Salmaan Al-Faarisiy (رضي الله عنه)
Salmaan Al-Faarisiy (Radhwiya Allahu ‘anhu)
Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)
Utangulizi
Huyu ni Swahaba aliyepania kuutafuta ukweli, kuitafuta haki, kuitafuta nuru ya Rabb wake, na kwa ajili ya lengo hilo adhimu ilimbidi awakimbie wazazi wake, aukimbie mji wake, aifunge safari ndefu iliyomchukua miaka mingi na kumuingiza katika shida, matatizo na adhabu mbali mbali, bila kukata tamaa wala kuvunjika moyo, mpaka alipofanikiwa kulifikia lengo lake.
Swahaba huyu si mwengine isipokuwa ni Salmaan Al-Faarisiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) mwana wa mkuu wa kijiji kimojawapo katika nchi ya Persia (Iran) kiitwacho Jiyyan, aliyekuwa tajiri kupita wote katika kijiji hicho.
Hebu tumuache Salmaan mwenyewe (Radhwiya Allahu ‘anhu) atuhadithie juu ya kisa chake hicho.
Anasema Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
“Nilikuwa kijana wa kawaida wa kifarisi nikiishi katika mji wa Asfahan (Iran) katika kijiji kiitwacho Jiyyan.
Baba yangu alikuwa mkuu wa kijiji chetu na alikuwa pia tajiri kupita wote katika kijiji chetu na alikuwa na daraja kubwa kupita wote, na tokea nilipokuwa mtoto mchanga alikuwa akinipenda kupita kiumbe chochote.
Mapenzi yake juu yangu yalikuwa yakikuwa na kuongezeka kila umri wangu unapokuwa na kuongezeka, na kutokana na wingi wa khofu yake juu yangu alikuwa akinizuwia nisitoke nje kama wanavyozuiwa watoto wa kike ili nisije nikadhurika.
Nilijitahidi sana kuitumikia dini ya ‘Majusi’ ‘Zoroastrian’ mpaka nikapewa mimi jukumu la ulinzi wa moto tuliokuwa tukiuabudu. Nikawa mtoaji amri ya kuongeza kuni pale panapohitajika wakati wowote ule usiku au mchana ili moto huo usipate kuzimika.
Baba yangu alikuwa na Shamba kubwa sana lililokuwa likituingizia mapato makubwa, na yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akisimamia na kuendesha shughuli zake.
Siku moja baba yangu alikuwa na mashughuli mengi na hakupata nafasi ya kwenda kijijini kusimamia shughuli za Shamba lake hilo, akanambia:
“Mwanangu! Kama uonavyo sikupata nafasi leo ya kwenda Shambani, kwa hivyo nenda wewe badala yangu ukasimamie shughuli zangu.”
Nikatoka kuelekea Shambani kwetu, lakini nilipokuwa njiani nilipita nje ya mojawapo ya makanisa ya Manaswara (Wakristo) nikavutiwa sana na sauti zao walipokuwa wakiswali, nikasimama kuwasikiliza.
Sikuwa na elimu yoyote juu ya dini ya Manaswara wala juu ya dini yoyote nyingine kutokana na kuzuiliwa na baba yangu nyumbani muda wa miaka mingi, na niliposikia sauti zao nikaingia ndani ya kanisa ili nipate kujua yale wanayotenda.
Nilipokuwa nikiwaangalia, nikavutiwa sana na namna waliyvokuwa wakiswali, nikatamani niingine katika dini yao, nikasema:
“Wa-Allaahi dini hii ni bora kuliko dini yetu’. Wa-Allaahi sijaondoka mpaka jua lilipozama, na sijawahi tena kwenda Shambani aliponituma baba yangu. Na kabla ya kuondoka nikawauliza:
“Dini hii asili yake inatokea wapi?”
Wakanambia;
“Nchi ya Shaam (Syria).”
Ulipoingia usiku nikarudi nyumbani kwetu na baba yangu akawa anataka kujuwa habari za Shambani alikonituma. Nikamwambia:
“Ewe baba yangu! Nilipita mahali penye kanisa, nikaona watu wakiswali nikavutiwa sana na dini yao, nikabaki hapo mpaka jua lilipozama.”
