Ndimi Zetu Zinasema: “Tunaitaka Ramadhaan Na Tunaipenda” Lakini Vitendo Vyetu Ni Kinyume Chake!
Ndimi Zetu Zinasema: “Tunaitaka Ramadhaan Na Tunaipenda”
Lakini Vitendo Vyetu Ni Kinyume Chake!
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):
أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنْ تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ
Je, haujafika wakati kwa walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah na yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawatawilikia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki. [Al-Hadiyd: 16]
Ramadhwaan inakaribia! Umefika wakati kwa wale waliozama katika shirki, ulevi, (kila aina ya) madhambi na bid’ah, kujirekebisha na kujitakasa kwa Tawhiyd, utiifu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kufuata Sunnah ya Rasuli Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo:
- Tujirekebishe kuanzia sasa ili itakapoingia Ramadhwaan, nyoyo na viungo vyetu viwe vinamwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Pekee bila ya kumshirikisha.
- Tujirekebishe sasa ili itakapoingia Ramadhwaan, viungo vyetu vitende amali zenye kumridhisha Allaah!
- Tujirekebishe sasa ili inapoingia Ramadhwaan, vitendo vyetu viendane sawa na Sunnah ya mpenzi wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ili tuwe ni wenye kuwafuata Swahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum) ambao ni viumbe bora kabisa baada ya Rusuli.
Kujirekebisha na kujitakasa kunahitaji muda, na hakuna muda mzuri kama huu unaokaribia mwezi wa Ramadhwaan!
Salafus-Swaalih walikuwa wakiitarajia Ramadhwaan na wakijitayarisha mapema mno. Walikuwa wakiiomba du’aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Awawezeshe kuifikia Ramadhwaan.
Vipi basi wewe? Umefikia wapi katika kutarajia, kujitayarisha na kuomba du’aa?
Au utakuwa miongoni mwa wale wajinga wanaosubiri siku ya kwanza ya Ramadhwaan ndio uanze kupapatika kurekebisha nafsi yako hali ya kuwa bado umezamia katika shirki, madhambi na bid’ah? Matokeo yake basi ni kwamba mwezi utakapomalizika utakuwa bado una athari za maovu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):
وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ
Na iogopeni Siku mtayorejeshwa ndani yake kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. [Al-Baqarah: 281]
Na Anasema pia:
وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَى﴿٤٠﴾ فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَى ﴿٤١﴾
Ama yule aliyekhofu kisimamo cha mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa. Basi hakika Jannah (itakuwa) ndio mahali pake pa kukimbilia. [An-Naziaat: 40-41]
Na Anasema pia:
أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنْ تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ
Je, haujafika wakati kwa walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah na yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawatawilikia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki. [Al-Hadiyd: 16]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Atuongoze sote na ndimi zetu zinazosema: “Tunaitaka Ramadhwaan na tunaipenda” huku (niyyah zetu na) vitendo vyetu ni kinyume chake. Na uhakika wenyewe ni kwamba wako wanaosema: “Hatupendi Ramadhwaan! Isitufikie! Hatutaki kuzindukana madhambi yetu na maasi! Hatutaki kuathirika tukatoka kwenye shirki, bid’ah na dhambi na hali tumeshaizoea! Tafadhali msitukere!
Ndugu yetu Muislam! Anza haraka kujitakasa ili Ramadhwaan itakapoingia, moyo wako na viungo vyako viweze kukubali kwa sahali kutekeleza kheri nyingi. Hivi ndivyo mtu anavyojitayarisha kikweli na ndipo atakapofaidika na mwezi mtukufu wa Ramadhwaan.