Ushindi Katika Ramadhwaan

Ushindi Katika Ramadhwaan

Imekusanywa Na: Muhammad Al-Ma'awy

 Alhidaaya.com

 

 

Utangulizi

 

Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi uliojaa juhudi na fadhila tele na nyingi ambazo lau zitatiliwa maanani, Ummah huu utanyanyuka kutoka daraja moja hadi nyengine. Huu ni mwezi wa Qur-aan, kwa kuwa iliteremshwa kwayo. Hivyo ni juu yetu kuisoma kwa kuzingatia na kufanyia kazi amri zilizotolewa ndani yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah: 185].

 

Huu ni mwezi wa Usiku wa Qadari (wenye Nguvu – Laylatul Qadr), ambao usiku huo ni bora kuliko miezi elfu moja. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

 

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾

Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu. [Al-Qadr: 3].

 

Huu ndio mwezi wa Funga ya Faradhi, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183].

 

Huu pia ndio mwezi wa Sadaka, ‘Umrah, Du’aa, Subira na Jihadi. Hii haimanishi miezi mingine huwa hivi vitu havifai kufanywa. Laa hasha! Maana yake ni kuwa katika mwezi wa Ramadhwaan Muislam anatakiwa aongeze amali hizi. Tufahamu ya kuwa huu sio mwezi wa kulala kupindukia au kula sana bali ni mwezi ambao tunafaa tuongeze ‘Ibadah zetu kwa kiasi kikubwa zaidi.

 

Masharti Ya Ushindi 

 

Ushindi hauteremki kutoka katika ombwe wala hauji bila kutarajiwa. Ushindi na kushindwa zipo na kutawaliwa na kanuni na njia, ambazo zimenukuliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Qur-aan ili Waumini waweze kuzijua kwa yakini, elimu ya uhakika na kwa upeo mkubwa zaidi. Kanuni hizi hazibadiliki kwa kiasi kikubwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema yafuatayo kuhusu kanuni hizi:

 

قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكذِّبِينَ ﴿١٣٧﴾

Kwa hakika zimekwishapita kabla yenu nyendo (kama zenu), basi tembeeni katika ardhi kisha mtazame vipi ilikuwa khatima ya wenye kukadhibisha. [Aal-‘Imraan: 137].

 

Na pia Anesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾

Ni desturi ya Allaah kwa wale waliopita kabla. Na wala hutopata mabadiliko katika desturi ya Allaah. [Al-Ahzaab: 62].

 

Na Anasema tena Aliyetukuka:

 

سُنَّةَ اللَّـهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا﴿٢٣﴾

Desturi ya Allaah ambayo imekwishapita kabla, na wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Allaah. [Al-Fat-h: 23].

 

Shida kubwa ya Ummah huu ambao unakumbana nao leo ni kuwa wafuasi wake (Waislam) wameleweshwa na kasumba za Kimagharibi na za kigeni, zilizopotoka kutoka katika njia nyoofu na wamesahau ujumbe wao. Tumeshindwa kutofautisha baina ya adui na rafiki na hatujui mikakati na njama dhidi yake na yetu. Hivyo, kwa Umma wowote kuweza kushinda dhidi ya adui yake masharti fulani ni lazima yapatikane. Ikiwa kipote (kundi) kimoja au chochote kimeweza kutekeleza masharti hayo, ushindi utakuwa wao. Nyakati za ushindi na kushindwa zinabadilishana mikono kutegemea kanuni fulani. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ ۚ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنكُمْ شُهَدَاءَ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴿١٤٠﴾

Inapokuguseni majeraha basi yamekwisha wagusa watu majeraha kama hayo. Na hizo ni siku Tunazizungusha zamu (za mabadiliko ya hali) baina ya watu na ili Allaah Adhihirishe waloamini na Afanye miongoni mwenu mashahidi. Na Allaah Hapendi madhalimu. [Aal ‘Imraan: 140]

 

 

Masharti Yenyewe Yameelezwa Hapa Chini:

 

1.  - Imani Yenye Nguvu

 

Imani ni sharti kwetu sisi kuweza kuwashinda makafiri. Ikiwa Waislam ni wakweli na Waumini wa kihakika basi wataweza kuwashinda maadui zao kila wakati na lau hatutaweza kuwa juu yao itakuwa sisi ndio wenye shida kubwa sana. Waumini ndio walengwa wa kupata ushindi, na kuhusu suala hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamzungumzia Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ifuatavyo:

