02-Wewe Pekee Tunakuabudu: Hali Ya Du’aa Baada Ya Kuombwa

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada.

 

02- Hali Ya Du’aa Baada Ya Kuombwa

 

 

 

Kuomba du’aa wakati mwingine huwa ni mtihani wa kujaribiwa Iymaan ya Muislamu pale du’aa yake inapochelewa au isipotakabaliwa. Shaytwaan hapo humchochea binaadamu kwa kumkatisha tamaa na kumtia dhana mbaya kuhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Inapofika hali hii anapaswa Muislamu kujikinga na Shaytwaan na kuendelea kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) bila ya kuchoka na bila kukata tamaa kwa sababu hakuna shaka kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameshaisikia du’aa ya mja Wake:

 

عَنْ سَلْمَانَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ رَبَّكُمْ تَبَارَكَ وَتَعَالَى حَيِيٌّ كَرِيمٌ يَسْتَحْيِي مِنْ عَبْدِهِ إِذَا رَفَعَ يَدَيْهِ إِلَيْهِ أَنْ يَرُدَّهُمَا صِفْرًا))

Kutoka kwa Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Rabb wenu Aliyebarikika na Aliyetukuka, Yuhai, Mkarimu, Anastahi kutoka kwa mja Wake anaponyanyua mikono yake kisha Airudishe sifuri)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah]

 

 

Na Muislamu anapomkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kumuomba jambo, du’aa yake huwa katika hali tatu kama iivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلاَ قَطِيعَةُ رَحِمٍ إِلاَّ أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثلاَثٍ:  إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الأَخِرَةِ وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهَا))  قَالُوا إِذًا نُكْثِرُ قَالَ:  ((اللَّهُ أَكْثَرُ))

Kutoka kwa Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Muislamu atakayeomba du’aa ambayo haina dhambi wala kukata undugu wa uhusiano wa damu isipokuwa Allaah Atampa mojawapo ya matatu; ima Amharakishie du’aa yake, au Amuwekee akiba Aakhirah au ima Amuepushe nayo ovu kama hilo)) Wakasema: Basi tutazidisha (kuomba du’aa). Akasema: ((Allaah Mwingi zaidi [wa kuongeza])) [Ahmad]

 

Hali tatu hizo ni:

 

1-Kutakabaliwa du’aa yake; huenda akatakabaliwa hapo hapo, au baada ya muda mfupi au muda mrefu.

 

2-Kumwekea akiba Aakhirah ambako malipo yake huko ni bora zaidi na ya kudumu kuliko duniani.

 

3-Kutokutakabaliwa kwani huenda ikawa anachokiomba kina shari naye Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾

Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]

 

  

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) katika Fatwa ya: “Hukmu Ya Kusema Wazi (Au Kudhihirisha Wasiwasi) Kwa Kutokubaliwa Du'aa” kama ifuatavyo: 

 

Swali: 

 

Je inapokuwa haijahakiki kwangu jambo niloliomba huwa naghadhibika na husema maneno katika nafsi yangu na kuhusu Allaah mfano husema: “Kwanini Yaa Rabb Huitikii du'aa yangu?” Na husema mengineyo pia. Naomba tafadhali uniongoze kuhusu haya. Na je, binaadamu anapohisi kuwa du'aa yake haikutakabaliwa afanyeje?

 

Akajibu:

 

“Ni juu yako ee muulizaji na kila Muislamu mwanamme na mwanamke inapochelewa kutakabaliwa (du'aa yako) basi jirudie nafsi yako na ujipime kwani Allaah ni Hakiymun-‘Aliym (Mwenye hikma na Mjuzi) Huenda Anaichelewesha kutakabaliwa (hiyo du'aa) kwa hikma kubwa ili mja akithirishe du’aa kwa Muumba wake, na kujilazimisha Kwake, na  kujidhalilisha kwa Utukufu Wake na kungʼangʼania katika kuomba haja yake na kuzidisha kurudi Kwake na kunyenyekea Kwake. Ili kwa kufanya hivyo, (mja mwenye kuomba) apate kheri na manufaa mengi na aweze kuutengeneza moyo na kumridhia Rabb wake. Yote haya ni adhimu zaidi na yenye manufaa zaidi kuliko haja yake. 

