09-Wewe Pekee Tunakuabudu: Kwanini Du’aa Hazitakabaliwi
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
09- Kwanini Du’aa Hazitakabaliwi
Muislamu huwa ni mtihani kwake pale anapoomba du’aa na ikawa haikukubaliwa, hasa anapopatwa na shida, dhiki na akahitaji faraja ya haraka. Ingawa kutokutakabaliwa du’aa huenda ikawa ni khayr kwa mwenye kuomba kama ilivyotangulia dalili yake, lakini pia huenda ikawa zipo sababu za kutokutakabaliwa du’aa. Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijinga dhidi ya kutokutakabaliwa du’aa kwa kuomba:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ قَلْبٍ لاَ يَخْشَعُ وَمِنْ دُعَاءٍ لاَ يُسْمَعُ وَمِنْ نَفْسٍ لاَ تَشْبَعُ وَمِنْ عِلْمٍ لاَ يَنْفَعُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَؤُلاَءِ الأَرْبَعِ))
((Ee, Allaah, hakika mimi najikinga Kwako dhidi ya moyo usionyenyekea, na dhidi ya du’aa isiyosikilizwa, na dhidi ya nafsi isiyoshiba, na dhidi ya elimu isiyonufaisha. Najikinga Kwako na haya manne)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (3482), Swahiyh Al-Jaami’ (1297)]
Na katika Muslim na An-Nasaaiy Hadiyth ya Zayd bin Arqam (Radhwiya Allaahu ‘anhu)
وَمِنْ دَعْوَةٍ لَا يُسْتَجَابُ لَه
((Na kutokana na du’aa isiyoitikiwa)) [Muslim, Swahiyh An-Nasaaiy (5473)
Baadhi ya yanayosababisha du’aa kutokutakabaliwa na dalili zake:
1- Kutokufuata Yanayosababisha Du’aa Kutakabaliwa
Kama vile; adabu za du’aa, sababu za kutakabaliwa du’aa, nyakati na sehemu za kutakabaliwa du’aa, na kutokutumia Tawassul zinazokubalika ki-shariy’ah, na kadhaalika.
02– Kuchuma Na Kula Vya Haraam
Mwenye kutaka du’aa yake ikubaliwe, ni muhimu ahakikishe kuwa chakula chake, mavazi yake na uchumi wake unapatikana kihalali, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hapokei isipokuwa yaliyo mema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّ اللَّهَ طَيِّبٌ لاَ يَقْبَلُ إِلاَّ طَيِّبًا, وَإِنَّ اللَّهَ أَمَرَ الْمُؤْمِنِينَ بِمَا أَمَرَ بِهِ الْمُرْسَلِينَ فَقَالَ: ((يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ)) وَقَالَ: ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ (( ثُمَّ ذَكَرَ الرَّجُلَ يُطِيلُ السَّفَرَ أَشْعَثَ أَغْبَرَ يَمُدُّ يَدَيْهِ إِلَى السَّمَاءِ يَا رَبِّ يَا رَبِّ وَمَطْعَمُهُ حَرَامٌ وَمَشْرَبُهُ حَرَامٌ وَمَلْبَسُهُ حَرَامٌ وَغُذِيَ بِالْحَرَامِ فَأَنَّى يُسْتَجَابُ لِذَلِكَ
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi watu, hakika Allaah ni Mzuri na Hapokei ila kilicho kizuri. Na Allaah Amewaamrisha Waumini yale yale Aliyowaamrisha Rusuli (Mitume) Akasema:
يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾
“Enyi Rusuli! Kuleni katika vizuri na tendeni mema, hakika Mimi kwa yale myatendayo Ni Mjuzi.” [Al-Muuminuwn (23:51)]
Na Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ
“Enyi walioamini! Kuleni vizuri Tulivyokuruzukuni.” [Al-Baqarah (2:172)].
