027 - An-Naml

 

  النَّمْل

 

027-An-Naml 

 

027-An-Naml: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

طس ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْقُرْآنِ وَكِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿١﴾

1.     Twaa Siyn.[1] Hizi ni Aayaat za Qur-aan na Kitabu bainifu.

 

 

 

هُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٢﴾

2.  Ni mwongozo na bishara kwa Waumini. 

 

 

 

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ ﴿٣﴾

3. Ambao wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah, nao kuhusu Aakhirah ni wenye yakini nayo.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ زَيَّنَّا لَهُمْ أَعْمَالَهُمْ فَهُمْ يَعْمَهُونَ ﴿٤﴾

4. Hakika wale wasioiamini Aakhirah Tumewapambia amali zao, basi wao wanatangatanga kwa upofu.

 

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَهُمْ سُوءُ الْعَذَابِ وَهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْأَخْسَرُونَ ﴿٥﴾

5. Hao ni wale ambao watapata adhabu mbaya kabisa, nao katika Aakhirah ndio wenye kukhasirika zaidi.

 

 

 

وَإِنَّكَ لَتُلَقَّى الْقُرْآنَ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ عَلِيمٍ ﴿٦﴾

6. Na hakika wewe unaletewa Qur-aan kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

إِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِأَهْلِهِ إِنِّي آنَسْتُ نَارًا سَآتِيكُم مِّنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ آتِيكُم بِشِهَابٍ قَبَسٍ لَّعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ ﴿٧﴾

7. (Kumbuka) pale Muwsaa alipowaambia ahli yake: Hakika mimi nimeona moto, nitakuleteeni kutoka upande wake khabari, au nitakuleteeni kijinga kinachowaka ili mpate kuota moto.

 

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَهَا نُودِيَ أَن بُورِكَ مَن فِي النَّارِ وَمَنْ حَوْلَهَا وَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨﴾

8. Basi alipoujia, ilinadiwa kwamba: Amebarikiwa aliye karibu na moto, na aliye pembezoni mwake. Na Utakasifu ni wa Allaah Rabb wa walimwengu.

 

 

 

يَا مُوسَىٰ إِنَّهُ أَنَا اللَّـهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٩﴾

9. Ee Muwsaa! Hakika Ni Mimi Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

  

وَأَلْقِ عَصَاكَ ۚ فَلَمَّا رَآهَا تَهْتَزُّ كَأَنَّهَا جَانٌّ وَلَّىٰ مُدْبِرًا وَلَمْ يُعَقِّبْ ۚ يَا مُوسَىٰ لَا تَخَفْ إِنِّي لَا يَخَافُ لَدَيَّ الْمُرْسَلُونَ ﴿١٠﴾

10. Na tupa fimbo yako. Basi alipoiona inataharuki kama kwamba ni nyoka, aligeuka nyuma kukimbia na wala hakurudi. Ee Muwsaa! Usikhofu. Hakika Mimi hawakhofu Mbele Yangu Rusuli.

 

 

 

إِلَّا مَن ظَلَمَ ثُمَّ بَدَّلَ حُسْنًا بَعْدَ سُوءٍ فَإِنِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١﴾

11. Isipokuwa yule aliyedhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya uovu, basi hakika Mimi Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَأَدْخِلْ يَدَكَ فِي جَيْبِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاءَ مِنْ غَيْرِ سُوءٍ ۖ فِي تِسْعِ آيَاتٍ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَقَوْمِهِ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿١٢﴾

12. Na ingiza mkono wako katika uwazi wa nguo yako kifuani, utatoka kuwa mweupe bila ya dhara yoyote. Ni miongoni mwa Aayaat (Ishara, Miujiza) tisa[2] kwa Firawni na watu wake. Hakika wao wamekuwa ni watu mafasiki.

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ آيَاتُنَا مُبْصِرَةً قَالُوا هَـٰذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿١٣﴾

13. Basi ilipowajia Aayaat (Ishara, Miujiza) Yetu yenye kuonekana wazi, wakasema: Hii ni sihiri bayana.

 

 

 

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٤﴾

14. Wakaikanusha kwa dhulma na majivuno na hali kuwa nafsi zao zimeiyakinisha. Basi tazama vipi ilikuwa hatima ya mafisadi.

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ عِلْمًا ۖ وَقَالَا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي فَضَّلَنَا عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّنْ عِبَادِهِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٥﴾

15. Na kwa yakini Tulimpa Daawuwd na Sulaymaan ilimu. Wakasema: AlhamduliLLaahi (Himidi Anastahiki Allaah) Ambaye Ametufadhilisha kuliko wengi katika Waja Wake Waumini.

 

 

 

وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ ۖ وَقَالَ يَا أَيُّهَا النَّاسُ عُلِّمْنَا مَنطِقَ الطَّيْرِ وَأُوتِينَا مِن كُلِّ شَيْءٍ ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْفَضْلُ الْمُبِينُ ﴿١٦﴾

16. Na Sulaymaan alimrithi Daawuwd, akasema: Enyi watu! Tumefunzwa lugha ya ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii bila shaka ndio fadhila bayana.

 

 

 

وَحُشِرَ لِسُلَيْمَانَ جُنُودُهُ مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ وَالطَّيْرِ فَهُمْ يُوزَعُونَ ﴿١٧﴾

17. Na alikusanyiwa Sulaymaan majeshi yake miongoni mwa majini na wanaadam na ndege, nao wamedhibitiwa kwa mpango kabambe.

