036 - Yaasiyn

 

   يس

 

036-Yaasiyn

 

 

036-Yaasiyn: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

يس ﴿١﴾

1. Yaa Siyn.[1]

 

 

 

وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾

2. Naapa kwa Qur-aan yenye Hikmah.

 

 

 

إِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٣﴾

3. Hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka ni miongoni mwa Rusuli.

 

 

 

عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤﴾

4. Uko juu ya njia iliyonyooka.

 

 

 

تَنزِيلَ الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ ﴿٥﴾

5. Ni Uteremsho wa Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أُنذِرَ آبَاؤُهُمْ فَهُمْ غَافِلُونَ ﴿٦﴾

6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi wao ni wenye kughafilika.

 

 

 

 

لَقَدْ حَقَّ الْقَوْلُ عَلَىٰ أَكْثَرِهِمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٧﴾

7. Kwa yakini imethibiti kauli (ya adhabu) juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini.

 

 

 

 

إِنَّا جَعَلْنَا فِي أَعْنَاقِهِمْ أَغْلَالًا فَهِيَ إِلَى الْأَذْقَانِ فَهُم مُّقْمَحُونَ ﴿٨﴾

8. Hakika Sisi Tumeweka kwenye shingo zao minyororo ikawafika videvuni, basi vichwa vyao vinanyanyuka juu na kufumba macho. 

 

 

 

 

وَجَعَلْنَا مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ سَدًّا وَمِنْ خَلْفِهِمْ سَدًّا فَأَغْشَيْنَاهُمْ فَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ ﴿٩﴾

9. Na Tumeweka mbele yao kizuizi na nyuma yao kizuizi, Tukawafunika, basi wao hawaoni.

 

 

 

 

وَسَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٠﴾

10. Na ni sawasawa tu juu yao, ukiwaonya au usiwaonye hawaamini.

 

 

 

 

 

إِنَّمَا تُنذِرُ مَنِ اتَّبَعَ الذِّكْرَ وَخَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ ۖ فَبَشِّرْهُ بِمَغْفِرَةٍ وَأَجْرٍ كَرِيمٍ ﴿١١﴾

11. Hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unamuonya yule anayefuata Ukumbusho na akamkhofu Ar-Rahmaan kwa ghaibu, basi mbashirie maghfirah na ujira karimu.

 

 

 

 

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿١٢﴾

12. Hakika Sisi Tunahuisha wafu, na Tunaandika yale waliyoyakadimisha (ya kheri na shari) na athari zao, na kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari bayana.[2]

 

 

 

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا أَصْحَابَ الْقَرْيَةِ إِذْ جَاءَهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿١٣﴾

13. Na wapigie mfano watu wa mji[3] walipowajia Wajumbe.[4]

 

 

إِذْ أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمُ اثْنَيْنِ فَكَذَّبُوهُمَا فَعَزَّزْنَا بِثَالِثٍ فَقَالُوا إِنَّا إِلَيْكُم مُّرْسَلُونَ ﴿١٤﴾

14. Tulipowapelekea wawili, wakawakadhibisha, Tukawaongezea nguvu kwa wa tatu, wakasema: Hakika sisi (ni wajumbe) tumetumwa kwenu.

 

 

 

 

قَالُوا مَا أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَمَا أَنزَلَ الرَّحْمَـٰنُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَكْذِبُونَ ﴿١٥﴾

15. (Watu wa mji) wakasema: Nyinyi si chochote isipokuwa ni watu tu kama sisi, na wala Ar-Rahmaan Hakuteremsha chochote. Hamkuwa nyinyi isipokuwa mnaongopa tu.[5]

 

 

 

قَالُوا رَبُّنَا يَعْلَمُ إِنَّا إِلَيْكُمْ لَمُرْسَلُونَ ﴿١٦﴾

16. (Wajumbe) wakasema: Rabb wetu Anajua kwamba sisi kwa hakika tumetumwa kwenu.

 

 

 

 

وَمَا عَلَيْنَا إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿١٧﴾

17. Na hapana juu yetu lolote isipokuwa ubalighisho wa bayana.

 

 

 

 

 

قَالُوا إِنَّا تَطَيَّرْنَا بِكُمْ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهُوا لَنَرْجُمَنَّكُمْ وَلَيَمَسَّنَّكُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٨﴾

18. (Watu wa mji) wakasema: Hakika sisi tumepata nuksi[6] kwenu. Msipokoma, basi hakika tutakurajimuni, na bila shaka itakuguseni kutoka kwetu adhabu iumizayo.

 

 

 

قَالُوا طَائِرُكُم مَّعَكُمْ ۚ أَئِن ذُكِّرْتُم ۚ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ مُّسْرِفُونَ ﴿١٩﴾

19. (Wajumbe) wakasema: Nuksi yenu mnayo wenyewe. Je, kwa vile mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu wapindukao mipaka.

 

 

 

 

وَجَاءَ مِنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَىٰ قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ ﴿٢٠﴾

20. Akaja mtu mbio kutoka upande wa mbali wa ule mji, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni wajumbe.[7]

 

 

 

 

اتَّبِعُوا مَن لَّا يَسْأَلُكُمْ أَجْرًا وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٢١﴾

21. Wafuateni wale wasiokuombeni ujira, nao ni wenye kuongoka.

 

 

 

 

وَمَا لِيَ لَا أَعْبُدُ الَّذِي فَطَرَنِي وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na kwa nini mimi nisimwabudu Ambaye Ameniumba na Kwake mtarejeshwa?

 

 

 

 

أَأَتَّخِذُ مِن دُونِهِ آلِهَةً إِن يُرِدْنِ الرَّحْمَـٰنُ بِضُرٍّ لَّا تُغْنِ عَنِّي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا وَلَا يُنقِذُونِ ﴿٢٣﴾

23. Je, nijichukulie badala Yake waabudiwa, na hali Akinitakia Ar-Rahmaan dhara yoyote hautonifaa chochote uombezi wao wala hawatoniokoa!

