Dhul-Hijjah: Inafaa Kufunga (Swawm) Siku Zote 9 Za Dhul-Hijjah?

 

Inafaa Kufunga (Swawm) Siku Zote 9 Za Dhul-Hijjah?

 

www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum warhma tullahi wabarakatu......

Jee inapasa ama inafaa kufunga yale masiku kumi ya dhul hajj,. Na vile vile kuna zile saum za siku tatu kabla hajj.

Kwani kuna baadhi wanaosema ni sunna siku kumi ama tatu. Shukran wa jazakallah

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ni muhimu tujue ya kwamba zile siku 10 za awali za mwezi wa 12 (Dhul Hijjah) katika kalenda ya Kiislamu zina fadhila kubwa. Haifai zikawa siku hizi zitampita mtu bila kufaidika. Zikipita siku hizi bila faida yoyote basi mtu kama huyo atakuwa amekhasirika. Allaah ('Azza wa Jalla) Anatutajia fadhila za masiku hayo kwa kusema:

 

Naapa kwa Alfajiri. Na kwa masiku kumi” [89: 1-2].

 

Haya masiku kumi 'Ulamaa wengi wamesema ni siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah kwani hayo ni masiku bora katika mwaka. Hii imethibiti katika Hadiyth iliyopokewa na al-Bukhaariy: “Hakuna masiku ambayo amali njema zinapendwa na Allaah ndani yake kuliko masiku haya – yaani masiku kumi ya Dhul Hijjah”. Akaulizwa: “Hata Jihaad katika njia ya Allaah?” Akasema: “Hata Jihaad katika njia ya Allaah ila mtu aliyetoka mwenyewe na mali yake, kisha asirudi na chochote (akafariki shahidi)”.

 

Amali njema ni nyingi zikijumlisha hata Swawm.

 

Ingawa kuna Hadiyth iliyosimuliwa na mmoja wa wakeze ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga masiku tisa ya mwanzo ya Dhul Hijjah, siku ya ‘Ashuuraa, na masiku matatu ya kila mwezi” [Abuu Daawuud] Ila Hadiyth hii kwa mujibu wa Wanachuoni wa fani ya Hadiyth, wanasema ina utata.

 

Lakini kutokana na Hadiyth nyingine iliyo sahihi inaonyesha kuwa hakuna uwajibu wa kufunga masiku hayo, na wala si Sunnah iliyojulikana kuwa akiifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Anasema mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): “Sikumuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifunga masiku kumi (ya Dhul-Hijjah)” [Muslim]

 

Hivyo, unapoingia mwezi wa Dhul Hijjah mtu anaweza kufunga kuanzia tarehe moja hadi tarehe 9 (ambayo ni siku ya Arafah). Tarehe kumi haifai kufungwa na Muislamu kwani ni siku ya ‘Iyd na Waislamu wanafaa kusherehekea kwa kula. Katika mwezi huu zile siku tatu za Swawm zinakuwa hazipatikani kwani hizo huwa ni tarehe 13, 14 na 15 ambazo zinajulikana kama masiku meupe. Sasa siku ya 13 inakuwa ni Tashriyq ambayo ni siku ya mwisho ya kuchinja kwa mwenye uwezo.

 

Na kufunga siku hizo 9 unaweza kufunga kwa kadiri ya uwezo wako, ukipenda unaweza kufunga siku zote hizo au moja tu au mbili au tatu n.k. Na wala hakuna kufunga siku tatu hasa za kabla ya Hajj.

 

 

Muhimu zaidi mtu asikose siku ya ‘Arafah kwa sababu ya fadhila zake nyingi na pia kwa kuthibiti kwake ushahidi kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Vilevile anatakiwa Muislam ajue kuwa ushahidi wenye nguvu ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hakufunga masiku hayo, hivyo pamoja na kuwa Maulamaa wamependekeza kutokana na kheri za masiku hayo na pia inasemekana kuwa baadhi ya wema waliopita walifunga, ila asije Muislam kuitakidi kuwa ni lazima kufunga masiku hayo na hata kuwalazimisha watu au kusumbuana na wengine kwa hilo.

 

Siku ya ‘Arafah ni ile siku ambayo Mahujaji wamesimama katika wangwa (bonde) la ‘Arafah, tarehe 9 katika kalenda inayofuatwa na Saudia kwani Hijjah inafanywa huko. Hili wameafikiana wanazuoni wote. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hajj ni ‘Arafah”. Hii inamaanisha ukikosa kuwepo katika sehemu hiyo basi huna Hijjah ya mwaka huo. Ama Swawm siku hiyo, Abuu Qataadah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, aliulizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Swawm siku ya ‘Arafah, akasema: “Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na unaokuja” [Muslim, Abuu Daawuwd na Ibn Maajah].

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida ziyada:

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share