Baba yangu akaghadhibika sana na yale niliyotenda akaniambia:
“Ewe mwanangu! Dini ile haina khayr yoyote. Dini yako na dini ya baba zako ndiyo yenye Khayr.”
Nikamwambia:
“Hapana Wa-Allaahi! dini yao ni bora kupita dini yetu.”
Maneno yangu yakamtia khofu baba yangu, akaogopa nisije nikatoka katika dini yake, akanizuwia nisitoke tena nyumbani, na akanifunga miguu yangu.
Safari Ya Kuutafuta Ukweli
Nilipopata fursa nikamtuma mtu ende kwa wale Manaswara kanisani na awaambie kuwa wanijulishe iwapo watasikia juu ya msafara wowote ule utakaokwenda nchi ya Shaam.
Haukupita muda wakaniletea habari juu ya msafara unaokwenda nchi ya Shaam, na baada ya kufanikiwa kuzifungua kamba nilizofungwa na baba yangu, nikakimbia na kuungana na msafara huo na kuianza safari ndefu kuelekea Shaam.
Mara baada ya kuwasili nikawa nawauliza watu:
“Mtu gani aliye bora kupita wote wenye kufuata dini hii?”
Wakaniambia:
“Askofu anayesimamia kanisa.”
Nikamwendea na kumwambia:
“Mimi nimependezewa na dini ya kinaswara na napenda niwe pamoja nawe, niwe nikikutumikia na kujifunza kutoka kwako, na kuswali pamoja nawe.”
Akaniambia:
“Ingia!.”
Nikaingia ndani kwake, na nikawa namtumikia, na haukupita muda nikatambua kuwa alikuwa mtu muovu aliyekuwa akikusanya pesa za sadaka kutoka kwa wafuasi wake huku akiwafundisha juu ya thawabu nyingi zinazopatikana ndani yake, kisha wanapompa pesa hizo kwa ajili ya kuzigawa katika njia ya Allaah, yeye alikuwa akizificha na kuzirimbikiza kwa ajili ya nafsi yake na wala hakuwa akiwapa masikini wala mafakiri chochote katika pesa hizo, mpaka akaweza kujaza makasiki saba ya dhahabu.
Nilimchukia sana kwa yale niliyoyaona kutoka kwake, lakini hakuishi muda mrefu akafariki dunia, na Manaswara wafuasi wake walipojikusanya kwa ajili ya kumzika nikawaambia:
“Sahibu yenu huyu alikuwa mtu muovu, akikuamrisheni kutoa sadaka na kukujulisheni juu ya thawabu nyingi zinazopatikana ndani yake, kisha mnapomletea pesa hizo, yeye anazikusanya kwa ajili ya nafsi yake na wala hakuwa akiwapa masikini chochote katika mali hiyo.”
Wakaniuliza:
“Umejuwaje?”
Nikawaambia:
“Nikuonesheni ilipo hazina yake?”
Wakaniambia:
“Tuoneshe.”
Nikawaonesha mahali pesa zilipo, wakatoa makasiki saba yaliyojaa dhahabu na fedha, kisha wakasema:
“Wa-Allaahi hatumziki.”
Wakamsulubu na kumpiga mawe, na haukupita muda mrefu wakamteua mtu mwengine kushika mahali pake, nikawa naye, na sijapata kumuona mtu aliyeikinai dunia na kuipenda Aakherah kupita yeye. Alikuwa mtu mwenye kufanya ibada usiku na mchana, na kwa ajili hiyo nikampenda sana na nikawa pamoja naye kwa muda wa miaka mingi.
Alipokuwa anafariki dunia nikawa namuuliza:
“Ewe fulani! Unaniusia niende kwa nani baada ya kufariki kwako?’
Akaniambia:
“Ewe mwanangu! Simjuwi yeyote mwenye kufuata ninayofuata mimi isipokuwa mtu mmoja anayeishi katika mji wa Mousil na jina lake ni fulani. Mtu huyu hajabadilisha wala kuongeza, kwa hivyo mwendee.”
