058 - Al-Mujaadalah

 

  الْمُجَادلَة

 

058-Al-Mujaadalah

 

058-Al-Mujaadalah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

قَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّـهِ وَاللَّـهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ﴿١﴾

1. Allaah Amekwishasikia kauli ya yule mwanamke anayejadiliana nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mumewe, na anamshitakia Allaah, na Allaah Anayasikia majibizano yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.[1]

 

 

 

 

الَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِنكُم مِّن نِّسَائِهِم مَّا هُنَّ أُمَّهَاتِهِمْ ۖ إِنْ أُمَّهَاتُهُمْ إِلَّا اللَّائِي وَلَدْنَهُمْ ۚ وَإِنَّهُمْ لَيَقُولُونَ مُنكَرًا مِّنَ الْقَوْلِ وَزُورًا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ﴿٢﴾

2. Wale miongoni mwenu wanaowatamkia wake zao dhwihaar,[2] hao wake zao si mama zao. Hawakuwa mama zao isipokuwa wale waliowazaa. Na hakika wao bila shaka wanasema yasiyokubalika na kauli ya kuchukiza na uongo. Na hakika Allaah bila shaka Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria.  

 

 

 

 

وَالَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِن نِّسَائِهِمْ ثُمَّ يَعُودُونَ لِمَا قَالُوا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مِّن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا ۚ ذَٰلِكُمْ تُوعَظُونَ بِهِ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴿٣﴾

3. Na wale wanaowatamkia wake zao dhwihaar, kisha wakarudi katika waliyoyasema (kuitengua dhwihaar), basi (adhabu yao) ni kuacha huru mtumwa kabla ya kugusana. Hayo mnawaidhiwa kwayo. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

 

فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ مِن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا ۖ فَمَن لَّمْ يَسْتَطِعْ فَإِطْعَامُ سِتِّينَ مِسْكِينًا ۚ ذَٰلِكَ لِتُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۚ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۗ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤﴾

4. Na yule asiyepata (mtumwa au thamani yake) basi (afunge) Swiyaam miezi miwili mfululizo kabla ya kugusana. Na yule asiyeweza, basi alishe chakula masikini sitini. Hivyo ili mumuamini Allaah na Rasuli Wake. Na hiyo ni Mipaka ya Allaah. Na makafiri watapata adhabu iumizayo.

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يُحَادُّونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ كُبِتُوا كَمَا كُبِتَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ وَقَدْ أَنزَلْنَا آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ ۚ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ مُّهِينٌ﴿٥﴾

5. Hakika wale wanaopinzana na Allaah na Rasuli Wake wamefedheheshwa kama walivyofedheheshwa wale wa kabla yao. Na Tumekwishateremsha Aayaat bayana, na makafiri watapata adhabu ya kudhalilisha.[3]

 

 

 

 

يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا ۚ أَحْصَاهُ اللَّـهُ وَنَسُوهُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٦﴾

6. Siku Atakayowafufua Allaah wote, Awajulishe yale waliyoyatenda. Allaah Ameyatia hesabuni barabara nao wameyasahau. Na Allaah Ni Shahidi juu ya kila kitu.

 

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧﴾

7. Je, huoni kwamba Allaah Anajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye Ni wa Nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye Ni wa Sita wao, na wala chini kuliko ya hivyo, na wala wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao (kwa Ujuzi Wake)[4] popote watakapokuwa. Kisha Siku ya Qiyaamah Atawajulisha yale waliyoyatenda. Hakika Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi.

 

 

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ نُهُوا عَنِ النَّجْوَىٰ ثُمَّ يَعُودُونَ لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَيَتَنَاجَوْنَ بِالْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَمَعْصِيَتِ الرَّسُولِ وَإِذَا جَاءُوكَ حَيَّوْكَ بِمَا لَمْ يُحَيِّكَ بِهِ اللَّـهُ وَيَقُولُونَ فِي أَنفُسِهِمْ لَوْلَا يُعَذِّبُنَا اللَّـهُ بِمَا نَقُولُ ۚ حَسْبُهُمْ جَهَنَّمُ يَصْلَوْنَهَا ۖ فَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴿٨﴾

8. Je, huwaoni wale waliokatazwa kunong’ona, kisha wanarudia yale waliyokatazwa! Na wananong’onezana kuhusu dhambi na uadui na kumuasi Rasuli. Na wanapokujia wanakuamkia kwa maamkizi Asiyokuamkia kwayo Allaah, na wanasema katika nafsi zao: Mbona Allaah Hatuadhibu kwa yale tunayoyasema?! Jahannam inawatosheleza, wataingia waungue. Basi ubaya ulioje mahali pa kuishia![5]

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا تَنَاجَيْتُمْ فَلَا تَتَنَاجَوْا بِالْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَمَعْصِيَتِ الرَّسُولِ وَتَنَاجَوْا بِالْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴿٩﴾

9. Enyi walioamini! Mnaponong’onezana, basi msinong’onezane kuhusu dhambi na uadui na kumuasi Rasuli, bali nong’onezaneni kuhusu wema na taqwa. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake Pekee mtakusanywa.

