13-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kutundika Kitu Kwa Ajili Ya Kinga, Kumlinganisha Allaah

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

13- Kutundika Kitu Kwa Ajili Ya Kinga Na Kumlinganisha Allaah

Alhidaaya.com

 

 

Katika kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni kutundika vitu ukatani au milangoni n.k. Itikadi ya kitendo hiki ni aina mbili;

 

Kwanza: kutundika kwa kuitakidi kwamba hicho kitu kilichotundikwa ni kinga ya jicho au husda n.k. Vinavyotundikwa huenda ikawa ni fremu za Aayah katika Qur-aan, au du’aa au Majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Au wengine hutundika vitu kama pilipili na ndimu, aina ya vijiwe vya buluu vyenye jicho n.k.  Yote haya ni shirki kwa hiyo haijuzu abadani kwa sababu hakuna baya lolote la kumdhuru mtu isipokuwa kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amelikidhia kama Anavyosema:

 

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿١١﴾

Hausibu msiba wowote isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Na yeyote   anayemuamini Allaah, (Allaah) Huuongoza moyo wake. Na Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi. [At-Taghaabun: 11]

 

Na kinyume chake ni kukosa kutawakali Kwake Subhaanahu wa Ta’aalaa na kukosa kufuata kinga iliyothibiti. Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Hukaym ifuatayo imethibitisha katazo hilo:  

 

((مَنْ تَعَلَّقَ شَيْئًا؛ وُكِّلَ إِلَيْهِ)) رَوَاهُ أَحْمَدُ وَالتِّرْمِذِيُّ

((Atakayetundika kitu (kuitakidi ni kinga) basi amejiweka katika ulinzi wa hicho kitu alichokivaa)) [na kitamdhalilisha]. [Ahmad na At-Tirmidhiy. Hadiyth Marfu’w]

 

Tanbihi: Mifano ya vitu vinavyotundikwa kuitakidi kuwa kitamfaa au kumzuia shari ni: talasimu, hirizi, zindiko na vinginveyo kama ilivyobainishwa katika makala hizi.  

 

Haijuzu kabisa kutundikia kitu kuitakidi ni kinga, bali inatosha kabisa kutawakali kwa Allaah  kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema  :

 

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza.  [Atw-Twalaaq: 3]

 

Na mafunzo Swahiyh ya kujikinga ni kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

عن خَوْلَةَ بِنْتَ حَكِيمٍ (رضي الله عنها) قالت: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ:  ((مَنْ نَزَلَ مَنْزلاَ ثُمَّ قَالَ: "أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللَّهِ التَّامَّاتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ" لَمْ يَضُرَّهُ شَيْءٌ حَتَّى يَرْتَحِلَ مِنْ مَنْزِلِهِ ذَلِكَ)) رواه مسلم

Imepokelewa toka kwa Khawlat bint Hakiym (Radhiwa Allaahuu ‘anhaa) kwamba kamsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayefikia mahali kisha akasema: 

أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللَّهِ التَّامَّاتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ

 

A’uwdhu bikalimati-LLaahit-taammati min sharri maa Khalaq' (Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia na shari ya Alichokiumba), hakuna kitakachomdhuru hadi atakapoondoka mahali pake hapo)). [Muslim]

 

 

Mafunzo mengine sahihi ni kusoma Adhkaar na nyiradi za asubuhi na jioni zilizothibiti.

 

Ama kuhusu kutundika Qur-aan, baadhi ya watu wanaona ni jambo la kupendeza lakini hakika haijuzu kwa sababu Qur-aan imeteremshwa kwa ajili ya Mwongozo, mawaidha, ukumbusho, na kusomwa na kufanyia kazi maamrisho yake na kuacha makatazo yake, na wala si kwa ajili ya kutundikwa. 

 

Ibnul-‘Arabiyy Al-Maalikiyy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kutundika Qur-aan si katika Sunnah, bali Sunnah ni kuisoma bila ya kuitundika.”

 

 

Aghlabu ya watu hutundika Aayatul-Kursiyy au Al-Maw’idhataan na Suwratul-Ikhlaasw ambazo ni nyepesi kabisa kuzihifadhi na kuzisoma na ndizo zilizothibiti katika mafunzo Swahiyh kwamba ni kinga ya Muislamu. Basi kwanini mtu atundike badala ya kuzisoma na kuzihifadhi?

 

Picha za baadhi ya vitu ambavyo baadhi ya watu wanavitundika wakiamini ni kinga:

 

                                       

 

 

     

                          

  

 

Pia kutundika vitu madukani au majumbani kama pilipili, ndimu n.k.

 

         

 

 

        

 

 

 

Pili: Kutundika Jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukutani mifano kama ifuatavyo:

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Haijuzu kutundika picha kama hizo, kwani haiwezekani kuwa Muumba na aliyeumbwa wawe katika daraja moja, hata kama niyyah ni kupamba nyumba au kudhihirisha mapenzi yao, kwa sababu wengi hudai kuwa hawakusudii kumlinganisha sawa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Basi kujiepusha na hilo ni bora hata kama mtu haitakidi hilo, kwani kukaa mbali na utata ndio njia ya salama katika Dini ya mtu.