Safari Ya Mousil Na Nasibeen
Alipofariki swahibu yangu huyu, nikaifunga safari ya kwenda mji wa Mousil alikoninasihi niende, na nilipowasili kwake nikamhadithia habari zangu, nikamwambia:
“Fulani alipokuwa akifariki aliniusia nije kwako, na akaniambia kuwa wewe umeshikamana na haki kama alivyokuwa yeye.”
Akaniambia:
“Kaa kwangu. Nikakaa kwake na alikuwa mtu mwema sana, lakini haukupita muda naye pia akafariki dunia. Na alipokuwa akifariki nikamuuliza:
“Ewe fulani! Amri ya Allaah ishakujia, na mimi kama unavyonijuwa. Unaninasihi niende kwa nani?”
Akaniambia:
“Ewe mwanangu! Wa-Allaahi simjuwi yeyote mwenye kufuata ninayofuata isipokuwa mtu mmoja tu anayeishi mji wa Nasibeen, na jina lake ni fulani bin fulani, kwa hivyo mwendee huyo.”
Alipofariki dunia, nikamzika, kisha nikaifunga safari ya kumwendea mtu huyo anayeishi katika mji wa Nasibeen, nikajijulisha juu yangu na juu ya yale aliyoniusia swahibu yangu, akaniambia:
“Ishi pamoja nami.”
Nikaishi pamoja naye, na alikuwa mtu mwema sana kama walivyokuwa swahibu zake waliotangulia, lakini Wa-Allaahi haukupita muda mrefu naye pia akafariki dunia. Na alipokuwa akikata roho nikamuuliza:
“Habari zangu ndiyo kama unavyozijuwa, unaniusia niende kwa nani?”
Akanambia:
“Ewe mwanangu! Mimi simuelewi mwengine anayefuata mwenendo wetu isipokuwa mtu mmoja anayeishi mji wa ‘Umuuriyyah, na jina lake ni fulani, mwendee huyo.”
Safari Ya Kwenda ‘Umuuriyyah
Nikamwendea mtu wa ‘Umuuriyyah na kumueleza habari zangu, akaniambia:
“Ishi pamoja nami.”
Nikaishi kwa mtu huyo na alikuwa – Wa-Allaahi – katika uongofu kama walivyokuwa swahibu zake, nilipokuwa kwake nilipata ng’ombe na mbuzi wengi sana.
Kisha naye pia kama swahibu zake ikamfikia amri ya Allaah, na alipokuwa akikata roho nikamwambia:
“Hakika wewe unaelewa vizuri nini ninachokitaka, kwa hivyo unaniusia niende kwa nani au nifanye nini?”
Akaniambia:
“Ewe mwanangu! Wa-Allaahi sidhani kamayupo mtu yeyote ulimwenguni aliyekamatana na yale tuliyokamatana nayo sisi, lakini ushakaribia wakati wa kuja kwa Rasuli katika bara ya Arabu mwenye kufuata dini ya Nabiy Ibrahiym, na Rasuli huyo atauhama mji wake na atakwenda kuishi katika mji wenye mitende mingi uliopo penye majabali mingi meusi. Na Mtu huyo ana alama zisizofichika, maana yeye anakula alichopewa zawadi lakini hali anachopewa swadaqah, na baina ya mabega yake ana alama za Rasuli.
Kwa hivyo ukiweza kuufikia mji huo basi fanya hivyo.”
Kisha akafariki dunia.
Safari ya kwenda Madiynah
Nikabaki katika mji wa ‘Umuuriyyah muda kidogo, mpaka siku ile ulipopita msafara wa waarabu wa kabila la Kalbin, nikawaambia:
“Ikiwa mtanichukuwa na kunipeleka Bara ya Arabu nitakupeni mbuzi wangu wote hawa.”
Wakaniambia:
“Sawa tutakuchukuwa.”
Nikawapa mbuzi wangu na kufuatana nao mpaka tulipofika katika bonde la Al-Quraa, lililopo baina ya mji wa Madiynah na nchi ya Shaam wakaniendea kinyume na kuniuza kwa Myahudi, na nikawa namtumikia.