 

 

 

 

 

إِنَّمَا النَّجْوَىٰ مِنَ الشَّيْطَانِ لِيَحْزُنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيْسَ بِضَارِّهِمْ شَيْئًا إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿١٠﴾

10. Hakika mnong’ono unatokana na shaytwaan ili awahuzunishe wale walioamini, na wala hawezi kuwadhuru chochote isipokuwa kwa Idhini ya Allaah. Na kwa Allaah watawakali Waumini.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قِيلَ لَكُمْ تَفَسَّحُوا فِي الْمَجَالِسِ فَافْسَحُوا يَفْسَحِ اللَّـهُ لَكُمْ ۖ وَإِذَا قِيلَ انشُزُوا فَانشُزُوا يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴿١١﴾

11. Enyi walioamini! Mnapoambiwa: Fanyeni nafasi katika mabaraza, basi fanyeni nafasi, Allaah Atakufanyieni nafasi. Na mnapoambiwa: Inukeni, basi inukeni, Allaah Atawainua wale walioamini miongoni mwenu, na waliopewa ilimu wana daraja nyingi. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَاجَيْتُمُ الرَّسُولَ فَقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَةً ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَأَطْهَرُ ۚ فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾

12. Enyi walioamini! Mnapotaka kushauriana siri na Rasuli basi kadimisheni swadaqa kabla ya mnong’ono wenu. Hivyo ni kheri kwenu na utakaso zaidi. Na msipopata, basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.[6]

 

 

 

 

أَأَشْفَقْتُمْ أَن تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَاتٍ ۚ فَإِذْ لَمْ تَفْعَلُوا وَتَابَ اللَّـهُ عَلَيْكُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٣﴾

13. Je, mnakhofu (umasikini kwa) kukadimisha swadaqa kabla ya mnong’ono wenu? Ikiwa hamjafanya na Allaah Akapokea tawbah yenu, basi simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Allaah na Rasuli Wake. Na Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo.

 

 

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ تَوَلَّوْا قَوْمًا غَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مَّا هُم مِّنكُمْ وَلَا مِنْهُمْ وَيَحْلِفُونَ عَلَى الْكَذِبِ وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴿١٤﴾

14. Je, hukuona wale waliofanya urafiki na watu ambao Allaah Ameghadhibika nao?  Wao si miongoni mwenu na wala si miongoni mwao, na wanaapia uongo nao wanajua.[7]

 

 

 

 

أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا ۖ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿١٥﴾

15. Allaah Amewaandalia adhabu kali. Ni uovu mbaya kwa hakika wa waliyokuwa wakiyatenda.

 

 

 

 

اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ فَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ﴿١٦﴾

16. Wamevifanya viapo vyao kuwa ni kinga na hivyo wakazuia Njia ya Allaah. Basi watapata adhabu idhalilishayo.

 

 

 

 

 

لَّن تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا ۚ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴿١٧﴾

17. Hazitowafaa kitu chochote mali zao wala watoto wao mbele ya Allaah.[8] Hao ni watu wa motoni, wao humo watadumu.

 

 

 

 

يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيَحْلِفُونَ لَهُ كَمَا يَحْلِفُونَ لَكُمْ ۖ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ عَلَىٰ شَيْءٍ ۚ أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْكَاذِبُونَ﴿١٨﴾

18. Siku Atakayowafufua Allaah wote, watamwapia kama wanavyokuapieni nyinyi, na watadhania kwamba wameegemea kitu (cha kuwafaa). Tanabahi!  Hakika wao ni waongo.

 

 

 

 

اسْتَحْوَذَ عَلَيْهِمُ الشَّيْطَانُ فَأَنسَاهُمْ ذِكْرَ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ الشَّيْطَانِ ۚ أَلَا إِنَّ حِزْبَ الشَّيْطَانِ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿١٩﴾

19. Shaytwaan amewatawala, akawasahaulisha kumdhukuru Allaah. Hao ndio kundi la shaytwaan. Tanabahi! Hakika kundi la shaytwaan ndio lenye kukhasirika.

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يُحَادُّونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ أُولَـٰئِكَ فِي الْأَذَلِّينَ﴿٢٠﴾

20. Hakika wale wanaopinzana na Allaah na Rasuli Wake, hao ndio katika waliodhalilishwa.

 

 

 

 

كَتَبَ اللَّـهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي ۚ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ﴿٢١﴾

21. Allaah Amekwishaandika kwamba: Bila shaka Nitashinda Mimi na Rusuli Wangu.  Hakika Allaah Ni Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika.