 

 

 

إِنِّي إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٤﴾

24. Hakika mimi hapo nitakuwa katika upotofu bayana.

 

 

 

 

إِنِّي آمَنتُ بِرَبِّكُمْ فَاسْمَعُونِ ﴿٢٥﴾

25. Hakika mimi nimemwamini Rabb wenu, basi nisikilizeni!

 

 

 

 

قِيلَ ادْخُلِ الْجَنَّةَ ۖ قَالَ يَا لَيْتَ قَوْمِي يَعْلَمُونَ ﴿٢٦﴾

26.  Ikasemwa (alipouliwa): Ingia Jannah. Akasema: Laiti watu wangu wangelijua.[8]

 

 

 

 

بِمَا غَفَرَ لِي رَبِّي وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُكْرَمِينَ ﴿٢٧﴾

27. Namna ambavyo Rabb wangu Amenighufuria, na Akanijaalia kuwa miongoni mwa waliokirimiwa.

 

 

 

 

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ قَوْمِهِ مِن بَعْدِهِ مِن جُندٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَمَا كُنَّا مُنزِلِينَ ﴿٢٨﴾

28. Na Hatukuwateremshia watu wake baada yake jeshi lolote kutoka mbinguni, na wala Hatukuwa Wateremshao.

 

 

 

 

إِن كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ خَامِدُونَ ﴿٢٩﴾

29. Haikuwa isipokuwa ukelele angamizi mmoja tu, basi mara hao wamezimika.

 

 

 

 

يَا حَسْرَةً عَلَى الْعِبَادِ ۚ مَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٣٠﴾

30. Ee! Ole na majuto juu ya waja!  Hawafikiwi na Rasuli yeyote isipokuwa walikuwa wakimfanyia istihzai.

 

 

 

 

أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّنَ الْقُرُونِ أَنَّهُمْ إِلَيْهِمْ لَا يَرْجِعُونَ ﴿٣١﴾

31. Je, hawajaona karne ngapi Tumeangamiza kabla yao na kwamba wao hawatorejea kwao?

 

 

 

وَإِن كُلٌّ لَّمَّا جَمِيعٌ لَّدَيْنَا مُحْضَرُونَ ﴿٣٢﴾

32. Na hapana yeyote ila wote watahudhurishwa Kwetu. 

 

 

 

 

وَآيَةٌ لَّهُمُ الْأَرْضُ الْمَيْتَةُ أَحْيَيْنَاهَا وَأَخْرَجْنَا مِنْهَا حَبًّا فَمِنْهُ يَأْكُلُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na Aayah (Ishara, Dalili)[9] kwao ni ardhi iliyokufa, Tukaihuisha, na Tukatoa humo nafaka, wakapata kuzila.[10]

 

 

 

 

وَجَعَلْنَا فِيهَا جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ وَفَجَّرْنَا فِيهَا مِنَ الْعُيُونِ ﴿٣٤﴾

34. Na Tukafanya humo mabustani ya mitende, na mizabibu, na Tukabubujua humo chemchemu.

 

 

 

لِيَأْكُلُوا مِن ثَمَرِهِ وَمَا عَمِلَتْهُ أَيْدِيهِمْ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ ﴿٣٥﴾

35. Ili wale katika matunda yake, na haikuyafanya hayo mikono yao Je, basi hawashukuru?

 

 

 

 

سُبْحَانَ الَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّهَا مِمَّا تُنبِتُ الْأَرْضُ وَمِنْ أَنفُسِهِمْ وَمِمَّا لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٦﴾

36. Utakasifu ni wa Ambaye Ameumba dume na jike katika vyote ambavyo inaotesha ardhi, na katika nafsi zao, na katika vile wasivyovijua.

 

 

 

 

وَآيَةٌ لَّهُمُ اللَّيْلُ نَسْلَخُ مِنْهُ النَّهَارَ فَإِذَا هُم مُّظْلِمُونَ ﴿٣٧﴾

37. Na Aayah (Ishara, Dalili) kwao ni usiku, Tunauvua humo mchana, basi tahamaki wao ni wenye kuwa kizani.

 

 

 

 

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٣٨﴾

38. Na jua linatembea hadi matulio yake.[11] Hayo ni Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.[12]

 

 

وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ ﴿٣٩﴾

39. Na mwezi Tumeukadiria vituo mpaka ukarudi (mwembamba) kama kwamba ni karara kongwe la shina la mtende lililopinda.

 

 

 

 

لَا الشَّمْسُ يَنبَغِي لَهَا أَن تُدْرِكَ الْقَمَرَ وَلَا اللَّيْلُ سَابِقُ النَّهَارِ ۚ وَكُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ ﴿٤٠﴾

40. Halipasi jua kuudiriki mwezi, wala usiku kuutangulia mchana, na vyote viko katika falaki vinaogelea.

 

 

 

 

وَآيَةٌ لَّهُمْ أَنَّا حَمَلْنَا ذُرِّيَّتَهُمْ فِي الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ ﴿٤١﴾

41. Na Aayah (Ishara, Dalili) kwao, ni kwamba Sisi Tumebeba vizazi vyao katika merikebu iliyosheheni.

 

 

 

 

وَخَلَقْنَا لَهُم مِّن مِّثْلِهِ مَا يَرْكَبُونَ ﴿٤٢﴾

42. Na Tukawaumbia kutoka mfano wake wa vile wanavyovipanda.

 

 

 

 

وَإِن نَّشَأْ نُغْرِقْهُمْ فَلَا صَرِيخَ لَهُمْ وَلَا هُمْ يُنقَذُونَ ﴿٤٣﴾

43. Na kama Tungetaka, Tungeliwagharikisha, basi hakuna wa kupiga kelele kuwasaidia na wala hawatookolewa.

 