Haukupita muda akaja kumtembelea bin ‘amiy yake anayetokana na kabila la Bani-Quraydhah, akaninunua kutoka kwake na akanichukua mpaka nchi ya Yathrib (Madiynah), na huko nikaiona mitende alonihadithia swahibu yangu wa ‘Umuuriyyah na nikautambua mji huo kutokana na sifa alizonielezea swahibu yangu yule, na nikaishi hapo kwa yule Myahudi aliyeninunua.
Na wakati huo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) alikuwa akiwalingania watu katika mji wa Makkah, na mimi sikuwa nikisikia lolote juu yake kutokana shughuli nyingi za kitumwa nilizokuwa nikipewa.
Haukupita muda mrefu, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) akahamia mji wa Yathrib, na siku moja nilipokuwa juu ya mtende wa bwana wangu niliyekuwa nikimtumikia, na bwana wangu huyo alikuwa amekaa chini ya mtende huo, akatokea bin ‘amiy yake na kumwambia:
“Allaah Awaangamize watu wa kabila la Aus na Khazraj! Wa-Allaahi hivi sasa wote wamejikusanya katika mji wa Qubaa kwa ajili ya kumpokea mtu anayekuja leo kutoka Makkah anayejidai kuwa eti yeye ni Rasuli.”
Nilipomsikia akitamka maneno hayo nilikuwa kama mtu aliyepata homa kali sana, nikatetemeka mtetemeko mkubwa sana mpaka nikaogopa nisije nikaanguka kutoka juu ya mtende na kumuangukia bwana wangu. Nikateremka taratibu na kumuuliza mtu yule:
“Unasemaje? Hebu rudia tena maneno yako.”
Bwana wangu akaghadhibika sana akanipiga ngumi nzito, kisha akaniambia:
“Imekuhusu nini wewe! Yallah! rudi kwenye kazi yako.”
Alama ya U-Rasuli
Ulipoingia usiku, nikachukuwa tende kidogo katika tende zangu nilizokuwa nikijiwekea, nikaelekea moja kwa moja mahali alipofikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam), nikaingia kwake na kumwambia:
“Nimeambiwa kuwa wewe ni mtu mwema, na kwamba una swahibu zako wageni wenye shida, kwa hivyo pokea tende hizi niliziweka tokea zamani kwa ajili ya kutoa swadaqah na nikaona kuwa nyinyi mnazistahikia zaidi kuliko wenzenu.”
Nikaziweka na kumsogezea karibu yake, na yeye akawasogezea swahibu zake na kuwaambia:
“Kuleni.”
Lakini yeye hakula. Nikajisemea nafsini mwangu “Moja hiyo.”
Kisha nikaondoka na kuanza kukusanya tena tende kidogo kidogo, na siku ile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) alipoondoka Qubaa na kuhamia Madiynah mjini nikamuendea na kumwambia:
“Nilikuona kuwa wewe huli kitu cha swadaqah, kwa hivyo hii ni zawadi kutoka kwangu nataka kukukirimu.”
Akaipokea, akala kisha akawakaribisha swahibu zake, wakala pamoja naye.
Nikajisemea nafsini mwangu; “Mbili hiyo.”
Kisha nilimuendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) siku nilipomuona katika makaburi ya Al-Baqiy akiwa amekaa akihudhuria mazishi ya mmoja wa swahibu zake.
Alikuwa amejifunika maguo mawili, nikamsalimia kisha nikamzunguka na kusimama nyuma yake huku nikiutizama mgongo wake ili niweze kuuona mhuri wa U-Rasuli. Alipolijuwa kusudi langu akaliangusha guo alojifunikia nalo mgongoni, nikauona mhuri, nikaujuwa, na hapo hapo nikamkumbatia na kuanza kumbusu huku nikilia, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) akaniambia:
“Nini kisa chako?”
Nikamuhadithia kisa changu chote, na yeye akafurahishwa nacho na akanitaka niwahadithie mwenyewe swahibu zake, nikawahadithia, na wao pia wakafurahishwa nacho.
Salmaan Anajigomboa
Hakuwahi kupigana vita vya Badar wala vya Uhud kwa sababu alikuwa akimilikiwa na Myahudi, ndipo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) alipowataka Maswahaba (Radhwiya Allahu anhum) wamsaidie kumgomboa mwenzao, kisha akamwambia Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amjulishe Myahudi wake kuwa anataka kujigomboa, na Myahudi akamwambia kuwa thamani ya uhuru wake ni mitende mia tatu, ampandie mpaka itakapositawi, hapo ndipo atakubali kumuacha huru.
