013-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-WAAHIDU, AL-AHAD

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الْوَاحِدُ - الأحَدُ

AL-WAAHIDU – AL-AHAD

 

 

 

Al-Waahid – Al-Ahad: Mmoja Pekee Asiye Na Mfano

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mmoja Pekee Asiye na mfano. Ni Mmoja Pekee kwa dhati Yake Na Sifa Zake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mmoja Pekee katika Sifa Zake za Rubuwbiyyah (Uumbaji, Ufalme, Uola, Kuruzuku, Kuendesha mambo ya Waja Wake), na katika Uluwhiyyah (kuabudiwa Kwake) na katika Asmaa na Swifaat (Majina na Sifa).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alikuwa ni Mmoja Pekee hapo awali hapakuwa na kitu kabla Yake na Yungali Mmoja Pekee, na Atakuwa Mmoja Pekee Milele, hakuna kitu baada Yake. 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mmoja Pekee, Hana mshirika, Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾

1. Sema: “Yeye ni Allaahu Mmoja Pekee.

 

اللَّـهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾

2. “Allaah ni Aliyekamilika sifa za utukufu Wake, Mkusudiwa haja zote. 

 

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ﴿٣﴾

3. “Hakuzaa na wala Hakuzaliwa.

 

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾

4. “Na wala haiwi Awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye.” [Al-Ikhlaasw: 112]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

Na sema: “AlhamduliLLaah Kuhimidiwa ni kwa Allaah Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala hakuwa dhalili hata awe (anahitaji) mlinzi, msaidizi; basi mtukuze matukuzo makubwa kabisa (Sema Allaahu Akbar!) [Al-Israa: 111]

 

 

Ni Mmoja Pekee na Atabaki kuwa Pekee na Hatokuwa na mwengine pamoja Naye [An-Nihaayah (1/35)]

  

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wametofautisha baina ya Al-Waahid na Al-Ahad wakasema kwamba: ‘Waahid’ inawezekana kugawika katika mbili na zaidi. Mfano husemwa: Waahid (moja), ithnaan (mbili), thalaathah (tatu). Ama ‘Ahad’ maana yake ya kiasili ni kuwa haiwezekani kugawika katika mbili au zaidi; hivyo husemwa: ‘Ahad’ (moja pekee) na hiasemwi: ‘ahad, ithnaan, thalaathah n.k.  Na wakasema pia: ‘Al-Waahid’ ni Mmoja Pekee,kwa dhati Yake. Ama ‘Ahad’ Ni Mmoja Pekee katika dhati Yake na Sifa Zake. [Tafsiyr Asmaa Allaah - Az-Zajjaaj (Uk.58)].

 

Hivyo basi, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Al-Waahid, Al-Ahad Ambaye hakuna wa pili Naye, wala Hana mshirika, wala mfano Wake. Naye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ambaye waja Wake wote wanamtegemea Yeye, na wanamkusudia Yeye kwa kila jambo na wala hawatawakali kwa yeyote ispokuwa Kwake Yeye [Ishtiqaaq Asmaai Allaah (90-93)]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye ni Al-Waahid hakuna chochote au yeyote mwenye mfano Wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11]

 

 

Na Ibn Jariyr akasema kuhusu maana ya ‘Kumpwekesha Allaah’ katika kuifasiri kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٣﴾

“Na Ilaah wenu (Allaah) ni Ilaah Mmoja, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mwingi wa rahmah, Mwenye kurehemu.” [Al-Baqarah: 163]

 

 

“Na Ambaye Anastahiki kutiiwa nanyi enyi watu! Na imekuwajibikieni kufanya ‘ibaadah kwa Mwenye kustahiki kuabudiwa Mmoja Pekee na Rabb Mmoja Pekee, basi msimwabudu mwengine wala msimshirikishe na yeyote, kwani mkimshirikisha na mwengine katika ‘ibaadah zenu, basi huyo mnayemshirikisha ni kiumbe kama nyinyi katika viumbe vya Ilaah wenu (Mwabudiwa wa haki). Na Ilaah wenu ni Illaah Mmoja Pekee Hana  mfano Wake wala aliye sawa Naye. [Tafsiyr Atw-Twabariy].