 

 

إِلَّا رَحْمَةً مِّنَّا وَمَتَاعًا إِلَىٰ حِينٍ ﴿٤٤﴾

44. Isipokuwa Rehma kutoka Kwetu, na starehe kwa muda tu.

 

 

 

 

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّقُوا مَا بَيْنَ أَيْدِيكُمْ وَمَا خَلْفَكُمْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٤٥﴾

45. Na wanapoambiwa: Ogopeni yale yaliyo mbele yenu na yale yaliyo nyuma yenu ili mpate kurehemewa (wao huzidi jeuri).

 

 

 

 

 

وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ ﴿٤٦﴾

46. Na haiwafikii Aayah (Ishara, Dalili) yoyote katika Aayaat za Rabb wao, isipokuwa walikuwa ni wenye kuzikengeuka.

 

 

 

 

 

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنُطْعِمُ مَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ أَطْعَمَهُ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٤٧﴾

47. Na wanapoambiwa: Toeni katika vile Alivyokuruzukuni Allaah, wale waliokufuru husema kuwaambia walioamini: Je, tumlishe ambaye Allaah Angelitaka Angelimlisha? Nyinyi hamumo isipokuwa katika upotofu bayana.

 

 

 

 

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٨﴾

48. Na wanasema: Ni lini hiyo ahadi (ya kufufuliwa) mkiwa ni wasemao kweli?[13]

 

 

 

مَا يَنظُرُونَ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً تَأْخُذُهُمْ وَهُمْ يَخِصِّمُونَ ﴿٤٩﴾

49. Hawangojei isipokuwa ukelele mmoja tu, uwachukue hali wao wanakhasimiana.

 

 

 

فَلَا يَسْتَطِيعُونَ تَوْصِيَةً وَلَا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ يَرْجِعُونَ ﴿٥٠﴾

50. Basi hawatoweza kuusia, wala kurejea kwa ahli zao.

 

 

 

 

 

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ ﴿٥١﴾

51. Na litapulizwa baragumu[14], basi tahamaki wanatoka makaburini mwao wakienda mbio mbio kwa Rabb wao.

 

 

 

قَالُوا يَا وَيْلَنَا مَن بَعَثَنَا مِن مَّرْقَدِنَا ۜ ۗ هَـٰذَا مَا وَعَدَ الرَّحْمَـٰنُ وَصَدَقَ الْمُرْسَلُونَ ﴿٥٢﴾

52. Waseme: Ole wetu! Nani ametufufua katika malazo yetu? (Wataambiwa): Haya ndio Aliyoahidi Ar-Rahmaan na Rusuli walisema kweli.

 

 

 

 

إِن كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ جَمِيعٌ لَّدَيْنَا مُحْضَرُونَ ﴿٥٣﴾

53. Haitokuwa isipokuwa ukelele mmoja tu, tahamaki wote watahudhurishwa mbele Yetu.

 

 

 

 

فَالْيَوْمَ لَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٤﴾

54. Basi leo nafsi yoyote haitodhulumiwa kitu chochote, na wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

 

إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾

55. Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi.

 

 

 

 

 

هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾

56. Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea.

 

 

 

لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾

57. Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba.

 

 

 

 

سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾

58. Salaamun![15] Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

وَامْتَازُوا الْيَوْمَ أَيُّهَا الْمُجْرِمُونَ ﴿٥٩﴾

59. (Itasemwa): Na jitengeni leo enyi wahalifu.

 

 

 

 

أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٦٠﴾

60. Je, Sijakuusieni enyi wanaadam kwamba: Msimwabudu shaytwaan, hakika yeye kwenu ni adui bayana!

 

 

 

 

وَأَنِ اعْبُدُونِي ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٦١﴾

61. Na kwamba Niabuduni Mimi? Hii ndio njia iliyonyooka.

 

 

 

 

وَلَقَدْ أَضَلَّ مِنكُمْ جِبِلًّا كَثِيرًا ۖ أَفَلَمْ تَكُونُوا تَعْقِلُونَ ﴿٦٢﴾

62. Na kwa yakini (shaytwaan) amekwishawapotoa viumbe wengi miongoni mwenu. Je basi hamkuwa wenye kutia akilini?

 

 

 

هَـٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿٦٣﴾

63. Hii ni Jahannam ambayo mlikuwa mkiahidiwa.

 

 

 

 

اصْلَوْهَا الْيَوْمَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٦٤﴾

64. Ingieni leo humo muungue kwa sababu ya mlivyokuwa mkikufuru.

 

 

 

 

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾

65. Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na mikono yao itusemeshe na miguu yao itoe ushahidi kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.[16]  

 

 

 

 

وَلَوْ نَشَاءُ لَطَمَسْنَا عَلَىٰ أَعْيُنِهِمْ فَاسْتَبَقُوا الصِّرَاطَ فَأَنَّىٰ يُبْصِرُونَ ﴿٦٦﴾

66. Na lau Tungelitaka, Tungelipofua macho yao, wakashindana mbio kuitafuta njia, lakini kutoka wapi wataona?

 

 

 

 

وَلَوْ نَشَاءُ لَمَسَخْنَاهُمْ عَلَىٰ مَكَانَتِهِمْ فَمَا اسْتَطَاعُوا مُضِيًّا وَلَا يَرْجِعُونَ ﴿٦٧﴾

67. Na lau Tungelitaka, Tungeliwaumbua (na kuwalemaza) hapo mahali walipo, basi wasingeliweza kwenda mbele wala wasingerudi.   

 

 

 

 

وَمَن نُّعَمِّرْهُ نُنَكِّسْهُ فِي الْخَلْقِ ۖ أَفَلَا يَعْقِلُونَ ﴿٦٨﴾

68. Na yule Tunayempa umri mkubwa, Tunamrejesha nyuma katika umbo (kumdhoofisha). Je, basi hamtii akilini?

 

 

 

 

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾

69. Na Hatukumfunza (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mashairi[17] na wala haipasi kwake. Haya si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan bayana.