Maswahaba wakamsaidia Salmaan, wengine wakamletea miche ya mitende, na wengine wakamletea mali, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) akamsaidia kuipanda miche hiyo na yote ikamea vizuri.
Anasema Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
“Wa-Allaahi miche yote ilimea na haukufa hata mti mmoja.”
Na kwa njia hiyo akaweza kujigomboa na hatimaye akaweza kushiriki vita vyote vilivyopiganwa.
Vita vya Khandaq (Handaki)
Vita vya mwanzo alivyoshiriki akiwa mtu huru ni vya Khandaq, na yeye ndiye aliyetoa rai ya kuchimbwa handaki wakati Waislamu walipozungukwa na jeshi kubwa sana la washirikiana Maquraysh wakishirikiana na makabila mbali mbali ya kiarabu chini ya uongozi wa Abuu Sufyan yaliyokuja kufanya jaribio la mwisho la kuuteka mji wa Madiynah.
Vita hivyo vilipiganwa katika mwaka wa tano baada ya Hijrah, baada viongozi wa Mayahudi wa Madiynah kwenda Makkah na kuwatia choko choko watu wa huko na hatimaye wakafanikiwa kuwaunganisha Maquraysh na makabila mbali mbali ya kiarabu na kuunda jeshi kubwa kwa ajili ya kumpiga vita Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam), na Mayahudi hao wakatoa ahadi kuwa na wao watawaShaambulia Waislamu wakiwa ndani ya Madiynah.
Mpango wa siri ukapangwa baina ya Maquraysh na Mayahudi, na Waislamu wakashtukia jeshi kubwa lenye idadi ya watu wasiopungua elfu ishirini na nne likiusogelea mji wao huo kutoka kila pembe ya Madiynah, huku likiteka kijiji baada ya kijiji.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
إِذْ جَاءُوكُم مِّن فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّـهِ الظُّنُونَا ﴿١٠﴾
Walipokujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu, na macho yalipokodoka, na nyoyo zikafikia kooni na mkamdhania Allaah dhana nyingi. [Al-Ahzaab: 10]
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawakusanya Maswahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwa ajili ya mashauriano, na wote wakamhakikishia kuwa wapo tayari kupigana kufa na kupona na kuwazuia makafiri hao wasiweze kuingia ndani ya mji wao.
Lakini vipi watapigana na jeshi kubwa kamahilo wakati idadi yao haizidi watu elfu mbili?
Wakati mashauriano yalipokuwa yakiendelea akainuka Salmaan Al-Farsiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), akamkabili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:
“Sisi katika nchi ya Faaris (Iran) tunapozungukwa na jeshi kubwa kama hili na kama idadi yetu ni ndogo sana, huwa tunajenga handaki kubwa kuuzunguka mji wetu ili adui asiweze kuingia kwa urahisi na kwa nguvu zake zote.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafurahishwa sana na rai hiyo, rai ambayo waarabu hawakuwa wakiijuwa kabla ya hapo.
Salmaan (Radhwiya Allahu ‘anhu) akapanda juu ya kilele cha jabali mojawapo ya mji wa Madiynah, na baada ya kutizama huku na kule na kuona kuwa mji wote umezungukwa na majabali na mapori na kwamba ipo sehemu moja tu ambayo adui anaweza kupitia hapo, ndipo alipoteremka na kuashiria mahali hapo kuwa ndipo panapofaa kuchimbwa handaki hilo.
Handaki liliweza kuyazuwia majeshi ya makafiri muda wa mwezi mzima, wakabaki nje ya mji wa Madiynah, mpaka pale Allaah alipowapiga kwa dharuba na upepo mkali ulioyang’oa mahema yao na kuwarudisha walikotoka.
