Kuswali Kabla Ya Wakati Nchi Za Ulaya Siku Za Baridi

SWALI:

Asalaam aleikum

Mimi nilikuwa nnauliza kuhusu nyakati za sala, na kama tunavyojuwa time ya sala ikiingia tu tunatakiwa kusali, sasa suali langu ni hivi,kama sisi tunaokaa Europe nyakati za sala huwa zinabadilika sana kutokana na winter au summer,kwa hivi sasa kama ni winter sala ya alfajiri  huku kwetu inaingia saa  ( 06.39)  maana juwa hutoka ( 8.37).

Sasas suali ni hivi mimi hanza kazi saa moja kamili (07.00 ) na mimi inanichukuwa 30 to 45 minutes kuelekea kazini kwangu jee nnaweza kusali kabla ya kutoka nyumbani?

Asante

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Katika shuruti za kuswihi Swalah, moja wapo ni kuingia wakati wake. Huwezi kuswali hadi uhakikishe kama ni wakati wa Swalah umewadia ndio uswali au sivyo Swalah haitoswihi. 

Nyakati za Swalah zote tano ni kama zilivyoelezewa katika Hadiyth ifuatayo:

عن‏ ‏عبد الله بن عمرو ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال ‏(( ‏وقت الظهر إذا ‏ ‏زالت ‏ ‏الشمس وكان ظل الرجل كطوله ما لم يحضر العصر ووقت العصر ما لم تصفر الشمس ووقت صلاة المغرب ما لم يغب الشفق ووقت صلاة العشاء إلى نصف الليل الأوسط ووقت صلاة الصبح من طلوع الفجر ما لم تطلع الشمس فإذا طلعت الشمس فأمسك عن الصلاة فإنها تطلع بين قرني شيطان))  مسلم  

Imetoka kwa 'Abdullah bin 'Amr رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Wakati wa Dhuhuri unabakia mpaka jua linapopita kilele chake, na kivuli cha mtu kinakuwa ni  sawa na urefu wa mtu  na madamu wakati wa Alasiri bado haukufika. Na wakati wa Alasiri unaendelea kubakia madamu jua halikugeuka kuwa manjano. Na wakati wa Magharibi unabakia madamu rangi nyekundu ingalipo, na wakati wa 'Ishaa unabakia mpaka katikati ya usikuna wakati wa Alfajiri unaanza baada ya kupambazuka hadi kabla ya jua kuchomoza, acheni kuswali wakati huo kwani jua huchomoza baina ya pembe mbili za shaytwaani)) [Muslim]

Na Anasema Allaah سبحانه وتعالى  

َ(( إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا))

((Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu))) [An-Nisaa:103]

Kutokana na maelezo yako kuhusu wakati unaotoka na kufika kazini, inaonyesha kuwa unapofika kazini itakuwa bado wakati wa Alfajiri kutoweka, kwa hiyo ni vizuri kama utatoka nyumbani mapema kidogo ili ufikie kazini kabla ya wakati wa kuanza kazi ili uweze kuswali Swalah ya Alfajiri. 

Ikiwa kuna shida ya kupata sehemu ya kuswali kazini basi unaweza kuswali njiani ukiwa umekaa kitako katika safari ikiwa huendeshi gari mwenyewe yaani katika basi au treni na uelekee popote kinapoelekea chombo cha safari, lakini hili litafanyika tu kukiwa na dharura ya hali ya juu kwani haikubaliwi kuswali Swalah ya fardh kwenye chombo bila dharura, na hali yako inaonyesha kuwa unaweza kuswali kazini au hata popote penye nafasi japokuwa sehemu unayopaki gari lako kazini, kwani ardhi yote ni pahali pa kuswaliwa maadam hakuna najisi wala si kwenye kaburi au kuwepo na vinavyokatazwa kisheria kuswaliwa.   

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share