04-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Maamrisho Ya Swalah Kwetu
Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake
04- Maamrisho Ya Swalah Kwetu
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemuamrisha Rasuli Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na sisi kuamrisha familia zetu na watu wetu kutekelza Swalaah, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا
Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo [Twaahaa: 132]
Aayah hiyo tukufu inatupa dokezo kwamba kudumisha Swalaah ni jambo gumu hasa kwa watoto na vijana wetu. Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatutia nguvu kwa kututaka tusichoke kuimarisha ibaadah hii, bali tuendelee nayo kwa kuvumilia tabu zake.
Swalaah huwa nzito kwa wengi wanapokuwa usingizini. Lakini haitupasi kuwaonea huruma watoto wetu na wanaotuhusu kuwaamsha kwa ajili ya kuswali, kwani kufanya hivyo haimaanishi kuwa ni kuwapenda bali ni kuwaangamiza kwa sababu Muislamu anapodumisha Swalaah yake, hujiepusha na maovu na machafu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ
na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. [Al-'Ankabuwt: 45]
Na maovu humpeleka mtu motoni, na moto huo ndio tuliotahadharishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) tujikinge nao:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾
Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]
Naye Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile ametuamrisha Swalaah, akatusisitiza na kutubainishia fadhila na malipo yake adhimu:
عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى اللّه عليه وسلم أنه قال: ((مُرُوا أَوْلادَكُمْ بِالصَّلاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ، وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ، وَفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ فِي الْمَضَاجِعِ)) البخاري
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Amrisheni watoto wenu kuswali wakiwa na umri wa miaka saba, na wapigeni (pigo khafifu wakiwa hawataki kuswali) wakiwa na umri wa miaka kumi, na watenganisheni vitanda.”(kuwatenganisha wasichana na wavulana vyumbani) [Al-Bukhaariy]
Amri ya kukidhi Swalaah:
Swalaah inapaswa kukidhiwa kwa mwenye kuisahau au kwa mwenye kupitiwa kwa usingizi:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍعَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((مَنْ نَسِيَ صَلَاةً فَلْيُصَلِّ إِذَا ذَكَرَهَا لَا كَفَّارَةَ لَهَا إِلَّا ذَلِكَ)) الصحيحين و سننابن ماجة و الترمذي
Kutoka kwa Anas bin Maalik kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kusahau Swalaah, aswali atakapokumbuka na hakuna kafara isipokuwa hivyo)) [Al-Bukhaariy, Muslim, Sunan Ibn Maajah na At-Tirmidhy]
Na katika Riwaayah nyingine:
(( مَنْ نَسِىَ صَلاَةً أَوْ نام عَنْها فَكَفَّارَتها أنْ يُصَلِّيها إِذَا ذَكَرَهَا ، لاَ كَفَّارَةَ لَهَا إِلاَّ ذَلِكَ)) رواه مسلم
((Atakayesahau Swalaah au ikampita akiwa amelala basi kafara yake ni kuiswali atakapokumbuka, hakuna kafara isipokuwa hiyo)) [Muslim]
Hii ni rahmah ya Allaah kwetu sisi waja kwamba tumepewa udhuru kama huo wa kusahau au kupitiwa na usingizi katika ibaadah muhimu kama hii. Inamaanisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hatukalifishi kwa mambo yanayotushinda nguvu. Na ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipowatakabalia Waumini katika du'aa yao walipomuomba:
لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٢٨٦﴾
Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata (thawabu) iliyoyachuma, na ni dhidi yake (kwa maovu) iliyojichumia. “Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu, Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu, Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Mola Mlinzi wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri. [Al-Baqarah: 286]