 

 

 

 

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ ۖ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ ۚ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٢٢﴾

22. Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanafanya urafiki na kuwapenda wanaompinga Allaah na Rasuli Wake, japo wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao (Allaah) Amewaandikia katika nyoyo zao imaan, na Akawatia nguvu kwa Ruwh[9] (Wahyi) kutoka Kwake, na Atawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito wadumu humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio Kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika Kundi la Allaah ndio lenye kufaulu.[10]

 

[2] (ظِهَارُ) Dhwihaar:

 

“Dhwihaar” (ظِهَارُ)imetokana na neno “dhwahr”(ظَهْرُ) ; kwa maana ya mgongo au nyuma.  Ni kumfananisha mke wa mtu na mgongo wa mama yake. Aina hii ya mazungumzo katika lugha ya kiarabu ina maana ya kuwa: “Wewe ni kama mama yangu, na ni haraam kwa ndoa yangu, au kukuoa au kukuingilia.” Kulingana na istilahi za kisharia, “dhwihaar” ni kumfananisha mke wa mtu na mama wa mtu na hivyo kumfanya kuwa ni haraam kwake. Jambo hili kisharia halizingatiwi kuwa ni talaka, lakini ni lazima mtu atoe kafara kabla ya kumrudia mke wake. Kafara yake ni kumuacha huru mtu mtumwa, au kufunga Swiyaam siku sitini kwa mfululizo, au kuwalisha maskini sitini. Hukumu hii imetajwa katika Suwrah Al-Mujaadalah (58:3-4). Ni wajibu kutekeleza moja ya adhabu hizo. Bonyeza viungo vifuatavyo kwa faida nyenginezo:

 

09-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Nikaah: Mlango Wa Al-Iylaa, Dhwihaar, Kafaara

 

 

[3] Aina Za Adhabu Katika Qur-aan:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja aina mbalimbali za adhabu katika Qur-aan na kila moja ina sifa yake. Miongoni mwazo ni hizi zifuatazo pamoja na baadhi ya rejea zake:

 

عذاب عظيم Adhabu kuu kabisa. Rejea An-Nuwr (24:14).

 

عذاب كبير Adhabu kubwa. Rejea Al-Furqaan (25:19)

 

  عذاب اليمAdhabu ya kuumiza. Rejea Al-Maaidah (5:36).

 

عذاب مهين Adhabu ya kudhalilisha. Rejea Luqmaan (31:6).

 

عذاب مقيم Adhabu ya kudumu. Rejea Az-Zumar (39:40).  

 

عذاب غليظ Adhabu ngumu. Rejea Fusw-Swilat (41:50).

 

عذاب شديد Adhabu kali. Rejea Sabaa (34:46).

 

عذاب الحريق Adhabu ya kuunguza. Rejea Al-Buruwj (85:10).

 

عذاب النار  Adhabu ya moto. Rejea Al-Anfaal (8:14).

 

عذاب الخزي Adhabu ya hizaya. Rejea Yuwnus (10:98).

 

عذاب السعير Adhabu ya moto uliowashwa vikali mno. Rejea Al-Mulk (67:5).

 

عذاب الخلد  Adhabu ya kudumu milele. Rejea As-Sajdah (32:14).

 

عذاب واصب Adhabu ya kuendelea. Rejea Asw-Swaaffaat (37:9).

 

عذاب النكر Adhabu kali kabisa ya kukirihisha, isiyovumilika. Rejea Al-Kahf (18:87).

 

عذاب حميم Adhabu ya maji yachemkayo mno. Rejea Ad-Dukhaan (44:48).

 

عذاب السموم Adhabu ya moto unaobabua. Rejea Atw-Twuur (52:27).

 

عذاب مستقر Adhabu ya  kuendelea. Rejea Al-Qamar (54:38).

 

Rejea Al-Hashr (59:4) kwenye faida kuhusu tofauti ya adhabu na ikabu:

 

[4] Allaah (سبحانه وتعالى) Huwa Yuko Pamoja Na Viumbe Vyake Kwa Ujuzi Wake.

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anapotaja kuwa Yuko pamoja na Viumbe Vyake basi inamaanisha kwamba Yuko pamoja nao kwa Ujuzi Wake. Bali Yeye Amethibitisha kuwa Yuko mbinguni kwa Dhati Yake. Na hii ni ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah. Rejea Al-Mulk (67:16), Al-A’raaf (7:54). 

 

Ilokusudiwa ya kuwa huko ni kuwa Yeye Yu pamoja nao kwa Ilimu Yake ambayo inajumlisha yale wanayoyazungmza kwa siri na kuyaficha. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho chenye maelezo ziada ya bayana:

 

Allaah Yuko Wapi?

