17-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kutabarruk (Kutafuta Kupata Baraka)
إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
17 -Kutabarruk (Kutafuta Kupata Baraka)
Maana ya barakah ni wingi wa khayr na kuthibitika kwake.
Tabarruk ni aina mbili; iliyothibiti ki-shariy’ah kwa kutajwa kitu fulani kina baraka kama Anavyosema Allaah (Subahaanahu wa Ta’aalaa) kuhusu Qur-aan:
كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾
Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili. [Swaad: 29]
Mfano wa kutaka baraka za Kitabu hiki (Qur-aan) ni kama vile alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ الله عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ قَرَأَ حَرْفًا مِنْ كِتَابِ اللَّهِ فَلَهُ بِهِ حَسَنَةٌ وَالْحَسَنَةُ بِعَشْرِ أَمْثَالِهَا لَا أَقُولُ الم حَرْفٌ وَلَكِنْ أَلِفٌ حَرْفٌ وَلَامٌ حَرْفٌ وَمِيمٌ حَرْفٌ))
Imetoka kwa 'Abdullaahi bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, ((Atakayesoma herufi moja katika Kitabu cha Allaah atapata hasanah (jema) moja, na kila hasanah moja ni sawa na thawabu kumi, wala sisemi 'Alif-Laam-Miym' ni herufi moja, bali Alif ni herufi moja na Laam ni herufi moja na Miymni herufi moja)) [At-Tirmidhiy (2910) na ameisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3327), Swahiyh Al-Jaami’ (6469)]
Tabarruk inagawanyika sehemu mbili:
1-Iliyothibiti katika Shariy’ah ambayo inatokana na Muislamu kufanya juhudi katika ‘amali fulani ili achume thawabu nyingi na apate khayr nyingi kabisa. Mifano ni michache ni:
i) Kusoma Qur-aan na kufuata hukumu na maamrisho yake kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah (Aayah na Hadiyth zilizotangulia kutajwa juu). Na pia Anasema Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa):
إنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾
Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri wanataraji tijara isiyoteketea.
لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾
Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila Zake, hakika Yeye ni Mwingi wa kughufuria, Mwingi wa kupokea shukurani. [Faatwir: 29-30]
ii) Kuomba maghfirah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ambayo matokeo yake ni kujipatia khayr nyingi kama ilivyo tajwa kuhusu kauli ya Nabiy Nuwh (عليه السلام) alipowalingania watu wake:
اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾
Nikasema: “Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu; hakika Yeye ni Mwingi mno wa kughufuria.
يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾
“Atakutumieni mvua tele ya kuendelea.”
وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾
“Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito.” [Nuwh: 10-12]
Na mifano michache miongoni mwa mingineyo katika Sunnah:
i) Kuswali katika Masjid Al-Haraam, Makkah ambayo Swalaah humo thawabu zake ni maradufu.
عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((صَلَاةٌ فِي مَسْجِدِي أَفْضَلُ مِنْ أَلْفِ صَلَاةٍ فِيمَا سِوَاهُ إِلَّا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ، وَصَلَاةٌ فِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ أَفْضَلُ مِنْ مِائَةِ أَلْفِ صَلَاةٍ فِيمَا سِوَاهُ)) رواه أحمد وابن ماجه
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalaah katika Msikiti wangu ni bora kuliko Swalaah elfu kwengineko isipokuwa Al-Masjid Al-Haraam. Na Swalaah katika Al-Masjid Al-Haraam ni bora kuliko Swalaah elfu mia (laki moja) kwengineko)) [Ahmad, Ibn Maajah na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy; Swahiyh Ibn Maajah (1163), Swahiyh Al-Jaami’ (3838)]
Pia:
عن أبي هريرة رضي الله عنه ان رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((من قال : لا إلهَ إلَّا اللهُ وحدَه لا شريكَ له، له المُلْكُ وله الحمْدُ، وهو على كلِّ شيءٍ قديرٌ . في يومٍ مائةَ مرَّةٍ ، كانت له عِدلُ عشرِ رِقابٍ ، وكُتِبت له مائةُ حسنةٍ، ومُحِيَتْ عنه مائةُ سيِّئةٍ ، وكانت له حِرزًا من الشَّيطانِ يومَه ذلك حتَّى يُمسيَ ، ولم يأتِ أحدٌ بأفضلَ ممَّا جاء به إلَّا رجلٌ عمِل أكثرَ منه))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ’anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayesema: Laa ilaaha illa-Allaahu Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku walahul-Hamdu wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr [Hapana muabudiwa wa haki ila ni Allaah Peke Yake, hana mshirika, ni Wake Ufalme, na ni Zake Himdi na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza], mara mia kwa siku, basi atapata sawa na thawabu za kuwaacha huru watumwa kumi na ataandikiwa mema mia moja na atafutiwa makosa mia moja, na atakuwa na kinga ya shaytwaan kwa siku hiyo yote hadi jioni na hatakuwa mtu yeyote mbora kumshinda ila yule aliyefanya zaidi yake)) [Al-Bukhaariy pamoja na Al-Fat-h, (4/95) [3293], Muslim (4/2071) [2691].