 

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا أَتَوْا عَلَىٰ وَادِ النَّمْلِ قَالَتْ نَمْلَةٌ يَا أَيُّهَا النَّمْلُ ادْخُلُوا مَسَاكِنَكُمْ لَا يَحْطِمَنَّكُمْ سُلَيْمَانُ وَجُنُودُهُ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١٨﴾

18. Mpaka walipofika kwenye bonde la sisimizi, akasema sisimizi mmoja: Enyi sisimizi! Ingieni masikanini mwenu, asikupondeni Sulaymaan na majeshi yake, na hali wao hawahisi.

 

 

 

 

فَتَبَسَّمَ ضَاحِكًا مِّن قَوْلِهَا وَقَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَدْخِلْنِي بِرَحْمَتِكَ فِي عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ ﴿١٩﴾

19. (Sulaymaan) akatabasamu kuchekea kauli yake, akasema: Rabb wangu! Nipe ilhamu na uwezo nishukuru Neema Yako ambayo Umenineemesha juu yangu na wazazi wangu, na nipate kutenda mema Utakayoridhia, na Niingize kwa Rehma Yako katika Waja Wako Swalihina.

 

 

 

وَتَفَقَّدَ الطَّيْرَ فَقَالَ مَا لِيَ لَا أَرَى الْهُدْهُدَ أَمْ كَانَ مِنَ الْغَائِبِينَ ﴿٢٠﴾

20. Akakagua ndege, akasema: Imekuwaje, mbona simuoni al-hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walioghibu?[3]

 

 

 

لَأُعَذِّبَنَّهُ عَذَابًا شَدِيدًا أَوْ لَأَذْبَحَنَّهُ أَوْ لَيَأْتِيَنِّي بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٢١﴾

21. Bila shaka nitamuadhibu adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee hoja bayana.

 

 

 

فَمَكَثَ غَيْرَ بَعِيدٍ فَقَالَ أَحَطتُ بِمَا لَمْ تُحِطْ بِهِ وَجِئْتُكَ مِن سَبَإٍ بِنَبَإٍ يَقِينٍ ﴿٢٢﴾

22. Basi (hud-hud) hakukaa kitambo kirefu, akasema: Nimegundua ambayo wewe hukuyagundua na nimekujia kutoka Saba-a na khabari za yakini.

 

 

 

إِنِّي وَجَدتُّ امْرَأَةً تَمْلِكُهُمْ وَأُوتِيَتْ مِن كُلِّ شَيْءٍ وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ ﴿٢٣﴾

23. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, na amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa mno.

 

 

 

وَجَدتُّهَا وَقَوْمَهَا يَسْجُدُونَ لِلشَّمْسِ مِن دُونِ اللَّـهِ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ فَهُمْ لَا يَهْتَدُونَ ﴿٢٤﴾  

24. Nimemkuta na watu wake wanalisujudia jua badala ya Allaah, na shaytwaan amewapambia amali zao na akawazuia na njia, kwa hiyo hawaioni njia (ya haki).

 

 

 

أَلَّا يَسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي يُخْرِجُ الْخَبْءَ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُخْفُونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ﴿٢٥﴾

25. Na ili wasimsujudie Allaah Ambaye Anatoa yenye kufichika katika mbingu na ardhi, na Anayajua yale mnayoyaficha na yale mnayoyadhihirisha.

 

 

 

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ۩﴿٢٦﴾

26. Allaah hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa ‘Arsh Adhimu.

 

 

 

قَالَ سَنَنظُرُ أَصَدَقْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٢٧﴾

27. (Sulaymaan) akasema: Tutaona, kama umesema kweli, au ulikuwa miongoni mwa waongo?

 

 

 

اذْهَب بِّكِتَابِي هَـٰذَا فَأَلْقِهْ إِلَيْهِمْ ثُمَّ تَوَلَّ عَنْهُمْ فَانظُرْ مَاذَا يَرْجِعُونَ ﴿٢٨﴾

28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha ujitenge nao utazame watarudisha nini.

 

 

 

قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ إِنِّي أُلْقِيَ إِلَيَّ كِتَابٌ كَرِيمٌ ﴿٢٩﴾

29. (Malkia) akasema: Enyi wakuu! Hakika nimeletewa barua tukufu.

 

 

 

إِنَّهُ مِن سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣٠﴾

30. Hakika inatoka kwa Sulaymaan, na hakika (imeanza) Kwa Jina la Allaah, Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu.[4]

 

 

 

أَلَّا تَعْلُوا عَلَيَّ وَأْتُونِي مُسْلِمِينَ ﴿٣١﴾

31. Msinifanyie jeuri, na nijieni mkiwa mmesilimu.

 

 

 

قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي أَمْرِي مَا كُنتُ قَاطِعَةً أَمْرًا حَتَّىٰ تَشْهَدُونِ ﴿٣٢﴾

32. (Malkia) akasema: Enyi wakuu! Nipeni shauri katika jambo langu, maana sikuwa mwenye kuamua jambo mpaka mhudhurie nami.

 

 

 

قَالُوا نَحْنُ أُولُو قُوَّةٍ وَأُولُو بَأْسٍ شَدِيدٍ وَالْأَمْرُ إِلَيْكِ فَانظُرِي مَاذَا تَأْمُرِينَ ﴿٣٣﴾

33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu, na wenye uwezo mkali wa vita, na amri iko kwako, basi tazama unaamrisha nini?