Salmaan Wetu Watu Wa Nyumba
Siku ya vita vya Khandaq, watu wa Madiynah walikuwa wakitamba huku wakisema: “Salmaan wetu!” na watu wa Makka walikuwa nao wakisema: “Bali Salmaan wetu!.” lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaita na kuwaambia:
“Salmaan ni wetu ‘Ahlil bayt![1]”
‘Aliy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimpa Salmaan jina la ‘Luqmaan mwenye hekima’, na hii inatokana na wingi wa elimu na hekima alokuwa nazo Swahaba huyu mtukufu.
Alikuwa akisema:
“Mtu huyu ni wetu watu wa nyumba ya Rasuli. Yupi kati yenu mwenye mtu kama Luqmaan mwenye hekima. Amepewa elimu ya kitabu cha mwanzo na kitabu cha mwisho.”
Akimaanisha kuwa amevisoma vitabu vyote hivyo (Tawraat na Injiyl) alipokuwa akifuata diyn ya Manaswara na elimu ya wanaoabudu moto ‘Zoroastrian’, kisha akapata elimu ya Qur-aan pamoja na mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Salmaan, Gavana Wa Mji Wa Madaa’in
Wakati wa ukhalifah wa ‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa msitari wa mbele katika kupigana Jihaad kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah , na alishiriki katika vita vya kuziteka nchi nyingi ikiwemo nchi ya Persia (Iran hivi sasa) akiwa chini ya uongozi wa Sa’d bin bin Abi Waqaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na yeye ndiye aliyekuwa mfasiri wa mazungumzo ya kusalimu amri baina ya jeshi la Waislamu na majeshi ya mji wa Madaa’in wanaozungumza lugha ya kifarsi, na majeshi hayo yalisalimu amri bila umwagaji wa damu.
‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamchaguwa Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Gavana wa mji huo, akakataa, lakini ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimshikilia mpaka akakubali kulibeba jukumu hilo.
Twendeni Tukampokee Salmaan
Maswahaba wote (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakimheshimu sana Salmaan, na siku ile alipokuja kuuzuru mji wa Madiynah wakati wa ukhalifah wa ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Llahu ‘anhu), ‘Umar alifanya jambo ambalo hakuwahi kumfanyia mtu yeyote kabla ya hapo.
Aliwakusanya Maswahaba wote (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na kuwataka kwenda kumpokea Salmaan nje ya mji wa Madiynah, akawaambia:
“Yallah! Twendeni tukampokee Salmaan.”
Mshahara Wake
Alikuwa akipokea mshahara wa Dirham 500, na alikuwa akizigawa zote baina ya masikini na mafakiri wa mji huo, na kujibakishia mwenyewe Dirham chache alizokuwa akizitumia kwa kununua ng’ongo na ukili vilivyotengenezwa kwa majani ya mitende kisha akisuka mikoba na kuiuza kwa bei ya Dirham tatu kila mmoja.
Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mtu aliyeikinai dunia, kwani imepokelewa kuwa hata pesa hizo alizokuwa akizichuma kwa mikono yake mwenyewe, alikuwa akizigawa mafungu matatu. Katika kila Dirham tatu anazopata anapouza mkoba, alikuwa moja akiwapa masikini, ya pili akiitumia mwenyewe, na ya tatu alikuwa akiinunulia ngo’ngo na ukili kwa ajili ya kusuka mikoba mingine.
Nibebee Mzigo Wangu Huu
Hakuwa akivaa nguo za kifahari na wala hakuwa akijiweka kama wafalme wanavyojiweka, bali alikuwa akiishi kama mtu wa kawaida, na siku ile msafiri aliyekuja kutoka nchi ya Shaam aliyekuwa na mzigo mzito wa tini na tende alipomuona Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akitembea akiwa katika hali ile, akadhani kuwa ni raia wa kawaida, akamwita na kumwambia:
“Nibebee mzigo wangu huu!”
Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaubeba na kufuatana naye kwa utiifu bila kumjibu neno lolote.
Walipokuwa njiani wakakutana na kundi la watu, na Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipowasalimia, wakamjibu:
“Wa ‘alaykumus salaam Ee Amiri wetu (Gavana wetu).”
Yule msafiri aliyetoka Shaam alishangazwa na majibu ya watu hao, akawauliza:
“Amiri gani mnayemkusudia?”
Akashangazwa zaidi alipowaona watu hao wakimwendea Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakitaka kumsaidia kumbebea mzigo wake huku wakimwambia:
“Wacha tuubebe sisi Ee Amiri.”