 

 

 

لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧٠﴾

70. Ili imuonye yule aliye hai,[18] na neno lihakikike juu ya makafiri.

 

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ ﴿٧١﴾

71. Je, hawaoni kwamba Sisi Tumewaumbia kutokana na yale iliyofanya Mikono Yetu wanyama wa mifugo, basi wao wakawa wanawamiliki?

 

 

 

 

وَذَلَّلْنَاهَا لَهُمْ فَمِنْهَا رَكُوبُهُمْ وَمِنْهَا يَأْكُلُونَ ﴿٧٢﴾

72. Na Tumewadhalilisha kwao, basi miongoni mwao ni vipando vyao na miongoni mwao wanawala?

 

 

 

 

وَلَهُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَمَشَارِبُ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ ﴿٧٣﴾

73. Na wanapata humo manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?

 

 

 

 

وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لَّعَلَّهُمْ يُنصَرُونَ ﴿٧٤﴾

74. Na wamejichukulia badala ya Allaah waabudiwa ili wakitumaini kuwa watanusuriwa!

 

 

 

لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَهُمْ وَهُمْ لَهُمْ جُندٌ مُّحْضَرُونَ ﴿٧٥﴾

75. Hawawezi kuwanusuru, na watahudhurishwa (adhabuni) kama askari dhidi ya hao (waliowaabudu).

 

 

 

 

فَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّا نَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ ﴿٧٦﴾

76. Basi yasikuhuzunishe maneno yao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Hakika Sisi Tunajua yale wanayoyaficha na yale wanayoyatangaza.

 

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ ﴿٧٧﴾

77. Je, binaadam haoni kwamba Sisi Tumemuumba kutokana na tone la manii, mara yeye anakuwa mpinzani bayana?[19]

 

 

 

 

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ ۖ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ ﴿٧٨﴾

78. Na akatupigia mfano, akasahau kuumbwa kwake akasema: Ni nani atakayehuisha mifupa hii na hali imeshaoza na kusagika na kuwa kama vumbi![20]

 

 

 

قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ ﴿٧٩﴾

79. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Ataihuisha Yule Aliyeianzisha mara ya kwanza. Naye Ni Mjuzi wa kila kiumbe.

 

 

 

 

الَّذِي جَعَلَ لَكُم مِّنَ الشَّجَرِ الْأَخْضَرِ نَارًا فَإِذَا أَنتُم مِّنْهُ تُوقِدُونَ ﴿٨٠﴾

80. Ambaye Amekujaalieni moto kutokana na miti ya kijani, kisha nyinyi mnauwasha.

 

 

 

 

أَوَلَيْسَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُم ۚ بَلَىٰ وَهُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ ﴿٨١﴾

81. Je, kwani Yule Aliyeumba mbingu na ardhi (mnadhani) Hana uwezo wa kuumba mfano wao? Sivyo hivyo (Anaweza bila shaka)!  Naye Ni Mwingi wa Kuumba Atakavyo, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾

82. Hakika Amri Yake Anapotaka chochote Hukiambia: Kun! (Kuwa), nacho huwa.

 

 

 

فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٣﴾

83. Basi Utakasifu Ni wa Ambaye Mkononi Mwake kuna ufalme wa kila kitu, na Kwake mtarejeshwa.

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Sababu Ya Kuteremshwa Aayah:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho chenye Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah au Suwrah:

 

036-Asbaabun-Nuzuwl: Yaasiyn Aayah 12: إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ

 

Mema Na Mabaya Aliyoyatanguliza Mtu Na Athari Za Hayo Yote Yanadhibitiwa:

 

Tafsiyr Ya Aayah: Hakika Sisi ndio Tunaohuisha wafu wote kwa kuwafufua Siku ya Qiyaamah. Na Tunaandika waliyoyafanya ya kheri na ya shari pamoja na athari zao njema ambazo wao walikuwa ndio sababu ya kufanyika katika maisha yao na baada ya kufa kwao kama vile mtoto mwema, ilimu yenye manufaa na swadaqa yenye kuendelea. Pia Tunaandika amali na athari zao mbaya kama vile ushirikina na uasi. Na Tumedhibiti kwa hesabu kila kitu katika Kitabu chenye ufafanuzi, ambacho ni Ummul-Kitaab, na humo ndio marejeo ya yote hayo, nacho ni Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa). Basi ni juu ya mwenye akili airudie nafsi yake, ili awe ni kiigizo katika wema ndani ya maisha yake na baada ya kufa kwake. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Na Hadiyth kadhaa zimethibitisha amali kubakia baada ya mtu kufariki. Miongoni mwazo ni:

 

Na Hadiyth kadhaa zimethibitisha amali kubakia baada ya mtu kufariki; Miongoni mwazo ni:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِذَا مَاتَ ابْنُ آدَم انْقَطَعَ عَمَلُهُ إلاَّ مِنْ ثَلاَث: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ  أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ)) مسلم

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Binaadam akifa, amali zake hukatika isipokuwa mambo matatu: Swadaqa inayoendelea, au ilimu inayonufaisha, au mtoto mwema anayemuombea duaa. [Muslim]

 

Pia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

 

 مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا ، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْءٌ . وَمَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً سَيِّئَةً فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ كُتِبَ عَلَيْهِ مِثْلُ وِزْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا ، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أَوْزَارِهِمْ شَيْءٌ   أخرجه مسلم في صحيحه

“Atakayefufua tendo jema katika Uislaam na watu wakalitenda baada yake, basi ataandikiwa ujira sawa na yule atakayelitenda, na hakipungui chochote katika ujira wao. Na atakayebuni kitendo kibaya katika Uislamu na watu wakakifanya baada yake, basi ataandikiwa dhambi sawa na yule atakayekifanya, na wala hakipungui chochote katika madhambi yao.” [Muslim]  

