03-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Watiifu Wanaume Na Wanawake

 

 Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

03 – Watiifu Wanaume Na Wanawake  

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) :

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Maana ya Qunuwt (kutii) kwa ujumla katika lugha ya  Qur-aan na katika tafsiyr ya Aayah zinazotaja neno hilo ni: Utiifu katika hali ya utulivu.

Kwa ufafanuzi zaidi ni; kukaa kimya na kuleta du'aa, tasbihi, Swalaah, unyenyekevu katika ‘ibaadah khasa kisimamo cha usiku cha Swalaah na kusoma Qur-aan. Ndio maana du'aa katika Swalaah ya mwisho ya usiku ikaitwa  du'aa ya Qunuwt Al-Witr na ambayo inasomwa katika hali ya kusimama. Na pia Hadiyth ifuatayo imethibitisha maana hiyo:

 

 

عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وسلم ((من قام بعشرِ آياتٍ لم يُكتبْ من الغافلينَ ، ومن قام بمئةِ آيةٍ كُتبَ من القانتينَ ومن قام بألفِ آيةٍ كُتبَ من المُقَنْطِرينَ)) صحيح أبي داود  

 

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesimama usiku kuswali na akasoma Aayah kumi, hatoandikiwa kuwa miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah mia, ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah elfu, ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi (ya thawabu).’ [Abuu Daawuwd, Al-Albaaniy ameisahihisha: Swahiyh Abiy Daawuwd (1398), Swahiyh Al-Jaami’ (6439)]

 

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ

Je, yule aliye mtiifu nyakati za usiku akisujudu, au akisimama (kuswali), anatahadhari na Aakhirah na anataraji rahmah ya Rabb wake (ni sawa na aliyekinyume chake?). [Az-Zumar: 9]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ﴿٢٣٨﴾

na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu. [Al-BaqaraH; 238]

 

Maryam mama yake Nabiy ‘Iysaa ‘('Alayhis-Salaam) amepewa sifa hiyo ya kuwa miongoni mwa A-Qaanitiyn katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهِ مِن رُّوحِنَا وَصَدَّقَتْ بِكَلِمَاتِ رَبِّهَا وَكُتُبِهِ وَكَانَتْ مِنَ الْقَانِتِينَ﴿١٢﴾

Na Maryam binti wa ‘Imraan ambaye amehifadhi tupu yake, Tukampulizia humo (katika nguo yake) kupitia kwa Ruwh Wetu (Jibriyl), na akasadikisha Maneno ya Rabb wake, na Vitabu Vyake, na akawa miongoni mwa watiifu na wanyenyekevu. [At-Tahriym: 12]

 

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamumrisha:

 

يَا مَرْيَمُ اقْنُتِي لِرَبِّكِ وَاسْجُدِي وَارْكَعِي مَعَ الرَّاكِعِينَ ﴿٤٣﴾

 “Ee Maryam!  Kuwa mtiifu kwa Rabb wako, na sujudu, na rukuu pamoja na wanaorukuu.” [Al'Imraan: 43]

 

 

Kisa Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa ‘('Alayhis-Salaam) kinachothibitisha sifa yake ya utiifu:

 

 

Hannah bint Faaquwdh alikuwa mke wa Bwana 'Imraan. Imesemekena kwamba alikuwa hakujaaliwa kupata watoto na kwamba siku moja aliona ndege akimlisha kinda chake. Alipoona hivyo akatamani sana kupata mtoto akaomba du'aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amjaalie kizazi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtakabalia du'aa yake akashika mimba. Akaweka nadhiri kumfanya mwanawe awe mwenye kumakinika katika ‘ibaadah na kuihudumia Baytul-Maqdis (Msikiti wa Aqswaa). Hivyo alipotambua kuwa amekwishabeba mimba akaweka hiyo nadhiri. Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِذْ قَالَتِ امْرَأَتُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٥﴾ 

Pale aliposema mke wa ‘Imraan: “Rabb wangu, hakika mimi nimeweka nadhiri Kwako kilichomo katika tumbo langu kuwa ni wakfu kukutumikia, basi nitakabalie. Hakika wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-'Imraan: 35]