 

 

 

قَالَتْ إِنَّ الْمُلُوكَ إِذَا دَخَلُوا قَرْيَةً أَفْسَدُوهَا وَجَعَلُوا أَعِزَّةَ أَهْلِهَا أَذِلَّةً ۖ وَكَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ ﴿٣٤﴾

34. Akasema: Hakika wafalme wanapoingia mji huufisidi, na huwafanya watukufu wake kuwa dhalili, na hivyo ndivyo wafanyavyo.

 

 

 

وَإِنِّي مُرْسِلَةٌ إِلَيْهِم بِهَدِيَّةٍ فَنَاظِرَةٌ بِمَ يَرْجِعُ الْمُرْسَلُونَ ﴿٣٥﴾

35. Nami nitawapelekea hadiya, kisha nitangojea kutazama watakayorudi nayo wajumbe.

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَ سُلَيْمَانَ قَالَ أَتُمِدُّونَنِ بِمَالٍ فَمَا آتَانِيَ اللَّـهُ خَيْرٌ مِّمَّا آتَاكُم بَلْ أَنتُم بِهَدِيَّتِكُمْ تَفْرَحُونَ ﴿٣٦﴾

36. Basi alipomjia (mjumbe) Sulaymaan, alisema: Je, mnanisaidia kwa mali? Basi Aliyonipa Allaah ni bora kuliko Aliyokupeni nyinyi, bali nyinyi mnafurahia hadiya yenu.

 

 

 

ارْجِعْ إِلَيْهِمْ فَلَنَأْتِيَنَّهُم بِجُنُودٍ لَّا قِبَلَ لَهُم بِهَا وَلَنُخْرِجَنَّهُم مِّنْهَا أَذِلَّةً وَهُمْ صَاغِرُونَ ﴿٣٧﴾

37. Rudi kwao. Bila shaka tutawaendea kwa jeshi wasiloweza kukabiliana nalo, na bila shaka tutawatoa humo hali ya kuwa wamedhalilika na walio duni.

 

 

 

قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَن يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ ﴿٣٨﴾

38. Akasema: Enyi wakuu! Nani kati yenu ataniletea kiti chake cha enzi kabla hawakunijia wakiwa wamesilimu?

 

 

 

قَالَ عِفْرِيتٌ مِّنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن تَقُومَ مِن مَّقَامِكَ ۖ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ ﴿٣٩﴾

39. Akasema ‘Ifriti miongoni mwa majini: Mimi nitakuletea kabla hujasimama kutoka mahali pako, na hakika mimi kwa hilo, bila shaka ni mwenye nguvu mwaminifu.

 

 

 

قَالَ الَّذِي عِندَهُ عِلْمٌ مِّنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ ۚ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِندَهُ قَالَ هَـٰذَا مِن فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ ۖ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Akasema yule ambaye ana ilimu[5] kutoka katika Kitabu: Mimi nitakuletea kabla halijapepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, (Sulaymaan) alisema: Hii ni katika Fadhila za Rabb wangu, Anijaribu; je, nitashukuru, au nitakufuru. Na yeyote yule anayeshukuru, basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na yeyote yule asiyekuwa na shukurani, basi hakika Rabb wangu ni Mkwasi, Mkarimu.

 

 

 

قَالَ نَكِّرُوا لَهَا عَرْشَهَا نَنظُرْ أَتَهْتَدِي أَمْ تَكُونُ مِنَ الَّذِينَ لَا يَهْتَدُونَ ﴿٤١﴾

41. (Sulaymaan) akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi tutazame, ataongoka au atakuwa miongoni mwa ambao wasioongoka.

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَتْ قِيلَ أَهَـٰكَذَا عَرْشُكِ ۖ قَالَتْ كَأَنَّهُ هُوَ ۚ وَأُوتِينَا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهَا وَكُنَّا مُسْلِمِينَ ﴿٤٢﴾

42. Basi (Malkia) alipokuja, ikasemwa: Je, ni kama hiki kiti chako cha enzi? Akasema: Kama ndicho hicho. (Sulaymaan akasema): Na tumepewa ilimu kabla yake na tukawa Waislamu.

 

 

 

وَصَدَّهَا مَا كَانَت تَّعْبُدُ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهَا كَانَتْ مِن قَوْمٍ كَافِرِينَ ﴿٤٣﴾

43. Na yale aliyokuwa akiyaabudu badala ya Allaah yalimzuia (Uislamu). Hakika alikuwa miongoni mwa watu makafiri.

 

 

 

قِيلَ لَهَا ادْخُلِي الصَّرْحَ ۖ فَلَمَّا رَأَتْهُ حَسِبَتْهُ لُجَّةً وَكَشَفَتْ عَن سَاقَيْهَا ۚ قَالَ إِنَّهُ صَرْحٌ مُّمَرَّدٌ مِّن قَوَارِيرَ ۗ قَالَتْ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي وَأَسْلَمْتُ مَعَ سُلَيْمَانَ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٤﴾

44. Akaambiwa: Ingia katika kasri la fakhari. Alipoliona alilidhania ni bwawa refu la maji, akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaymaan) akasema: Hakika hilo ni kasri la fakhari lilosakafiwa kwa vigae. (Malkia) akasema: Rabb wangu! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na nimesilimu pamoja na Sulaymaan kwa Allaah Rabb wa walimwengu.

 

 

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ فَإِذَا هُمْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٥﴾

45. Na kwa yakini Tuliwapelekea kina Thamuwd ndugu yao Swaalih kwamba: Mwabuduni Allaah. Tahamaki wakawa makundi mawili yanayogombana.

 

 

 

قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ ۖ لَوْلَا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٤٦﴾

46. (Swaalih) akasema: Enyi kaumu yangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya mema? Kwa nini msimwombe Allaah maghfirah ili huenda mkarehemewa?

