031 - Luqmaan
لُقْمَان
031-Luqmaan
031-Luqmaan: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
الم ﴿١﴾
1. Alif Laam Miym.[1]
تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
2. Hizi ni Aayaat za Kitabu chenye hikmah.
هُدًى وَرَحْمَةً لِّلْمُحْسِنِينَ ﴿٣﴾
3. Zikiwa ni mwongozo na rehma kwa wafanyao ihsaan.
الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ ﴿٤﴾
4. Ambao wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah, nao ni wenye yakini na Aakhirah.
أُولَـٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥﴾
5. Hao wako juu ya mwongozo kutoka kwa Rabb wao, na hao ndio wenye kufaulu.
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾
6. Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) Njia ya Allaah bila ilimu, na huzichukulia (Aayaat) mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha.[2]
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا وَلَّىٰ مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا كَأَنَّ فِي أُذُنَيْهِ وَقْرًا ۖ فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٧﴾
7. Na anaposomewa Aayaat Zetu, hugeuka huku akitakabari kama kwamba hazisikii, kama kwamba kuna uziwi masikioni mwake. Basi mbashirie adhabu iumizayo.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتُ النَّعِيمِ ﴿٨﴾
8. Hakika wale walioamini na wakatenda mema watapata Jannaat za Neema.
خَالِدِينَ فِيهَا ۖ وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٩﴾
9. Wadumu humo. Ni Ahadi ya Allaah ya haki. Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.
خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ ۚ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿١٠﴾
10. (Allaah) Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona, na Akaweka katika ardhi milima iliyosimama imara ili isiyumbe nanyi, na Akaeneza humo kila viumbe vinavyotembea. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji, Tukaotesha humo kila aina ya mimea mizuri yenye manufaa.
هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾
11. Huu ni Uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye.[3] Bali madhalimu wamo katika upotofu bayana.
وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ أَنِ اشْكُرْ لِلَّـهِ ۚ وَمَن يَشْكُرْ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿١٢﴾
12. Kwa yakini Tulimpa Luqmaan[4] hikmah kwamba: Mshukuru Allaah. Na anayeshukuru, basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na anayekufuru, basi hakika Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.
وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾
13. Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno![5]
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿١٤﴾
14. Na Tumemuusia binaadam kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa katika miaka miwili; ya kwamba, unishukuru Mimi, na wazazi wako,[6] Kwangu ndio mahali pa kuishia. [7]
وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾
15. Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani, [8] na fuata njia ya anayerudi kutubia Kwangu. Kisha Kwangu ndio marejeo yenu, na Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda.
يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿١٦﴾
16. Ee mwanangu! Hakika likiweko (zuri au ovu) lolote lenye uzito wa punje ya hardali, likawa katika jabali au mbinguni au ardhini, Allaah Atalileta tu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.[9]
يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾
17. Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.
وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾
18. Na wala usiwageuzie watu uso wako kwa kiburi, na wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah Hampendi kila mwenye kujivuna mwenye kujifakharisha.
وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ ۚ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ ﴿١٩﴾
19. Na kuwa wastani katika mwendo wako, na teremsha sauti yako, hakika sauti mbaya inayokirihisha zaidi bila shaka ni sauti ya punda.[10]
أَلَمْ تَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَأَسْبَغَ عَلَيْكُمْ نِعَمَهُ ظَاهِرَةً وَبَاطِنَةً ۗ وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ ﴿٢٠﴾
20. Je, hamuoni kwamba Allaah Amekutiishieni vile vilivyomo mbinguni na vile vilivyomo ardhini, na Akakutimizieni kitimilifu Neema Zake kwa dhahiri na siri?[11] Na miongoni mwa watu, wako wanaobishana kuhusu Allaah bila ya ilimu yoyote ile, na bila ya mwongozo wowote ule, na bila ya kitabu chochote kile chenye nuru.
وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ قَالُوا بَلْ نَتَّبِعُ مَا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا ۚ أَوَلَوْ كَانَ الشَّيْطَانُ يَدْعُوهُمْ إِلَىٰ عَذَابِ السَّعِيرِ ﴿٢١﴾
21. Na wanapoambiwa: Fuateni yale Aliyoyateremsha Allaah, husema: Bali tunayafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu.[12] Je, japokuwa shaytwaan anawaita katika adhabu ya moto uliowashwa vikali mno?
وَمَن يُسْلِمْ وَجْهَهُ إِلَى اللَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ ۗ وَإِلَى اللَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ ﴿٢٢﴾
22. Na anayeusalimisha uso wake kwa Allaah, naye akawa ni mtenda ihsaan, basi kwa yakini ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika. Na kwa Allaah ni hatima ya mambo yote.
وَمَن كَفَرَ فَلَا يَحْزُنكَ كُفْرُهُ ۚ إِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ فَنُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٢٣﴾
23. Na anayekufuru, basi isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ni marejeo yao, Tutawajulisha yale waliyoyatenda. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
نُمَتِّعُهُمْ قَلِيلًا ثُمَّ نَضْطَرُّهُمْ إِلَىٰ عَذَابٍ غَلِيظٍ ﴿٢٤﴾
24. Tunawastarehesha kidogo, kisha Tutawasukumiza kwenye adhabu nzito.
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٥﴾
25. Na ukiwauliza: Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi? Bila shaka watasema: Allaah.[13] Sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah). Bali wengi wao hawajui.
لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٢٦﴾
26. Ni vya Allaah Pekee vyote vile viliomo katika mbingu na ardhi. Hakika Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.
وَلَوْ أَنَّمَا فِي الْأَرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلَامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٧﴾
27. Na lau kama miti yote iliyomo katika ardhi ingekuwa ni kalamu, na bahari (ikafanywa wino), ikaongezewa juu yake bahari saba, yasingelimalizika Maneno ya Allaah.[14] Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.
مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ﴿٢٨﴾
28. Hakukuwa kuumbwa kwenu wala kufufuliwa kwenu isipokuwa ni kama nafsi moja tu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى وَأَنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿٢٩﴾
29. Je, huoni kwamba Allaah Anauingiza usiku katika mchana, na Anauingiza mchana katika usiku? Na Amelitiisha jua na mwezi, vyote vinakwenda mpaka muda maalumu uliokadiriwa? Na kwamba Allaah kwa yale mnayoyatenda ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri?
ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٣٠﴾
30. Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba wale wanaowaomba badala Yake, ni baatwil, na kwamba Allaah Ndiye Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa.[15]
أَلَمْ تَرَ أَنَّ الْفُلْكَ تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِنِعْمَتِ اللَّـهِ لِيُرِيَكُم مِّنْ آيَاتِهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ ﴿٣١﴾
31. Je, huoni kwamba merikebu zinapita baharini kwa Neema ya Allaah ili Akuonyesheni baadhi ya Aayaat (Ishara, Uwezo, Dalili) Zake? Hakika katika hayo kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa kila mwingi wa ustahamilivu na kushukuru.
وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ فَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ ۚ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا كُلُّ خَتَّارٍ كَفُورٍ ﴿٣٢﴾
32. Na yanapowafunika mawimbi kama mawingu, humwomba Allaah wakiwa wenye kumtakasia Yeye Dini. Lakini Anapowaokoa katika nchi kavu, basi kuna miongoni mwao mwenye kushika mwendo wa wastani.[16] Na hazikanushi Aayaat (na Ishara, Dalili) Zetu isipokuwa kila khaini mkubwa, mwingi wa kukufuru.[17]
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ وَاخْشَوْا يَوْمًا لَّا يَجْزِي وَالِدٌ عَن وَلَدِهِ وَلَا مَوْلُودٌ هُوَ جَازٍ عَن وَالِدِهِ شَيْئًا ۚ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ ۖ فَلَا تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَلَا يَغُرَّنَّكُم بِاللَّـهِ الْغَرُورُ ﴿٣٣﴾
33. Enyi watu! Mcheni Rabb wenu, na iogopeni Siku ambayo mzazi hatomfaa mwanawe na wala mwana hatomfaa mzazi wake chochote.[18] Hakika Ahadi ya Allaah ni haki. Basi usikughururini kabisa uhai wa dunia, na wala (shaytwaan) mwenye kughuri asikughururini kabisa kuhusu Allaah.
إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾
34. Hakika Allaah Ana ujuzi wa Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika matumbo ya uzazi. Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani. Hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri.[19]
[1] الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):
Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).
[2] Haramisho La Muziki:
Hadiyth na kauli za Salaf zifuatazo zimethibitisha uharamisho wa muziki:
عن ابن عباس قال عن آية: ((وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ)، قال :الغناء وأشباهه إسناده صحيح - المحدث: الألباني
Ibn 'Abbaas (رضي الله عنهما) amesema kuhusu Aayah hii:
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ
“Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi.”
"Ni nyimbo na maneno yanayofanana (ya upuuzi)" [Swahiyh Adab Al-Mufrad (603) - Ameisahihisha Al-Albaaniy]
Na Ibn Mas‘uwd (رضي الله عنه) amesema kuhusu Aayah hii: "Naapa kwa Allaah, hii inamaanisha ni muziki (au nyimbo)." Akaikariri mara tatu. [At-Twabariy (20:127)]
Rejea pia Al-Israa (17:64) kwenye kauli ya Mujaahid ambaye amesema kuwa imekusudiwa ni nyimbo (na aina zote za muziki).
[3] Wanaoabudiwa Pasi Na Allaah Hawawezi Kuumba Chochote:
Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ
“Huu ni Uumbaji wa Allaah.”
Yaani: Uumbaji wa ulimwengu wa juu na wa chini, vitu visivyo na uhai na viumbe hai, na utoaji wa rizki kwao. Ni Uumbaji wa Allaah Pekee Asiye na mshirika, kila mtu anakiri hayo hata nyinyi enyi washirikina! Akasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ
“Basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye.”
Yaani: Wale mnaowafanya kuwa ni washirika wa Allaah, na mnawaomba na kuwaabudu. Na kama mambo ni hivi, basi ni lazima hao wanaumba kama Anavyoumba Allaah (سبحانه وتعالى) na wawe wanaruzuku kama Anavyoruzuku Allaah Ikiwa wanacho chochote katika haya mawili, basi nionyesheni ili kuthibitisha madai yenu kwamba wanastahili kuabudiwa.
Na kwa vyovyote inajulikana kwamba hawawezi kumwonyesha chochote walichoumba waabudiwa wao hao, kwa sababu, washirikina hawa wanakiri kwamba vitu vyote vilivyotajwa hapa vimeumbwa na Allaah (سبحانه وتعالى) Peke Yake, hakuna kitu kingine kinachojulikana zaidi ya kile kilichotajwa hapa. Hivyo imethibitika kuwa hawawezi kuthibitisha chochote kile kilichoumbwa na waabudiwa (miungu) wao, ambacho kwacho wangestahili kuabudiwa. [Tafsiyr As-Sa’diy].
Rejea Al-Ahqaaf (46:4) kwenye maelezo na rejea nyenginezo. Rejea pia Atw-Twuur (52:35-36).
Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amewatangazia tangazo watu wote wakusanyike na miungu yao wajaribu kuumba nzi lakini hakuna awezaye! Rejea Al-Hajj (22:73). Rejea pia An-Nahl (16:20), Al-Furqaan (25:2-3), An-Naml (27:60), Faatwir (35:40), Ghaafir (40:62), Al-Waaqi’ah (56:57-59), Atw-Twuwr (52:36).
