Hiwsnul-Muslim: Utangulizi Wa Alhidaaya

Hiwsnul Muslim (Toleo Lilohaririwa)

Utangulizi Wa Alhidaaya

www.alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمن الرَّحيم

 

Himdi Anastahiki Allaah (سبحانه وتعالى ) Rabb  wa walimwengu, Rahmah na amani zimshukie kipenzi chetu Nabiy Muhammad (صلى الله عليه  وآله وسلم ) na ahli zake, na Swahaba zake (رضي الله عنهم)  na wote waliotangulia kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tunamshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kutuwezesha kukifanyia kazi upya kitabu cha Hiswnul-Muslim ili kizidi kuleta manufaa kwa jamii yetu. Tumeonelea kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kukifanyia kazi upya kwa kufanya yafuatayo:

 

 

1.  Kuweka Aayah na Suwrah zote kamilifu ili  imtosheleze msomaji  kutimiza nyiradi zake zote. Mfano Suwrah ya Aliyf Miym As-Sajdah, Al-Mulk, Al-Ikhlaasw, Al-Mu’awwidhataan n.k., ambazo anatakiwa Muislamu azisome kabla ya kulala.

 

 

2.  Kutaja Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وسلم) kwa ukamilifu katika baadhi ya nyiradi au du’aa yenyewe na pia katika marejeo chini ya ukurasa pamoja na kuweka tarjama yake.

 

 

3.  Kuweka marejeo bayana ya Hadiyth; Raawiy (msimulizi) na Muhaddithuwna (wakusanyaji wa Hadiyth) kwa kunukuu marejeo yao. Tumebainisha marejeo ya mjalada na ukurasa katika mabano ya (   ) na tumebainisha nambari ya Hadiyth katika mabano ya [   ]. Baadhi ya sehemu tumeweza kuongezea marejeo zaidi ya yale yaliyotajwa katika kitabu cha asili.

 

 

4.   Kuweka sauti za Adhkaar na Du’aa hizo pamoja na matamshi yake ili msomaji aliye na udhaifu wa kusoma Kiarabu aweze kusikiliza na kuweza kufuatilia kutamka vizuri Adhkaar na Du’aa hizo.

 

 

5.  Kubainisha Ahaadiyth na Adhkaar ambazo baadhi ya ‘Ulamaa wameona kuwa hazijathibiti hivyo ni dhaifu, na badala yake kutaja ambazo zilizo Swahiyh.

 

 

6.   Kubainisha nyiradi au du’aa ambazo si za Nabiy (صلى الله عليه وسلم) bali ni Athar (za Salafus-Swaalih).   

 

 

7.  Kuzitaja Adhkaar au Du’aa  (khasa zile ambazo aghlabu hutumika kusomwa), kwa kubadilisha sarufi mfano; inapokuwa ni mwanamke au hali ya wingi, mfano Du’aa ya maiti, au Du’aa Ukiwa Na Wahka Na Huzuni  (namba 120), ambayo mwanamke anapaswa aseme:

 

أللَّهُمَّ إنِّي أَمَتُك، بِنْتُ عَبْدِك، بنتُ أَمَتِك

Allaahumma inniy amatuka, bintu ’abdika, bintu amatika ... 

 

Ee Allaah, hakika mimi mja Wako mwanamke, binti wa mja wako, binti wa mja Wako mwanamke...

 

Pia mfano wa du’aa namba (79) ya Sayyidul-Istighfaar iliyopo katika Nyiradi za Asubuhi Na Jioni ambayo inataja kwa kumkusudia mwanamume, hivyo mwanamke aseme:

 

اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ، خَلَقْتَنـي وَأَنا أَمَتُكَ

Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illaa Anta Khalaqtaniy wa ana amatuka...

 

Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako mwanamke...

 

Na kadhaalika .

 

 

8. Kumwekea msomaji asiyefahamu lugha ya Kiarabu kwa kutaja du’aa au nyiradi kamilifu kutokana na kubadilika wakati mfano du’aa namba  (80) katika  Nyiradi za Asubuhi Na Jioni pale inapotakiwa kubadilisha neno la

أَصْبَحْنا

Aswbahnaa (Tumeingia asubuhi)

 

Liwe badala yake:     

أَمْسَيْنا

Amsaynaa (Tumeingia jioni)

 

 

9. Kuipa maana sahihi baadhi ya misamiati khasa ambazo zinahusiana na mas-ala ya ‘Aqiydah.

 

 

10. Kufanya ulinganifu wa misamiati na kufafanua zaidi baadhi ya maana.

 

 

11.  Kutanabahisha makosa yanayotendwa na baadhi ya watu katika kutamka yasiyopasa ilhali yapasayo kutamkwa yamo katika kitabu hiki. Pia, kuongezea faida na fafanuzi ya baadhi ya maneno na kuweka tanbihi kadhaa.

           

 

Kwa ujumla tumejaribu kadiri Alivyotuwezesha Allaah (سبحانه وتعالى) kukifanyia kazi upya kwa kukiboresha ili kitoe faida kwa wingi kwa kila upande. 

 

 

Marekebisho yetu hayo, hatumaanishi kwamba tutakuwa kamilifu katika kukiweka sawa kitabu hiki, kwani ukamilifu pekee ni wa Allaah (سبحانه وتعالى).  Mwandishi wa Kitabu hiki amechukua juhudi kubwa kabisa kuaandaa kitabu kama hiki. Tunamuombea Allaah (سبحانه وتعالى) Amlipe malipo mazito kabisa katika Miyzaan yake ya hasanaat. Tunaomba vilevile thawabu ziwafikie pia kila atakayekifanyia kazi na kila atakayekitumia kitabu hiki.

 

 

Tunawaomba wasomaji pindi watakapoona kosa lolote lile watujulishe kupitia webmaster@alhidaaya.com

 

 

Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Atusamehe makosa yetu na Atutaqabalie hii kazi iwe kwa ajili ya kupata Radhi Zake Pekee na Atulipe malipo mema kwayo.

 

وبِالله التَّوْفيق  وَصَلَّى اللهُ وَسَلَّمَ وَبَارَكَ عَلى نَبِيِّنَا مُحَمَّدٍ وَعَلى آلِهِ وَأَصْحَابِهِ أَجْمَعِينَ

 

Alhidaaya

 

 

 

Share