04-Wewe Pekee Tunakuabudu: Umuhimu Wa Kuomba Du’aa
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
04 -Umuhimu Wa Kuomba Du’aa
Muislamu mwenye akili, hathubutu kumkabili kiumbe yeyote mwingine kumuomba haja ambayo binaadamu hana uwezo nayo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwa sababu tofauti baina ya kumkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kumuomba na kumkabili kiumbe ni:
Kumkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
1-Kupata linaloombwa
2-Kupata manufaa kama thawabu kwa kutekeleza ‘ibaadah ya du’aa.
3-Kuepushwa na shari ya linaloombwa.
4-Kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa vile ni ‘amali Aipendayo Allaah.
5-Du’aa ni kitendo chepesi kabisa hakina masharti mazito kama sharti za fardhi au ‘amali nyinginezo. Popote ulipo; safarini bara au baharini, umesimama, umekaaa, umelala unaweza kutekeleza ‘ibaadah hii tukufu, hata moyoni mtu anaweza kuomba du’aa yake
Kumkabili kiumbe kwa ambalo hana uwezo nalo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
1-Anayekabiliwa hawezi kumiliki chochote ila kwa idhni ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)
2-Ni kujiingiza katika maasi makubwa ya kumshirkisha (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na hivyo ni kuchuma dhambi.
3-Kujiingiza katika shari, balaa kwa sababu hakuna dhamana kwamba anayeombwa atakuwa ana ikhlaasw kwa muombaji yaani huenda hamtakii kheri, hivyo huenda akamdhuru badala ya kumnufaisha.
4-Kujidhalilisha kwa binaadamu kwa kudhihirisha shida, malalamiko n.k.
5-Ni kujitia katika taklifu ya nafsi na mali kumfuata anayeombwa. Aghlabu mahali pa anayefuatwa kuombwa huwa ni mahali mahsusi mfano wanaowaomba maiti kaburini, au kumwendea shekhe, mganga, mtabiri n.k.
Umuhimu mwengineo wa kuomba du’aa ni kama ifautavyo:
1- Kutokuomba du’aa ni kudhihirisha kibri:
Kuhusu Hadiyth:
عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فِي قَوْلِهِ ((وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ)) قَالَ: ((الدُّعَاءُ هُوَ الْعِبَادَةُ)) وَقَرَأَ ((وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ)) إِلَى قَوْلِهِ: ((دَاخِرِينَ))
Amesimulia Nu’maan bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kauli yake [Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa] ((Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni)) Amesema: ((Du’aa ni ‘ibaadah)) kisha akasoma: ((Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni)) mpaka kauli Yake: ((daakhiriyn)) [Ghaafir 40:60] [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad – Hadiyth Hasan Swahiyh]
Kauli hiyo tukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) inamalizika:
إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ﴿٦٠﴾
Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingika Jahanam wadhalilike. [Ghaafir: 60]
Ash-Shawkaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: “Aayah hii tukufu ni dalili kwamba du’aa ni kitendo cha ‘ibaadah kwa sababu Ameamrisha waja Wake wamwombe Yeye. Na kauli Yake: ((Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu)) inadhihirisha pia kuwa du’aa ni ‘ibaadah, na kuacha kuomba du’aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni kudhihirisha kibri, bali hakika ni chukizo kubwa. Vipi mja atakabari kuomba du’aa kwa Ambaye Amemuumba na hali hakuwa chochote, Akampa rizki? Ambaye Ameumba ulimwengu na Akakipa kila kitu mahitaji yake, Akawapa maisha, Naye Ndiye Mwenye kufisha kisha Awalipe malipo mema au Awaadhibu? Bila ya shaka kibri kama hiki ni aina ya wazimu na ni dalili za wazi za kutokuwa na shukurani” [Tuhfat Adh-Dhaakiriyn]
2- Kuomba du’aa ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuamrisha katika kauli Zake mbali mbali tumuombe, Anasema:
قُلْ أَمَرَ رَبِّي بِالْقِسْطِ ۖ وَأَقِيمُوا وُجُوهَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ
Sema: “Rabb wangu Ameniamrisha uadilifu; na muelekeze nyuso zenu kwenye kila mahali pa kusujudu na mumuombe Yeye, muwe wenye kumtakasia Yeye Dini [Al-A’raaf: 29]
Anasema pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ
Na muombeni Allaah fadhila Zake. [An-Nisaa: 32]
Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
هُوَ الْحَيُّ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ ۗ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿٦٥﴾
Yeye Ndiye Aliye hai daima hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye; basi muombeni Yeye wenye kumtakasia Dini. AlhamduliLLaah, Himidi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu. [Ghaafir: 65]
Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾
186. Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]
Pia rejea Aayah ilotangulia ya [Suwrat Ghaafir: 60]
3- Asiyeomba du’aa, Allaah Humghadhibikia:
Kinyume na binaadamu ambaye huenda akachoshwa na kuchukizwa na maombi ya binaadamu mwenzake. Ama Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Humpenda mwenye kumuomba bali Hughadhibika na mja Wake asipomuomba:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((مَنْ لَمْ يَسْأَل اللَّهَ يَغْضَب عَلَيْهِ)) حسنه الألباني في صحيح سنن الترمذي برقم 2686
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Asiyemuomba Allaah, Humghadhibikia)) [At-Tirmidhiy ameipa daraja ya Hasan Imaam Al-Albaaniy taz Swahiyh At-Tirmidhiy (2686)]
4- Kuomba du’aa ni kuepushwa na adhabu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿٣٣﴾
Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu hali wao wanaomba maghfirah. [Al-Anfaal: 33]
5- Majaaliwa Yaliyoandikwa Na Waandishi Wawili (Malaika) Hayabadilishwi Ila Kwa Du'aa:
عَنْ ثَوْبَانَ (رضي الله عنه) أن النبي (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يَرُدُّ الْقَدَرَ إلاَّ الدُّعَاءُ وَلاَ يَزِيدُ فِي الْعُمُرِ إلاَّ الْبِرُّ وَإِنَّ الْعَبْدَ لَيُحْرَمُ الرِّزْقَ بِالذَّنْبِ يُصِيبُهُ))
Kutoka kwa Thawbaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hairudishwi Qadar (majaaliwa) ila kwa du’aa, wala hauzidi umri ila kwa wema, na hakika mja anaharamishiwa rizki kutokana na dhambi aitendayo)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad na ameisahihisha Al-Albaaniy ktk Swahiyh At-Targhiyb (638)]
6- Du’aa ni sababu kuu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutujali:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
قُلْ مَا يَعْبَأُ بِكُمْ رَبِّي لَوْلَا دُعَاؤُكُمْ ۖ فَقَدْ كَذَّبْتُمْ فَسَوْفَ يَكُونُ لِزَامًا ﴿٧٧﴾
Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Rabb wangu Asingekujalini lau kama si du’aa zenu; kwa yakini mmekadhibisha, basi adhabu itakuwa ya lazima kukugandeni tu! [Al-Furqaan: 77]
Aayah hii tukufu ni hitimisho baada ya kutaja Sifa za ‘Ibaadur-Rahmaan (Waja wa Rahmaan) ambazo humo zimo pia du’aa za kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
7- Du’aa ni silaha ya Muumini:
Du’aa ni silaha ya Muumini aliye dhaifu, aliyedhulumiwa, na pia kwa yeyote asiyekuwa na matumaini ya kupata faraja kutokana na shida na dhiki zake, au kupata ushindi dhidi ya adui yake. Manabiy wangapi walipata faraja baada ya madhara, mateso, na bughudha za watu wao hatimaye wakapata ushindi na wakainusuru Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa sababu ya kuomba du’aa?
Nuwh (‘Alayhis-salaam) baada ya kulingania kaumu yake miaka 950 hatimaye alikata tamaa akamuelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Naye Akampa faraja na Akumnusuru na Akawaangamiza waovu katika kaumu yake: [Al-Qamar: 9-16, Al-‘Ankabuwt: 14-15]
Nabiy Ayyuwb (‘Alayhis-salaam) alipatwa na mitihani ya kila aina, alikumbwa na maradhi na ufakiri naye akavumilia mwishowe akamkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Naye Akamuondoshea maradhi na kumpa yaliyo kheri zaidi. [Al-Anbiyaa: 83-84, Swaad: 41-44].
Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) alipatwa na mitihani wa baba yake na watu wake, na hadi kutumbukizwa kwenye moto lakini du’aa yake ya kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndio iliyomuokoa na moto huo baada ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuufanya moto uwe wenye amani na baridi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akambariki kwa vizazi vyema naye akawa baba wa Manabiy wote baada yake. [Al-Anbiyaa: 51-73].
Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam) alikuwa kila inapomfika mtihani mkubwa au mdogo akimuelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Naye Akamghufuria makosa yake, Akampa faraja baada ya kumuokoa kutokana na adui yake Fir’awn [Ash-Shu’araa: 63-67]
Nabiy Yuwnus (‘Alayhis-salaam) baada ya kufanya kosa kukimbia watu wake, akamezwa na nyangumi akawa katika kiza na dhiki, akamuelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kumuomba maghfirah, akaokolewa na kupewa faraja kwa kuamrishwa nyangumi amcheuwe fukoni. [Al-Anbiyaa: 87-88]
Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye mitihani yake ilikuwa ya aina mbali mbali zikiwemo njama za kuuliwa na watu wake. Lakini kila mara alikuwa akimuelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ambaye Alimlinda na Akampa ushindi wa Dini ya Kiislamu.
Basi Muumini hana budi kuithamini du’aa na kuitegemea kuwa ni silaha yake katika hali yoyote ya mitihani atakayoikabili ikiwa ni mitihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) au inayosababishwa na binaadamu.
8- Kuomba du’aa ni kujiepusha na ubakhili na ukataji tamaa:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((إنَّ أَعْجَز النَّاس مَنْ عَجَزَ عَنْ الدُّعَاء وَأَبْخَل النَّاس مَنْ بَخِلَ بِالسَّلاَمِ))
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika aliye bakhili kabisa miongoni mwa wa watu ni mwenye kufanya ubakhili katika kutoa salaam, na mkataji tamaa kabisa miongoni mwa watu ni mwenye kukata tamaa na du’aa)) [Ameipa daraja ya Swahiyh Al-Albaaniy Taz. As-Silsilah Asw-Swahiyhah (601)]
9- Takrima kwa muombaji du’aa na ni sababu ya kupata unyenyekevu:
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾
28. Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. Na wala macho yako yasiwavuke kwa kutaka pambo la uhai wa dunia. Na wala usimtii Tuliyemghafilisha moyo wake na Ukumbusho Wetu akakafuata hawaa zake, na jambo lake limekuwa la kuzidi kuvuka mipaka. [Al-Kahf: 28]
Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٢﴾
Na wala usiwafukuze wale wanaomwomba Rabb wao asubuhi na jioni wanataka Wajihi Wake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, na wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, hata ukawafukuza; utakuja kuwa miongoni mwa madhalimu. [Al-An’aam: 52]
10 – Du’aa inamtoa mja katika unyonge na ufidhuli:
Mafunzo kutoka kwa Manabiy watukufu; Nabiy Zakariyyah (‘Alayhis-salaam) alipoomba alisema:
رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ﴿٤﴾
“Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi, na wala sikuwa kwa kukuomba Rabb wangu, mwenye kukosa baraka.” [Maryam: 4]
Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) baada ya kufukuzwa na baba yake:
سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾
“Amani iwe juu yako. Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima kwangu ni Mwenye huruma sana.”
وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾
“Na natengana nanyi na mnavyoviomba pasi na Allaah; na namuomba Rabb wangu asaa nisijekuwa kwa kumwomba Rabb wangu, mwenye kukosa baraka.” [Maryam: 47-48]
11- Mwenye kuomba ana uhakika wa kutakabaliwa du’aa yake:
Licha ya umuhimu wote wa du’aa na fadhila zake, linalotia moyo zaidi ni kwamba lolote tumuombalo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tujue kwamba Analipokea na Atatutakabalia kwa njia moja au nyingine:
عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ يَقُولُ: ((مَا مِنْ أَحَدٍ يَدْعُو بِدُعَاءٍ إلاَّ آتَاهُ اللَّهُ مَا سَأَلَ أَوْ كَفَّ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهُ مَا لَمْ يَدْعُ بِإِثْمٍ أَوْ قَطِيعَةِ رَحِمٍ))
Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakuna mtu aombaye du’aa ila Allaah Humpa Alichoomba au Akamupeusha kwayo shari kama hiyo, madamu haombi dhambi au kukata undugu)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Taz Swahiyh At-Tirimidhy (3381) na Swahiyh Al-Jaami’ (5678)