18-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Habiyb Bin Zayd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'Anhu)
Swabrun Jamilyl (Subira njema)
18- Subira Za Maswahaba - Habiyb Bin Zayd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'Anhu)
Habiyb bin Zayd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitumwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Musaylimah al-Kadhaab kumpelekea majibu ya barua yake aliyomtumia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukiri urasuli wake wa uongo. Musaylimah alikwishajitangaza kwa watu na wengi kuwa yeye ni rasuli na watu wakaanza kumfuata na kumwamini. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu barua yake kwa kumtaka Musaylimah aache madai yake ya urasuli. Barua hiyo ilimghadhibisha sana Musaylimah akatoa amri afungwe Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kupelekwa katika hadhara ya wakuu wake. Akaanza kumuuliza:
“Unashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah”
Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu: “Ndiyo nashuhudia hivyo”.
Musaylimah akamuuliza: “Na unashuhudia kuwa mimi pia ni rasuli wa Allaah?”
Habiyb akajibu: “Masikio yangu yamezibwa kusikia madai yako hayo”
Akamuuliza tena: “Unashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah?”
Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu tena: “Ndiyo nashuhudia hivyo”.
Musaylimah akamuuliza tena: “Na unashuhudia kuwa mimi pia ni rasuli wa Allaah?”
Habib akajibu tena: “Masikio yangu yamezibwa kusikia madai yako hayo.”
Akawa anaendelea kumuuliza hivyo, na kila anapoulizwa Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) iwapo anashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah, alikiri. Na anapoulizwa iwapo anashuhudia kuwa Musaylimah pia ni rasuli wa Allaah, alijibu vile vile kuwa yeye kiziwi hasikii madai yake.
Mwisho Musaylimah akasema: “Niitieni mshika panga wangu na mpiga mjeledi.”
Wakaanza kumtesa Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) huku wakimpiga mijeledi na kumkata vipande vipande. Wakaanza kumkata mkono mmoja, ukaanguka chini. Kisha Musaylimah akamuuliza tena maswali yale yale, lakini Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa thabiti na kuwapa majibu yale yale. Musaylimah akatoa amri akatwe mkono mwengine ukaanguka mbele ya mkono wa awali uliokatwa. Wakamtesa mpaka akafa shahidi (Radhwiya Allaahu 'anhu). Ummu ‘Ammaarah aliposikia juu ya kuuliwa kwa mwanawe akasema: “Mwanangu keshanitangulia Jannah.”