiavyo, madhali hakuamrishwa kufanya dhambi. Iwapo ataamrishwa kutenda dhambi, basi asisikilize wala kutii.”[3].

 

Taifa au rangi au sura ya nje, isikuzuie kuukubali ukweli, kwenda kinyume na msingi huu unakupeleka kwenye majaribio/mtihani mgumu na makinzano.

 

“Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migogoro mikubwa” Hapa ndipo tulipo, tunaishi katika zama za mikinzano na kutokubaliana – kutokubaliana katika imani, Fiqh, siasa, lakini inasikitisha sana katika mioyo yetu. Lilikuwa kundi moja na jamii moja, sasa tuna makundi chungu nzima, na kila moja linalingania misingi yake yenyewe.

 

Vipi wingi wa vitabu kwenye safu za maktaba, bado kuna tofauti nyingi za rai katika vitabu hivyo: Waislamu hawajui lipi la kulikubali na lipi na kulikataa! Na litalovunja moyo zaidi ni kuwa tofauti na migongano inapelekea kuangamiza taifa:

 

“...wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu…” (8: 46).

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

“Msitofautiane, kwani waliokuja kabla yenu walitofuatiana wao kwa wao, na kisha waliangamizwa.” [4]

 

Mataifa tofauti ya dunia hayajaungana dhidi yetu kwa sababu eti idadi yetu ni ndogo, kwani idadi yetu sio ndogo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

“Mataifa karibu yatajiunga juu yenu (walialikana ili kuwaua na kuwapora ardhi yenu) kama watu wanaoitana kwa ajili ya chakula kwenye Qis’ah yao (sinia la watu kumi).” Mtu mmoja alisema, “Wakati huo tutakuwa wachache?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu, “Bali, mtakuwa wengi wakati huo, lakini mtakuwa kama povu la mafuriko (yaani – mapovu na uchafu wote yatakoyachukua. Na Allaah Ataondoa katika vifua vya maadui zenu chuki waliyonayo dhidi yenu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ataingiza katika mioyo yenu Wahn (udhaifu). “Muulizaji aliuliza, “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni nini Wahn? “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Kupenda dunia na kuchukia kifo.”[5]

 

‘….Tutaona mapambano zaidi.” Kwa nini migongano mingi?  Kwa sababu watu watategemea mifumo na shari’ah zilizotungwa na binaadamu, na huku wakitelekeza yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola (Subhaanahu wa Ta’ala). Watayapa kipaumbele yaliyosemwa na Zayd na ’Amr juu ya ya yale yaliyosemwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“…Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Allaah bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi.” (4: 82).

 

Sababu migongano tuliyo wadhukuru hapo juu ni kuacha mafunzo ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume. Chochote kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni sababu ya umoja na utulivu, lakini kinachokuja kutoka kwa asiye kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni sababu/chanzo cha mfarakano na ugomvi.

 

 

 



[1] Al-Bukhaariy (7142).

[2] Al-Bukhaariy (7143).

[3] Ilisimuliwa na Al-Bukhaariy (7144); mtu anaweza kutumia mapokezi ya Hadiyth hizi na kutolea hoja  kuwa mtu anaweza kuwa kwenye kundi moja, lakini si Swahiyh kwani huongeza tofauti kati ya Waislamu. Tunaomba mwongozo wa Allaah.

[4] Al-Bukhaariy (24:10)

[5] Ilisimuliwa na Abu Daawuud na wengine, imo katika al-Swahiyhah (958).

Share