 

 

 

قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ ۚ قَالَ طَائِرُكُمْ عِندَ اللَّـهِ ۖ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تُفْتَنُونَ ﴿٤٧﴾

47. Wakasema: Tumepata nuksi kwa sababu yako na kwa wale walio pamoja nawe. (Swaalih) akasema: Nuksi yenu iko kwa Allaah. Bali nyinyi ni watu mliojaribiwa.

 

 

 

وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ ﴿٤٨﴾

48. Na kulikuweko katika mji ule watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi na wala hawafanyi yenye manufaa.

 

 

 

قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّـهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٤٩﴾

49. Wakasema: Apishaneni kwa Jina la Allaah kwamba tutamhujumu (Swaalih) kwa siri usiku na ahli yake, kisha tutasema kwa jamaa yake wa karibu: Hatukushuhudia maangamizi ya ahli yake, nasi hakika ni wakweli.

 

 

 

وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٥٠﴾

50. Wakapanga makri (njama). Nasi Tukapanga mipango ya kuvurumisha makri, nao huku hawatambui. 

 

 

 

فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥١﴾

51. Basi tazama vipi ilikuwa hatima ya njama zao, kwamba Tuliwadamirisha na watu wao wote.

 

 

 

فَتِلْكَ بُيُوتُهُمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَمُوا ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٥٢﴾

52. Basi hizo ni nyumba zao zimebakia magofu kwa sababu ya

walivyodhulumu. Hakika katika hayo kuna Aayah (Ishara, Mazingatio) kwa watu wanaojua.

 

 

 

وَأَنجَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٥٣﴾

53. Na Tukawaokoa wale walioamini, na waliokuwa na taqwa.

 

 

 

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ وَأَنتُمْ تُبْصِرُونَ ﴿٥٤﴾

54. Na (kumbuka) Luutw alipowaambia watu wake: Je, mnafanya machafu na hali nyinyi mnaona?

 

 

 

أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِّن دُونِ النِّسَاءِ ۚ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ ﴿٥٥﴾

55. Je, nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake?! Bali nyinyi ni watu majahili.

 

 

 

فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا أَخْرِجُوا آلَ لُوطٍ مِّن قَرْيَتِكُمْ ۖ إِنَّهُمْ أُنَاسٌ يَتَطَهَّرُونَ ﴿٥٦﴾

56. Basi halikuwa jawabu la watu wake isipokuwa kusema: Watoeni watu wa Luutw kutoka mji wenu, hakika wao ni watu wanaojiweka katika utakaso.

 

 

 

فَأَنجَيْنَاهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَاهَا مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٥٧﴾

57. Basi Tulimuokoa na ahli yake isipokuwa mke wake, Tulimkadiria miongoni mwa watakaobakia nyuma.

 

 

 

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا ۖ فَسَاءَ مَطَرُ الْمُنذَرِينَ ﴿٥٨﴾

58. Na Tukawanyeshea mvua. Basi uovu ulioje mvua ya walioonywa!

 

 

 

قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ وَسَلَامٌ عَلَىٰ عِبَادِهِ الَّذِينَ اصْطَفَىٰ ۗ آللَّـهُ خَيْرٌ أَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٥٩﴾

59. Sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) na amani iwe juu ya Waja Wake Aliowakhitari. Je, Allaah Ni bora au wale wanaowashirikisha (Naye)?

 

 

 

أَمَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا بِهِ حَدَائِقَ ذَاتَ بَهْجَةٍ مَّا كَانَ لَكُمْ أَن تُنبِتُوا شَجَرَهَا ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ يَعْدِلُونَ ﴿٦٠﴾

60. Au nani Aliyeumba mbingu na ardhi, na Akakuteremshieni kutoka mbinguni maji, kisha Tukaotesha kwayo mabustani anisi ya kupendeza kabisa? Nyinyi hamna uwezo wa kuotesha miti yake. Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Bali wao ni watu wanaomfanya Allaah sawa na viabudiwa vyao. (wanaoikengeuka haki).[6]

 

 

 

أَمَّن جَعَلَ الْأَرْضَ قَرَارًا وَجَعَلَ خِلَالَهَا أَنْهَارًا وَجَعَلَ لَهَا رَوَاسِيَ وَجَعَلَ بَيْنَ الْبَحْرَيْنِ حَاجِزًا ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٦١﴾

61. Au nani Aliyeijaalia ardhi kuwa mahali pa matulio, na Akajaalia baina yake mito, na Akaiwekea milima mirefu thabiti, na Akajaalia baina ya bahari mbili (ya chumvi na tamu) kizuizi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Bali wengi wao hawajui.

 

 

 

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

62. Au nani Anayemuitika mwenye dhiki mno anapomwomba, na Akamuondoshea uovu na Akakufanyeni warithi wa ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka.

 

 

 

أَمَّن يَهْدِيكُمْ فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَن يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ تعَالَى اللَّـهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٦٣﴾

63. Au nani Anayekuongozeni katika viza vya nchi kavu na bahari? Na nani Anayetuma pepo za kheri na za bishara kabla ya Rehma Yake?  Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Ametukuka Allaah kutokana na yale wanayomshirikisha.

 

 

 

أَمَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَمَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٦٤﴾

64. Au nani Anayeanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha? Na nani Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Sema: Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli.

 

 

 

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ ﴿٦٥﴾

65. Sema: Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye ghaibu[7] isipokuwa Allaah. Na wala hawatambui lini watafufuliwa.