 

وَإِن يُرِيدُوا أَن يَخْدَعُوكَ فَإِنَّ حَسْبَكَ اللَّـهُ ۚ هُوَ الَّذِي أَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ﴿٦٢﴾ وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ ۚ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ ۚ .. ﴿٦٣﴾

Na wakitaka kukuhadaa, basi Allaah Anakutosheleza. Yeye Ndiye Ambaye Amekusaidia kwa nusra Yake, na kwa Waumini. Na Akaunganisha nyoyo zao. Lau ungelitoa vyote vilivyomo ardhini, basi usingeliweza kuunganisha nyoyo zao; lakini Allaah Amewaunganisha. [Al-Anfaal: 62-63].

 

Wakati mwengine Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawatumia Malaika ili wawasaidie Waumini kama Alivyosema:

 

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا ..﴿١٢﴾

Pindi Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia): Hakika Mimi Niko pamoja nanyi; basi wathibitisheni wale walioamini. Nitavurumisha kizaazaa katika nyoyo za waliokufuru. [Al-Anfaal: 12].

 

 

Yeye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema tena:

 

ثُمَّ أَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَنزَلَ جُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا وَعَذَّبَ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْكَافِرِينَ﴿٢٦﴾

Kisha Allaah Akateremsha utulivu Wake kwa Rasuli Wake na kwa Waumini, na Akateremsha majeshi (ya Malaika) msiyoyaona; na Akawaadhibu wale waliokufuru. Na hivyo ndio jazaa ya makafiri. [At-Tawbah: 26].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatumia njia nyengine yoyote Anayopenda kuwasaidia Waumini katika vita dhidi ya mushirikina kama kwa mfano Alipotumia kimbunga kuwasambaratisha katika Vita vya Handaki,

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَاءَتْكُمْ جُنُودٌ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا وَجُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا ۚ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا ﴿٩﴾

Enyi walioamini! Kumbukeni neema ya Allaah juu yenu, pale yalipokujieni majeshi Tukawapelekea upepo wa dhoruba na majeshi msiyoyaona (ya Malaika). Na Allaah daima ni Mwenye kuona myatendayo.   [Al-Ahzaab: 9].

 

Au kutuma mvua kama rehema kwa Waislam katika Vita vya Badr,

 

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ﴿١١﴾

Pindi Alipokufunikeni kwa usingizi kuwa ni amani kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, ili Akutwaharisheni kwayo, na Akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan, na ili Atie nguvu nyoyo zenu, na Athibitishe kwayo miguu. [Al-Anfaal: 11]

 

Au Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) wakati mwengine Anatumia jeshi la adui lenyewe kuuana wenyewe kwa wenyewe kama ilivyotokea kwa kabila la Kiyahudi la Nadhiir lililokuwa likiishi katika mji wa Madinah,

 

هُوَ الَّذِي أَخْرَجَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مِن دِيَارِهِمْ لِأَوَّلِ الْحَشْرِ ۚ مَا ظَنَنتُمْ أَن يَخْرُجُوا ۖ وَظَنُّوا أَنَّهُم مَّانِعَتُهُمْ حُصُونُهُم مِّنَ اللَّـهِ فَأَتَاهُمُ اللَّـهُ مِنْ حَيْثُ لَمْ يَحْتَسِبُوا ۖ وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ ۚ يُخْرِبُونَ بُيُوتَهُم بِأَيْدِيهِمْ وَأَيْدِي الْمُؤْمِنِينَ فَاعْتَبِرُوا يَا أُولِي الْأَبْصَارِ﴿٢﴾

Yeye Ndiye Aliyewatoa wale waliokufuru miongoni mwa Ahlil-Kitaabi kutoka majumbani mwao katika mkusanyiko wa kwanza. Hamkudhania kwamba watatoka, nao wakadhani kwamba husuni zao zitawakinga dhidi ya Allaah. Lakini hukmu ya Allaah ikawafikia kutoka ambako wasipotazamia, na Akavurumisha kiwewe katika nyoyo zao. Wanaziharibu nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini, basi pateni funzo enyi wenye uoni wa kutia akilini. [Al-Hashr: 2]

 

Sharti kubwa ya kushinda maadui ni kuwepo kwa pote (kundi) la “Waumini”. Na lau Waumini watasimama imara basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atawafanya wao waweze kuitawala ardhi hii, ikitokea kinyume na hilo basi watakuwa ni wenye kutawaliwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba bila shaka Atawafanya makhalifa katika ardhi kama Alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao, na bila shaka Atawamakinishia Dini yao Aliyowaridhia, na bila shaka Atawabadilishia amani badala ya khofu yao; wawe wananiabudu Mimi wasinishirikishe na chochote; na yeyote yule atakayekufuru baada ya hapo, basi hao ndio mafasiki. [An-Nuwr: 55].

