Jimai: Kufanya Mapenzi Na Kitendo Cha Ndoa Wakati Wa Ramadhwaan Nini Hukmu Yake?

SWALI:

Asalam Aleykum! Ndugu zetu waislamu, Allaah awajaze na awape subra na muendele kutusaidia na maswali yetu. Inshallah.

Swali langu ni inafaa au ina kubalika kufanya mapenzi au kuingiliana wakati wa ramadhani? Na baada ya kitendo hicho wakaoga na kujitoharisha na kabla ya siku nyengine yaani ya kufunga tena. Na je ikiwa haikubaliki au haifai wafanye nini? na walifanya hivyo kama mara 9 hivi.

Tafadhali ningependa munijibu maswali yangu

Asanteni sana na Jaza yenu kwa Allaah

 

 


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allah Mtukufu, Swalah na salamu zimfikie kipenzi chetu, Mtume Muhammad (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Ahli zake na Maswahaba zake (Radhiya-Allaahu 'anhum) na Watangu Wema na waliowafuata kwa kheri mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Shukrani kwa maswali yako, na hapa tunakupatia majibu yako.

1. Dini ya Kiislamu ambayo ndiyo inakwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu inatupatia mwongozo wa kila kitu hata maingiliano baina ya mume na mke, ikiwa ni wakati wa Ramadhaan au baada ya yake. Lakini katika wakati wa Ramadhaan kuna mambo fulani hayafai kufanywa wakati wa mchana japokuwa ni halali kufanywa katika miezi mingine. Na moja katika hayo ni kukutana kimwili baina ya mume na mke wakati wa mchana, lakini baada ya muadhini wa Magharibi wanaweza kufanya mapenzi yao mpaka kabla ya kuingia alfajiri bila ya matatizo yoyote.

 

Ikiwa mapenzi hayo yalifanywa wakati wa mchana itabidi mume na mke watoe kafara ikiwa wamefanya kitendo hicho kwa makusudi pasina kulazimishwa. Kafara ni ima kuacha mtumwa huru, au kufunga miezi miwili mfululizo au kulisha masikini sitini (Imepokewa na al-Bukhariy na Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya-Allaahu 'anhu]).

Na kwa maelezo zaidi ingia katika "Fataawa za Ramadhaan" Kuhusu Kulipa Swawm ambazo ziko katika Alhidaaya. Kwa wepesi bonyeza kiungo kifuatacho:

 

 Hukmu Ya Kutenda Kitendo Cha Jimai  (Tendo La Ndoa) Mchana Wa Ramadhaan

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share