Na pia:
عن عقبة بن عامر رضي الله عنه أن خرج رسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليهِ وسلَّمَ ونحنُ في الصُفَّةِ. فقال: ((أيكم يحبُّ أن يغدو كلَّ يومٍ إلى بطحانَ أو إلى العقيقِ فيأتي منهُ بناقتيْنِ كوماويْنِ، في غيرِ إثمٍ ولا قطعِ رحمٍ؟)) فقلنا: يا رسولَ اللهِ نحبُّ ذلك. قال: ((أفلا يغدو أحدكم إلى المسجدِ فيُعَلِّمَ أو يقرأَ آيتيْنِ من كتابِ اللهِ عزَّ وجلَّ خيرٌ لهُ من ناقتيْنِ. وثلاثٌ خيرٌ لهُ من ثلاثٍ وأربعٌ خيرٌ لهُ من أربعٍ. ومن أعدادهنَّ من الإبلِ))
Imetoka kwa 'Uqbah bin 'Aamir (Radhwiya Allahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitujia wakati tulikuwa katika Swuffah akauliza, kuna yeyote miongoni mwenu anayependa kwenda soko la Butw-haan au Al-'Aqiyq na akapata humo ngamia wawili (wa thamani kabisa wa kike) bila ya kutenda dhambi au kukata undugu? Tukajibu: “Ee Rasuli wa Allaah! Tunapenda hivyo.” Akasema: ((Basi aende mmoja wenu Msikitini akajifunze au asome Aayah mbili katika Kitabu cha Allaah basi akifanya hivyo ni bora kuliko ngamia (wa thamani kabisa wa kike). Na Aayah tatu ni bora kuliko ngamia watatu, na Aayah nne ni bora kuliko ngamia wanne, na mfano wa hivyo hivyo wa Aayah kwa ngamia)) [Muslim]
2- Tabarruk iliyoharamishwa ambayo huwa shirki au bid’ah
Kuitakidi kwamba kiumbe fulani ana baraka na kumuomba kiumbe huyo khayr ambazo hana uwezo nazo isipokuwa Allaah, huwa ni shirki kwa sababu ni Allaah (Subhaanahu Ta’aalaa) Pekee Mwenye kutoka baraka kama alivyothibitisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
عن جابر بن عبد الله رضي الله عنه: رأيْتُني مع النبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم وقدْ حَضَرَتِ العَصْرُ، وليس معَنا ماءٌ غيرَ فَضلَةٍ، فجُعِلَ في إناءٍ فأُتيَ النبيُّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم بهِ، فأدْخَلَ يدَهُ فيه وفَرَّجَ أصابِعَهُ، ثم قال: ((حيَّ علَى أهلِ الوضوءِ، البَرَكَةُ مِن اللَّهِ)) فلقدْ رأيتُ الماءَ يَتَفَجَّرُ مِن بينِ أصابعِهِ، فتَوَضَّأ الناسُ وشَرِبوا، فجَعَلْتُ لا آلُو ما جَعَلتُ في بطْني منه، فعَلِمتُ أنَّه بَرَكَةٌ . قلتُ لجابرٍ :كَم كُنتُم يومَئِذٍ ؟ قال: ألْفًا وأربَعمِائةٍ
Imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Abdillaah akisema: “Nilikuwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na muda wa kuswali Swalaah ya Al-‘Aswr ukafika. Tulikuwa hatuna maji isipokuwa maji kidogo tu ambayo yalikuwa ndani ya chombo ambayo yaliletwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Basi aliweka mkono wake ndani ya maji hayo na kutandaza vidole vyake na huku akisema: ((Njooni Haraka watu wote ambao wanataka kutawadha Hii ni baraka kutoka kwa Allaah)). Nikaona maji yakibubujika kutoka katika vidole vyake. Hivyo watu walitawadha na wengine wakawa wanakunywa maji hayo na mie nilitaka kunywa maji mengi kupita kiasi (kwa sababu nilijua kuwa ilikuwa ni baraka). Mpokeaji wa Hadiyth hii kutoka kwa Jaabir alisema kuwa nilimuuliza Jaabir Je, mlikuwa watu wangapi wakati huo? Akajibu, “Tulikuwa watu elfu moja na mia nne.” [Swahiyh Al-Bukhaariy(7/543) Swahiyh Muslim (4/779)]