 

Waumini wanatakiwa kuwa na ufahamu na utambuzi na mas-ala kadhaa ya Uislaam. kwa huu ufahamu ina maana kuwa hata fikra zetu ziwe kwa ukamilifu wake zinakwenda sambamba na mambo yanayohusiana na maisha katika dunia hii. Katika haya Muumini anafaa afahamu mas-ala yafuatayo ambayo ni muhimu sana:

 

·    Tawhidi iliyo safi na ya asili isiyokuwa na mawaa (madoa) aina yoyote wala kuchanganyika na ushirikina aina yoyote ile kama Shriki Kubwa, Ndogo au Khafiy (isiyoonekana/iliyofichikamana). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ﴿١٩﴾

Basi jua kwamba: laa ilaaha illa-Allaah (hapana muabudiwa wa haki ila Allaah) na omba maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike. [Muhammad: 19].

 

·     Kujua misingi na mambo muhimu ya Uislaam na kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah za kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anasema:

  

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa: 59].

 

·      Uoni (kuona mbali) na uangalifu katika kazi na shughuli za Da‘wah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٨﴾

Sema: Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya nuru za elimu na umaizi, mimi na anayenifuata. Na Utakasifu ni wa Allaah, nami si miongoni mwa washirikina. [Yuwsuf: 108]

 

·     Kuwa na maadili madhubuti yenye kuigwa na wengine kwa sababu wewe umefuata kielelezo na ruwaza njema katika shakhsiya ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tukiiga Akhlaaq za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi hatutapotea bali tutakuwa na ufanisi wa hapa duniani na pia Kesho akhera. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia:

 

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

 Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi. [Al-Ahzaab: 21]

 

Na pia, 

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ﴿٤﴾

Na hakika wewe uko juu ya kiwango adhimu cha tabia njema. [Al-Qalam: 4]

 

Na pia kumfuata yeye ni kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama alivyosema Aliyetukuka:

  

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Aal-‘Imraan: 31].

 

Na Nabiy (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

 “Hakika mimi sikutumwa ila kukamilisha maadili mema” [Maalik, al-Bayhaqiy].

 

 

·     Kutafuta elimu yote yenye manufaa kwa Ummah huu wa Kiislamu na kushindaa katika hilo. Sababu ni kuwa kushindana katika wema ni thawabu kubwa elimu ikiwa ni mmoja wapo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

 وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ ۗ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴿٢٨﴾

Na miongoni mwa watu na viumbe wanaotembea na wanyama wa mifugo, wenye kutofautiana rangi zake kadhalika. Hakika wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni ‘Ulamaa. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Faatwir: 28]

 

·      Kuweza kufuatilia habari za yanayojiri kila leo pamoja na kujua habari za Waislam katika nchi nyengine.

 

 

2. - Ukimsaidia Allaah, Atakusaidia 

 

Hakika ni kuwa ushindi unakuja kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Yeyote anayesaidiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hakuna hata mmoja wa kumshinda na kumpiku, japokuwa huenda wakawa wao ni wengi na wenye silaha kali na kubwa za kisasa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

 إِن يَنصُرْكُمُ اللَّـهُ فَلَا غَالِبَ لَكُمْ ۖ وَإِن يَخْذُلْكُمْ فَمَن ذَا الَّذِي يَنصُرُكُم مِّن بَعْدِهِ ۗ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١٦٠﴾ 

Akikunusuruni Allaah, basi hakuna wa kukushindeni. Na Akikutelekezeni, basi nani atakunusuruni baada Yake? Na kwa Allaah Pekee watawakali Waumini. [Aal ‘Imraan: 160].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawasaidia Waumini japokuwa watakuwa kidogo kama vile jeshi la Twaalut, kama Anavyosema Aliyetukuka: 