Alipotambua kuwa aliyembebesha mizigo yake ni gavana wa nchi hiyo, hofu ikamuingia, na mzigo aloubeba ukamuanguka, akamkimbilia Salmaan huku akimuomba msamaha.
Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:
“Sikusamehe mpaka unikubalie nikufikishie mzigo wako pale ulipotaka nikufikishie.”
Sio Vizuri
Mmoja katika swahibu zake aliiingia nyumbani kwake siku moja, akamuona Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akikanda unga, akashangazwa na kumuuliza:
“Yuwapi mtumishi?”
Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:
“Nimemtuma, nikaona si vizuri nimuache azifanye kazi zote mbili yeye peke yake, kwa hivyo nikaamua kuifanya mimi kazi hii.”
Mwana Wa Uislamu
Siku moja Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliingia msikitini akawasikia watu wakijisifia, kila mmoja akijinasibisha na kabila lake. Mmoja akasema:
“Mimi natokana na kabila la Banu Tamiym.”
Mwengine akasema:
“Mimi natokana na kabila la Kiquraysh.”
Mwengine akasema:
“Na mimi natokana na kabila la ‘Aws.”
Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alinyamaza kimya huku akiwasikiliza. Na walipotaka kujuwa na yeye anatokana na kabila gani, akaona hii ndiyo fursa ya kuwafunza maana ya Uislaam, akawaambia:
“Mimi ni mwana wa Islaam. Nilikuwa nimepotoka Allaah Akaniongoza kupitia kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi waaalihi wa sallam). Nilikuwa masikini Allaah Akanipa utajiri kupitia kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nilikuwa mtumwa Allaah Akanipa uhuru kupitia kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hivyo Usilamu ndiyo kabila langu.”
Usia Wa Salmaan
Siku moja Sa’d bin Abiy Waqqaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokwenda kumtembelea Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiumwa, akamkuta analia, akamuuliza:
“Nini kinachokuliza ewe Abuu ‘Abdillaah na ilihali Rasuli wa Allaah alipofariki dunia alikuwa radhi nawe?”
Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akajibu:
“Wa-Allaahi silii kwa kuyahofia mauti wala kwa kuipenda dunia. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituambia:
‘Akiba mnayojiwekea isizidi kuliko mzigo wa msafiri, lakini njoo tizama hii mito iliyonijalia nyumbani kwangu.”
Anasema Sa’d (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
“Nikatizama nyumbani mwake na sikuona isipokuwa mito michache mibovu na ufagio.”
Nikamwambia:
“Tuusie Ee Salmaan.”
Akaniambia:
“Mkumbuke Allaah unapotaka kufanya jambo lolote, na umkumbuke unapohukumu baina ya watu, na unapogawa kwa mikono yako.”
Kufariki Kwake
Katika asubuhi mojawapo ya siku alizokuwa akiumwa maradhi yake ya mwisho, Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimwita mkewe na kumwambia:
“Niletee kile kichupa nilichokupa siku ile unifichie.”
Mkewe akaja nacho na kilikuwa kichupa cha hal miski. Akamwambia:
“Kifungue, changanya na maji kisha unimiminie nacho, kisha funga mlango utoke nje kidogo, kwani hivi sasa wananijia viumbe vya Allaah wasiokula wala kunywa na wanapenda manukato mazuri.”
Mkewe akafanya kama alivyoambiwa, kisha akasubiri kidogo, akatoka nje na kuufunga mlango, na haukupita muda mrefu mumewe akafariki dunia.”
Haya yalikuwa wakati wa utawala wa ‘Uthmaan bin ‘Affan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika mwaka wa thelathini na tatu baada ya Hijrah.
Allaah Akurehemu Ee Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) uliyeutafuta ukweli, mpaka ukaupata, kisha ukaufuata. Biidhini Allaah kisa chako kitafungua nyoyo zilizofungika, na masikio yaliyozibikia, na macho yaliyofumbika.
[1] [1]Hii ni Hadiyth dhaifu, lakini zipo riwaayah nyingi sahihi zilizosahihishwa na Shaykh ; Al-Albaaniy kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alitayamka hayo pia.