Zingatio: Dunia Haina Mkaazi
Zingatio: Dunia Haina Mkaazi
Naaswir Haamid
Kwa Nabiy Nuuh (‘Alayhis-salaam) aliyeishi duniani kwa miaka alfu kasoro hamsini, naye ilifika siku yake akaiaga dunia. Kwa kipenzi chake Rabb wetu na kipenzi cha Ummah wa Kiislamu, Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye ilifika siku yake akaiaga dunia. Sasa tupige hisabu tuangalie huo muda walioishi duniani na ule wanao endelea kuishi nao ndani ya makaburi, vipimo vya mwenye akili vyaonesha kwamba maisha ya kaburini ni marefu kuliko hapa duniani.
Kwa wale wenye kumiliki ardhi zilizo na rutba ya kila aina na kwa wenye majumba ya ghorofa hamsini, miliki hii waliyonayo waelewe kwamba sio chochote wala lolote iwapo wataacha kumuabudia Rabb wao wa Mbingu na Ardhi kama Anavyotuambia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndani ya Qur-aan:
فَأَمَّا مَن طَغَىٰ ﴿٣٧﴾ وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٣٨﴾ فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٣٩﴾
Basi yule aliyepindukia mipaka kuasi. Na akahiari uhai wa dunia. Basi hakika moto uwakao vikali mno ndio makaazi yake. [An-Naazi’at: 37-39]
Vumbua na tumia starehe kwa kadiri utakavyoweza, lakini cha muhimu ni kuelewa kwamba kuna kikomo chake. Kama wewe ni mpenzi wa chakula, ukawa unakula kwa kufakamia bila ya kiwango, basi inafika wakati unakuwa ushavimbiwa na huwezi tena kula; na ole wako uendelee kula, utaangukia moja kati ya mawili: hospitalini ama kaburini hapo hapo.
Ni hayo hayo yanayoweza kumkuta kwa mwenye kunywa pombe ama mzinifu; ni kwa kiwango gani kikubwa utatumia hadi nafsi yako iweze kukinaika? Hutafikia mwisho, na badala yake utalewa na utazini hadi utafikia kiwango huwezi tena kulewa na kuzini, na mwisho wake iwapo utalazimisha kuyaendea maovu hayo, utamalizia moja kati ya mawili: hospitalini ama kaburini.
Kundi hili ndilo lile alilolielezea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Watu watazuka kutoka katika Ummah wangu ambao watakuwa wamejaa matamanio kama ugonjwa wa kuambukizwa na mnyama unavyozagaa mwili mzima na kuathiri mishipa na viungo vyote.” [Imepokewa na Abu Daawuud]
Ndivyo ilivyo kwa afya na uzima wako, wewe tembea juu na chini, nenda Mashariki na Magharibi, tafuta daktari bingwa wa kila aina akutibu, lakini uelewe tu kwamba ipo siku, tena siku hiyo ni ya uhakika, siku ambayo nawe utaondoka duniani, kwani dunia haina mkaazi. Makaazi yetu ni ama Jannah - Rabb Atujaalie tuwemo humo, au ni Moto - Rabb Atuepushe nao; Aamiyn.
Basi kwa hapa, tunazinasihi nyoyo zetu na nyoyo za ndugu zetu kwamba; dunia hii tunayoishi nayo, sote hapa ni wageni, tena tumealikwa na Rabb wetu kuja kuchuma mema ili kuwa na maisha ya milele ambayo yananasibiana na maumbile ya mwaadamu: starehe na uzima wa kudumu. Tumche Rabb wetu kwa haki Anayopaswa kuabudiwa kwani tutayakuta mafanikio yake mbele ya Hukumu:
وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٤٠﴾ فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٤١﴾
Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa.Basi hakika Jannah ndio makaazi yake. [An-Naazi’at: 40-41]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Azithibitishe nyoyo zetu katika Diyn na Awaongoze wale Waislamu waliokwenda upande.