 

Jina la  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ‘Al-Waahid’ limetajwa katika Qur-aan zaidi ya mara  ishirini; Baadhi ya Aayah ni:

وَقَالَ اللَّـهُ لَا تَتَّخِذُوا إِلَـٰهَيْنِ اثْنَيْنِ ۖ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ ﴿٥١﴾

Na Allaah Anasema: “Msijichukulie waungu wawili; hakika Yeye Ndiye Muabudiwa wa haki Mmoja Pekee basi niogopeni Mimi tu.  [An-Nahl: 51]

 

فَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا ۗ وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ ﴿٣٤﴾

Kwa hiyo Muabudiwa wenu wa haki ni Ilaah Mmoja Pekee, basi Kwake jisalimisheni. Na wabashirie wanyenyekevu.  [Al-Hajj: 34]

 

 

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni mtu kama nyinyi, nafunuliwa Wahy kwamba: Hakika Muabudiwa wa haki wenu ni Ilaah Mmoja Pekee. Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asishirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake” [Al-Kahf: 110]

 

 

لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ ثَالِثُ ثَلَاثَةٍ ۘ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۚ وَإِن لَّمْ يَنتَهُوا عَمَّا يَقُولُونَ لَيَمَسَّنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni watatu wa utatu. ”Na hali hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Ilaah Mmoja Pekee. Na wasipoacha yale wanayoyasema, bila ya shaka itawagusa wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo. [Al-Maaidah: 73]

 

 

Na pia Jina hili la ‘Al-Waahid’ Limeungana mara sita katika Qur-aan pamoja na Al-Qahhaar’ (Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika):

 

لَّوْ أَرَادَ اللَّـهُ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا لَّاصْطَفَىٰ مِمَّا يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ سُبْحَانَهُ ۖ هُوَ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٤﴾

Lau Angelitaka Allaah kujichukulia mwana, Angelichagua Amtakaye miongoni mwa Aliowaumba. Subhaanah! Utakasifu ni Wake. Yeye Ndiye Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika. [Az-Zumar: 4]

 

 

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾

Sema: “Ni nani Rabb wa mbingu na ardhi?” Sema: “Ni Allaah.” Sema: “Je, mnawafanya wengineo badala Yake kuwa walinzi na hali hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao manufaa wala dhara?”  Sema: “Je,   kipofu analingana sawa na mwenye kuona, au je, viza vinalingana sawa na nuru?” Au wamemfanyia Allaah washirika wameumba kama kwamba uumbaji Wake, kisha yakafanana maumbile kwao?  Sema: “Allaah  ni Muumbaji wa kila kitu, Naye ni Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Mshindi, Asiyepingika.” [Ar-Ra’d: 16]

 

يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ ﴿١٦﴾

Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. “Ufalme ni wa nani leo?” (Allaah Mwenyewe Atajijibu): “Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika.” [Ghaafir: 16]

 

يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٣٩﴾

“Enyi sahibu zangu wawili wa jela. Je, marabi wengi wanaofarakana ni bora (kuabudiwa) au Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika.” [Yuwsuf: 39]

 

قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنذِرٌ ۖ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٦٥﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hakuna Muabudiwa wa haki yeyote isipokuwa Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika. [Swaad: 65]

 

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ ﴿٤٨﴾

Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia na (viumbe wote) watahudhuria kwa Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika.” [Ibraahiym: 48]

 

 

Kutajwa Majina mawili haya mazuri kwa pamoja,  inamaanisha kuwa ni Yeye Allaah Pekee Mwenye mamlaka na uwezo wa kufanya lolote Alitakalo, Hakuna wa kumpinga na hivyo kila kilichokuwa mbinguni na ardhini kinajisalimisha Kwake Yeye Pekee Al-Waahid. 