 

[6] An-Naasikh Wal-Mansuwkh (Kinachofuta Na Kinachofutwa):

 

Hukmu ya Aayah hii namba (12) imefutwa na badala yake ni Aayah inayofuatia namba (13). Rejea Al-Baqarah (2:106). Na bonyeza pia kiungo kifuatacho:

 

An-Naasikh Wal-Mansuwkh (Kinachofuta Na Kinachofutwa)

 

[7] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho:  

 

058-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Mujaadalah Aayah 14: وَيَحْلِفُونَ عَلَى الْكَذِبِ وَهُمْ يَعْلَمُونَ

 

[8] Undugu Hautamfaa Ndugu Mbele Ya Allaah:

 

Rejea Al-Mumtahinah (60:3) kwenye faida na rejea zake.

 

[9] Maana Za Wahy Katika Qur-aan:

 

Rejea An-Nahl (16:2).

 

[10]  Al-Walaa Wal-Baraa (Kupenda Na Kuandamana, Kuchukia Na Kutengana Kwa Ajili Ya Allaah):

 

Waumini wanapaswa kufanya urafiki na Waumini wenzao hata kama hawana uhusiano wa damu nao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾

“Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki wandani. Wanaamrisha mema na wanakataza munkari[10] na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.” [At-Tawbah (9:71)]

 

Na pindi ndugu na jamaa wenye uhusiano wa damu wakiwa ni wenye kumpinga Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli wake (صلى الله عليه وآله وسلم), basi wanapaswa kutengana nao katika mipaka ya sharia ya Dini. Rejea Al-Hujuraat (49:10) kwenye mfano wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutengana na jamaa zake, na pia Swahaba kutengana na mzazi wake. Na hi indio inajulikana kwa Al-Walaa Wal-Baraa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنِ الْبَرَاءِ بْنِ عَازِبٍ، عن النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، قال:   إِنَّ أَوْثَقَ عُرَى الْإِيمَانِ: أَنْ تُحِبَّ فِي اللهِ، وَتُبْغِضَ فِي اللهِ   .
رواه أحمد والطبراني والحاكم والبزار، وحسنه الألباني في "صحيح الترغيب” (3030) .

Amesimulia Al-Baraa Bin ‘Aazib (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Shikizo thabiti kabisa la imaan ni upende kwa ajili ya Allaah na uchukie kwa ajili ya Allaah.” [Ahmad, Atw-Twabaraaniy, Al-Haakim na ameipa daraja ya Hasan Imaam Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (3030)]

 

Na Hadiyth nyenginezo zenye mafundisho hayo:

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ ، قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :  ((مَنْ أَحَبَّ فِي اللَّهِ وَأَبْغَضَ فِي اللَّهِ وَأَعْطَى لِلَّهِ وَمَنَعَ لِلَّهِ فَقَدِ اسْتَكْمَلَ الإِيمَانَ))  

Amesimulia Abuu Umaamah  (رضي الله عنه):  “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Atakayependa kwa ajili ya Allaah, akachukia kwa ajili ya Allaah, akatoa kwa ajili ya Allaah, na akazuia kwa ajili ya Allaah, basi atakuwa amekamilisha imaan.”  [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy (4681)]

 

عَنْ أَنَسٍ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى أَكُونَ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِنْ وَلَدِهِ وَوَالِدِهِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ)) أَخْرَجَاهُ

 

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mmoja wenu hawi Muumini mpaka anipende mimi kuliko watoto wake na baba yake na watu wote.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((ثَلاَثٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ وَجَدَ حَلاَوَةَ الإِيمَانِ: أَنْ يَكُونَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِمَّا سِوَاهُمَا، وَأَنْ يُحِبَّ الْمَرْءَ لاَ يُحِبُّهُ إِلاَّ لِلَّهِ, وَأَنْ يَكْرَهَ أَنْ يَعُودَ فِي الْكُفْرِ كَمَا يَكْرَهُ أَنْ يُقْذَفَ فِي النَّارِ)) متفق عليه

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mambo matatu atakayekuwa nayo, atapata utamu wa imaan: Allaah na Rasuli Wake wawe vipenzi zaidi kwake kuliko wengineo, ampende mtu na wala asimpende isipokuwa kwa ajili ya Allaah, na achukie kurudi katika ukafiri baada ya Allaah kumwokoa kutoka huko kama anavyochukia kuingizwa motoni. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Bonyeza pia viungo vifuatavyo kupata faida ziyada:

 

17-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Tawhiyd Ndiyo Inayotenganisha Baina Ya Uislamu Na Ukafiri Au Baina Ya Muislamu Na Kafiri

 

25-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Ukitaka Mapenzi Ya Allaah, Thibitika Katika Tawhiyd

 

041-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Alama Tatu Za Kupata Utamu Wa Iymaan

 

Share