06-Wewe Pekee Tunakuabudu: Yasiyopasa Katika Du’aa
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
06- Yasiyopasa Katika Du’aa
Baadhi ya yasiyopasa katika kuomba du’aa na dalili zake:
1- Kumwomba Asiyekuwa Allaah Ta’aalaa:
Haipasi kumkabili kiumbe kingine chochote kumuomba du’aa kwa kudhani kwamba kiumbe huyo ana uwezo wa kukidhi haja za mtu. Kufanya hivyo ni miongoni mwa shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu. Naye Ametuonya Anaposema:
وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا﴿١٨﴾
Na kwamba Misikiti ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah. [Al-Jinn: 18]
Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((إِذَا سَأَلْتَ فَاسْأَلْ اللَّهَ وَإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ))
((Unapoomba basi muombe Allaah, na unapotaka msaada, basi taka msaada kwa Allaah)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]
2- Kuharakiza Du’aa Itakabaliwe
Kwa maana mtu anapoona du’aa yake haikutakabaliwa akaanza kulalamika. Muislamu anapaswa kuwa na yaqiyn kuwa du’aa yake itatakabaliwa tu kwa njia moja au nyingine madamu amekwishamkabili Rabb wake kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((يُسْتَجَابُ لإَحَدِكُمْ مَا لَمْ يَعْجَلْ يَقُولُ دَعَوْتُ فَلَمْ يُسْتَجَبْ لِي))
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli Wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atatakabaliwa mmoja wenu madamu hataharakiza akasema: “Nimeomba lakini sikutakabaliwa”)) [Al-Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy]
Pia,
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) أَنَّهُ قَالَ: ((لاَ يَزَالُ يُسْتَجَابُ لِلْعَبْدِ مَا لَمْ يَدْعُ بِإِثْمٍ أَوْ قَطِيعَةِ رَحِمٍ مَا لَمْ يَسْتَعْجِلْ)) قِيلَ "يَا رَسُولَ اللَّهِ مَا الإِسْتِعْجَالُ؟" قَالَ: ((يَقُولُ قَدْ دَعَوْتُ وَقَدْ دَعَوْتُ فَلَمْ أَرَ يَسْتَجِيبُ لِي فَيَسْتَحْسِرُ عِنْدَ ذَلِكَ وَيَدَعُ الدُّعَاءَ))
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja ataendelea kuitikiwa [du’aa yake] madamu hatoomba dhambi au kukata ukoo na madamu hatoharakiza)). Ikaulizwa: “Vipi kuharakiza”? Akasema: ((Aseme: “Nimeshaomba na kuomba lakini sikuona kuitikiwa”, akavunjikwa moyo akaacha kuomba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
3- Kuomba Dhambi Au Kukata Undugu:
Hadiyth iliyotangulia juu inakataza jambo hili. Hali kadhaalika Hadiyth ifuatayo pia:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلاَ قَطِيعَةُ رَحِمٍ إلاَّ أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثَلاَثٍ: إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الأَخِرَةِ وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهَا)) قَالُوا إِذًا نُكْثِرُ قَالَ: ((اللَّهُ أَكْثَرُ))
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Muislamu atakayeoomba du’aa isiyokuwa ni dhambi wala kukata undugu isipokuwa Allaah Atampa mojawapo ya matatu: Ima Amharakizie du’aa yake, au Amuewekee akiba Akhera, au Amuepushe nayo ovu kama hilo)) Wakasema: Basi tutazidisha [kuomba du’aa]. Akasema: ((Allaah Mwingi zaidi)) [wa kuongeza])). [Ahmad. Taz. Swahiyh At-Targhiyb (1633) na Swahiyh Al-Musnad (421)]
Mifano ya kuomba dhambi kusema: "Ee Allaah, nijaalie nichume mali nyingi japo ya haraam" au 'Ee Allaah, nijaalie nipende muziki na nihifadhi nyimbo nyingi” n.k. Ama kukata undugu,mfano kusema: "Ee Allaah, mjaalie fulani awe muasi kwa wazazi wake na atengane nao" au "Ee Allaah, mjaalie fulani akhasimikiane na jamaa zake".
4- Kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Kwa Kumpa Khiari
Hivyo haipasi kwani ni kuhusisha na majaaliwa na Qudra ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa mfano kusema: “Ee Allaah, Ukipenda nighufurie madhambi yangu” au: “Ee Allaah, Ukipenda nirehemu,” bali Muislamu anatakiwa awe na yaqiyn na yale anayoyaomba.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يَقُولَنَّ أَحَدُكُمْ اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي إِنْ شِئْتَ, اللَّهُمَّ ارْحَمْنِي إِنْ شِئْتَ, لِيَعْزِمْ الْمَسْأَلَةَ فَإِنَّهُ لاَ مُكْرِهَ لَهُ))
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Asiseme mmoja wenu: “Ee Allaah, nighufurie Ukitaka, Ee Allaah, nirehemu Ukitaka”, bali awe na azma na aliyoyaomba kwani hakuna wa kumlazimisha)) [Allaah kufanya Atakavyo] [Al-Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy]
5- Kuwekea Mipaka Rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
Haipasi kuwekea mipaka Rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwani Rahmah Yake ni pana, Anasema:
وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ
Na rahmah Yangu imeenea kila kitu. [Al-A’raaf: 156]
na hakuna awezaye kuizuia kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾
Rahmah yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake, Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Faatwir: 2]
Mfano mtu asiombe "Ee Rabb! Niteremshie Rahmah Yako mimi na ahli yangu, lakini usimteremshie fulani”. Makatazo yamethibiti katika Hadiyth ifuatayo:
عن أبي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَامَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فِي صَلاَةٍ وَقُمْنَا مَعَهُ فَقَالَ أَعْرَابِيٌّ وَهُوَ فِي الصَّلاَةِ: "اللَّهُمَّ ارْحَمْنِي وَمُحَمَّدًا وَلاَ تَرْحَمْ مَعَنَا أَحَدًا" فَلَمَّا سَلَّمَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ لِلأَعْرَابِيِّ: (( لَقَدْ حَجَّرْتَ وَاسِعًا)) يُرِيدُ رَحْمَةَ اللَّهِ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Alisimama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah, nasi tukasimama pamoja naye. Bedui mmoja akasema akiwa katika Swalaah: "Ee Allaah, nirehemu pamoja na Muhammad na wala Usimrehemu pamoja nasi yeyote mwengine”: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotoa salaam kumaliza Swalaah akamwabia bedui: ((Kwa yakini umewekea mipaka jambo pana mno)) [akikusudia Rahmah ya Allaah] [Al-Bukhaariy, Abu Daawuwd, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy]
6- Kupinduka Mipaka Katika Kuomba Du’aa
Amekataza Allaah (Subahaanu wa Ta’aalaa):
ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾
Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka. [Al-A’raaf: 55]
Imaam As-Sa’diy (Rahimahu Allaah) amesema katika Tafsiyr yake inamanisha:
“Wapindukaji mipaka katika kila jambo, na mfano wa mja kumuomba Allaah mas-alah yasiyompasa, au kujikalifisha na kuzidisha kupita kiasi au kufikisha kupandisha sauti yake katika du’aa; haya yote yanaingia katika katakazo la uvukaji mipaka”.
Kuvuka mipaka kwa Mfano kuomba kubadilishwa shariy’ah za Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa) Alizozihukumu; kama yaliyoharamishwa kuwa yawe halali. Au pia kuomba yasiyowezekana kama vile mfano wa walivyoomba Mayahudi kutaka kumwona Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) waziwazi, au Makafiri Quraysh walivyoomba kiteremshwe Kitabu kutoka mbinguni pamoja na Malaika wayaone hayo waziwazi.
Makatazo yamethibiti pia katika Hadiyth:
عن عبدَ اللَّهِ بنَ مُغفَّلٍ، سمعَ ابنَهُ يقولُ: اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ القَصرَ الأبيضَ، عن يمينِ الجنَّةِ إذا دخلتُها، فقالَ: أي بُنَيَّ، سلِ اللَّهَ الجنَّةَ، وتعوَّذ بِهِ منَ النَّارِ، فإنِّي سَمِعْتُ رسولَ اللَّهِ صلَّى اللَّهُ عليهِ وسلَّمَ يقولُ: ((إنَّهُ سيَكونُ فيهذِهِ الأمَّةِ قومٌ يَعتدونَ في الطَّهورِ والدُّعاءِ))
Imetoka kwa ‘Abdullaah bin Mughaffal kwamba amemsikia mwanawe akiomba: “Ee Allaah, nakuomba qasri jeupe na kuliani mwa Jannah nitakapoingia”. Akamwambia: “Ee mwanangu! Muombe Allaah Jannah na omba kinga Kwake ya Moto, kwani nimesikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Watakuweko watu katika Ummah huu wakipinduka mipaka katika twahaarah na duaa)) [Abu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy, taz. Swahiyh Abiy Daawuwd (96) na Swahiyh Al-Jaami’ (2396)]
7- Kuomba Mauti
