07 - Mambo Ya Haramu Kwa Vinyozi: Kubandikwa Mapicha Saluni Na Kuwakimbiza Malaika
Mambo ya Haramu yanayofanyika katika kazi ya Unyozi:
7. Kubandikwa Mapicha Mbalimbali Ndani Ya Saluni Zao Na Kuwakimbiza Malaika Katika Maeneo Yao
Inafahamika kuwa Malaika hawaingii sehemu yenye picha, na isitoshe picha zenyewe nyingi wanazobandika ni za watu zenye kuonesha mitindo ya nywele ya kikafiri na za ukosefu wa adabu na maadili. Na picha zingine ni za wanamuziki wakosa maadili na watu wajinga waliokosa mielekeo katika hii dunia.
Imepokewa kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kuwa niliupamba mto wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na picha (michoro) za wanyama ambacho kilionekana kama mto mdogo. Alikuja akasimama kati ya watu akiwa na taharuki iliyoonekana usoni mwake. Nikasema, “Ee Rasuli wa Allaah! Kuna nini?” Akasema: “Huu mto ni wa nini?” Nilisema: “Nimeutayarisha kwa ajili yako ili upate kuuegemea.” Alisema: “Kwani wewe hujui kuwa Malaika hawaingii katika nyumba ambazo kuna picha ndani yake; na yeyote mwenye kutengeneza picha ataadhibiwa Siku ya Qiyaamah na ataambiwa kukipatia uhai (kwa alichokiumba).” [Al-Bukhaariy]
Mambo ya picha za viumbe ni ya kuepukwa kwa makemeo makali yatokayo kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyosimulia Ibn Mas‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Hakika aliye na adhabu kali zaidi ya wote Siku ya Qiyaamah ni watengeneza picha.” [Al-Bukhaariy, Muslim na An-Nasaaiy]
Sa‘iyd bin Abil-Hasan amesema nilipokuwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuja mtu akasema, “Ee Ibn ‘Abbaas! Riziki yangu inatokana na kazi yangu ya kutengeneza picha hizi.” Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alisema: “Nitakuambia yale tu niliyoyasikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nilimsikia akisema, ‘Yeyote mwenye kutengeneza picha ataadhibiwa na Allaah mpaka aitie uhai na hatoweza kufanya hivyo.” Aliposikia hayo yule mtu alivuta pumzi na uso wake ukaiva. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alimuambia: “Sikitiko lilioje! Ikiwa huna budi mpaka ufanye picha basi nakunasihi uchore picha za miti na kitu chengine chochote ambacho hakina uhai.” [Al-Bukhaariy]
Hizo ni dalili chache katika nyingi zenye kuonesha ubaya wa picha, na inampasa yeyote yule mwenye kuiweka dini yake mbele kuliko matamanio ya nafsi yake na tamaa za chumo na kipato cha haraka, ajiepushe na mambo hayo ili kuilinda dini yake na kuhifadhi heshima yake.