20-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Tawhiyd Inamuepushia Mtu Majanga Na Balaa
Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd
20-Tawhiyd Inamuepushia Mtu Majanga Na Balaa
Majanga na balaa yanaondoshwa kwa Tawhiyd, na ndio maana du’aa za kuepushwa na hayo zimekuwa ni kwa Tawhiyd, na du’aa ya Nabiy Yuwnus (‘Alayhis-Salaam) alipokuwa katika kiza na dhiki ndani ya tumbo la samaki (nyangumi) ilikuwa ni ya Tawhiyd na kwayo akaokolewa na kupata faraja. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾
Na Dhan-Nuwn (Yuwnus) alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha; akaita katika kiza kwamba: “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.”
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamuitikia:
فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾
Basi Tukamuitikia na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokowavyo Waumini. [Al-Anbiyaa: 87-88]
Du’aa hiyo ya Nabiy Yuwnus (‘Alayhis-Salaam) pia ni sababu ya Muislamu kutakabaliwa haja zake kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ إِبْرَاهِيمَ بْنِ مُحَمَّدِ بْنِ سَعْدٍ عَنْ أَبِيهِ عَنْ سَعْدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم): ((دَعْوَةُ ذِي النُّونِ إِذْ دَعَا وَهُوَ فِي بَطْنِ الْحُوتِ: لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ .فَإِنَّهُ لَمْ يَدْعُ بِهَا رَجُلٌ مُسْلِمٌ فِي شَيْءٍ قَطُّ إِلاَّ اسْتَجَابَ اللَّهُ لَهُ))
Kutoka kwa Ibraahiym bin Muhammad bin Sa’d kutoka kwa baba yake kutoka kwa Sa’d (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Du’aa ya Dhan-Nuwn alipoomba alipokuwa katika tumbo la nyangumi, “Laa ilaaha illa Anta Subhaanaka inniy kuntu minadhw-dhwaalimiyn.” Basi hakika hakuna mtu Muislamu aombaye kwayo kitu chochote kile ila Allaah Atamuitikia)). [Swahiyh At-Tirmidhy]
Na Hadiyth zifuatazo zimetaja baadhi ya adhkaar ambazo zinamuondoshea mtu kila aina ya dhiki, janga na balaa.
Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa):
لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ الْعَظـيمُ الْحَلِـيمْ، لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ رَبُّ العَـرْشِ العَظِيـمِ، لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ رَبُّ السَّمَـوّاتِ ورّبُّ الأَرْضِ ورَبُّ العَرْشِ الكَـريم
Laa ilaaha illa-Allaahul-‘Adhwiymul-Haliym. Laa ilaaha illa-Allaahu Rabbul-‘Arshil-‘Adhwiym. Laa ilaaha illa-Allaahu Rabbus-samawaati wa Rabbul-Ardhwi wa Rabbul-‘Arshil-Kariym.
Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah Aliye Mtukufu Mpole. Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah Rabb wa ‘Arshi Tukufu. Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi na Rabb wa ‘Arshi tukufu. [Al-Bukhaariy (7/154) [6346], Muslim (4/2092) [2730] na Ahmad]
Hadiyth ya Abu Bakr Nafiy’ bin Haarith Ath-Thaqafiyy (Radhwiya Allaahu 'anhu):
اللّهُـمَّ رَحْمَتَـكَ أَرْجـو فَلا تَكِلـني إِلى نَفْـسي طَـرْفَةَ عَـيْن، وَأَصْلِـحْ لي شَأْنـي كُلَّـه لَا إِلَهَ إِلَّا أنْـت
Allaahumma Rahmataka arjuw falaa takilniy ilaa nafsiy twarfata ‘ayni, wa aswlih liy sha-niy kullahu, laa ilaaha illaa Anta.
Ee Allaah, Rehma Zako nataraji, usinitegemeze kwenye nafsi yangu japo kwa muda wa upepeso wa jicho, na Unitengenezee mambo yangu yote, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe. [Abu Daawuwd (4/324) [5090], Ahmad (5/42), ameipa daraja ya Hasan Al-Albaaniy (رحمه الله) katika Swahiyh Abiy Daawuwd (3/959)]
Hadiyth ya Asmaa bint ‘Umays (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((أَلَا أُعَلِّمُكِ كَلِمَاتٍ تَقُولِينَهُنَّ عِنْدَ الْكَرْبِ اللهُ اللهُ رَبِّي لا أُشْـرِكُ بِهِ شَيْـئاً))
((Je, nikufunidshe maneno uyaseme wakati wa janga: Allaah, Allaah, Rabb wangu, simshirikishi na chochote)). [Abu Daawuwd (2/87) [1525] na taz. Swahiyh Ibn Maajah (2/335)]
Hata makafiri waliondoshewa janga pale walipokuwa wakimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa ikhlaasw. Mfano pale walipopanda jahazi dhoruba kali ikawafikia iliyokaribia kuwazamisha, walimkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee bila ya kumshirikisha mtu kumuomba Awaokoe kama ilivyo dalili katika kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
هُوَ الَّذِي يُسَيِّرُكُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا كُنتُمْ فِي الْفُلْكِ وَجَرَيْنَ بِهِم بِرِيحٍ طَيِّبَةٍ وَفَرِحُوا بِهَا جَاءَتْهَا رِيحٌ عَاصِفٌ وَجَاءَهُمُ الْمَوْجُ مِن كُلِّ مَكَانٍ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ أُحِيطَ بِهِمْ ۙ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ لَئِنْ أَنجَيْتَنَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ﴿٢٢﴾
Yeye Ndiye Anayekuendesheni katika bara na bahari. Mpaka mnapokuwa katika majahazi na yanakwenda nao kwa upepo mzuri, na wakafurahia; mara ukawajia upepo wa dhoruba, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakayakinisha kwamba wameshazungukwa. Hapo humwomba Allaah wenye kumtakasia Yeye Dini (wakisema): “Ukituokoa katika haya, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.” [Yuwnus: 22]
Lakini baada ya kuwaokoa wanarudi kumshirikisha:
فَلَمَّا أَنجَاهُمْ إِذَا هُمْ يَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۗ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا بَغْيُكُمْ عَلَىٰ أَنفُسِكُم ۖ مَّتَاعَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ ثُمَّ إِلَيْنَا مَرْجِعُكُمْ فَنُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٢٣﴾
Lakini Anapowaokoa, tahamaki wao wanafanya baghi katika ardhi bila ya haki. Enyi watu! Hakika baghi yenu ni dhidi ya nafsi zenu. Ni starehe ya uhai wa dunia. Kisha Kwetu marejeo yenu; Tutakujulisheni kwa yale mliyokuwa mkiyatenda. [Yuwnus: 23]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ ﴿٦٥﴾
Wanapopanda merikebu humwomba Allaah wakiwa wenye kumtakasia Yeye Dini, lakini Anapowaokoa katika nchi kavu, tahamaki hao wanamshirikisha. [Al-‘Ankabuwt: 65]