Aghlabu shirki na bid’ah zinazotendwa katika kutabarruk:
i-Kufanya ‘ibaadah kadhaa kama kuomba du’aa na kuswali kuelekea kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuitakidi kuwa du’aa na Swalaah hiyo ni ya kutakabaliwa au inamridhisha Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa):
Amesema Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: “‘Ulamaa wengi wamewafikiana kwamba huu ni munkar uliozushwa na ni haraam, wala ma-Imaam wa Dini hawakutofautiana kwa hili.” [Ar-Radd ‘Alal-Bakriy, uk. 56]
Na akasema kuhusu du’aa mbele ya kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Wala asisimame mtu kujiombea kwani hiyo ni bid’ah, wala hakutokea Swahaabah akisimama kaburini kujiombea bali walikuwa wakielekea Qiblah na wakiomba katika Masjid yake.” [Majmuw’ah Ar-Rasaail Al-Kubraa li Ibn Taymiyyah (2/408)], na Iqtidhwaa Swiraatw Al-Mustaqiym (2/681)]
ii- Kugusa kaburi na kuta za kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Al-Ka’bah na kujipangusia mwilini, au kubusu kwa kutegemea kupata khayr na barakah.
Lililothibiti kubusiwa ni Al-Hajar Al-Aswad pekee lilioko katika Al-Ka’bah kwa dalili:
((إِنَّ مَسْحَ الْحَجَرِ الأَسْوَدِ ، والركنَ اليمانيِّ، يَحُطَّانِ الخطايا حطًّا))
((Kugusa Al-Hajar Al-As-wad na Ar-Rukn al-Yamaaniy ni kufutiwa madhambi)) [Hadiyth ya Ibn ‘Umar; Swahiyh Al-Jaami’ (2194)]
Na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipolibusu alisema:
"إني أَعْلَمُ أَنَّكَ حَجَرٌ لا تَضُرُّ ولا تَنْفَعُ، وَلَوْلا أَنِّي رأيت النبي صلى الله عليه وسلم يُقَبِّلُكَ ما قَبَّلْتُكَ" - البخاري و مسلم
“Hakika mimi najua kwamba wewe ni jiwe usiloweza kudhuru wala kunufaisha, na ingelikuwa sikumuona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakubusu basi nami nisingelikubsu.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
iii-Kutabarruk sehemu sehemu ambazo zimetajwa katika Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imedhihirika watu wengi kukosea wanapofika Makkah au Madiynah kutekeleza ‘Umrah kupendelea kutembelea sehemu hizo wakiitakidi kuwa zina baraka na wengine hufika kujikalifisha kupanda majabali kama Jabal Ath-Thawr, Ghaar Hiraa, Jabali la ‘Arafah na sehemu nyinginezo.
Haikuthibiti kuwa Swahaabah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walitabarruk na chochote au popote alipopita au alipokaa kitako Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuwa wao walikuwa na mapenzi makubwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wenye kutilia hima zaidi ya kutekeleza Sunnah.
