019-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-'AZIYZ
أسماء الله الحسنى وصفاته
Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake
الْعَزِيز
AL-‘AZIYZ
Al-‘Aziyz: Azizi, Mwenye Taadhima, Mwenye enzi, Mwenye nguvu, Asiyeshindika.
Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Ndiye Al-Aziyz; Azizi, Mwenye Taadhima, Mwenye enzi, Mwenye nguvu, Asiyeshindika. Ana maana zote za utukufu na wasifu na ufalme. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا ۚ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٦٥﴾
Na wala isikuhuzunishe kauli yao. Hakika taadhima zote ni za Allaah Pekee. Yeye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Yuwnus 10: 65]
وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٣٧﴾
Na Adhama, Utukufu, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini; Naye Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Jaathiyah 45: 37]
Al-Qurtwubiy amesema: “Al-‘Aziyz maana yake ni: Aliye Madhubuti Asiyedhurika, Ambaye Hadirikiwi wala Hashindwi.” [Tafsiyr Al-Qurtwubiy (2/131)]
Na Ibn Jariyr amesema: “Al-‘Aziyz yaani ni mkali katika kulipiza kwa adui Zake na ndio Anasema:
وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَن يُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٨﴾
Na hawakuwachukia isipokuwa kwa vile wamemwamini Allaah Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote. [Al-Buruwj 85: 8]
Ibnul-Qayyim katika An-Nuwniyyah amesema:
“Yeye ni Al-‘Aziyz Ambaye Ubwana Wake haufikiwi (haushindwi). Atafikiwaje Mwenye kumiliki nguvu zote?
Naye ni Al-‘Aziyz Ambaye ni Mwenye kudhibiti Asiyepingika, hakuna kitu kitakachomshinda, kwa hiyo hizi ni Sifa mbili.
Naye ni Al-‘Aziyz kwa kuwa na Nguvu nayo ni Sifa Yake. Kwa hiyo Al-‘Izz ina maana tatu.
Nazo ni ambazo zimekamilika Kwake, Ametakasika kutokana na mapungufu yote, kutoka katika kila upande, Ambaye Hana mapungufu, kasoro zozote zile.”
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Al-‘Aziyz Ambaye Ndiye Mwenye Nguvu na Uwezo wote. Naye ni Mkali na Mkali kwa nguvu Zake, Ambaye zimedhalilika kwa nguvu Zake vyote vilivyokuwa ni vigumu, na yakalainika kwa nguvu Zake yaliyo magumu.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Al-‘Aziyz Ambaye Hana mfanowe, wala Hana wa kumlinganisha kwa uadilifu na kwa ukamilifu Wake katika pande zote.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Al-‘Aziyz, Mwenye nguvu katika kulipiza Kwake kisasi, Anapolipiza kisasi kwa adui Zake, hakuna yeyote mwenye uwezo wa kumzuia Asifanye hilo muda Anaotaka kulifanya hilo.
Al-‘Aziyz; Mwenye nguvu Ambaye humpa Nguvu, mamlaka Amtakaye, Humtukuza Amtakaye, Humdhalilisha Amtakaye katika waja wake, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٦﴾
Sema: “Ee Allaah Mfalme Uliyemiliki ufalme wote, Unampa ufalme Umtakaye, na Unamuondoshea ufalme Umtakaye, na Unamtukuza Umtakaye, na Unamdhalilisha Umtakaye, khayr imo Mkononi Mwako. Hakika Wewe juu ya kila kitu ni Muweza. [Aal-‘Imraan 3: 26]
Al-‘Aziyz Ambaye Mwenye nguvu, na Ambaye Rusuli Wake hawadhalilishwi na watu, na Waumini wanapata nguvu na ‘izzah, bali makafiri ndio wenye kudhalilika. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَقُولُونَ لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ ۚ وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٨﴾
Wanasema: “Tutakaporudi Madiynah, mwenye hadhi zaidi atamfukuza humo aliye dhalili.” Na hali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui. [Al-Munaafiquwn 63: 8]
Al-‘Aziyz Mwenye shani ya juu na uwezo,p Mwenye utukufu wa dhati Yake, Mwenye Upekee katika ukamilifu Wake, katika sifa Zake zote. Na miongoni mwa ukamilifu wa nguvu Zake na ukamilifu Wake, ni kutakasika Kwake na upungufu wowote ule wa shari, aibu, na kushirikishwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿١٨٠﴾
Subhaana Rabbika! Utakasifu ni wa Rabb wako, Rabb Mtukufu kutokana na yale wanayoyavumisha. [Asw-Swaaffaat 37: 180]
Jina hili limetajwa zaidi ya mara tisini katika Qur-aan. Limeungana na Al-Hakiym zaidi ya mara ishirini. Na Limeungana zaidi ya mara kumi na Ar-Rahiym; katika Suwrah Ash-Shu’araa Limeungana na Ar-Rahiym mara tisa. Hivyo inadhihirisha kuwa kuna hikmah ndani yake kutajwa na kukaririwa kwake kwa wingi.
Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-‘Aziyz:
1. Anayetaka ‘izzah, basi ‘izzah iko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) muombe Yeye Pekee. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ ﴿١٠﴾
Yeyote Anayetaka utukufu, basi utukufu wote uko kwa Allaah. Kwake Pekee linapanda neno zuri na 'amali njema Huitukuza. Na wale wanaopanga njama za maovu watapata adhabu shadidi. Na njama za hao ni zenye kuangamia. [Faatwir 35: 10]
2. Ukitaka kutafuta nguvu, ushindi dhidi ya maadui na wanaojifanya majabari, basi tafuta nguvu kwa Al-‘Aziyz kwani Yeye Kwake hakuna linalomshinda, Analolitaka linakuwa na Asilolitaka haliwi.
Mnyenyekee kumuomba Yeye Al-‘Aziyz unaposhindwa jambo, na unapokuwa umekandamizwa na dhulma za wenye nguvu ili Allaah Mwenye nguvu zote, Asiyeshindika Akusaidie kuwashinda maadui zako. Kumbuka visa vya Manabii; mfano kisa cha Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam) jinsi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyomshinda Fir’awn aliyejiita yeye ni Ilaah (Muabudiwa), lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimshinda kwa kuteremsha miujiza Yake Akamvurumisha baharini na kufilia mbali.
3. Upe Uislamu wako ‘izzah (hadhi, utukufu) kwani utukufu si kuwa na mali wala nguvu wala mamlaka. Wala usitafute ‘izzah kwa maadui wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ukawa miongoni mwa wale ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
الَّذِينَ يَتَّخِذُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۚ أَيَبْتَغُونَ عِندَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا ﴿١٣٩﴾
Wale wanaofanya makafiri kuwa ni marafiki wandani badala ya Waumini. Je, wanatafuta utukufu kutoka kwao? Basi hakika utukufu wote ni wa Allaah Pekee. [An-Nisaa 4: 139]
Na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"نحن قوم أعزنا الله بالإسلام فمهما ابتغينا العزة بغيره أذلنا الله"
“Sisi ni watu ambao Allaah Ametupa ‘izzah kwa Uislamu, basi tutakapotafuta ‘izzah vyovyote vile kwa wengineo, Allaah Atatudhalilisha” [Mustadrak Al-Haakim (1/236/237) na Al-Haakim amesema: Swahiyh kwa sharti ya Ash-Shaykhayn]
Na ndio maana Uislamu utabakia kushinda Dini zote kama Anavyoahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾
Yeye Ndiye Aliyemtuma Rasuli Wake (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Mwongozo na Dini ya haki ili Aishindishe juu ya dini zote, japo watakirihika washirikina. [At-Twabah 9: 33]
4. Wape ‘izzah nduguzo Waumini wala usiwachafue heshima zao. Ameonya hivyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((بِحَسْبِ امْرِئٍ مِنْ الشَّرِّ أَنْ يَحْقِرَ أَخَاهُ الْمُسْلِمَ. كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حَرَامٌ دَمُهُ وَمَالُهُ وَعِرْضُهُ)) رواه مسلم
((Yatosha kuwa shari mtu kumdharau nduguye Muislamu. Kila Muislamu juu ya Muislamu mwenziwe ni haramu damu yake, mali yake, na heshima yake)) [Muslim]
Na pia:
وَعَنْ أَبِي اَلدَّرْدَاءِ رضى الله عنه عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَنْ رَدَّ عَنْ عِرْضِ أَخِيهِ بِالْغَيْبِ ، رَدَّ اَللَّهُ عَنْ وَجْهِهِ اَلنَّارَ يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ)) أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَحَسَّنَهُ
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayetetea kuihami heshima ya nduguye kwa siri, Allaah Atauhifadhi uso wake kutokana na moto Siku ya Qiyaamah)). [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan. Ameikusanya Al-Abaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (1931), na Swahiyh Al-Jaami’ (6262)]
5. Wenye mamlaka watafakari na kukumbuka kwamba mamlaka na hadhi hazishindi za Al-‘Aziyz, kwa hiyo wasiende kabisa kinyume na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wala wasivuke mipaka katika kudhulumu watu kutokana na mamlaka yao.