 

Na kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ 

“Tunaandika yale waliyoyakadimisha na athari zao.” [Yaasiyn (36:12)] 

 

Maelezo yamekuja katika Hadiyth ifuatayo:

 

حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ حَوْشَبٍ، قَالَ حَدَّثَنَا عَبْدُ الْوَهَّابِ، قَالَ حَدَّثَنَا حُمَيْدٌ، عَنْ أَنَسٍ، قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ يَا بَنِي سَلِمَةَ أَلاَ تَحْتَسِبُونَ آثَارَكُمْ ‏"‏‏.‏ وَقَالَ مُجَاهِدٌ فِي قَوْلِهِ ‏وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ   قَالَ خُطَاهُمْ‏.‏ وَقَالَ ابْنُ أَبِي مَرْيَمَ أَخْبَرَنَا يَحْيَى بْنُ أَيُّوبَ، حَدَّثَنِي حُمَيْدٌ، حَدَّثَنِي أَنَسٌ، أَنَّ بَنِي سَلِمَةَ، أَرَادُوا أَنْ يَتَحَوَّلُوا، عَنْ مَنَازِلِهِمْ، فَيَنْزِلُوا قَرِيبًا مِنَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ فَكَرِهَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ يُعْرُوا ‏{‏الْمَدِينَةَ‏}‏ فَقَالَ ‏"‏ أَلاَ تَحْتَسِبُونَ آثَارَكُمْ ‏"‏‏.‏ قَالَ مُجَاهِدٌ خُطَاهُمْ آثَارُهُمْ أَنْ يُمْشَى فِي الأَرْضِ بِأَرْجُلِهِمْ‏.‏

Amesimulia Humayd (رضي الله عنه):  Anas amesema:  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi Bani Salimah! Hamdhanii kuwa kwa kila hatua mnayopiga (kuelekea Msikitini) kuna malipo?” Mujaahid akasema kuhusu Kauli Yake Allaah (عزّ وجلّ): 

 وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ 

“Tunaandika yale waliyoyakadimisha na athari zao.” [Yaasiyn (36:12)]

 

Na Anas alisema kuwa watu wa Bani Salimah walitaka kuhamia sehemu ambayo ni jirani na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Lakini Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakupendezwa na fikra ya kuhama makazi yao akawaambia: “Hamdhani ya kuwa mtalipwa kwa nyayo zenu?” Mujaahid alisema: “Nyayo zao ina maana ya hatua zao za kwenda kwa miguu.” [Al-Bukhaariy]

 

[3] Watu Wa Mji:

 

Ibn ‘Abbaas na Salaf wengineo wamesema Ni mji wa Antwaakiyyah (Antioch) ambao alikuweko mfalme akiitwa Antiochus ambaye alikuwa akiabudu masanamu. Allaah (سبحانه وتعالى) Akawatumia wajumbe watatu ambao majina yao ni Swaadiq, Swaduwq na Shaluwm, nao wakawakanusha.  [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

[4] Rusuli Au Wajumbe Waliotumiwa:

 

‘Ulamaa wa Tafsiyr wamekhitilafiana katika kauli mbili kuhusu hao kama walikuwa ni Rusuli wa Allaah (عزّ وجلّ) au walikuwa ni wajumbe wa Nabiy ‘Iysaa ‘(عليه السّلام).

 

(i) Ni Rusuli wa Allaah kwa sababu Rusuli wa Allaah ni wengi kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ

“Na kwa yakini Tuliwapeleka Rusuli kabla yako. Miongoni mwao wako Tuliokusimulia na miongoni mwao wako ambao Hatukukusimulia.” [Ghaafir (40:78)]

 

Kauli hii imenukuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ka’b Al-Ahbaar na Wahab bin Munabbih. Lakini kauli hii haisihi kuwanasibishia, kwani Atw-Twabariy ameisimulia katika Jaami’u Al-Bayaan (20/500) ikiwa na mkatiko wa wazi katika Isnaad yake. Na Ibn Taymiyyah ameinukulu katika Al-Jawaab Asw-Swahiyh (2/247), kutokana na kauli ya Abuu Al-‘Aaliyah aliposema kuhusu wao: “Wakasema: Sisi ni Rusuli wa Rabb wa walimwengu.”

 

Kauli hii imekhitariwa na Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na Al-Haafidhw Ibn Kathiyr waliohakiki suala, na pia Imaam As-Sa’diy ameitegemea katika Tafsiyr yake “Taysiyr Al-Kariym Ar-Rahmaan (Uk. 693).

 

(ii) Hao ni wajumbe wa Nabiy ‘Iysaa mwana wa Maryam ambao aliwatuma katika mji wa Antwaakiyah. Na kauli hii imewafikiwa na ‘Ulamaa wengineo.

 

[5] Ada Ya Washirikina Kutokutaka Kutumiwa Wanaadam Kama Wao. 

 

Rejea Suwrah Al-Furqaan (25:7) kwenye maelezo bayana.

 

[6] Itikadi Za Shirki Kutabiria Mambo Ya Ghaibu:

 

Maana ya tatwayyur au twiyarah ni itikadi ya kutabiria nuksi, kisirani, mikosi na kadhaalika.