 

Pia huenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akachelewesha (kujibu du'aa) kwa sababu nyinginezo kama vile (muombaji) kujichanganya katika maasi kama kula chumo la haraam au kuwaasi wazazi wawili na maasi mengineyo.

 

Basi inawajibika kwa muombaji du’aa ajihesabu nafsi yake na akimbilie kuomba tawbah huku awe na matumaini kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamtakabalia tawbah yake na Atamuitikia du’aa yake.

 

Na huenda Akaichelewesha kwa hikma nyingine Anayoijua Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama vile ilivyo katika Hadiyth Swahiyh:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلاَ قَطِيعَةُ رَحِمٍ إِلاَّ أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثلاَثٍ:  إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الأَخِرَةِ وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهَا))  قَالُوا إِذًا نُكْثِرُ قَالَ:  ((اللَّهُ أَكْثَرُ))

Kutoka kwa Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Muislamu atakayeomba du’aa ambayo haina dhambi wala kukata undugu wa uhusiano wa damu isipokuwa Allaah Atampa mojawapo ya matatu; ima Amharakishie du’aa yake, au Amuwekee akiba Aakhirah au ima Amuepushe nayo ovu kama hilo)) Wakasema: Basi tutazidisha (kuomba du’aa). Akasema: ((Allaah Mwingi zaidi [wa kuongeza])) [Ahmad]

 

Basi itakapochelewa haja yako kutakabaliwa, usimlaumu Rabb wako wala usiseme: “kwanini, kwanini Yaa Rabb” bali ni juu yako kujirudi nafsi yako kwani Rabb wako ni Hakiymun-‘Aliym (Mwenye hikma, Mjuzi wa yote). Rudia nafsi yako na tazama kwani huenda una dhambi au maasi fulani ikawa ndio sababu ya kuchelewa kuitikiwa. Au huenda kuna jambo jengine lililosababisha kuchelewa kuitikiwa. Yote hayo huwa ni kheri kwako. Basi haijuzu kumlaumu Rabb wake yasiyomstahiki (Subhaanahu wa Ta’aalaa), lakini ni juu yako kujilaumu nafsi yako na utazame ‘amali zako na nyendo zako mpaka ujitengeneze nafsi yako ili uthibitike katika amri ya Rabb wako na uache kufanya Anayoyakataza na usimame (usivuke) katika mipaka Yake.

 

Pia inapasa kutambua kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) huenda Akachelewesha jibu kwa muda mrefu kama vile Alivyomcheleweshea kumtakabalia Nabiy Ya’quwb kuhusu kumrudisha kwake mwanawe Yuwsuf. Naye ni ni Nabiy mtukufu (‘Alayhis-ssalaam). Pia kama alivyochelewesha kumpa shifaa Nabiy Wake Ayyuwb (‘Alayhis-ssalaam).

 

Na huenda Allaah Akampa muombaji yaliyo kheri zaidi kuliko aliyoyaomba na huenda Akamuepusha na shari (ikawa kheri kwake) kuliko aliyoyaomba kama tulivyotaja katika Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (iliyotangulia...) Akabainisha (‘Alayhis-swalaatu was-salaam)) kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) huakhirisha jibu mpaka Aakhirah, au Huitakabali duniani, kutokana na hikma kubwa kwa sababu hivyo ina maslahi na manufaa zaidi kwa mja Wake, na Humuepusha na shari kubwa kabisa ikawa ni kheri kwake kuliko kutakabaliwa du’aa yake.

 

Basi kuwa na husnu-dhwann (dhana nzuri) kwa Allaah na endelea kuomba du’aa...”

[Fataawaa Ibn Baaz: Hukmu Al-Muswaarahah Bi ’Adami Qabuwl Ad-Du’aa, Juz. 5: 303].

 

 

 

Share