 

Kwa maana: Wewe Unasikia du'aa yangu na Unatambua niyyah yangu. Mama yake Maryam hakujua kama atajaaliwa mtoto wa kiume au wa kike. Alipojifungua mtoto wa kike aliona kwamba mwanamke sio kama mwanamume kwa kukusudia katika kujifunga na ‘ibaadah Msikitini. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَلَمَّا وَضَعَتْهَا قَالَتْ رَبِّ إِنِّي وَضَعْتُهَا أُنثَىٰ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا وَضَعَتْ وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنثَىٰ ۖ وَإِنِّي سَمَّيْتُهَا مَرْيَمَ وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴿٣٦﴾

Basi alipomzaa akasema: “Rabb wangu, hakika mimi nimezaa mwanamke,” na Allaah Anajua zaidi alichokizaa. “Na mwanamme si kama mwanamke. Nami nimemwita Mayram nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa. [Al-'Imraan: 36]

 

 

Maana ya Maryam ni 'Mtumishi wa Allaah'.

 

Aayah hiyo inathibitisha kuruhusiwa kumpa jina mtoto siku ile ile anayozaliwa (kama ambavyo imethibiti kumpa jina mtoto katika siku ya saba wakati wa kumfanyia 'Aqiyqah), na vile vile ni dhahiri katika Aayah hii kwamba hii ilikuwa pia ni shariy’ah ya watu waliokuwa kabla yetu.  Na pia iko katika Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 ((وُلِدَ لِي اللَّيْلَةَ وَلَد سَمَّيْتُهُ بِاسْمِ أبِي إبْرَاهِيمَ))

((Usiku huu mtoto (wa kiume) amezaliwa kwangu na nimemwita jina la baba yangu Ibraahiym)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kama Aayah ilivyomalizikia kwamba Bibi Hannah alimuomba  Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amkinge mwanawe na shaytwaan. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtakabalia du'aa yake na dalili ni Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

 ((مَا مِن مَوْلُودٍ يُولَدُ إلا مَسَّه الشَّيْطَانُ حِينَ يُولَدُ، فَيَسْتَهِلّ صَارخًا مِنْ مَسِّهِ إيَّاهُ، إلا مَرْيَم َوابْنَهَا)) ثم يقول أبو هريرة: اقرأوا إن شئتم: (( وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ))

((Hakuna kizazi chochote kinachozaliwa ila shaytwaan anakigusa kinapozaliwa, na mtoto huanza kulia kwa sababu ya kuguswa huko, isipokuwa Maryam na mtoto wake [yaani 'Iysaa ('Alayhis-Salaam)]

 

Abuu Hurayrah kisha akasema someni mkipenda: ((nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa.)) [Aal-‘Imraan: 36] [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Maryam akapelekwa Msikitini tokea utoto wake na akakulia huko na mama yake akamtoa kama ni zawadi ya Baytul-Maqdis.

 

Baada ya kufariki baba yake Maryam, wale waliokuwa na jukumu la kuihudumia Baytul-Maqdis waligombania kumlea Maryam.   Walisema kwamba kwa vile ni mtoto wa Bwana 'Imraan ambaye alikuwa ni Imaam wao basi ni jukumu lao kumlea. Zakariyyah ('Alayhis-Salaam)  naye akadai kumlea Maryam akasema: "Nipeni mimi kwani ndugu wa mama yake ni mke wangu." Wakasema: "Nyoyo zetu hazitopenda umlee wewe kwa sababu ni mtoto wa Imaam wetu." Ikabidi wafanye kura ya kutupa kalamu zao walizokuwa wakiandikia Tawrati katika mto wa Jordan. Yule ambaye kalamu yake itaelea katika mto ndiye atakayemlea Maryam.  Walipozitupa kalamu zao, zote zilizama isipokuwa ya Zakariyyah  ‘('Alayhis-Salaam) ambaye pia naye alikuwa ni bwana wao, Mwanachuoni wao na pia ni Rasuli wa Allaah. 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anakitaja kisa hiki katika Qur-aan kwa Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha Anawatanabahisha makafiri  kwamba hizi ni habari za ghaibu ambazo hakuzijua Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla, kwa maana, haya maelezo ya Qur-aan si maneno ya Rasuli wa Allaah  kama wanavyodai makafiri. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۚ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يُلْقُونَ أَقْلَامَهُمْ أَيُّهُمْ يَكْفُلُ مَرْيَمَ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٤﴾ 