 

 

 

بَلِ ادَّارَكَ عِلْمُهُمْ فِي الْآخِرَةِ ۚ بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ مِّنْهَا ۖ بَلْ هُم مِّنْهَا عَمُونَ ﴿٦٦﴾

66. Bali umefikia kikomo ujuzi wao kuhusu Aakhirah. Bali wao wamo katika shaka nayo. Bali wao ni vipofu nayo.

 

 

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا وَآبَاؤُنَا أَئِنَّا لَمُخْرَجُونَ ﴿٦٧﴾

67. Na wale waliokufuru wakasema: Je, tukiwa mchanga na baba zetu, hivi sisi kweli tutakuja kutolewa?[8]

 

 

 

لَقَدْ وُعِدْنَا هَـٰذَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا مِن قَبْلُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٦٨﴾

68. Tumekwishaahidiwa haya sisi na baba zetu hapo kabla. Haya si chochote isipokuwa ni hekaya za watu wa kale.

 

 

 

قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُجْرِمِينَ ﴿٦٩﴾

69. Sema: Tembeeni katika ardhi kisha mtazame vipi ilikuwa hatima ya wahalifu.[9]

 

 

 

وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُن فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ ﴿٧٠﴾

70. Na wala usihuzunike juu yao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na wala usiwe katika dhiki kutokana na njama wazipangazo.

 

 

 

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٧١﴾

71. Na wanasema: Ni lini hiyo ahadi mkiwa ni wakweli?[10]

 

 

 

قُلْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ رَدِفَ لَكُم بَعْضُ الَّذِي تَسْتَعْجِلُونَ ﴿٧٢﴾

72. Sema: Asaa yawe yamekurubia nyuma yenu baadhi ya mnayoyahimiza.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَشْكُرُونَ ﴿٧٣﴾

73. Na hakika Rabb wako Ni Mwenye Fadhila kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَيَعْلَمُ مَا تُكِنُّ صُدُورُهُمْ وَمَا يُعْلِنُونَ ﴿٧٤﴾

74. Na hakika Rabb wako bila shaka Anajua yale yanayofichwa na vifua vyao na yale wanayoyatangaza.

 

 

 

وَمَا مِنْ غَائِبَةٍ فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٧٥﴾

75.  Na hakuna chochote cha ghaibu katika mbingu na ardhi isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha.

 

 

 

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَقُصُّ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَكْثَرَ الَّذِي هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٧٦﴾

76. Hakika hii Qur-aan inawasimulia wana wa Israaiyl mengi zaidi ambayo wao wanakhitilafiana nayo.

 

 

 

وَإِنَّهُ لَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾

77. Nayo hakika ni mwongozo na rehma kwa Waumini.

 

 

 

إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُم بِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ ﴿٧٨﴾

78. Hakika Rabb wako Atahukumu baina yao kwa Hukumu Yake. Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.

 

 

 

فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۖ إِنَّكَ عَلَى الْحَقِّ الْمُبِينِ ﴿٧٩﴾

79. Basi tawakali kwa Allaah. Hakika wewe uko kwenye haki bayana.

 

 

 

إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ ﴿٨٠﴾

80. Hakika wewe huwezi kusikilizisha wafu, na wala huwezi kusikilizisha viziwi wito wanapokengeuka wakigeuza migongo yao.[11]

 

 

 

وَمَا أَنتَ بِهَادِي الْعُمْيِ عَن ضَلَالَتِهِمْ ۖ إِن تُسْمِعُ إِلَّا مَن يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا فَهُم مُّسْلِمُونَ ﴿٨١﴾

81. Na wala wewe huwezi kuwaongoa vipofu kutoka upotofu wao. Huwasikilizishi isipokuwa wale wanaoamini Aayaat Zetu, nao ndio wanaojisalimisha (kuwa Waislamu).

 

 

 

 

وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na itakapotimizwa kauli dhidi yao, Tutawatolea mnyama atembeaye katika ardhi atakayewasemezesha kwa sababu watu walikuwa hawana yakini na Aayaat (na Ishara) Zetu.[12]

 

 

 

وَيَوْمَ نَحْشُرُ مِن كُلِّ أُمَّةٍ فَوْجًا مِّمَّن يُكَذِّبُ بِآيَاتِنَا فَهُمْ يُوزَعُونَ ﴿٨٣﴾

83. Na Siku Tutakayokusanya katika kila Ummah makundi miongoni mwa wale wanaokadhibisha Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) Zetu nao watakusanywa waburuzwe.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوا قَالَ أَكَذَّبْتُم بِآيَاتِي وَلَمْ تُحِيطُوا بِهَا عِلْمًا أَمَّاذَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨٤﴾

84. Mpaka watakapokuja, Allaah) Atasema: Je, si mlikadhibisha Aayaat (na Ishara, Dalili, Hoja) Zangu bila ya kuzijua vyema? Au mlikuwa mnafanya nini?

 

 

 

وَوَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِم بِمَا ظَلَمُوا فَهُمْ لَا يَنطِقُونَ ﴿٨٥﴾

85. Na itatimizwa kauli dhidi yao kwa sababu ya kufanya kwao dhulma, nao hawatoweza kutamka lolote.

 

 

 

أَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا اللَّيْلَ لِيَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٨٦﴾

86. Je, hawaoni kwamba Tumejaalia usiku ili wapate utulivu humo, na mchana wenye kuangaza? Hakika katika hayo bila shaka mna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa watu wanaoamini.