 

فَلَمَّا فَصَلَ طَالُوتُ بِالْجُنُودِ قَالَ إِنَّ اللَّـهَ مُبْتَلِيكُم بِنَهَرٍ فَمَن شَرِبَ مِنْهُ فَلَيْسَ مِنِّي وَمَن لَّمْ يَطْعَمْهُ فَإِنَّهُ مِنِّي إِلَّا مَنِ اغْتَرَفَ غُرْفَةً بِيَدِهِ ۚ فَشَرِبُوا مِنْهُ إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ ۚ فَلَمَّا جَاوَزَهُ هُوَ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ قَالُوا لَا طَاقَةَ لَنَا الْيَوْمَ بِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ ۚ قَالَ الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلَاقُو اللَّـهِ كَم مِّن فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿٢٤٩﴾وَلَمَّا بَرَزُوا لِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ قَالُوا رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ﴿٢٥٠﴾ فَهَزَمُوهُم بِإِذْنِ اللَّـهِ وَقَتَلَ دَاوُودُ جَالُوتَ وَآتَاهُ اللَّـهُ الْمُلْكَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَهُ مِمَّا يَشَاءُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّفَسَدَتِ الْأَرْضُ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿٢٥١﴾

Alipoondoka Twaaluwt na jeshi akasema: Hakika Allaah Atakujaribuni kwa mto; atakayekunywa humo, hatokuwa pamoja nami; na ambaye hakuonja hakika huyu yu pamoja nami, isipokuwa atakayeteka teko mmoja kwa mkono wake. Basi wakanywa kutoka humo isipokuwa wachache miongoni mwao. Alipouvuka yeye na wale walioamini pamoja naye; wakasema: Leo hatuna nguvu kabisa dhidi ya Jaaluwt na jeshi lake. Wakasema wale walio na yakini kwamba wao ni wenye kukutana na Allaah: Makundi mangapi machache yameshinda makundi mengi kwa idhini ya Allaah? Na Allaah Yu pamoja na wenye kusubiri. Na walipojitokeza kupambana na Jaaluwt na jeshi lake wakasema: Rabb wetu Tumiminie subira na ithibitishe miguu yetu na Tunusuru dhidi ya watu makafiri. Wakawashinda kwa idhini ya Allaah na Daawuwd akamuua Jaaluwt; na Allaah Akampa ufalme na hikmah, na Akamfunza katika Aliyoyataka. Na lau Allaah Asingelizuia watu baadhi yao kwa wengine, basi ingelifisidika ardhi lakini Allaah ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu. [Al-Baqarah: 249-251].

 

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alimpatia ushindi Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake walipokuwa wachache kama katika Vita vya Badr, Khandaq, Taabuk, Mu’ta na vita vyenginezo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) wakati mwengine humsaidia mtu au watu japokuwa hana (hawana) silaha wala jeshi. Mfano wa hili ni usaidizi aliopata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr (Radhwiya Allahu ‘Anhu) walipokuwa pangoni wakati wa kuhama kwao kutoka Makkah kuelekea Madinah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا … ﴿٤٠﴾

Msipomnusuru (Rasuli), basi Allaah Amekwishamnusuru, pale walipomtoa (Makkah) wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili; walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi. Basi Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona... [At-Tawbah: 40].

 

Hivyo ni kuwa yeyote mwenye kumsaidia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametoa ahadi ya kumsaidia kwa msingi wa sharti hili. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ﴿٧﴾

Enyi mloamini! Mkisaidia kunusuru Dini ya Allaah, (Allaah) Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu.[Muhammad: 7]

 

 

3.  - Kushikamana Vilivyo Na Uislaam

 

Kushikamana kikweli na kwa ikhlasi na Uislaam ni sharti katika kufaulu na kupata ushindi. Lau watu watapotoka kutoka kwa mafundisho ya Qur-aan na Sunnah basi wakati huo tutakumbwa na matatizo na shida aina zote mpaka tutakaporudi katika mafundisho ya Dini yetu, sahihi na safi.

