Kisa Cha Kuzaliwa Maryam (عليها السلام) Mama Yake Nabiy 'Iysaa (عليه السلام) Na Kulelewa Kwake
Kisa Cha Kuzaliwa Maryam (عليها السلام) Mama Yake Nabiy 'Iysaa (عليه السلام)
Na Kulelewa Kwake
Alhidaaya.com
Hannah bint Faaquwdh alikuwa mke wa Bwana 'Imraan. Imesemekena kwamba alikuwa hakujaaliwa kupata watoto na kwamba siku moja aliona ndege akimlisha kinda chake. Alipoona hivyo akatamani sana kupata mtoto akaomba Du'aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amjaalie kizazi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtakabalia Du'aa yake akashika mimba. Akaweka nadhiri kumfanya mwanawe awe mwenye kumakinika katika ibada na kuihudumia Baytul-Maqdis (Msikiti wa Aqswaa). Hivyo alipotambua kuwa amekwishabeba mimba akaweka hiyo nadhiri.
إِذْ قَالَتِ امْرَأَتُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٥﴾
Pale aliposema mke wa ‘Imraan: Rabb wangu, hakika mimi nimeweka nadhiri Kwako kilichomo katika tumbo langu kuwa ni wakfu kukutumikia, basi nitakabalie. Hakika wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-'Imraan: 35]
Maana kwamba Wewe Unasikia Du'aa yangu na Unatambua niya yangu. Hakujua kama atajaaliwa mtoto wa kiume au wa kike. Alipojifungua mtoto wa kike aliona kwamba mwanamke sio kama mwanamume kwa kukusudia katika kujifunga na ‘ibaadah Msikitini.
فَلَمَّا وَضَعَتْهَا قَالَتْ رَبِّ إِنِّي وَضَعْتُهَا أُنثَىٰ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا وَضَعَتْ وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنثَىٰ ۖ وَإِنِّي سَمَّيْتُهَا مَرْيَمَ وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴿٣٦﴾
Basi alipomzaa akasema: Rabb wangu, hakika mimi nimezaa mwanamke, na Allaah Anajua zaidi alichokizaa. Na mwanamme si kama mwanamke. Nami nimemwita Mayram nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa. [Al-'Imraan: 36]
Maryam Maana Yake ni 'Mtumishi wa Allaah'.
Aayah hiyo inathibitisha kuruhusiwa kumpa jina mtoto siku ile ile anayozaliwa (kama ambavyo imethibiti kumpa jina mtoto katika siku ya saba wakati wa kumfanyia 'Aqiyqah), na vile vile ni dhahiri katika Aayah hii kwamba hii ilikuwa pia ni sheria ya watu waliokuwa kabla yetu. Na pia iko katika Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
وُلِدَ لِي اللَّيْلَةَ وَلَد سَمَّيْتُهُ بِاسْمِ أبِي إبْرَاهِيمَ
Usiku huu mtoto (wa kiume) amezaliwa kwangu na nimemwita jina la baba yangu Ibraahiym [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kama Aayah ilivyomalizikia kwamba Bibi Hannah alimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amkinge na shaytwaan. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtakabalia Du'aa yake na dalili ni Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
مَا مِن مَوْلُودٍ يُولَدُ إلا مَسَّه الشَّيْطَانُ حِينَ يُولَدُ، فَيَسْتَهِلّ صَارخًا مِنْ مَسِّهِ إيَّاهُ، إلا مَرْيَم َوابْنَهَا ثم يقول أبو هريرة: اقرأوا إن شئتم: وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيم
Hakuna kizazi chochote kinachozaliwa ila shaytwaan anakigusa kinapozaliwa, na mtoto huanza kulia kwa sababu ya kuguswa huko, isipokuwa Maryam na mtoto wake [yaani 'Iysa ‘Alayhis-salaam] . Abu Hurayrah kisha akasema someni mkipenda: ((Nami namkinga Kwako, yeye na uzao wake, Uwalinde na shaytwaan aliyelaaniwa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Akapelekwa Maryam tokea utoto wake msikitini na akakulia huko na akamtoa kama ni zawadi ya Baytul-Maqdis.