[4] Luqmaan:
Salaf wamekhitilafiana kama Luqmaan alikuwa ni Nabii au mja mwema. Na kauli ya nguvu kabisa ni kwamba, yeye ni mja mwema, kwa sababu Allaah (سبحانه وتعالى) Hakumtaja isipokuwa kutaja tu kuwa Alimpa hikma. [Tafsiyr As-Sa’diy]
Luqmaan alizaliwa katika Bara la Afrika. Jina lakeni Luqmaan bin 'Anqa' bin Sa’duwn. Ama Ibn Jariyr atw-Twabariy, yeye anasema jina lake lilikuwa Luqmaan bin Tharan kutoka watu wa Aylah (Quds). Alikuwa Swalihina; mtiifu, mwenye kumcha Allaah, mwenye busara na hikma tele. Rejea Alhidaaya.com > Maudhui Za Qur-aan > Visa Katika Qur-aan kupata historia yake na wasifu wake kwa bayana.
[5] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:
Bonyeza kiungo kifuatacho:
Miongoni Mwa Wasiya Wa Luqmaan: Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno:
عَنْ عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال: لَمَّا نَزَلَتْ هَذِهِ الآيَةُ: الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ، شَقَّ ذَلِكَ عَلَى النَّاس وَقَالُوا: أَيُّنَا لَمْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ؟! فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إنَّه لَيْسَ كَمَا تَعنُون! ألَمْ تَسْمَعوا ما قال الْعبْد الصَّالح؟ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ- إنَّما هُو الشِّرْك))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه): Ilipoteremshwa Aayah hii:
الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ،
“Wale walioamini na hawakuchanganya imaan zao na dhulma” [An-An’aam (6:82)]
Iliwatatiza watu wakasema: “Nani katika sisi hajadhulumu nafsi yake?” Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Si kama vile mnavyomaanisha! Hamsikii pale mja mwema (Luqmaan) aliposema:
يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾
“Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” [Luqmaan: (31:13] “Hakika hiyo ni shirk.” [Ahmad na riwaayah zinazofanana katika Al-Bukhaariy na wengineo]
Rejea Al-An’aam (6:82). Na rejea pia Alhidaaya.com kwenye makala ya:
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!- إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ
Makala hii imechambua na kuelezea kwa bayana maana ya shirki, dhulma, aina za shirki, makatazo na adhabu zake.
Kuanzia Aayah hii namba (13) na namba (16-19), Luqmaan anamuusia mwanawe nyasia zifuatazo muhimu katika maisha yake:
(i) Kutokumshirikisha Allaah, kwa sababu shirki ni dhulma kubwa mno! (ii) Kumcha na kumkhofu Allaah (سبحانه وتعالى), na kutenda ya utiifu kadiri inavyowezekana, na kumtahadharisha kutenda maovu. Mema na maovu yawe makubwa au madogo vipi, hata lenye uzito wa punje ya hardali, linapotendwa popote pale, basi Allaah Atalijua, kwani hakifichiki kitu Kwake, Yeye Ni Mjuzi wa dhahiri na ya siri. (iii) Kusimamisha Swalaah. (iv) Kuamrisha mema na kukataza ya munkari na kuazimia katika kuvuta subra katika jambo hili la daawah kwa kuwa bila shaka yatamsibu ya kumsibu. (v) Kutokuwafanyia watu kiburi (vi) Kutokuwa na maringo, majivuno na kujifakharisha, kwani Allaah Hampendi mwenye sifa hizi. (vii) Kutembea mwendo wa wastani (viii) Kutokuongea kwa sauti kubwa inayokirihisha.
[6] Kuwafanyia Wazazi Wawili Ihsaan, Mashaka Ya Mama Kubeba Mimba Na Kuzaa, Kunyonyesha, Kumshukuru Allaah Na Wazazi
Aayah hii imetaja maamrisho ambayo takriban ni sawa na maamrisho katika Suwrah Al-Ahqaaf. Rejea huko (46:15), kupata faida na rejea mbalimbali nyenginezo.