 

 

Ama Jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ‘Al-Ahad’ Limetajwa mara moja katika Suwrat Al-Ikhlaasw [114]

 

 

Vipi kuabudu na kufanyia kazi  Jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ‘Al-Waahid’ na ‘Al-Ahad’:

 

1. Mdhukuru Al-Waahid kwa kutamka neno la kumpwekesha Allaah, (Tawhiyd)  “Laa ilaaha illa Allaah” kwa wingi na ambayo ni maneno yanayotajwa katika adhaan na iqaamah za Swalaah, na ufanyie kazi maana yake. Pia kutamka du’aa au nyiradi inayosomwa katika adhkaar za kila baada ya Swalaah za fardhi, pamoja na nyakati nyinginezo ambazo zimejaa fadhila na faida zake kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:

 

((خَيْرُ الدُّعَاءِ دُعَاءُ يَوْمِ عَرَفَةَ، وخَيْرُ مَا قُلْتُ أنَا وَالنَّبيُّونَ مِنْ قَبْـلِي: لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ، ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِير)) روى الترمذي

((Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Manabii kabla yangu ni: 'Laa Ilaaha illa Allaah Wah-dahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku wa-Lahul-hamdu wa Huwa 'alaa kulli shay-in Qadiyr – Hapana Muabudiwa wa haki ila Allaah, Yu Pekee, Hana mshirika, ufalme wote ni Wake, na kuhimidiwa ni Kwake, Naye ni Mweza wa kila kitu daima)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (3/184), Silsilah Al-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (4/6)]

 

 

2. Mpwekeshe Muumba wako (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Al-Waahid, kwa kutokumshirkisha na chochote kwa sababu kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni dhulma kubwa mno.

 

 

3. Kuwa na ikhlaasw; kumsafishia niyyah Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Al-Waahid, katika ’amali zako zote kwa kuwa hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki ila Yeye, wala kuadhimishwa isipokuwa Yeye wala kutiiwa isipokuwa Yeye wala kuridhishwa isipokuwa Yeye. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.”

 

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza.  [Al-An’aam: 162-163]

 

 

4. Tafakari na zingatia dalili za Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Al-Waahid, katika uumbaji Wake (Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah) kwa kuangaza kila aina ya uumbaji Wake unaokuzunguka mahali popote ulipo, ujue kuwa hakuna yeyote awezaye kuumba kama uumbaji wa Al-Waahid.

 

5. Tawakali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee katika mambo yako yote. Usikhofu chochote kitakachokupeleka katika shirki, bali tawakali kwa Al-Waahid Al-Ahad.

 

Kumbuka kisa cha Bilaal (Radhwiya Allaahu ’anhu) ambaye alikuwa ni mtumwa wa Ummayyah bin Khalaf pale alipoghadhibika naye alipotambua kuwa ameacha dini yao ya kuabudu masanamu akaingia Uislamu.

 

Umayyah akawa anamtesa Bilaal (Radhwiya Allaahu ’anhu) kwa kumweka katika jua kali bila ya chakula wala maji huku akimwekea jiwe kubwa kifuani mwake lilokaribia kumzuia pumzi.

Aliendelea kumtesa kwa sababu Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimkatalia kumtaka kwake amkanushe Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) ili arudi katika ukafiri akimtishia kuwa atamuua pindi akikataa kumtii.

 

Lakini juu ya mateso hayo, Bilaal (Radhwiya Allaahu ’anhu) alitamka maneno mazito ya kusisimua yenye kumbukumbu katika Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) nayo ni  ”Ahadun Ahadun” (Mmoja, Mmoja Pekee).  Baada ya masiku kupita Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ’anhu) akamnunua na kumwacha huru, na ndipo Nabiy (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) akampa kazi tukufu kabisa ya kuadhini ambayo inashuhudia Tawhiyd ya Allaah na Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) akawa ni mwenye hadhi kubwa na maarufu mpaka kwa watoto wa Kiislamu kutokana na kisa chake hiki chenye mafunzo kwa kila mtu.  

 

 

 

 

Share