Waliokuwa na jukumu la kuihudumia Baytul-Maqdis waligombania kumlea Maryam baada ya kufariki baba yake. Walisema kwamba kwa-vile ni mtoto wa Bwana 'Imraan ambaye alikuwa ni Imaam wao basi ni jukumu lao kumlea. Zakariyyah (‘Alayhis-salaam) naye akadai kumlea Maryam akasema: "Nipeni mimi kwani ndugu wa mama yake ni mke wangu". Wakasema: "Nyoyo zetu hazitopenda umlee wewe kwa sababu ni mtoto wa Imaam wetu". Ikabidi wafanye kura ya kutupa kalamu zao walizokuwa wakiandikia Tawraat katika mto wa Jordan. Yule ambaye kalamu yake itaelea katika mto ndiye atakayemlea Maryam. Walipozitupa kalamu zao, zote zilizama isipokuwa ya Zakariyyah (‘Alayhis-salaam) ambaye pia naye alikuwa ni bwana wao, Mwanachuoni wao na pia ni Nabiy wao.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anampa kisa hiki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Wahyi (ufunuo) kisha Anawatanabahisha makafiri kwamba hizi ni khabari za ghaibu ambazo hakuzijua Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla, na kwa maana kwamba haya maelezo ya Qur-aan si maneno ya Nabiy kama wanavyodai makafiri:
ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۚ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يُلْقُونَ أَقْلَامَهُمْ أَيُّهُمْ يَكْفُلُ مَرْيَمَ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٤﴾
Hizo ni khabari za ghayb Tunakufunulia Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na hukuwa pamoja nao walipotupa kalamu zao, ili nani kati yao amlee Maryam. Na hukuwa pamoja nao walipokhasimiana. [Al-'Imraan: 44]
Tukirudia kisa alipozaliwa Maryam, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alikubali nadhiri ya mama yake Akamjaalia kuwa na tabia njema na kupata elimu ya dini yake kutoka kwa Nabiy Zakariyyah (‘Alayhis-salaam) hata akawa Mswahilina mno na akapata sifa ya 'utiifu' kama alivyotajwa katika Aayah hizo za juu. Kutwa kucha alikuwa akifanya ‘ibaadah. Ikawa kila mara Zakariyyah (‘Alayhis-salaam) anapoingia katika mihraab (sehemu yake aliyokuwa akiswalia) anamkuta ana matunda ya ajabu. Kwa maana kwamba msimu wa baridi anamkuta ana matunda ya msimu wa joto na msimu wa joto anamkuta ana matunda ya msimu wa baridi ndipo alipomuuliza kama yanavyokuja maelezo katika Aayah ifuatayo:
فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا ۖ كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِندَهَا رِزْقًا ۖ قَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّىٰ لَكِ هَـٰذَا ۖ قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٧﴾
Basi Rabb wake Akampokea kwa kabuli njema na Akamkuza mkuzo mzuri na Akamfanya Zakariyyaa kuwa mlezi wake. Kila Zakariyyaa alipoingia kwake katika chumba cha kuswalia alikuta kwake kuna riziki Akasema: Ee Maryam! Umepata wapi hivi? Akasema: Hivi ni kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah Anamruzuku Amtakaye bila ya hesabu. [Al-'Imraan: 37]
Kisa kama kilivyonukuliwa katika tafsiyr ya Ibn Kathiyr.
Baadhi Ya Aayah Husika Za Kisa Cha Kuzaliwa Maryam (عليها السلام) Na Kuzaliwa Nabiy ‘Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Katika Suwrah Aal-‘Imraan:
Kauli za Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى)
إِذْ قَالَتِ امْرَأَتُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٥﴾
35. Pale aliposema mke wa ‘Imraan: Rabb wangu, hakika mimi nimeweka nadhiri Kwako kilichomo katika tumbo langu kuwa ni wakfu kukutumikia, basi nitakabalie. Hakika wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.
فَلَمَّا وَضَعَتْهَا قَالَتْ رَبِّ إِنِّي وَضَعْتُهَا أُنثَىٰ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا وَضَعَتْ وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنثَىٰ ۖ وَإِنِّي سَمَّيْتُهَا مَرْيَمَ وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴿٣٦﴾
36. Basi alipomzaa akasema: Rabb wangu, hakika mimi nimezaa mwanamke, na Allaah Anajua zaidi alichokizaa. Na mwanamme si kama mwanamke. Nami nimemwita Mayram nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa.
فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا ۖ كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِندَهَا رِزْقًا ۖ قَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّىٰ لَكِ هَـٰذَا ۖ قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٧﴾
37. Basi Rabb wake Akampokea kwa kabuli njema na Akamkuza mkuzo mzuri na Akamfanya Zakariyyaa kuwa mlezi wake. Kila Zakariyyaa alipoingia kwake katika chumba cha kuswalia alikuta kwake kuna riziki Akasema: Ee Maryam! Umepata wapi hivi? Akasema: Hivi ni kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah Anamruzuku Amtakaye bila ya hesabu.
هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾
38. Hapo hapo Zakariyyaa akamwomba Rabb wake, akasema: Rabb wangu Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema hakika Wewe ni Mwenye kusikia du’aa yangu.
فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٣٩﴾
39. Basi mara Malaika akamwita (Zakariyyaa) naye akiwa amesimama anaswali katika chumba kwamba: Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa mwenye kusadikisha Neno (la Kun!) kutoka kwa Allaah na ni mwenye sharaf, busara na taqwa, na anayejitenga mbali na matamanio na Nabiy miongoni mwa Swalihina.[1]
قَالَ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَقَدْ بَلَغَنِيَ الْكِبَرُ وَامْرَأَتِي عَاقِرٌ ۖ قَالَ كَذَٰلِكَ اللَّـهُ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ﴿٤٠﴾
40. (Zakariyyaa) Akasema: Nitapataje ghulamu na hali uzee umeshanifikia na mke wangu ni tasa?! Akasema: Hivyo ndivyo Allaah Anafanya Atakavyo
قَالَ رَبِّ اجْعَل لِّي آيَةً ۖ قَالَ آيَتُكَ أَلَّا تُكَلِّمَ النَّاسَ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ إِلَّا رَمْزًا ۗ وَاذْكُر رَّبَّكَ كَثِيرًا وَسَبِّحْ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ ﴿٤١﴾
41. (Zakariyyaa) Akasema: Rabb wangu niwekee Aayah (ishara) Akasema: Ishara yako ni kwamba hutoweza kuwasemesha watu siku tatu ila kwa kuashiria tu. Na mdhukuru Rabb wako kwa wingi na msabihi jioni na asubuhi.
وَإِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَاكِ وَطَهَّرَكِ وَاصْطَفَاكِ عَلَىٰ نِسَاءِ الْعَالَمِينَ ﴿٤٢﴾
42. Na pale Malaika waliposema: Ee Maryam! Hakika Allaah Amekuteua na Amekutakasa na Amekukhitari juu ya wanawake wa walimwengu.
يَا مَرْيَمُ اقْنُتِي لِرَبِّكِ وَاسْجُدِي وَارْكَعِي مَعَ الرَّاكِعِينَ ﴿٤٣﴾
43. Ee Maryam! Kuwa mtiifu kwa Rabb wako, na sujudu, na rukuu pamoja na wanaorukuu.
ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۚ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يُلْقُونَ أَقْلَامَهُمْ أَيُّهُمْ يَكْفُلُ مَرْيَمَ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٤﴾
44. Hizo ni khabari za ghayb Tunakufunulia Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na hukuwa pamoja nao walipotupa kalamu zao, ili nani kati yao amlee Maryam. Na hukuwa pamoja nao walipokhasimiana.
إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٤٥﴾
45. Na pale Malaika waliposema: Ee Maryam! Hakika Allaah Anakubashiria Neno (la Kun!) kutoka Kwake (umzae mtoto), jina lake ni Al-Masiyhu ‘Iysaa mwana wa Maryam, mwenye taadhima katika dunia na Aakhirah na ni miongoni mwa waliokurubishwa (kwa Allaah).
وَيُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلًا وَمِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٤٦﴾
46. Na Atawasemesha watu katika utoto wake na utu uzima wake na ni miongoni mwa Swalihina.
قَالَتْ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي وَلَدٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ ۖ قَالَ كَذَٰلِكِ اللَّـهُ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ إِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٤٧﴾
47. (Maryam) Akasema: Itakuwaje nipate mtoto na hali hakunigusa mtu? (Malaika) Akasema: Hivyo ndivyo Allaah Huumba Akitakacho. Anapokidhia jambo basi huliambia: Kun! (Kuwa!) Basi nalo huwa.
وَيُعَلِّمُهُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَالتَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ ﴿٤٨﴾
48. Na Atamfunza Kitabu na Hikmah na Tawraat na Injiyl.
وَرَسُولًا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنِّي قَدْ جِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ ۖ أَنِّي أَخْلُقُ لَكُم مِّنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ فَأَنفُخُ فِيهِ فَيَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۖ وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۖ وَأُنَبِّئُكُم بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٤٩﴾
49. Na ni Rasuli kwa wana wa Israaiyl (akisema): Hakika mimi nimekujieni na Aayah (ishara, dalili) kutoka kwa Rabb wenu, kwamba mimi nakuundieni kutokana na udongo kama umbo la ndege, kisha napuliza humo basi huwa ndege kwa idhini ya Allaah. Na naponyesha vipofu na wenye ubarasi na nahuisha wafu kwa idhini ya Allaah. Na nakujulisheni mtakavyokula na mtakavyoweka akiba majumbani mwenu. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayah kwenu mkiwa Waumini.
وَمُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَلِأُحِلَّ لَكُم بَعْضَ الَّذِي حُرِّمَ عَلَيْكُمْ ۚ وَجِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿٥٠﴾
50. Na mwenye kusadikisha yaliyo kabla yangu katika Tawraat na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale yaliyoharamishwa kwenu. Na nimekujieni na Aayah (ishara, hoja) kutoka kwa Rabb wenu. Basi mcheni Allaah na nitiini.
إِنَّ اللَّـهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۗ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٥١﴾
51. Hakika Allaah ni Rabb wangu na Rabb wenu basi mwabuduni. Hii ndio njia iliyonyooka.
[1] Neno Kun! (Kuwa) rejea Aayah namba (47) Suwrah hii.