 

Utii kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni muhimu sana. Hebu tutazame mfano wa Vita vya Uhud (3H/ 625 Miladi) wakati ambapo Swahaba 50 (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliowekwa katika kijinjia kwenye mlima na maagizo makali wasiwe ni wenye kuondoka sehemu hiyo waliyowekwa kwa hali yoyote ile. Lakini pindi walipoondoka ule ushindi waliokuwa nao ukageuka na kuwa ni majuto na hasara. Takriban Swahaba 70 (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa ni wenye kupata shahada wakiwemo Hamzah ibn ‘Abdul-Mutallib, Musw‘ab ibn ‘Umayr, Julaybib, Anas ibn an-Nadhr (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na wengineo. Ikiwa kuacha agizo moja maafa yake ni hayo jee kuacha maagizo chungu mzima, itakuwaje?

 

Sayyidna ‘Umar ibn al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Sisi ni watu tuliopatiwa utukufu na nguvu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa Uislaam, pindi tu tukapokengeuka (na kupotoka) na Uislaam basi hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atatudhoofisha na kututweza”.

 

 

4. - Uongozi Wenye Ikhlasi

 

Wakati ambapo tulikuwa na uongozi wenye ikhlasi na uchaji wa Allaah, Waislam waliendelea kuwashinda maadui zao kwa usahali sana. Mfano ni katika kipindi cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), makhalifa waongofu (Radhwiya Allaahu ‘anhum), watawala wa awali baada yao (watawala wa Banu Umayyah na Banu ‘Abbaas). Pia wale watawala wema waliokuja muda mrefu baada yao waliweza kurudisha nguvu na utukufu wa Uislaam kama wakati wa Swalaah ud Diyn Hasan al-Ayyubiy, Nuur ud Diyn Zinkiy, Nuur ud Diyn Mahmuud, Qitz Mudhaffar Mahmuud na kadhalika. Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa awe ni mfano mzuri na ruwaza njema kwa wafuasi ili nao wapate kielelezo hai cha aliyejipamba kwa sifa kemkemu za Kiislamu. Miongoni mwa sifa ambazo kiongozi anafaa kuwa nazo ni Taqwa, uadilifu, elimu, utiifu kwa Qur-aan na Sunnah, maadili mema (ukweli, uaminifu, kutekeleza ahadi, upole na ulaini, na kadhalika), Istiqaamah, awe ni mwenye kuwataka washauri wenziwe, ujasiri na kutoogopa, na kadhalika.

 

 

Vita Wakati Wa Ramadhwaan 

 

Katika mwezi mtukufu wa Ramadhwaan, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwasaidia Waislam sana, ambao nao walikuwa msitari wa mbele katika kumridhisha Mola wao Mlezi. Walipata ushindi mmoja baada ya mwengine na hivyo kuweza kuutawala ulimwengu bila ya shida aia yoyote. Lakini pindi tu Ummah ulipo asi na kurudi nyuma kutoka kwa uimara wao katika malengo, kupotoka katika njia ya sawa ilinyooka, wakapuuza na kusahau ‘Ibadah, udhaifu mkubwa uliingia kati yao. Hivyo kwa wakati huu wanaonekana ni kama watumishi waliotiwa minyonyoro na Ummah mwengine. Katika udhaifu huu, Ummah umepata waumini washupavu waliosimama imara katika kuutetea Uislamu na hivyo kwa sasa kuweza kunyanyua kichwa tena.

 

Baadhi ya matukio ya kivita yaliyo muhimu ambayo yalitokea katika mwezi huu wa Ramadhwaan wakati ambao Waislam waliweza kupata ushindi ni:

  

a)    Vita vya Badr, vilivyopiganwa tarehe 17 Ramadhwaan 2 H (624 Miladi): Waislam walikuwa 313 dhidi ya makafiri 1000. Mbali na idadi ndogo na maandalizi duni, waliweza kuwashinda mahasimu wao. Hivi ndivyo vilivyokuwa vita vya kwanza, ambavyo viliwafungulia Waislam silsila ya ushindi.

 

b)   Maandalizi ya Vita vya Khandaq vilianza Ramadhwaan ya mwaka wa 5 H (627 M). Matayarisho yalikuwa ni kufukuliwa kwa handaki katika pande tatu za mji wa Madinah ili kuwa ni kizuizi kwa makafiri waliojiandaa na kushirikiana.

 

c)     Kufunguliwa kwa mji wa Makkah ambao ndio uliokuwa ushindi na ufanisi mkubwa wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dhidi ya mushirikina wa Makkah. Ushindi huu wa kuingia Makkah bila ya kumwagwa damu ulitokea 20 Ramadhaan 8 H (630 M).

