01-Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd: Tawhiyd Ni Elimu Tukufu Na Bora Kabisa

 

 

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

 

01-Tawhiyd Ni Elimu Tukufu Na Bora Kabisa

 

 

Binaadamu anahitaji kujifunza atambue maana, fadhila na umuhimu wa Tawhiyd, kisha afanyie kazi kuithibitisha.

 

 

Elimu ya Tawhiyd ni tukufu na bora kwa kuwa ni elimu anayoihitaji mja kila wakati, kwa sababu inahusiana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye Anapasa kupwekeshwa katika ‘ibaadah bila ya kumshirikisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

Basi jua kwamba: laa ilaaha illa-Allaah (hapana muabudiwa wa haki ila Allaah) na omba maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike. [Muhammad: 19]

 

Aayah hiyo imetanguliza elimu ya asasi ya Dini nayo ni maarifa ya Tawhiyd,

 

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ

Basi jua kwamba: laa ilaaha illa-Allaah (hapana muabudiwa wa haki ila Allaah)

 

kisha ikafuatia na maarifa ya elimu ya matawi ambayo ni kuomba maghfirah,

 

وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

 na omba maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike

 

Kwa hiyo imethibitisha ubora wa elimu ya Tawhiyd kabla ya ‘amali za mwana Aadam, sababu ‘ibaadah na ‘amali za mwana Aadam bila ya kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hazikubaliwi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Juu ya kuwa Aayah hiyo imeteremshwa kumkusudia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), lakini haimaanishi kwamba hiyo ni amri kwake kwamba amjue Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kwani ujuzi wa kumjua Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) umeshafunuliwa Wahyi kwake kabla ya hapo. Aayah hiyo imeteremshwa akiwa Madiynah na kabla yake imepita miaka 13 akiwa ni Rasuli mjini Makkah akiwalingania watu wake neno hilo la laa ilaaha illa Allaah. Lilokusudiwa ni kule kutajwa mwanzo elimu ya kumjua Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kabla ya elimu ya ‘amali kama hivyo kuomba maghfirah, au ‘amali nyinginezo kama Swalaah, Zakaah, Swawm, Hajj na kadhaalika.

 

Akathibitisha Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu ujuzi wake kuhusiana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akasema:

 

 فَوَاللَّهِ إنِّي لَأَعْلَمُكُمْ بِاَللَّهِ وَأَشَدُّكُمْ لَهُ خَشْيَة  رواه البخاري

Wa-Allaahi, (Naapa kwa Allaah) kwamba hakika mimi namjua zaidi Allaah na ni mwenye kumkhofu zaidi kuliko nyinyi. [Al-Bukhaariy]

 

Na ‘amali hazikubaliwi isipokuwa baada ya kumwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Imethibiti kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba aliulizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

أَيُّ الْعَمَلِ أَفْضَلُ؟ فَقَالَ: ((إِيمَانٌ بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ))

‘Amali ipi bora kabisa? Akajibu: ((Kumwamini Allaah na Rasuli Wake)) [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  katika Al-Bukhaariy]

 

Share