Muislamu anapofikwa na mitihani anapaswa kuwa mstahamilivu na kuridhika na majaaliwa ya Allaah hukuu aendelee kumuomba faraja. Haifai kutamani au kuomba mauti. Lakini pindi hali inapomfikisha kushindwa kuvumilia na kutamani mauti, aombe du’aa iliyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((لاَ يَتَمَنَّيَنَّ أَحَدُكُمْ الْمَوْتَ مِنْ ضُرٍّ أَصَابَهُ, فَإِنْ كَانَ لَا بُدَّ فَاعِلاً فَلْيَقُلْ: اللَّهُمَّ أَحْيِنِي مَا كَانَتْ الْحَيَاةُ خَيْرًا لِي وَتَوَفَّنِي إِذَا كَانَتْ الْوَفَاةُ خَيْرًا لِي))
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Asitamani mmoja wenu mauti kutokana na dhara ilomsibu. Akiwa hana budi kufanya, basi aseme: “Allaahumma Ahyiniy maa kaanat al-hayaatu khayran-liy, wa-tawaffaniy idhaa kaanat al-wafaatu khayran-liy - "Ee Allaah, nipe uhai ikiwa Unajua kwamba uhai ni bora kwangu, na nifishe ikiwa Unajua kuwa mauti ni bora kwangu "))[Al-Bukhaariy, Muslim]
Pia mauti hayaombwi isipokuwa anapokhofia mtu fitnah ya kumharibia Dini yake kwa dalili ya du’aa ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
وَإِذَا أَرَدْتَ بِعِبَادِكَ فِتْنَةً فَاقْبِضْنِي إِلَيْكَ غَيْرَ مَفْتُون
((…Na Utakapokusudia kwa waja Wako fitnah, basi nifishe Kwako bila ya kufitiniwa)) [At-Tirmidhiy, taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3233)]
8- Kulaani Mtu Au Kitu
Muislamu haipasi kumuombea mwenzake laana hata akiwa ni mtendaji maasi:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) أُتِيَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) بِرَجُلٍ قَدْ شَرِبَ قَالَ: ((اضْرِبُوهُ)) قَالَ أَبُو هُرَيْرَةَ: فَمِنَّا الضَّارِبُ بِيَدِهِ وَالضَّارِبُ بِنَعْلِهِ وَالضَّارِبُ بِثَوْبِهِ, فَلَمَّا انْصَرَفَ قَالَ بَعْضُ الْقَوْمِ: "أَخْزَاكَ اللَّهُ" قَالَ: ((لاَ تَقُولُوا هَكَذَا لاَ تُعِينُوا عَلَيْهِ الشَّيْطَانَ))
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekunywa pombe. Akasema ((Mpigeni)).Akasema Abuu Hurayrah: "Tukampiga kwa mikono yake, pigo kwa viatu vyake na pigo kwa nguo zake. Alipoondoka wakasema baadhi ya watu: “Allaah Akuhizi [Akulaani]” Akasema: ((Msiseme hivi, msimsaidie shaytwaan dhidi yake)) [Al-Bukhaariy] na katika riwaaya ya Ahmad ameongeza kusema: ((lakini semeni: “Allaah Akurehemu.”))
Hali kadhalika haipasi kulaani wanyama hata wale wanaosumbua au kuleta madhara. Au pia kulaani wakati, mvua, upepo. Hadiyth kadhaa zimethibitisha katazo hili; mojawapo ni Hadiyth ifuatayo ambayo inatoa onyo kuwa mwenye kulaani kitu; laana humrudia mwenyewe:
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ ((رضي الله عنهما) أَنَّ رَجُلاً لَعَنَ الرِّيحَ عند رسول الله (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لاَ تَلْعَنْهَا فَإِنَّهَا مَأْمُورَةٌ وَإِنَّهُ مَنْ لَعَنَ شَيْئًا لَيْسَ لَهُ بِأَهْلٍ رَجَعَتْ اللَّعْنَةُ عَلَيْهِ))
Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba mtu alilaani upepo mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akasema: ((Usiulaani kwani (huo upepo) umeamrishwa, na hakika mwenye kulaani kitu kisichostahiki inamrudia laana dhidi yake)) [At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd Swahiyh Abiy Daawuwd (4908)]
9- Kuwaombea Watoto Laana
Mzazi awe na tahadhari anapokuwa katika ghadhabu na mwanawe, asije kuteleza ulimi kwa kumuombea laana mwanawe, au kumuombea shari au kumtolea radhi kwa sababu; Kwanza: Du’aa ya mzazi hairudi kwa dalili ifuatayo:
عّنْ أَنسْ بِنْ ماَلِكْ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ): ((ثَلاَثُ دَعْواتِ لاَ تُرَدُّ: دَعْوَةُ الْوَالِدِ لِوَلَدِهِ، وَدَعْوَةُ الصَّائِم وَدَعْوَةُ الْمُسَافَرَ))
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ((Du’aa za watatu hazirudishwi; du’aa ya mzazi kwa mwanawe, na du’aa ya mwenye kufunga swawm, na du’aa ya msafiri)) [Al-Bayhaqiy Swahiyh Al-Jaami’ (3032) na pia katika Silsilatu Al-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (1797)]
Pili: Ameonya wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لاَ تَدْعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ ولاَ تَدْعُوا عَلَى أَولاَدِكُمْ ))
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msijiombee dhidi ya nafsi zenu wala msiombe dhidi ya watoto wenu)) [Muslim (3009), Abuu Daawuwd, taz. Swahiyh Abiy Daawuwd (1532) na Swahiyh Al-Jaami’ (7267)]
Inahitaji subira katika ghadhabu na kutokuazimia kulaani au kutoa radhi pindi mtoto anapovuka kumuasi mzazi. Ni bora kumchapa kuliko kumuombea laana kwani athari ya kumchapa itatoweka haraka kuliko athari ya kumlaani pindi du’aa itakapotakabaliwa na mtoto akadhurika na kisha yatabakia kuwa ni majuto!
