006-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-HAYYU
أسماء الله الحسنى وصفاته
Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake
الْحَيّ
006 - AL-HAYYU
AL-HAYYU: Aliye hai daima
Aliye hai kinyume na aliyekufa, mkamilifu katika maisha yake Aliyetukuka. Hakuna katika uwepo aliyekuwa na maisha yake mwenyewe kwa dhati yake, isipokuwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Peke Yake.
Mwenye uhai mkamilifu wa uwepo Wake, na mkamilifu kwa zama Zake.
Maisha Yake yametangulia; hakutanguliwa na kutokuwepo, wala hakumfikii kutokuwepo wala kuondoka. Kila kiumbe kitatoweka isipokuwa Yeye kama Anavyosema:
وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٨﴾
Na wala usiombe pamoja na Allaah mungu mwengine. Hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. Hukumu ni Yake Pekee na Kwake Pekee mtarejeshwa. [Al-Qaswasw: 88]
Na pia:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾
Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka.
وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾
Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali Na Ukarimu. [Ar-Rahmaan: 26-27]
Imaam As-Sa’dy (Rahimahu Allaah) amesema: “Yaani, kila kilichopo juu ya ardhi kati ya bin Aadamu na majini na wanyama na viumbe vyote vinginevyo vitatoweka na vitakufa na vitaangamia na Atabakia Aliye hai Ambaye hafi.”
Katika ukamilifu wa maisha Yake, Hachukuliwi na usingizi, wala upungufu wala udhaifu wala usahaulifu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ
Allaah, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Aliye hai daima, Msimamia kila kitu. Haumchukui usingizi wala kulala. [Al-Baqarah: 255]
Amethibitisha pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Jina Lake au Sifa Yake hiyo katika Aayah kadhaa nyinginezo: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ
Na tawakali kwa Aliye hai Ambaye Hafi. [Al-Furqaan: 58]
هُوَ الْحَيُّ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ ۗ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٥﴾
Yeye Ndiye Aliye hai daima hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye; basi muombeni Yeye wenye kumtakasia ‘ibaadah. AlhamduliLLaah, Himidi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu. [Ghaafir: 65]
Na Limetajwa Jina hili la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu) mara tatu katika Qur-aan:
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ
Allaah, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Aliye hai daima, Msimamia kila kitu [Al-Baqarah: 255]
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ﴿٢﴾
Allaah, Muabudiwa wa haki ila Yeye, Aliye hai daima, Msimamia kila kitu. [Aal-‘Imraan: 2]
وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَيِّ الْقَيُّومِ ۖ وَقَدْ خَابَ مَنْ حَمَلَ ظُلْمًا ﴿١١١﴾
Nyuso zitanyenyekea kwa Aliye hai daima, Msimamizi wa kila kitu. [Twaahaa: 111]
Na Majina haya mawili ndio ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa ni Majina Matukufu kabisa ambayo mtu akiomba du’aa kutawassal kwayo, du’aa yake huitikiwa, kwa dalili zifuatazo:
عَنْ الْقَاسِمِ عَنْ أَبِي أُمَامَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((اسْمُ اللَّهِ الأَعْظَمُ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ فِي سُوَرٍ ثَلاَثٍ: الْبَقَرَةِ ,وَآلِ عِمْرَانَ, وَطه))
Kutoka kwa Al-Qaasim, kutoka kwa Abuu Umaamaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Jina Tukufu kabisa la Allaah Ambalo likiombewa kwalo Anaitikia, limo katika Suwrah tatu; Al-Baqarah, Aal-‘Imraan, na Twaahaa)) [Swahiyh Ibn Maajah (3124)]
عَنْ أَسْمَاءَ بِنْتِ يَزِيدَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((اسْمُ اللَّهِ الأَعْظَمُ فِي هَاتَيْنِ الأَيَتَيْنِ: (وَإِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ لاَ إِلَهَ إلاَّ هُوَ الرَّحْمَنُ الرَّحِيمُ) وَفَاتِحَةِ آلِ عِمْرَانَ (الم اللَّهُ لاَ إِلَهَ إلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّوم).