Maamrisho hayo ni kama yafuatavyo:
(i) Kuwafanyia ihsaan wazazi wawili.
(ii) Mashaka ya mama wakati wa kubeba mimba, kuzaa na kunyonyesha.
(iii) Kumshukuru Allaah na kuwashukuru wazazi.
Na maamrisho ya kuwafanyia ihsaan wazazi wawili yametajwa pia katika Suwrah nyenginezo za Qur-aan. Miongoni mwazo ni Al-Baqarah (2:83), (2:215), An-Nisaa (4:36), Al-An’aam (6:151), Al-Israa (17:23-24), Al-‘Ankabuwt (29:8).
[7] Udhaifu Juu Ya Udhaifu:
Kauli za Salaf kuhusu maana ya udhaifu juu ya udhaifu: Mashaka ya kuzaa mtoto, juhudi baada ya juhudi, na udhaifu baada ya udhaifu.
[8] Katazo La Kuwatii Viumbe Katika Kumwasi Muumbaji Hata Kama Ni Wazazi:
Rejea pia Al-’Ankabuwt (29:8) kwenye maelezo kuhusu kuwafanyia ihsaan wazazi wasiokuwa Waislamu.
[9] Hakuna Kinachofichika Kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Ardhini Wala Baharini Hata Kiwe Chenye Uzito Wa Hardali:
Rejea Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) nyenginezo katika Suwrah Al-An’aam (6:59) kwenye faida na maelezo bayana. Na rejea pia Ghaafir (40:19) kwenye maelezo na rejea mbalimbali. Rejea pia Yuwnus (10:62), Saba-a (34:3).
[10] Mwendo Wa Wastani, Sauti Ya Punda:
Na Kauli Yake:
وَاقْصِدْ فِي مَشْيِك
“Na kuwa wastani katika mwendo wako.”
Yaani: Nenda kwa unyenyekevu hali ya kuwa mtulivu, si kwenda kwa kiburi na kujikweza, wala mwendo wa kujinyongesha.
Na Kauli Yake:
وَاغْضُضْ مِنْ صَوْتِكَ
“Na teremsha sauti yako.”
Yaani: Ikiwa ni adabu kwa watu pamoja na Allaah.
Na Kauli Yake:
إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ ﴿١٩﴾
“Hakika sauti mbaya inayokirihisha zaidi bila shaka ni sauti ya punda.”
Yaani: Sauti iliyo mbaya zaidi. Basi lau kama ingekuwa kuna faida na maslahi katika kunyanyua sauti ya juu, basi asingekuwa mahsusi ni punda katika hilo, (mnyame dhalili) ambae kimejulikana chakula chake na makazi yake
[11] Neema Za Allaah (سبحانه وتعالى) Za Dhahiri Na Siri:
Rejea Suwrah Ibraahiym (14:34) kwenye uchambuzi wa Neema za Allaah za zinazoonekana na zisizoonekana.
[12] Kufuata Mababa Na Mababu Japokuwa Hawakuwa Na Ilimu Au Walikuwa Ni Wapotofu:
Rejea Az-Zukhruf (43:22-23).
[13] Washirikina Waliamini Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah Lakini Walikanusha Tawhiyd Al-Uluwhiyyah.
Rejea Yuwnus (10:31), Al-‘Ankabuwt (29:61).
[14] Maneno Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Hayahesabiki, Hayamaliziki Wala Hayana Mwisho:
Kisha Akaelezea kuhusu upana wa Maneno Yake na ukubwa wa Kauli Zake, kwa ufafanuzi unaofika ndani ya nyoyo, na akili zinashtuka kwa jambo hilo, na nyoyo kuchanganywa akili ndani yake, na hutembea katika kumjua watu wenye akili na uoni, Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ أَنَّمَا فِي الْأَرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلَامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ
“Na lau kama miti yote iliyomo katika ardhi ingekuwa ni kalamu, na bahari (ikafanywa wino), ikaongezewa juu yake bahari saba.”