 

Katika itikadi za washirikina, walikuwa wakichukua ndege (طير) na humtumilia kutabiri mambo ya ghaibu kwa kutaka kujua kama kuna ishara nzuri au mbaya katika jambo. Mfano wanapotaka kusafiri humrusha ndege yule, akiruka upande wa kulia, basi wanaamini kuwa ni safari ya salama, na kama akiruka upande wa kushoto, basi huwa hawasafiri. Uislamu umekuja na kuondoa shirki kama hiyo kama alivyoharamisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth kadhaa, miongoni mwa hizo ni: 

 

عَنْ أَنَسٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لَا عَدْوَى وَلَا طِيَرَةَ وَيُعْجِبُنِي الْفَأْلُ))  قَالُوا:  وَمَا الْفَأْلُ؟ قَالَ: ((الْكَلِمَةُ الطَّيِّبَةُ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه):   Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna ‘adwaa wala hakuna twiyarah (itikadi ya kutabiri mkosi, nuksi) na inanipendekeza Al-Fa-l.” Wakauliza: Nini Al-Fa-lu? Akajibu: “Neno zuri.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na pia:

 

عن ابْنِ مَسْعُودٍ مَرْفُوعًا: ((الطِّيَرَةُ شِرْكٌ، الطِّيَرَةُ شِرْكٌ، وَمَا مِنَّا إِلاَّ وَلَكِنَّ اللَّهَ يُذْهِبُهُ بِالتَّوَكُّلِ)) رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَالتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ. وَجَعَلَ آخِرَهُ مِنْ قَوْلِ ابْنِ مَسْعُودٍ

Amesimulia Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atw-Twiyarah (itikadi ya kutabiri nuksi, mikosi n.k) ni shirki! Atw-Twiyarah ni shirki. Na hakuna yeyote miongoni mwetu asiyehisi jambo moyoni (kuhusu Atw-Twiyarah) lakini Allaah Huiondoa kwa kutawakali Kwake.” [Hadiyth Marfuw’ ameipokea Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth hii Hasan Swahiyh - Na imetajwa kwamba kauli ya mwisho ni ya Ibn Mas’uwd]

 

Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akafundisha kubadilisha hayo kwa:

 

عنْ عُرْوَةَ بْنِ عامِرِ (رضي الله عنه) قال: ذُكِرتِ الطَّيَرَةُ عِنْد رَسُولِ اللَّه صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فقَالَ: ((أحْسَنُهَا الْفَألُ، وَلا تَرُدُّ مُسْلِماً، فَإذا رأى أحَدُكُمْ ما يَكْرَه، فَلْيقُلْ: اللَّهُمَّ لا يَأتى بالحَسَناتِ إلاَّ أنتَ، وَلا يَدْفَعُ السَّيِّئاتِ إلاَّ أنْتَ، وَلا حوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بك)) حديثٌ صَحيحٌ رَوَاهُ أبو داودُ بإسنادٍ صَحيحٍ

Amesimulia ‘Urwah bin ‘Aamir (رضي الله عنه): Ilitajwa habari ya kupiga fali mbaya (mkosi) mbele ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ilio bora zaidi ni kupiga fali nzuri, wala (kupiga fali mbaya) haimrudishi Muislamu (kutokutenda aliloazimia). Mmoja wenu atakapoona analochukia, aseme:

 

اللَّهُمَّ لا يَأتى بالحَسَناتِ إلاَّ أنتَ، وَلا يَدْفَعُ السَّيِّئاتِ إلاَّ أنْتَ، وَلا حوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بك

Ee Allaah, hakuna anayeweza kuleta mambo mema isipokuwa ni Wewe, wala hakuna anayeweza kukinga mabaya isipokuwa ni Wewe. Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kutoka Kwako. [Hadiyth Swahiyh ameipokea Abu Daawuwd kwa Isnaad Swahiyh]

 

[7] Mtu Aliyetoka Mbali Ya Mji:

 

Salaf wamesema kuwa jina lake ni Habiyb na wengine wamesema ni Habiyb Bin Muraa.

 

Watu wa mji walidhamiria kuwaua Rusuli (au wajumbe) wao, basi akawajia mtu mbio kutoka upande wa mbali wa mji ili kuwanusuru na watu wao. Naye ni Habiyb ambaye alikuwa ni msukaji kamba, na alikuwa mgonjwa wa ukoma uliomwathiri kwa haraka. Na alikuwa akitoa swadaqa kwa wingi, akitoa nusu ya mapato yake kama swadaqa, na alikuwa na mwono ulionyooka. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[8] Takrima Ya Mtu Mwema Ya Kuingizwa Jannah (Peponi):

 

Aayah hii namba (25) na ifuatayo namba (26).

 

Kutoka kwa baadhi ya Swahaba, kutoka Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه)  amesema: Walimkanyaga na kumponda ponda kwa miguu yao mpaka bomba lake la kupitisha hewa likatokea kwenye duburi yake. Allaah (سبحانه وتعالى)  Akamuingiza Jannah akiwa anaruzukiwa humo kila aina ya neema za kudumu. Na hivyo ni jazaa na thawabu kutokana na subira yake na himma yake ya kuwalingania watu wake wahidike.  Na akaondoshewa ugonjwa wake duniani, na huzuni yake na mateso yake. Basi alipoingizwa humo akasema: Laiti watu wangu wangelijua.” Takrima za Allaah humo kwake.  [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[9] Aayah (آية) : Ishara, Ushahidi Wa Muumbaji, Mkadiriaji, Mweza Na Kadhaalika:

 

Rejea Ash-Shu’araa (26:8) kwenye maana za آية (Aayah) au  آيات   (Aayaat).

 

Aayah zifuatazo, kama vile Aayah katika Suwrah nyenginezo, mfano: An-Nahl (16:11-13), Ar-Ruwm (30:20-25),  zimetajwa  آية (Aayah) au  آيات   (Aayaat) ambazo maana zake ni: Ishara, Dalili, Hoja, Burhani, Muujiza, Mazingatio, Mafunzo, Ushahidi na kadhaalika. Aayah ua Aayaat hizo, ni dalili ya wazi kubisa za Uwepo wa Allaah (سبحانه وتعالى) Muumbaji wa kila kitu, na kwamba Ni Mmoja Pekee na Hana mshirika katika Uumbaji Wake, hivyo basi Yeye Ndiye Anayestahiki kuabudiwa.