 

d)    Safari ya kuelekea Taabuk kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jeshi lake ili kupambana na dola kuu ya wakati huo, Warumi wakati uliokuwa mzito wa joto kali na msimu wa mazao na masafa marefu. Kurudi kwa jeshi hilo ilisibu kuwa ni mwezi wa Ramadhwaan 9 H (631 M).

 

e)   Kufunguliwa na kutawaliwa kwa Maghrib al-Awswat (Morocco ya Kati) na Waislam ilitokea tarehe 2 Ramadhwaan 82 H (701M).

 

f)      Ufuo wa Pwani wa Andalus (Spain) ulitekwa na jemadari jeshi wa Kiislamu, Twaariq ibn Ziyaad mnamo 28 Ramadhwaan 92 H (711 M).

 

g)      Amuriah ilitekwa tarehe 6 Ramadhaan 222 H.

 

h)    Mujaahid Nuur ud Diyn Zinkiy aliwashinda Wakristo wa msalaba na kuurudisha mji Harem mnamo 9 Ramadhaan 559 H.

 

i)   Sultan wa Misri wakati huo wake, Qitz Mahmuud Mudhaffar akiongoza jeshi waliokuwemo wanazuoni, vijana, wazee na hata wanawake, mkewe akiwemo ndani yake walipambana na Matatari ambao walikuwa wanatisha na kuogopewa. Hawa watu walivamia na kuiteka miji mingi katika dola ya Kiislamu pamoja na kumuua Khalifah wa Banu ‘Abbaas, mwaka 1258 M. Baghdad ambao ulikuwa ni mji mkuu wa dola hiyo ulivunjwa kabisa. Kwa hofu waliokuwa nayo Waislam walikuwa na msemo: “Ukisikia Matatari wameshindwa basi usisadiki”. Lakini walitokea waliowashinda watu hao majabari. Sultan Qitz na mujahidina wake walipambana na Matatari katika Vita vya ‘Ayn Jaalut huko Palestina tarehe 25 Ramadhwaan 658 H (1260 M) miaka miwili pekee baada ya kuuliwa kwa Khalifa. Qitz alinyanyua hima na hamasa ya mujahidina wake. Chini ya uongozi wake, Waislam walishikanishwa juu ya Imani, umoja, zana za kivita za chuma ili kupambana na adui. Matokeo yake yalikuwa ni ushindi wa wazi kabisa katika wakati wa udhaifu na unyonge. Hata leo tunaweza kupata ushindi na aina hiyo ya uongozi. Kadhiya ya Afghanistan iko hai machoni petu walipoondoa tofauti zao na kupigania kwa sababu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwasaidia na kuweza kuishinda dola iliyokuwa kuu ya USSR (Urusi).

 

j)      Ndugu zetu huko Afghanistan walipigana na Warusi kwa Ramadhwaan mfululizo (1979 – 1988) bila kupumua.

 

k)   Ukinzani na mapigano dhidi ya maadui wa Uislaam bado yanaendelea kwa miongo kadhaa katika nchi kama Palestina, Kashmir, Phillipine, Bosnia, Chechniya na kadhalika.

 

l)     Vita vya Ramadhwaan 1973 baina ya majeshi ya Kiarabu na Waisraeli imeonyesha kuwa lau nchi za Mashariki ya Kati zitashikana mikono na kuungana kwa ikhlasi na kupigana dhidi ya adui kwa ajili ya Allaah basi adui atatoka mwenyewe katika eneno hilo.

 

Lakini wakati masharti ya kupata ushindi yalikosekana Waislam walishindwa katika mwezi huo mtukufu wa Ramadhwaan. Mojawapo ya kushindwa vibaya sana Waislam ilikuwa ni katika Vita vya Balata Shuhadaa, pale Waislam waliposhindwa na Wakristo katika eneo la milima huko Ufaransa mnamo tarehe 1 Ramadhwaan 114 H. Katika enzi zetu hizi mauaji ya Waislam ndani ya Msikiti wa Ibraahimiy huko Khaliil (Hebron), Palestina ni ya kuzingatiwa. Waislam walikuwa wakiswali Swalah yao ya Alfajiri mnamo tarehe 15 Ramadhwaan 1414 H (25 Februari 1994) pale Mzeyuni mwenye siyasa kali, Dkt. Bharuch Goldstein alipoingia ndani ya Msikiti huo huku nje jeshi la Israeli likimlinda na kufyatua risasi. Kwa dakika chache aliwaua muswalina 30 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 75.