Yaani: Kalamu ambazo hutumika kuandikia wino uongezwao, basi hizo kalamu zingevunjika na huo wino ungeisha, na wala yasiishe Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى).
Na hii si kuzidisha kusiko na uhalisia, bali wakati Allaah (سبحانه وتعالى) Alipojua ya kwamba akili zinashindwa kudhibiti baadhi ya Sifa Zake, na akatambua Allaah (سبحانه وتعالى) ya kwamba Waja Wake kumjua Yeye ni neema bora zaidi ambayo Amewaneemesha juu yao.
Na ni uchochoro bora zaidi wa kuifikia, nayo haiwezi kukamilika vile ilivyo. Lakini kisichopatikana chote basi hakiachwi chote. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawazindua uzinduzi unaotia Nuru moyoni, na vifua kufunguka kwa uzinduzi huo, na hutoa hoja kwa kile walichofikia katika kile ambacho hawajakifikia. Na wanasema kama alivyosema Mbora wao Mjuzi zaidi wa Rabb wake, yaani Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
لا أُحْصـي ثَنـاءً عَلَـيْك، أَنْـتَ كَمـا أَثْنَـيْتَ عَلـى نَفْسـِك
“Siwezi kuzidhibiti sifa Zako, Wewe ni kama ulivyojisifu Mwenyewe.”
(Hii ni katika duaa za Swalaah kwenye kusujudu, na katika ibaada nyenginezo).
Na kama si hivyo, basi jambo ni kubwa na tukufu zaidi ya hilo.
Na huku kufananisha ni katika mlango wa kuweka maana karibu, ambayo haiwezi kufikiwa na ufahamu na akili, na kama si hivyo basi miti hata ikizidi juu ya iliyotajwa zaidi na zaidi, na bahari lau kama zingeongezwa mara nyingi zaidi nyongeza kwa nyongeza, kwani hakika hutazamiwa kuisha kwake na kumalizika, kwa kuwa hizi bahari ni zimeumbwa.
Ama Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) haitazamiwi kuisha kwake, bali imetujulisha hoja ya kisharia na kiakili ya kwamba hayamaliziki wala hayana mwisho, na kila kitu kinaisha isipokuwa Muumbaji na Sifa Zake kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنتَهَىٰ ﴿٤٢﴾
“Na kwamba kwa Rabb wako ndio kikomo.” [An-Najm (53:42)]
Na pindi akili itakapohisi uhalisia wa umwanzo wake Allaah (سبحانه وتعالى) na umwisho wake, na kwamba kila kilichofanyiwa tathmini na akili katika zama zilizopita, vyovyote itakavyoungana tathmini hiyo, basi yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Yupo kabla ya hilo na mpaka kusiko na mwisho. Na kwamba vyovyote itakavyotathmini fahamu na akili katika zama za mwisho, na zikaunganika tathmini na akasaidia juu ya hilo mwenye kusaidia, kwa moyo wake na ulimi wake, basi Allaah (سبحانه وتعالى) baada ya hilo ni mpaka kusiko na lengo wala mwisho.
Na Allaah katika nyakati zote Anahukumu, na Anazungumza, na Anasema, na Anafanya namna Atakavyo, na Anapotaka, hakuna cha kumzuia katika maneno na vitendo. Na pindi akili itakapotengeneza picha ya hilo, itatambua ya kwamba, mfano ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Ameupiga katika Maneno Yake ili waja wajue kitu katika hilo, na kama si hivyo basi jambo ni kubwa na tukufu zaidi.
Kisha Allaah (عزّ وجلّ) Akataja Utukufu Wake na Ukamilifu wa Hikma Zake, Akasema
إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٧﴾
“Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.”