Juu ya hivyo, kumuombea mtu laana ni kama kumuua. Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
لَعْنُ المُؤْمِنِ كَقَتْلِه
((Kumlaani Muumini kama kumuua)) [Swahiyh Al-Jaami’y (710)]
10- Kuomba Yenye Manufaa Ya Dunia Pekee
Anapoomba Muislamu du’aa zake za manufaa ya kidunia daima aongoezee na du’aa za manufaa ya Aakhirah kwani hayo ndio yaliyo bora zaidi na ya kudumu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
فَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ﴿٢٠٠﴾
Kwani kuna baadhi ya watu wasemao: “Rabb wetu Tupe katika dunia;” naye katika Aakhirah hana sehemu yoyote.
وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿٢٠١﴾
Na miongoni mwao kunawasemao: “Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto.”
أُولَـٰئِكَ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّمَّا كَسَبُوا ۚ وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٢٠٢﴾
Hao watapata pato lao kutokana na waliyoyachuma, na Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu. [Al-Baqarah: 200-202]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾
Yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya Aakhirah Tunamzidishia katika mavuno yake; na yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote. [Ash-Shuwraa: 20]
11- Kutokujiombea Mwenyewe Na Badala Yake Kutegemea Watu Wengine Kukuombea Du’aa
Kutegemea watu wengine wakuombee du’aa kwa kujidharau mwenyewe kwa vile labda una kasoro fulani kama kukosa kuwa na ‘ilmu ya Dini au una madhambi kadhaa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hakutofautisha waja Wake kumuomba kati ya mtu aasi na mwenye taqwa Aliposema:
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾
Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]
Inampasa hata mtu ambaye ni 'Aaswi (Mwenye kufanya maasi) ategemee Rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuwa Atamtakabalia du’aa yake. Kwa hiyo haipasi kuitakidi kuwa du’aa ya mtu Swaalih (mwema) au Shaykh au Imaam au mtu mwenye hadhi fulani ndiyo itakayotakabaliwa. Hakuna ajuaye uhakika wa hayo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ ﴿٣٢﴾
Basi msizitakase nafsi zenu. Yeye Anamjua zaidi aliyekuwa na taqwa. [An-Najm: 32]
12- Kuomba Hadharani Kwa Sauti
Kuomba kwa sauti ni kinyume na miongoni mwa adabu za kuomba du’aa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾
Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka. [Al-A’raaf: 55]
13- Kuweka Nadhiri Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Kutokumuomba Haja Nyingine
Haipasi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atakabali haja kisha kuweka nadhiri kwamba pindi Akitakabali haja uliyoiomba, hutomkabili kumuomba jambo jingine kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ni Mkwasi wala hakipungui chochote katika ufalme Wake hata Akiitikia haja za viumbe Wake wote kama Anavyosema Mwenyewe (‘Azza wa Jalla) katika Hadiyth Al-Qudsiy:
...يا عِبادِي لوْ أَنَّ أَوَّلَكُمْ وآخِرَكُمْ وإنْسَكُمْ وجنَّكُمْ قاموا في صَعِيدٍ وَاحِدٍ، فَسَأَلُوني، فأَعْطَيْتُ كلَّ واحدٍ مَسْأَلَتَهُ ما نَقَصَ ذلك مِمَّا عِنْدِي إلا كما يَنْقُصُ الْمِخْيَطُ إذا أُدْخِلَ الْبَحْرَ
((…Enyi waja Wangu ingelikuwa wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, binaadamu katika nyinyi na majini katika nyinyi mkasimama pahala pamoja na mkaniomba, na Nikawapa kila mmoja alichoomba, haitonipunguzia katika nilicho Nacho zaidi kuliko sindano inavyopunguza bahari inapochovywa. [Muslim]
Na ni Mkarimu Humruzuku Amtakaye bila ya kipimo, Anasema:
وَاللَّـهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٢١٢﴾
Na Allaah Humruzuku Amtakaye bila ya hesabu. [Al-Baqarah: 212]