 

 

 

وَيَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ ﴿٨٧﴾

87. Na Siku litakapopulizwa baragumu, watakufa kwa mshtuko waliomo mbinguni na waliomo ardhini isipokuwa Amtakaye Allaah.[13] Na wote watamfikia wakiwa duni wamedhalilika.

 

 

 

وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ ۚ صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ ۚ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾

88. Na unaona milima unaidhania imetulia thabiti nayo inapita mpito wa mawingu. Utengenezaji wa Allaah Ambaye Ametengeneza kwa umahiri kila kitu. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myafanyayo.

 

 

 

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ ﴿٨٩﴾ ﴾

89. Atakayekuja na jema, basi atapata bora zaidi kuliko hilo, nao watakuwa katika amani na mafazaiko (kifo cha mshtuko) Siku hiyo.

 

 

 

وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَكُبَّتْ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٩٠﴾

90. Na atakayekuja na ovu, basi zitatupwa gubigubi nyuso zao katika moto (wataambiwa): Je, kwani mnalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda?

 

 

 

إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَـٰذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٩١﴾

91. Hakika nimeamrishwa nimwabudu Rabb wa mji huu (wa Makkah) Ambaye Ameufanya mtukufu, na Ni Vyake Pekee vitu vyote. Na nimeamrishwa kwamba niwe miongoni mwa Waislamu.

 

 

 

وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴿٩٢﴾

92. Na kwamba nisome Qur-aan. Hivyo anayehidika, basi hakika anahidika kwa ajili ya manufaa ya nafsi yake. Na anayepotoka, basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji.

 

 

 

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ سَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَتَعْرِفُونَهَا ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾

93. Na sema: AlhamduliLLaahi (Himidi Anastahiki Allaah) Atakuonyesheni Aayaat (Ishara, Dalili) Zake na mtazitambua. Na Rabb wako Si Mwenye Kughafilika na yale wanayoyatenda.

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Aayaat (Ishara, Miujiza) Tisa Ya Allaah Kwa Watu Wa Firawni: Rejea Al-A’raaf (7:130), (133).

 

[3] Hud-hud:

 

Ni ndege wenye vishungi, wenye manyoa ya rangi ya samaki wa samoni. Kupitia ndege huyu, katika kisa chake hiki na Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام), umedhihirika muujiza na Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba ndege mdogo ameweza kusafiri hadi mji mwengine wa mbali, akakuta watu wanamshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى), naye akakanusha hilo na akataka kuthitibisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى). Amedhihirika kuwa ni ndege mwerevu, mwenye busara na aliyelingania Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kukanusha shirki zao za kuabudu jua. Na hatimaye, ndege huyu hud-hud, akawa ni sababu ya Malkia wa Saba-a kusilimu na kuingia katika Uislamu.   

 

[4] Kuanza Kusoma Qur-aan Kwa Basmalah:

 

 Mtu anapotaka kuanza kusoma Suwrah yoyote ile ya Qur-aan anapaswa aanze kwa

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu).

 

Lakini kabla ya Basmalah, aanze kwa Isti’aadhah, yaani kuomba kinga (dhidi ya shaytwaan) ambayo ni kusema:

أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْـطانِ الرَّجيـم

Najikinga kwa Allaah kutokana na shaytwaan aliyeepushwa na kuwekwa mbali na Rehma za Allaah.

Rejea An-Nahl (16:98).

 

Hivyo basi kuanzwa kusoma Qur-aan kwa kuanza kwa Basmalah:

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

kunapatikana baraka katika kisomo cha Qur-aan na kumtegemea Allaah (سبحانه وتعالى) na kutaqabaliwa amali hii ya kusoma Qur-aan. Na sehemu nyengineyo inayopasa kutamkwa kikamilifu ni katika kuandika barua. Ama katika kuanza kufanya jambo lolote jengine, ili kupata baraka au kujikinga na shaytwaan, basi ni kuanza kwa tasmiyah (ambayo ni):

بِسْمِ اللَّـهِ

Lakini itambulike kuwa, kuanza kwa Basmalah ni katika Suwrah zote isipokuwa Suwrah At-Tawbah, haijuzu kuanza kwa Basmalah. Rejea At-Tawbah (9) ambako kuna maelezo bayana ya sababu ya kukatazwa kuanzia Suwrah hii kwa Basmalah.

 

[5] Mwenye Ilimu:

 

Wafasiri wa Qur-aan wamesema kuwa aliyekusudiwa kuwa mwenye ilimu, anaitwa Aaswif Bin Barkhiyaa. Alikuwa mwanachuoni mwema enzi ya Nabiy Sulaymaan, na alikuwa anajua Jina Tukufu kabisa la Allaah Ambalo Kwalo akimwomba Allaah jambo lolote Humwitikia na kumpa. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[6] Miongoni Mwa Neema Za Allaah (سبحانه وتعالى) Na Uwezo Wake Na Uthibitisho Wa Tawhiyd Ya Allaah:

 

Kuanzia Aayah hii hadi namba (65), Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja miongoni mwa Neema Zake na Uwezo Wake, na uthibitisho wa Tawhiyd Yake ya Ar-Rubuwbiyyah (Urabb) na Al-Uluwhiyyah (Uilahi). 

 

[7] Hakuna Ajuaye Ghaibu Ya Yaliyoko Mbinguni Na Ardhini:

 

Ghaibu ni ilimu ya mambo asiyoyajua mtu isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:3), Luqmaan (31:34), Al-An’aam (6.59).