 

 

Hitimisho 

 

Kwetu sisi kutoka katika janga hili la balaa inafaa tuwe na suluhisho, la sivyo shida na matatizo yatazidi. Kwa mtazamo wa haraka ni kuwa mustakabali katika hii dunia ni kwa Uislaam hata wakichukia makafiri, lakini majukumu ni lazima yabebwe na kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu anafaa kucheza dauru yake ili kuweza kufikia malengo yetu. Hili ni lazima lichukuliwe kama timu ambapo kila mmoja ana jezi na namba. Je, mimi na wewe tutacheza namba gani katika timu hiyo?

 

Mabadiliko ni lazima yaanze sana kwani kesho kesho haifiki na ngoja ngoja huumiza matumbo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatueleza:

 

 إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ 

Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. [Ar-Ra’d: 11]

 

Njia Ya Sisi Kwenda Mbele Ni Kufuatilia Muongozo Ufuatao:

 

i.       Mazoezi ya Kimwili: Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatueleza kwamba:

 

وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّـهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّـهُ يَعْلَمُهُمْ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ﴿٦٠﴾

Na waandalieni nguvu zozote mziwezazo na farasi waliofungwa tayari (kwa vita) muwaogopeshe kwayo maadui wa Allaah na maadui zenu, na wengineo wasiokuwa wao, hamuwajui, (lakini) Allaah Anawajua. Na chochote mkitoacho katika njia ya Allaah mtalipwa kikamilifu, nanyi hamtodhulumiwa. [Al-Anfaal: 60]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:

 

“Muumini aliye na nguvu ni bora na anapendwa zaidi na Allaah kuliko Muumini aliye dhaifu” [Muslim]

 

Hata wanawake hawakuachwa nyuma katika mas-ala haya ya kujiweka katika hali ya maandalizi na mazoezi. Wakati mmoja ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alishindana mbio na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akashinda [Ahmad na Abu Daawuud]. Hivyo, ni muhimu sana kwetu kuwa na matayarisho hayo.

 

ii.    Mazoezi ya Kiroho: Ni muhimu kwa Waislam kujitolea mhanga kwa ajili ya kuzisafisha nyoyo zao kwa kusoma, kujua maana na kuzingatia maamrisho yaliyomo ndani ya Qur-aan pamoja na kushikamana barabara na Sunnah. Ni lazima walime na kupalilia ndani ya nafsi zao hisia ya kutekeleza ‘Ibadah kwa mfano Swalah, Funga, Dhikr na aina nyengine za ‘Ibadah ambazo zitatuleta sisi karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) za faradhi na za Sunnah. Hii itaitakasa na kuisafisha roho zetu. Jambo hili linatakiwa lipatiwe umuhimu mkubwa kabisa.

 

iii.  Mazoezi ya Kiakili: Ikiwa ni katika Misikiti au katika vyuo vya masomo Waislam wanatakiwa wajengwe kiakili. Akili zao zinatakiwa zifunguliwe na masikio yao yatolewe taka na uchafu. Hili litawaimarisha na wao kuweza kutathmini mambo yanavyoendelea kwa muono wa Kiislamu. Ni muhimu kuwa na programu na duruus ambazo zitamlenga Muislamu pamoja na changa moto aina zote zinazomkumba katika ulimwengu huu wa utandawazi. Hizi halawaat za taalimu zitawaimarisha Waislam katika dini yao pamoja akili zao. Vitabu tofauti vinaweza kuchaguliwa ili mradi baada ya miaka kama 2 – 3 tunaweza kukaa na kutathmini faida pamoja na kuangalia udhaifu uliopo. Masomo ambayo yanaweza kuwepo ni kama Tajwiyd. Tafsiri ya Qur-aan, Hadiyth, Siyrah, ‘Aqiydah, Fiqhi, mambo yanavyojiri wakati huu, kutazama dini na madhehebu nyengine pamoja na kuangalia zile itikadi na harakati zilizo dhidi pamoja na kuwa na uadui mkubwa na Uislaam, na kadhalika.

 

 

Wabillahi at-Tawfiyq

 

Share