Kisha akamtaja mtu aliyekuwa safarini, nywele zimemsimama timtim na mwili umejaa vumbi, anainua mikono yake mbinguni akiomba: Ee Rabb! Ee Rabb! Na hali chakula chake ni haramu, kinywaji chake ni haramu na mavazi yake ni haramu, na amelishwa vya haramu, basi vipi ataitikiwa duaa yake?!” [Muslim]
03- Kutenda Madhambi
Muislamu anapoomba du’aa ukapita muda mrefu asitakabaliwe du’aa yake, arudie kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuomba maghfirah na atubie sababu huenda akawa ametenda dhambi kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya ‘Uthmaan bin Abiy Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
(( تُفْتَحُ أَبْوَابُ السَّمَاءِ نِصْفَ اللَّيْلِ فَيُنَادِي مُنَادٍ: هَلْ مِنْ دَاعٍ فَيُسْتَجَابَ لَهُ؟ هَلْ مِنْ سَائِلٍ فَيُعْطَى؟ هَلْ مِنْ مَكْرُوبٍ فَيُفَرَّجَ عَنْهُ؟ فَلا يَبْقَى مُسْلِمٌ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ إِلا اسْتَجَابَ اللَّهُ لَهُ إِلا زَانِيَةٌ تَسْعَى بِفَرْجِهَا أَوْ عَشَّارٌ))
((Milango ya mbingu hufunguliwa inapofika nusu ya usiku, kisha hunadiwa na mwenye kunadi: “Je, yupo mwenye kuomba du’aa aitikwe? Je, yupo kwenye kutaka jambo apewe? Je, yupo mwenye dhiki afarijiwe? Basi habakii Muislamu yeyote anayeomba du’aa ila Allaah Anamtakabalia, isipokuwa mwanamke mzifinifu anayekimbia [kuuza] kwa uchi wake au mkusanyaji pesa kiharamu)) [Atw-Twabaraaniy katika Al-Mu’jam Al-Kabiyr (9/59) na Al-Mu’jam Al-Awsatw (3/154) na amesema Al-Albaaniy Isnaad yake ni Swahiyh; Swahiyh At-Targhiyb (786), Swahiyh Al-Jaami’ (2971)]
04- Kutokuamrisha Mema Na Kutokukataza Maovu:
عَنْ حُذَيْفَةَ بْنِ الْيَمَانِ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) قَالَ: ((والَّذي نَفسي بيدِهِ لتأمُرُنَّ بالمعروفِ ولتَنهوُنَّ عنِ المنكرِ أو ليوشِكَنَّ اللَّهُ أن يبعثَ عليكُم عقابًا منهُ ثمَّ تَدعونَهُ فلا يَستجيبُ لَكُم))
Kutoka kwa Hudhayfah bin Al-Yamaani (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mkononi Mwake! Mtaamrisha mema na mtakataza maovu au sivyo Allaah Atakuleteeni adhabu kutoka Kwake, kisha mtamuomba wala Hatokuitikieni)) [Ahmad na At-Tirmidhy - Swahiyh At-Tirmdhiy (2169), Swahiyh Al-Jaami’ (7070)]
Na Al-Qurtwubiy ameleza kisa cha Ibraahiym bin Ad-ham kifuatacho:
Ibraahiym bin Ad-ham aliulizwa: “Kwa nini du’aa zetu hazitakabaliwi?” Alijibu: “Kwa sababu mnamjua Allaah lakini hamumtii. Mnaisoma Qur-aan lakini hamtekelezi yaliyomo. Mnajidai kumpenda Rasuli wa Allaah lakini hamfuati Sunnah zake. Mnamjua shaytwaan, lakini hampigani naye badala yake mnamtii. Mnadai mnaijua Jannah na kuitamani, lakini hamuikimbilii kwa juhudi. Mnadai mnaujua Moto lakini hamjiepushi nao. Mnasema mauti ni haki yatawafika tu, lakini hamtayarishi nafsi zenu kwayo. Mnashughulika na aibu za watu mnaacha zenu. Mnakula katika neema za Allaah, lakini hamshukuru. Mnazika maiti zenu lakini hamjifunzi kwayo. Basi vipi mtataitikiwa?”
[Tafsiyr Al-Qurtwubiy, mj. 2, uk.312]
Na ameelezkisa hicho vilevile Ibn 'Abdil-Barr katika "Jaami' Bayaan Al-'Ilm Wa Fadhwlih", isipokuwa yeye kataja mambo matano na si kumi kama aliyoyataja Al-Qurtwubiy.