 

Hakuna ajuaye yaliyoko mbinguni wala katika ardhi. Haya yamo katika  Ujuzi wa Allaah (سبحانه وتعالى). Wala watu hawajui lini watafufuliwa kutoka makaburini mwao kitakaposimama Qiyaamah. Bali watakijua na kukishuhudia Qiyaamah huko Aakhirah (watakapofufuliwa). Huko watakuwa na yakini juu ya Nyumba ya Aakhirah na vitisho vilivyomo watakaposhuhudia (matukio). Na wao walipokuwa duniani walikuwa na shaka nayo, bali akili zao zilikuwa zimepofuka hawaoni (wala hawaamini). [At-Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[8] Makafiri Hawakuamini Kufufuliwa:

 

Rejea Al-Muuminuwn (23:35-36), pia Rejea Al-Israa (17: 49) ambako kuna maelezo bayana.

 

[9] Watembee Katika Ardhi Watambue Adhabu Zilizowafika Waliokadhibisha Na Hatima Zao.

 

Rejea Faatwir (35:43-44), Al-An’aam (6:11), Yuwsuf (12:109), Al-Kahf (18:55) na Al-Hajj (22:46).

 

[10] Ada ya Makafiri Kutokuamini Saa (Qiyaamah) Na Kutokuamini Kuwateremkia Adhabu:

 

Rejea Al-An’aam (6:158), Al-Ahzaab (33:63), An-Naazi’aat (79:42),  Al-Mulk (67:25), Al-A’raaf (7:187), Ash-Shuwraa (42:18). Na hawakuamini pia kama adhabu ya Allaah (سبحانه وتعالى) itawateremkia wakawa wanaihimizia. Rejea Al-Hajj (22:47), Al-Anfaal (8:32), Swaad (38:16).

 

[11] Wafu, Viziwi:

 

Hakika yako ee Rasuli! Huwezi kumsikilizisha haki yule ambaye Allaah Amepiga mhuri juu ya moyo wake Akaufisha. Nahumsikilizishi daawah (ulinganizi) yako yule ambaye Allaah Ameyafanya masikizi yake kuwa kiziwi asiisikie haki, pindi wanapogeuka kukupa mgongo wewe. Kwani kiziwi hasikii daawah akiwa amekuelekea, basi itakuwa vipi akiwa katika hali ya kukupa mgongo na kugeuka?! [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[12] Mnyama Atakayewasemezesha Watu Ni Katika Alama Kuu Za Qiyaamah:

 

Rejea Al-An’aam (6:158) kumetajwa alama kumi kuu za Qiyaamah, miongoni mwazo ni mnyama atakayewasemezesha watu.

 

[13] Malaika Israafiyl Amewakilishwa Kupuliza Baragumu Na Watakaosalimika Na Mfazaiko (Kifo Cha Mshtuko):

 

وعن أَبي سعيد الخدري رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( كَيْفَ أنْعَمُ ! وَصَاحِبُ القَرْنِ قَدِ التَقَمَ القَرْنَ ، وَاسْتَمَعَ الإذْنَ مَتَى يُؤمَرُ بالنَّفْخِ فَيَنْفُخُ )) فَكَأنَّ ذلِكَ ثَقُلَ عَلَى أصْحَابِ رسولِ الله صلى الله عليه وسلم فَقَالَ لَهُمْ : (( قُولُوا : حَسْبُنَا الله وَنِعْمَ الوَكِيلُ )) رواه الترمذي ، وَقالَ : (( حديث حسنٌ )) .

Amesimulia Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Vipi nitakuwa na furaha na mwenye baragumu (Malaika Israafiyl) ametia mdomoni mwake hilo baragumu huku akisubiri idhini ni lini atapatiwa ili apulize! Kana kwamba jambo hili lilikuwa zito kwa Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), hivyo akawaambia semeni:

حَسْبُنَا الله وَنِعْمَ الوَكِيلُ

Allaah Anatutosha, Naye ni mbora wa Kutegemewa.” [At-Tirmidhiy, ambaye amesema ni Hadiyth Hasan]

 

Kauli Za ‘Ulamaa Kuhusu Watakaofazaika (kifo cha mshtuko) Na Watakaosalimika Na Mfazaiko (Kifo Cha Mshtuko) Kwa Mpulizo Wa Kwanza:

 

Watakaofazaika (kifo cha mshtuko) kwa mpulizo wa kwanza wa baragumu ni viumbe wote waovu isipokuwa Amtakaye Allaah (سبحانه وتعالى) asifazaike. Na hawa ni wale Aliowakirimu, Aliowathibitisha na  Akawahifadhi kutokana na mfazaiko (kifo cha mshtuko).  [Tafsiyr Al-Muyassar, Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Watakaofazaika (kifo cha mshtuko) ni viumbe waovu.Watakaosalimika ni Shuhadaa [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Na Hadiyth ifuatayo imetaja hayo:

 