 

Na kuhusu kuwaradd washirikina kwamba hawawezi kuleta uumbaji kama Uumbaji wa Allaah (سبحانه وتعالى), rejea Luqmaan (31:10-11) na Al-Ahqaaf (46:4) kwenye maelezo bayana na rejea nyenginezo. 

 

[10] Allaah (سبحانه وتعالى) Kuhuisha Ardhi Iliyokufa Ni Mfano Wa Kufufuliwa Watu:

 

Rejea Ar-Ruwm (30:50), Al-An’aam (6:95).

 

[11] Jua Linaomba Idhini Kusujudu Chini Ya ‘Arsh:

 

Rejea Al-Hajj (22:18).

 

[12] Takdiri: Qudura, Uwezo Wa Allaah (سبحانه وتعالى), Ukadiriaji:

 

Katika Aayah za Suwrah hii tukufu Yaasiyn (36:33-42), Allaah (سبحانه وتعالى) Anadhihirisha Qudura (Uwezo) na Takdiri (Ukadiriaji) Yake katika kuumba vitu ulimwenguni; katika ardhi, bahari na falaki (angani) kwa ajili ya manufaa ya viumbe Vyake ili waweze kuishi katika ulimwengu huu.

 

Katika Aayah za Suwrah hii tukufu Yaasiyn (36:33-42), Allaah (سبحانه وتعالى) Anadhihirisha Qudura (Uwezo) na Takdiri (Ukadiriaji) Yake katika kuumba vitu ulimwenguni; katika ardhi, bahari na falaki (angani) kwa ajili ya manufaa ya viumbe Vyake ili waweze kuishi katika ulimwengu huu.

 

Vya ardhini ni kama mimea ya kila aina, mazao na matunda yake, majani, na miti shamba yenye shifaa (poza) ya maradhi. Pia Ameumba milima na majabali ambayo nayo yana faida mbalimbali kama kuweko ndani yake mapango ya kujifichia, na nyuki ambao Allaah Amewapa ilhamu waende humo kutoa asali yenye shifaa ya maradhi pamoja na faida nyenginezo. Rejea An-Nahl (16:68-69). Pia Ameumba wanyama wa ardhini, Akahalalisha baadhi yao nyama zao kuliwa na kunywewa maziwa yao. Baadhi yao wanatoa sufi na wengine ngozi ambazo wanaadam wananufaika nazo kwa kutengenezea nguo, fanicha na vifaa mbalimbali. Rejea An-Nahl (16:80). Na pia Amewatiisha wanyama wengineo kwa binaadam ili wawatumie kwa vipando na utumikaji wa mashambani na kadhaalika. Rejea Suwrah hii Yaasiyn (36:71-73), na pia An-Nahl (16:5-8). Pia katika tumbo la ardhi, Allaah Amejaalia ipatikane humo gesi na petroli vitu ambavyo vinahitajika katika matumizi ya wanaadam.  Pia humo ardhini, Allaah Amejaalia yapatikane madini yanayochimbwa ambayo yana umuhimu mkubwa mno katika maisha ya wanaadam kama vile metali, chuma, shaba, zinki, nikeli, bati, risasi. n.k. Hali kadhaalika, zinapatikana humo dhahabu, almasi, fedha na johari nyenginezo za thamani ambazo wanaadam wananufaika nazo kwa mapambo na biashara. Haya yote na mengineyo mengi mno tunayoyajua na tusiyoyajua, tunayoyakumbuka na tusiyoyakumbuka ni katika Neema na Fadhila za Allaah (سبحانه وتعالى) na ni “Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.”

 

Na baharini, Allaah Amejaalia pia ipatikane nyama safi ya kila aina ya samaki. Vile vile Amejaalia baharini kuweko vitu vya thamani vya mapambo kama lulu na marijani. Na pia Uwezo Wake wa Kuitiisha bahari hata merikebu ziweze kupita kuwasafirisha watu ulimwenguni huku zikibeba mizigo mikubwa mno. Haya yote na mengineyo mengi mno tunayoyajua na tusiyoyajua, tunayoyakumbuka na tusiyoyakumbuka ni katika “Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.”

 

Na katika falaki (angani), Allaah Amewawezesha ndege waruke bila ya kushikiliwa na chochote. Rejea Al-Mulk (67:19), An-Nahl (16:79), na An-Nuwr (24:41). Na katika Uwezo na Qudura Yake, ni kutiisha anga ili ndege za kuwasafirisha watu ulimwenguni na mizigo ziweze kupaa na kupita. Hali kadhalika, Anatiisha  mawingu ya mvua huko mbinguni, mvua ikawateremkia wanaadam na wanyama wapate kunywa na kulisha wanyama wao na iwanyeshee mashambani mwao.  Isitoshe, katika falaki (angani), Allaah Ameumba sayari mbali mbali pamoja na jua, mwezi, nyota n.k ambavyo Anavithibiti na Kuviendesha kwa ajili ya kupata usiku na mchana, na kuendeleza mzunguko wake ili yapatikane  masaa, masiku na miaka. Rejea Al-Israa (17:12). Na Uendeshaji Wake huo wa sayari, jua, mwezi, nyota n.k hauendi kinyume wala hausimami hadi Atakapotaka Mwenyewe. Haya yote na mengineyo mengi mno tunayoyajua na tusiyoyajua, tunayoyakumbuka na tusiyoyakumbuka ni katika “Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.”

 

Hizo ndizo Neema Zake, miongoni mwa Neema nyingi mno ambazo baadhi yake tunazijua na tunazikumbuka, na baadhi nyingine hatuzijui wala hatuzikumbuki, hivyo hatuwezi kuziorodhesha hesabuni. Rejea Suwrah Ibraahiym (14:34) ambako kuna maelezo kuhusu Neema za Allaah (عزّ وجلّ) na kwamba  haiwezekani kuziorodhesha hesabuni.