Yaani: Ni Zake Yeye nguvu zote, Ambaye hakuna nguvu katika ulimwengu wa juu wala wa chini ispokuwa kutoka Kwake. Amewapa nguvu hizo viumbe, basi hakuna ujanja wala nguvu ispokuwa Zake. Na kwa Nguvu Zake, Amewashinda viumbe vyote, na Kuwaendesha, na Kuwapangilia, na kwa Hikma Zake, Ameumba viumbe, na Akalianzisha kwa hikma, na Akafanya lengo lake na makusudio yake ni hikma. Na vile vile amri na makatazo yamepatikana kwa hikma, na ikawa lengo lake na makusudio ni hikma. Basi Yeye ni Mwenye hikma katika kuumba Kwake na Amri Zake. [Tafsiyr As-Sa’diy]
Rejea pia Al-Kahf (18:109) kwenye Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) kama hii.
[15] Al-‘Aliyyu:
Allaah (سبحانه وتعالى) Ametukuka, Ana Uadhama Kuliko wote kuliko vyote, Yuko juu Kabisa juu ya viumbe Vyake vyote.
Al-Kabiyr: Mkubwa Kabisa wa Dhati kwa Sifa na matendo.
Rejea Fahara ya Majina Mazuri Kabisa Na Sifa Za Za Allaah.
[16] Makundi Mawili: Wenye Mwendo Wa Wastani Na Waliokufuru:
Kundi moja ni wenye mwendo wa wastani ambao hawatoi shukurani ipasavyo kwa Allaah bali wanafanya dhambi na kujidhulumu nafsi zao. Kundi jengine limekufuru Neema za Allaah na kuzikanusha. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[17] Washirikina Walipofikwa Na Janga Walimwelekea Allaah Kumuomba Kisha Wakarudi Kumshirikisha:
Rejea Yuwnus (10:22) ambako kuna maelezo kwamba shirki za washirikina wa zama hizi ni kubwa zaidi kuliko shirki za washirikina wa awali.
[18] Siku Ya Qiyaamah Hakutakuwa Na Unasaba Hata Wazazi Watakanana Na Watoto Wao:
Rejea ‘Abasa (80:34).
[19] Mambo Matano Ya Ghaibu:
Maana Ya Ghaibu: Rejea Al-Baqarah (2:3), Al-An’aam (6:59), An-Naml (27:65).
Aayah hii tukufu imetaja mambo matano ya ghaibu ambayo hakuna ayajuaye. Hata Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakutambulishwa ujuzi wake. Basi wanaodai kuwa wanajua ya ghaibu kama watabiri wanaotabiri mambo kwa unajimu (kutabiri kwa nyota) na mengineyo ya ukahini, wamo hatarini kwa sababu kufanya hivyo ni miongoni mwa shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameonya katika Hadiyth kadhaa, na miongoni mwazo ni:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، عَنْ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: مَنْ أَتَى كَاهِنًا، أَوْ عَرَّافًا، فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ، فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم .
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemwendea kahini au mpigaji ramli akamuamini ayasemayo, basi atakuwa ameshakufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).’” [Ahmad, na Aswhaabus-Sunan wanne, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb (3047)]
Na wanaotabiri mvua pia wamehukumiwa kuwa wanakufuru:
عَنْ زَيْدِ بْنِ خَالِدٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: صَلَّى لَنَا رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) صَلاةَ الصُّبْحِ بِالْحُدَيْبِيَةِ عَلَى إِثْرِ سَمَاءٍ كَانَتْ مِنَ اللَّيْلِ، فَلَمَّا انْصَرَفَ أَقَبْلَ عَلَى النَّاسِ، فَقَالَ: هَلْ تَدْرُونَ مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ؟ قَالُوا: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمَ. قَالَ: قَالَ أَصْبَحَ مِنْ عِبَادِي مُؤْمِنٌ بِي وَكَافِرٌ، فَأَمَّا مَنْ قَالَ مُطِرْنَا بِفَضْلِ اللَّهِ وَرَحْمَتِهِ، فَذَلِكَ مُؤْمِنٌ بِي كَافِرٌ بِالْكَوْكَبِ، وَأَمَّا مَنْ قَالَ مُطِرْنَا بِنَوْءِ كَذَا وَكَذَا، فَذَلِكَ كَافِرٌ بِي مُؤْمِنٌ بِالْكَوْكَب .