عن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما ، قال : قال رسولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( يَخْرُجُ الدَّجَّالُ في أُمَّتِي فَيَمْكُثُ أرْبَعِينَ ، لاَ أدْرِي أرْبَعِينَ يَوماً أو أرْبَعِينَ شَهْراً ، أو أرْبَعِينَ عَاماً ، فَيَبْعَثُ اللهُ تَعالَى عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ (عَلَيْهِ السَّلام) ، فَيَطْلُبُهُ فَيُهْلِكُهُ ، ثُمَّ يَمْكُثُ النَّاسُ سَبْعَ سِنِينَ لَيسَ بَينَ اثْنَينِ عَدَاوةٌ ، ثُمَّ يُرْسِلُ اللهُ عزوجل ، ريحاً بَارِدَةً مِنْ قِبَلِ الشَّامِ ، فَلاَ يَبْقَى عَلَى وَجْهِ الأَرْضِ أَحَدٌ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ مِنْ خَيرٍ أو إيمَانٍ إلاَّ قَبَضَتْهُ ، حَتَّى لو أنَّ أَحَدَكُمْ دَخَلَ فِي كَبِدِ جَبَلٍ ، لَدَخَلَتْهُ عَلَيهِ حَتَّى تَقْبِضَهُ ، فَيَبْقَى شِرَارُ النَّاسِ في خِفَّةِ الطَّيْرِ ، وأحْلامِ السِّبَاعِ ، لاَ يَعْرِفُونَ مَعْرُوفاً ، ولا يُنْكِرُونَ مُنْكَراً ، فَيَتَمَثَّلُ لَهُمُ الشَّيْطَانُ ، فيَقُولُ : ألاَ تَسْتَجِيبُونَ ؟ فَيَقُولُونَ : فَمَا تأمُرُنَا ؟ فَيَأمُرُهُمْ بِعِبَادَةِ الأوْثَانِ ، وَهُمْ في ذلِكَ دَارٌّ رِزْقُهُمْ ، حَسَنٌ عَيشُهُمْ ، ثُمَّ يُنْفَخُ في الصُّورِ ، فَلاَ يَسْمَعُهُ أحَدٌ إلاَّ أصْغَى لِيتاً وَرَفَعَ لِيتاً ، وَأوَّلُ مَنْ يَسْمَعُهُ رَجُلٌ يَلُوطُ حَوْضَ إبِلِهِ فَيُصْعَقُ ويُصْعَقُ النَّاسُ حولهُ ، ثُمَّ يُرْسِلُ اللهُ -أو قالَ: يُنْزِلُ اللهُ - مَطَراً كَأَنَّهُ الطَّلُّ أو الظِّلُّ ، فَتَنْبُتُ مِنهُ أجْسَادُ النَّاسِ ، ثُمَّ يُنْفَخُ فِيهِ أُخْرَى فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنْظُرُونَ ، ثُمَّ يُقالُ : يا أَيُّهَا النَّاسُ هَلُمَّ إلَى رَبِّكُمْ ، وَقِفُوهُمْ إنَّهُمْ مَسْئُولُونَ ، ثُمَّ يُقَالُ : أخْرِجُوا بَعْثَ النَّارِ فَيُقَالُ : مِنْ كَمْ ؟ فَيُقَالُ : مِنْ كُلِّ ألْفٍ تِسْعَمِئَةٍ وَتِسْعَةً وتِسْعِينَ ؛ فَذَلِكَ يَومٌ يَجْعَلُ الوِلْدَانَ شِيباً ، وَذَلِكَ يَومَ يُكْشَفُ عَنْ سَاقٍ )) . رواه مسلم .

Amesimulia 'Abdullaah bin 'Amr bin Al-'Aasw (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Dajjaal atatokea kwa Ummah wangu na ataishi arobaini, (sina hakika ni siku arobaini au miezi arobaini au miaka arobaini). Kisha Allaah (تبارك وتعالى) Atamtuma 'Iysaa mwana wa Maryam, ambaye atamwinda na kumuua. Kisha watu wataishi kwa miaka saba hapana kabisa uadui wala ugomvi baina ya watu wawili. Baadae Allaah (عزّ وجلّ) Atatuma upepo baridi kutoka Shaam, na hatobaki juu ya mgongo wa ardhi yeyote mwenye chembe ndogo kabisa ya kheri au imaan moyoni mwake isipokuwa utachukua roho yake hata lau mmoja wenu ataingia katika pango la jabali, upepo huo utamwingilia humo uchukue roho yake.  Hapo watabaki walio waovu pekee miongoni mwa watu ambao watapaparikia uasherati kama anavyopaparika ndege na watakuwa na tabia za kinyama. Hawatajua mema wala hawatakataza maovu. Shaytwaan atakuja kwao kwa mfano wa mwanaadam na kuwauliza: Je, mutaniitikia wito wangu?  Watasema: Kwani unatuamuru nini? Atawaamuru waabudu masanamu, na wao katika kufanya hivyo watapata riziki zao na maisha yao yatakuwa mazuri. Kisha baragumu litapulizwa, hakuna atakayesikia isipokuwa atageuza shingo upande wake (wa hiyo sauti) na kuinyanyua. Wa kwanza kuisikia atakuwa ni mtu anayeshughulika katika kutengeneza birika ya maji kwa ajili ya ngamia wake. Atakapoisikia sauti hiyo atafazaika (atakufa kwa mshtuko) na watu wengine nao watakufa kwa mshtuko. Kisha Allaah Atatuma au alisema: Allaah Atateremsha - mvua kana kwamba ni matone ya umande au kivuli. Hii itafanya miili ya watu ikue, kisha baragumu litapulizwa mara nyengine na hapo watasimama watu na huku wanaangalia. Kisha kutasemwa: Enyi watu! Njooni mbele ya Rabb wenu na wasimamisheni kwani wao wataulizwa. Kisha itatolewa amri: Watoeni wale ambao ni wa motoni. Kutaulizwa: Wangapi? Wataambiwa: Katika kila elfu watoeni mia tisa na tisini na tisa (999). Hiyo ndiyo siku ambayo itawafanya watoto wadogo waote mvi, na hiyo ni siku ambayo muundi (wa Allaah) utawachwa wazi." [Muslim]

 

Rejea Az-Zumar (39:68), Al-Haaqqah (69:13).

 

Share