 

Na Neema hizi zote ni uthibitisho juu ya Uwezo Wake mkubwa. Na Anazitaja katika Aayah nyingi nyenginezo ambazo miongoni mwazo zipo kwenye Aal-‘Imraan (3:190), na (3:26-27), Al-An’aam (6:96), Ibraahiym (14:32-33), An-Nahl (16:3-16), (16:66-69), na (16:81), Al-Hajj (22:65), Luqmaan (31:20), Al-Jaathiyah (45:12-13), Ar-Ra’d (13:2-4), Az-Zumar (39:5), Al-Baqarah (2:164), Al-A’raaf (7:54), Faatwir (35:12-13), na kwengineko katika Qur-aan.

 

Basi hayo yote ni dalili juu ya Upweke wa Allaah (عزّ وجلّ), na Uumbaji Wake ambao hakuna yeyote awezaye kuumba kama Anavyoumba Yeye Allaah (عزّ وجلّ). Ndipo Anawataka washirikina na makafiri walete wao uumbaji wao kama huu kama wanaweza! Rejea Luqmaan (31:10-11), Al-Ahqaaf (46:4) kwenye maelezo bayana na rejea nyenginezo.

 

[13] Ada Ya Makafiri Kuuliza Lini Ahadi Ya Kutokea Qiyaamah Itatimizwa:

 

Rejea Yuwnus (10:48).

 

[14] Baragumu 

 

Rejea An-Naml (27:87), Az-Zumar (39:68) kwenye faida na maelezo bayana.

 

[15] Salaam, Salaamun ‘Alaykum Ni Maamkizi Ya Jannah (Peponi).

 

Kama vile ilivyokuwa maamkizi ya Waislamu duniani ni Assalaamu ‘alaykum, na Peponi pia maamkizi ni hayo hayo. Bali huko ni maamkizi yatokayo kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na mara nyengine kutoka kwa Malaika, na mara nyengine ni maamkizi baina ya Waumini kwa Waumini.

 

Rejea Al-A’raaf (7:46), Yuwnus (10:10), Ar-Ra’d (13:24), Ibraahiym (14:23), An-Nahl (16:32), Al-Ahzaab (33:44), Az-Zumar (39:73), Al-Furqaan (25:75), Qaaf (50:34),

 

Na Jannah pia imeitwa Daarus-salaam (Nyumba ya amani). Rejea Al-An’aam (6:127), Yuwnus (10:25).

 

[16] Viungo Vya Mwili Vitashuhudia Matendo Ya Binaadam:

 

Rejea Fusw-Swilat: (41:20-22), An-Nuwr (24:24).

 

Na binaadam hataweza kukanusha ovu lolote alilolitenda duniani: Rejea Al-Israa (17:13-14).

 

[17] Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) Si Mshairi:

 

Tafsiyr ya Aayah (69-70):

 

Na Sisi Hatukumfundisha Rasuli Wetu Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) mashairi, na haiwezekani kabisa yeye kuwa mshairi. Hiki alichokuja nacho si kingine chochote bali ni ukumbusho ambao wenye akili huuzingatia na kuukumbuka. Ukumbusho huu ni hii Qur-aan ambayo inaweka wazi haki na baatwil kwa dalili bayana, na inabainisha hukumu zake, sharia zake na mawaidha yake kwa lugha nyepesi, ili apate kuonyeka na kufaidika kila mwenye moyo ulio hai na baswiyrah yenye nuru, na adhabu ipate kuthibitika kwa wenye kumpinga Allaah. Kwa hawa, Hoja ya Allaah isiyo na utata wowote ambayo imebainishwa na Qur-aan, itakuja kusimama dhidi yao. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi na rejea mbalimbali kuhusu: Kufru Za Washirikina Kumkanusha, Kumsingizia, Kumpachika Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) Sifa Kadhaa Ovu, Kumfanyia Istihzai Yeye Pamoja Na Kuifanyia Istihzai Qur-aan Na Kuikanusha:

 

[18] Qur-aan Imuonye Hai:

 

Qur-aan imuonye ambaye moyo wake uko hai na wenye fahamu, kwani huyo ndiye anayetakaswa na hii Qur-aan, na ndiye anayezidisha ilimu na amali kutoka humo, na Qur-aan inakuwa kwa  moyo wake kama mvua kwa ardhi nzuri yenye kuotesha kwa wingi. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[19] Sababu Ya Kuteremshwa Aayah:

 

Kuanzia Aayah hii (77) hadi Aayah namba (83), bonyeza kiungo kifuatacho chenye Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah au Suwrah.

 

036-Asbaabun-Nuzuwl: Yaasiyn Aayah 77-83: أَوَلَمْ يَرَ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ

 

[20] Washirikina Hawakuamini Kwamba Watafufuliwa:

 

Rejea Al-Israa (17:49-52) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali kuhusu makafiri kutokuamini kufufuliwa. Rejea pia Al-Waaqi’ah (56:47-50), Ar-Ra’d (13:5). Na pia zifuatazo ni baadhi ya Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى) kuthibitisha Uwezo Wake wa kuwafufua viumbe:

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَلَّن نَّجْمَعَ عِظَامَهُ﴿٣﴾ بَلَىٰ قَادِرِينَ عَلَىٰ أَن نُّسَوِّيَ بَنَانَهُ﴿٤﴾

“Je, anadhani binaadam kwamba Hatutoikusanya mifupa yake? Sivyo hivyo! Bali Tuna Uwezo wa kusawazisha sawasawa ncha za vidole vyake.” [Al-Qiyaamah (75:3-4)]

 

Rejea pia:

 

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ ۚ بَلَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٣٣﴾

“Je, hawaoni kwamba Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na wala Hakuchoka kwa kuziumba kwake, kwamba Yeye Ni Muweza wa Kuwafufua wafu. Naam bila shaka!  Hakika Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza.” [Al-Ahqaaf (46:33)]

 

 

Share