 

Kadhaalika, Wanachuoni wamekemea jambo hili kama ifutavyo:

 

Fatwa ya 1 - Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah Lil-Buhuwth Al-'Ilmiyyah Wal-Iftaa imepitia yaliyofikishwa kwa Mufti Mkuu kutoka kwa muulizaji Humuwd ‘Abdul-Aziyz As-Saayigh kwa marejeo Nambari 6860 9/11/1421H.

 

Muulizaji ameuliza swali na haya hapa maelezo yake:

“Allaah Akuhifadhini, na kukhofia yanayojiri katika Dini hii na kutilia mkazo yanayofisidi ‘Aqiydah na ambayo yanaenea kwa Ummah huu kutoka kwa maadui wa Allaah na wa Dini Yake na wepesi wa watu kufuata mambo wanayodhania ni madogo mno lakini kumbe ni makubwa mno na ikawa kuondosha madhara yake ni vigumu. Kama ilivyokuwa hali katika watu wa Nuwh na masanamu yao; walivyoanza kuweka picha za waja wema wakaanza kuziabudu wakidhania ni jambo jema kumbe ni shirki iliyowasababisha watu waliofuata kuabudu masanamu.

 

Tunadhihirisha mbele yenu aina mbali mbali za picha zilizotayarishwa kuwekwa pande mbili; upande kuna Jina la Allaah (’Azza wa Jalla) na upande wa jina la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wala sijui lipi bado litakalojiri baada ya haya! Na baadhi ya ndugu wamewaandikia Baraza la Fatwa maombi haya ili kufuatilia maovu ya ‘Aqiydah wakitaraji mtoe maoni yenu ambayo huenda ikiwa ni sababu ya ufumbuzi na tiba ya kuondosha uovu huu, Allaah Awathibitishieni na Akulipeni kwa kuwanufaisha waja Wake Katika utiifu Wake.”

 

Jibu la Baraza la Fatwa:

 

Haijuzu kuandika Jina la Allaah Aliyetukuka [Allaah] pamoja na [Muhammad] jina la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sambaba katika karatasi au kwenye ubao [au vitambaa], au kutundika ukutani [kwa hali yoyote]. Huko ni kupindukia mipaka kwa haki yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kumlinganisha yeye sawa na Allaah. Haya ni mas-alah miongoni mwa masuala ya shirki na hali yeye mwenyewe amekataza katika kauli yake, aliposema:

“Msinitukuze kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake.”

 

Na hivyo ni wajibu kuondosha picha hizo au karatasi na kufutilia mbali maandishi kama hayo katika kuta au popote penye aina hizo za picha, ili tuilinde ‘Aqiydah na kufuata wasia wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 

Wa biLLaahi At-tawfiyq. Wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyinaa wa ‘alaa aalihi wa swahbihi wa sallam.

 

[Fataawa Al-Lajnah Ad-Daaimah Lil-Buhuwth Al-'Ilmiyyah Wal-Iftaa]

 

 

Fatwa ya 2:  Fatwa ya Shaykh Ibn ‘Uthaymin (Rahimahu Allaah):  

Hakika kuandikwa Jina la Allaah (الله) upande mmoja na jina la (محمد) upande wa pili, yakiwa majina hayo yako sambamba na kama hivi:

 الله   ***  محمد     yanamfanya anayetazama kuona kwamba wako katika cheo kimoja na hali Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimjibu mtu mmoja aliyemwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Atakavyotaka (au Akipenda) Allaah [In Shaa Allaah) na ukataka wewe.” Akamjibu: ((Je umenilinganisha mimi kuwa sawa Allaah? Bali sema: Akipenda Allaah [In Shaa Allaah] pekee)).

 

Na ikiwa maandishi kama hayo yamewekwa hivyo mbele ya wanaoswali, yatakuwa ni sababu ya kuwashughulisha watu na Swalaah zao. Pia ‘Ulamaa wakubwa wamechukizwa [na kukataza] kuandikwa kitu mbele ya Qiblah kwa sababu kitamshughulisha na kumshawishi mwenye kuswali. Hivyo, haipasi kuandikwa hivyo; namaanisha الله   ***  محمد    Na popote palipoandikwa hivyo panapaswa kufutiliwa mbali!

Na katika sharh yake ya Kitabu cha Buluwghul-Maraam, Kitabu cha Swalaah, Mlango wa Misikiti, Mkanda namba 16 upande wa pili, anasema Shaykh kuwa, kwa uchache maandishi kama haya ni shirk ndogo.”

Ameandika: Muhammad Bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn 9/1/1420H.

 

 

Basi ndugu Waislamu tutahadhari kutundika vitu kama hivyo au chochote kile mfano wa hivyo kwa kuitakidi ni kinga au baraka.

 

 

 

 

Share