6. Rejea Qur-aan, uisome ukitaka kufaulu duniani na Aakhirah. Tafakari na zingatia maana zake, na kama ilivyotangulia kutajwa kwamba humo kumetajwa mara nyingi Jina la Al-‘Aziyz. Na Qur-aan yenyewe imeitwa Al-‘Aziyz Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ ﴿٤١﴾
Hakika wale waliokanusha Ukumbusho ulipowajia (wataangamia). Na hakika hicho ni Kitabu chenye utukufu na udhibiti.
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ ﴿٤٢﴾
Hakitokifikia ubatili mbele yake, na wala nyuma yake; ni uteremsho kutoka kwa Mwenye hikmah wa yote, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote. [Fusw-swilat 41: 41-42]
7. Miongoni mwa sababu za kupata ‘izzah na kupandishwa daraja ni kusamehe watu na kuwa na unyenyekevu mbele yao.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ، وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إلاَّ عِزًّا ، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kutoa swadaqah hakupunguzi mali, Allaah Humzidishia mja ‘izzah (utukufu) kwa ajili ya kusamehe kwake. Na yeyote anayenyenyekea kwa ajili ya Allaah, Allaah Aliyetukuka Atampandisha Daraja [Atamtukuza])) [Muslim]
8.Muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Jina hili la Al-‘Aziyz. Nyenyekea Kwake na utawakali Kwake kwa kila jambo, na kila shida.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba:
للَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ وَبِكَ آمَنْتُ وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ وَبِكَ خَاصَمْتُ. اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِعِزَّتِكَ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ أَنْ تُضِلَّنِي أَنْتَ الْحَيُّ الَّذِي لاَ يَمُوتُ وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ يَمُوتُونَ
Allaahumma Laka aslamtu, wa Bika aamantu, wa ‘Alayka tawakkaltu, wa Ilayka anabtu, wa Bika khaaswamtu. Allaahumma inniy a’uwdhu bi -’izzatika laa ilaaha illa Anta an-tudhwillaniy Antal-Hayyu Alladhiy laa yamuwtu wal-jinnu wal-insu yamuwtuwna.
Ee Allaah, Kwako najisalimisha na Kwako naamini na Kwako natawakali na Kwako narejea kutubu na Kwako nagombana [dhidi ya adui]. Ee Allaah, hakika mimi najikinga kwa ‘Izzah (Nguvu) Yako, hapana Muabudiwa wa haki ila Wewe Usije kunipotoa Wewe Uliye Hai daima Ambaye Hafi ilhali majini na watu wanakufa[ [Muslim]
9. Muombe pia Allaah kwa Jina hili la ‘Aziyz pale unapopata maumivu mwilini kama ilivyothibiti katika Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba ufanye ifuatavyo:
Weka mkono wako juu ya sehemu iliyo na maumivu kisha sema mara tatu:
بِسْمِ اللهِ
BismiLLaah
Kisha useme mara saba:
أَعُوذُ بِعِزَّةِ اللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَ أُحاذِرُ
A’uwdhu bi ‘Izzati-LLaahi wa-Qudratihi min sharri maa ajidu wa uhaadhiru
Najikinga kwa ‘Izzah ya Allaah na kwa uwezo Wake kutokana na shari ya ninachokisikia na ninachokiogopa)). [Muslim, Ibn Maajah na wengineo kwa usimulizi tofauti kidogo]