Shaykh Al-Islaam amesema: “Kina Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan na wengineo miongoni mwa Al-Muhaajiriyn na Answaar walikuwa wakisafiri kutoka Madiynah mpaka Makkah kutekeleza Hajj na ‘Umrah wala haikupokelewa kutoka kwao kuwa mmoja wao alikuwa akitafuta sehemu alizokuwa akiswali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salalm). Basi ni dhahiri kwamba ingekuwa ni jambo la kupendekezwa wangekuwa wao ni wa kwanza kutangulia kufanya, kwani wao ni wajuzi zaidi wa Sunnah zake na wenye kufuata mno kuliko wengineo.” [Iqtidhwaa Swiraatw Al-Mustaqiym (2/748)]
Katika moja ya msafara wake kwenda vitani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba zake walipitia sehemu wakataka kutafuta baraka kwa kuweka silaha zao katika mti, lakini aliwakataza. Na hii ni dalili pia haipasi kutabarruk kwa miti na vitu kama hivyo.
عن أَبِي وَاقٍد اللَّيْثِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: خَرَجْنَا مَعَ النَّبِيِّ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآله وَسَلَّمَ) إِلَى حُنَيْنٍ وَنَحْنُ حُدَثَاءُ عَهْدٍ بِكُفْرٍ، وَلِلِمُشْرِكِينَ سِدْرَةٌ، يَعْكُفُونَ عِنْدَهَا وَيُنَوِّطُونَ بِهَا أَسْلِحَتَهُمْ، يُقَالَ لَهَا ذَاتُ أَنْوَاطٍ، فَمَرَرْنَا بِسِدْرَةٍ فَقُلْنَا: يَا رَسُولَ اللهِ اجْعَلْ لَنَا ذَاتَ أَنْوَاطٍ كَمَا لَهُمْ ذَاتُ أَنْوَاط. فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم):َ((الله أكبر! هَذَا كَمَا قَالَ قَوْمُ مُوسَى "اجْعَلْ لَنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ" وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَتَرْكَبُنَّ سُنَّةَ مَنْ كَانَ قَبْلَكُمْ))
Imepokewa kutoka kwa Abuu Waaqid Al-Laythiyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Tulitoka pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda (vitani) Hunayn nasi ndio kwanza tumetoka katika ukafiri, na washirikina walikuwa na mkunazi wanaufanyia ‘ibaadah na walikuwa wakitundika silaha zao (kupata baraka). Wakiuita ‘Dhaatu Anwaatw’. Tukapita mbele ya mkunazi tukasema: “Ee Rasuli wa Allaah, tufanyie nasi Dhaata Anwaatw kama walivyokuwa nao (makafiri) Dhaatu Anwaatw.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Allaahu Akbar! (Allaah ni Mkubwa!) Hivi ni kama walivyosema watu wa Muwsa “Tufanyie nasi muabudiwa kama walivyokuwa nao muabudiwa.” Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, mtafuata nyendo za walio kabla yenu [za ujahili na kufru].)) [At-Tirmidhiy; Swahiyh At-Tirmidhiy (2180)]
iv- Kutabarruk kwa Msahafu:
Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amejibu Swali: “Kuweka Msahafu katika gari kwa ajili ya kujikinga na khatari au kujikinga na jicho ni bid’ah, kwani Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) hawakuwa wakibeba Misahafu walipokuwa wakipanda ngamia wao kwa ajili ya kujikinga na khatari au jicho baya.” [Fataawaa Nuwr ‘Alad-Darb (2/4)]
v-Kutabarruk kwa watu kama mashekhe na wanaoitwa masharifu, kwa kuwagusa au kupangusa nguo zao au kuvaa nguzo zao au kunywa kinywaji walichoanza kunywa, au maji waliyoyatemea mate n.k. kwa kutegemea au kuitakidi vitu hivyo vina baraka.
Haikuthibiti kutoka kwa Swahaba kwamba walitabarruk kwa Swahaabah watukufu, kama Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wala wengineo waliobashiriwa Jannah wala watu wa nyumba ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo kufanya hivyo si jambo lenye kukubalika katika Shariy’ah.