Hizo ni khabari za ghayb Tunakufunulia Wahy (ee Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Na hukuwa pamoja nao walipotupa kalamu zao, ili nani kati yao amlee Maryam. Na hukuwapamoja nao walipokhasimiana. [Al-'Imraan: 44]

 

Basi alipozaliwa Maryam, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alikubali nadhiri ya mama yake Akamjaaliya kuwa na tabia njema na kupata elimu ya Dini yake kutoka kwa Nabiy Zakariyyah ‘('Alayhis-Salaam) hata akawa mtiifu mwenye taqwa ya hali ya juu na akapata sifa ya 'utiifu' kama alivyotajwa katika Aayah hizo za juu. Alikuwa akifanya ‘ibaadah kutwa kucha.    Ikawa kila mara Zakariyyah ‘('Alayhis-Salaam) anapoingia katika mihraab (sehemu yake aliyokuwa akiswalia) anamkuta ana matunda ya ajabu; yaani, pindi ukiwa ni msimu wa baridi anamkuta ana matunda ya msimu wa joto na pindi akiingia msimu wa joto anamkuta ana matunda ya msimu wa baridi, ndipo alipomuuliza kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا ۖ كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِندَهَا رِزْقًا ۖقَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّىٰ لَكِ هَـٰذَا ۖ قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٧﴾ 

Basi Rabb wake Akampokea kwa kabuli njema na Akamkuza mkuzo mzuri na Akamfanya Zakariyyaa kuwa mlezi wake. Kila Zakariyyaa alipoingia kwake katika chumba cha kuswalia alikuta kwake kuna riziki Akasema: “Ee Maryam! Umepata wapi hivi? ”Akasema: “Hivi ni kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah Anamruzuku Amtakaye bila ya hesabu.” [Al-'Imraan: 37]

 

[Kisa kama kilivyonukuliwa katika tafsiyr ya Ibn Kathiyr]

 

Na Maryam mama yake Nabiy ‘Iysaa ‘('Alayhis-Salaam) ni miongoni mwa wanawake walio bora kabisa kama alivyotujulisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:

 

عن أبي موسى الأشعري قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم  ((كَمُلَ مِنَ الرِّجَالِ كَثِيرٌ وَلَمْ يَكْمُلْ مِنَ النِّسَاءِ إِلا مَرْيَمُ بِنْتُ عِمْرَانَ وَآسِيَةُ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ"))

 

 وقد أخرجه الجماعة إلا أبا داود  ولفظ البخاري:

((كَمُلَ مِنَ الرِّجَالِ كَثِيرٌ وَلَمْ يَكْمُلْ مِنَ النِّسَاءِ إِلا آسِيَةُ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ، وَمَرْيَمُ بِنْتُ عِمْرَانَ ، وَإنَّ فَضْلَ عَائِشَةَ عَلَى النِّسَاءِ كَفَضْلِ الثَّرِيدِ عَلَى سَائِرِ الطَّعَامِ)).

Kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash'ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)     amesema: ((Wanaume wamepata ukamilifu, na hawakukamilika wanawake ila  Maryam bint 'Imraan na Aasiyah mke wa Fir'awn)) [Imesimuliwa na wote isipokuwa Abu Daawuwd.

 

Na katika usemi wa Al-Bukhaariy]:

 

((Wanaume wengi wamefikia daraja ya ukamilifu lakini hakuna mwanamke aliyefikia daraja hiyo isipokuwa Aasiyah mke wa Fir'awn, na Maryam bint 'Imraan. Na ubora wa 'Aishah (mke wake) kwa wanawake wengine ni kama mfano wa ubora wa thariyd (chakula cha mchuzi wa nyama na mkate) kwa vyakula vingine))  

 

 

Share