Amesimulia Zayd bin Khaalid (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alituswalisha Swalaah ya asubuhi Hudaybiyah baada ya usiku wa mvua. Alipomaliza akawakabili watu akasema: “Je, mnajua Rabb wenu Amesema nini?” Wakajibu: Allaah na Rasuli Wake ndio Wajuao. Akasema: “Allaah Amesema: Baadhi ya waja Wangu wameamka leo wakiwa wenye kuniamini, na wengine wamekufuru. Aliyesema kuwa mvua ni kutokana na Fadhila na Rehma za Allaah, basi huyo ni mwenye kuniamini wala haamini nyota. Ama aliyesema: Tumenyeshewa mvua kutokana na nyota fulani, basi yeye ni mwenye kunikufuru na mwenye kuamini nyota.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Tafsiyr ya Aayah:
Imeshathibiti ya kwamba Ilimu ya Allaah (سبحانه وتعالى) imedhibiti yaliyofichika na yaliyowazi, ya siri na ya dhahiri, na Allaah Anaweza kuwadhihirishia Waja Wake mambo mengi yaliyofichika.
Na mambo haya Matano, ni katika mambo ambayo Ilimu Yake imefichwa kabisa kwa viumbe vyote, hayajui Nabii aliyetumwa, wala Malaika aliyekurubishwa, wala wengineo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ
“Hakika Allaah Ana ujuzi wa Saa (Qiyaamah).”
Yaani: Anajua ni lini kitakuwa, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ۚ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً ۗ يَسْأَلُونَكَ كَأَنَّكَ حَفِيٌّ عَنْهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨٧﴾
“Wanakuuliza (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Saa (Qiyaamah), lini kutokea kwake? Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Rabb wangu. Hakuna wa kuidhihirisha wakati wake isipokuwa Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitokufikieni isipokuwa kwa ghafla. Wanakuuliza kama kwamba wewe unaijua vyema. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Allaah (Pekee), lakini watu wengi hawajui.” [Al-A’raaf (7:187)]
Na Kauli Yake:
وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ
“Na Anateremsha mvua.”
Yaani: Ni Yeye Pekee Anayeiteremsha, na Anajua ni wakati gani itateremka.
Na Kauli Yake:
وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ
“Anajua yale yaliyomo katika matumbo ya uzazi.”
Yaani: Yeye Ndiye Ambaye Amekianzisha kilichomo ndani yake, na kukijua ni kipi, je ni mume au mke. Na kwa hili Malaika anayewakilishwa katika vilivyomo matumboni humuuliza Rabb Wake: Je yeye ni mume au mke? Basi Allaah Anahukumu Anachokitaka.
Na Kauli Yake:
وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ
“Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho.”
Yaani: Katika chumo la Dini yake na dunia yake.
Na Kauli Yake:
وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ
“Na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani.”
Yaani: Bali Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Pekee Anaejua hayo yote.
Na Alipoyataja mambo haya matano kwa umahususi kwamba Ni Yeye Tu Anayajua, Akatueleza hapo hapo kwamba Ilimu Yake imeenea vile vile kwa mambo mengine yote Akisema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾
“Hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri.”
Yaani: Yeye Ndiye Mwenye Kudhibiti ya nje na ya ndani, na yaliyofichika na ya siri. Na katika Hikma Zake zilizokamilika, ni pale Alipoficha kwa waja, ilimu ya haya mambo matano, kwa sababu kuna maslahi katika hilo ambayo hayafichiki kwa mwenye kuzingatia hilo. [Tafsiyr As-Sa’diy]