Kutoka kwa Asmaa bint Yaziyd (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Jina Tukufu kabisa la Allaah limo katika Aayah zifuatazo: “Na Ilaah wenu (Allaah) ni Ilaah Mmoja, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mwingi wa rahmah, Mwenye kurehemu.” (Al-Baqarah: 163) na ufunguo (mwanzo) wa Aal-‘Imraan: “Allaah, Muabudiwa wa haki ila Yeye, Aliye hai daima, Msimamia kila kitu. (Aal-‘Imraan: 2). [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah – Hadiyth Hasan Swahiyh]
Na katika du’aa za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ وَبِكَ آمَنْتُ وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ وَبِكَ خَاصَمْتُ. اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِعِزَّتِكَ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ أَنْ تُضِلَّنِي أَنْتَ الْحَيُّ الَّذِي لاَ يَمُوتُ وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ يَمُوتُونَ
Allaahumma Laka aslamtu, wa Bika aamantu, wa ‘Alayka tawakkaltu, wa Ilayka anabtu, wa Bika khaaswamtu. Allaahumma inniy a’uwdhu bi-Izzatika laa ilaaha illa Anta an-tudhwillaniy Antal-Hayyu Alladhiy laa Yamuwtu wal-jinnu wal-insu yamuwtuwna.
Ee Allaah, Kwako najisalimisha na Kwako naamini na Kwako natawakali na Kwako narejea kutubia na Kwako nagombana [dhidi ya adui]. Ee Allaah, hakika mimi najikinga kwa ‘Izzah Utukufu wako, Hapana Muabudiwa wa haki ila Wewe Usije kunipotoa Wewe Uliye hai daima Ambaye Hafi ilihali majini na watu wanakufa. [Muslim, Ahmad]
لا إلهَ إلاّ اللّه وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُلْـكُ ولهُ الحَمْـد، يُحْيـي وَيُميـتُ وَهُوَ حَيٌّ لا يَمُـوت، بِيَـدِهِ الْخَـيْرُ وَهوَ عَلىَ كلّ شيءٍ قَدِيرٌ.
Laa ilaaha illa Allaahu Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku wa Lahul-Hamdu, Yuhyiy wa Yumiytu wa Huwa Hayyun laa yamuwtu, Biyadihil-khayru wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr
Hapana Muabudiwa wa haki ila Allaah, Yu Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake Ufalme na Himdi ni Zake, Anahuisha na Anafisha, Naye ni hai Asiyekufa, khayr iko mikononi Mwake, na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza. [Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khattwaab kaikusanya At-Tirmidhiy (5/291) [3429], Al-Haakim (1/538), Ibn Maajah [2235] Ad-Daarimiy na ameipa daraja ya Hasan Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (2/21) na Swahiyh At-Tirmidhiy (3/152). Na vilevile katika Swahiyh Al-Jaami’ (6231)]
يا حَـيُّ يا قَيّـومُ بِـرَحْمَـتِكِ أَسْتَـغـيث، أَصْلِـحْ لي شَـأْنـي كُلَّـه، وَلا تَكِلـني إِلى نَفْـسي طَـرْفَةَ عَـين
Yaa Hayyu Yaa Qayyuwm bi-Rahmatika astaghiythu, Aswlih-liy sha-ani kullahu walaa takilniy ilaa nafsiy twarfata ‘aynin
Ee Uliye hai daima, Msimamizi wa kila kitu, kwa rahmah Zako ninakuomba uniokoe, nitengenezee mambo yangu yote, wala usiniachie mambo yangu mwenyewe (pasina kunisaidia) hata kwa (muda mdogo kama muda wa) kupepesa jicho. [Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) - Abuu Daawuwd (4/3180), At-Tirmidhiy (5/465), Al-Haakim, Swahiyh At-Targhiyb (1/273), Swahiyh Al-Jaami’ [5820]
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) إِذَا كَرَبَهُ أَمْرٌ قَالَ: ((يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ))
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapofikwa na janga husema: ((Yaa Hayyu Yaa Qayyuwm bi Rahmatika astaghiythu - Ee Uliye hai daima, Msimamia wa kila kitu, kwa rahmah Zako naomba uokozi)) [At-Tirmidhy Hadiyth Hasan]
من قالَ: أستَغفرُ اللَّهَ الَّذي لا إلَهَ إلَّا هوَ الحيَّ القيُّومَ، وأتوبُ إليهِ، غُفِرَ لَهُ، وإن كانَ قد فرَّ منَ الزَّحفِ
Atakayesema: “AstaghfiruLLaah Alladhiy laa ilaaha illa Huwa Al-Hayyu Al-Qayyuwm, wa atuwbu Ilayhi.
Naomba maghfirah kwa Ambaye hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye Aliye hai daima, Msimamizi wa kila kitu, na natubia Kwake,
Ataghufuriwa hata akiwa amekimbia katika vita. [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Al-Haakim Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Mas’uwd, Zayd bin Haarithah mkombolewa wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr Asw-Swiddiyq, Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy, Anas bin Maalik, Baraa bin ‘Aazib (Radhwiya Allaahu ‘anhum) – As-Silsilah Asw-Swahiyhah (2727), Swahiyh At-Targhiyb (1623). Swahiyh Abiy Daawuwd (1517)]