Dujayn bin Thaabit Al-Fazaariy (رحمه الله) (Aliyenasibishwa Kuwa Ni Juha)

 

Dujayn bin Thaabit Al-Fazaariy (Rahimahu Allaahu)

 

(Aliyenasibishwa Kuwa Ni Juha) 

Alikuwa Katika Taabi'iyn Na Si Kikatuni (Mchekeshaji)

 

Imetarjumiwa na Abu ‘Abdir-Rahmaan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Kumezoeleka kuwa Juha ni mtu mchekeshaji au mjinga, na hata vimetungwa vitabu vingi vya watoto vyenye kuelezea visa mbalimbali kumhusisha navyo Juha.

 

Jambo la kushangaza vilevile hata walinganiaji wa makundi potofu, hutumia jina hilo kuwakebehi watu wa Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah! Kuonesha ni jinsi gani hao walinganiaji wa makundi potofu walivyokuwa hawana utafiti na kutofuatilia mambo kisawasawa.

 

 

Juha ni nani?

 

Juha jina lake halisi ni Dujayn bin Thaabit Al-Fazaariy (Allaah Amrehemu).

 

Alikutana na Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na amesimulia kutoka kwake, pia kutoka kwa Aslam mtumwa aliyeachwa huru na ‘Umar bin Al-Khatwaab, na Hishaam bin ‘Urwah na ‘Abdullaah bin Al-Mubaarak na wengine waliomsimulia.

 

Ash-Shiraaziy alisema: “Juha lilikuwa jina la utani.” Na kusema alikuwa mchekeshaji hiyo ni katika kumchafua jina lake na ni uongo.”

 

Al-Haafidhw Ibn ‘Asaakir alisema: “Aliishi kwa miaka mia moja.”

 

Na utakutana na makala katika kitabu kiitwacho: “Historia” cha Ibn Shaakir, ukurasa namba 373.

 

Na katika kitabu kiitwacho: “Mizani ya Haki” cha Adh-Dhahabiy, katika Juzuu ya kwanza ukurasa 326; ambapo kuna maelezo.

 

Juha alikuwa katika ma Taabi’iyn na mama yake alikuwa ni mtumishi wa Anas bin Maalik. Alikuwa ni mtu mwenye subra na muadilifu kinyume na maelezo yaliyomo kwenye ngano ambazo zinamhusisha yeye zenye kumfanyia dhihaka na utani wa kila aina.

 

As-Suyuwtwiy alisema: “Karibu ngano zote anazohusishwa nazo Juha, hazina asili.”

 

Imesimuliwa na Adh-Dhahabiy katika wasifu wake kwamba ‘Ubaad bin Suhayb alisema:

“Kuhusu Abu Al-Ghusn (Juha) alikuwa akitusimulia, na sijapata kumuona mtu mwenye fahamu nzuri kama yeye.”

 

Pia alisema kuhusu yeye:

“Huenda alikuwa mtu wa dhihaka katika ujana wake, lakini katika utu uzima wake alikuwa mtu mtulivu, na Wanachuoni wa Hadiyth wakisimulia kutoka kwake.

 

Al-Haafidhw Ibn Al-Jawziy (Allaah Amrehemu):

“Na kutoka kwao ni Juha, na Kun-yah yake ni Abu Al-Ghusn, imeelezewa kuwa alikuwa ni mtu mwerevu mwenye fahamu nzuri lakini wamegeuza na kumfanya kama ni kiroja na mtu mjinga.”

Na katika hizo riwaya ni kuonesha chuki kwake kwa kumzushia visa vya ajabu ajabu. Allaah Ndiye Ajuae zaidi.

 

Kwa hiyo, chunga ulimi wako kumzungumzia Juha vibaya, huenda akawa hoja dhidi yako siku ya hukumu. Kucha za Juha, Bata wa Juha, Punda wa Juha, Juha Kalulu; na kila kitu kuhusu Juha. Wa Allaahul-Musta’aan.

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا

Enyi mloamini! Mcheni Allaah na semeni kauli ya kweli (ya sawasawa).

 

يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا

Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu. [Al-Ahzaab 33:70-71]

 

 

Share