21-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Zinazokubalika: Kutawassal Kwa Maajabu ya Allaah Na Neema Zake
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
Tawassul Zinazokubalika
21-Kutawassal Kwa Maajabu ya Allaah Na Neema Zake
a) Kutawassal Kwa Neema Na Majabu Ya Allaah ('Azza wa Jalla):
Inafaa kutawassal uonapo maajabu au neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana na mifano ifuatayo katika Qur-aan:
Nabiy Zakariyyaa ('Alayhis Salaam) ambaye alikuwa ni mlezi wa Maryam, pale alipoingia katika mihraab ya Maryam akakuta maajabu ya rizqi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا ۖ كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِندَهَا رِزْقًا ۖقَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّىٰ لَكِ هَـٰذَا ۖ قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٧﴾
Basi Rabb wake Akampokea kwa kabuli njema na Akamkuza mkuzo mzuri na Akamfanya Zakariyyaa kuwa mlezi wake. Kila Zakariyyaa alipoingia kwake katika chumba cha kuswalia alikuta kwake kuna riziki Akasema: “Ee Maryam! Umepata wapi hivi? ”Akasema: “Hivi ni kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah Anamruzuku Amtakaye bila ya hesabu.” [Aal-‘Imraan: 37]
Maajabu zaidi ni kwamba yalikuwa ni matunda ya msimu wa baridi wakati wa msimu wa joto, na matunda ya msimu wa joto katika msimu wa baridi . [Tafsiyr Atw-Twabariy, Ibn Kathiyr]
Basi hapo hapo Nabiy Zakariyyaa ('Alayhis Salaam) aliomba naye du’aa ya kutaka mtoto japokuwa alikwishakata tamaa kutokana na uzee na vilevile mkewe akiwa ni tasa.
هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾
Hapo hapo Zakariyyaa akamwomba Rabb wake, akasema: “Rabb wangu Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema hakika Wewe ni Mwenye kusikia du’aa yangu.” [Aal-‘Imraan: 38]
Kisha hapo hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akambashiria kumruzuku mwana aliyemtani, tena mwana mwema mwenye sifa njema:
فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٣٩﴾
Basi mara Malaika akamwita (Zakariyyaa) naye akiwa amesimama anaswali katika chumba kwamba: “Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa mwenye kusadikisha Neno (la Kun!) kutoka kwa Allaah na ni mwenye sharaf, busara na taqwa, na anayejitenga mbali na matamanio na Nabiy miongoni mwa Swalihina.” [Aal-‘Imraan: 39]
Imaam As-Sa’dy amesema: “Na katika Aayah hii:
هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ
Hapo hapo Zakariyyaa akamwomba Rabb wake … [Aal-‘Imraan: 37]
ni dalili kuthibitika karama za awliyaa za kimiujiza, kinyume na wanaopinga hayo.
Basi Zakariyyaa ('Alayhis Salaam) alipoona yale ambayo Allaah Amemneemesha kwayo Maryam, na ambayo Amemkirimisha kwayo katika rizki Yake njema ya siha, ambayo Alimpa bila ya juhudi zake wala kuzihangaikia, nafsi yake ikapata tamaa ya kupata mtoto, ndio maana hapo Allaah (Ta’aalaa) Anasema… (Aayah za 38-41]" (mwisho wa kunukuu).
b) Kutawassal Kwa Neema Za Allaah ('Azza wa Jalla):
Malaika wanamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awaghufurie Waumini dhambi zao na Awaepushe na maovu, wanaanza kwa kutawassal kwa kutaja neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kueneza rahmah Yake kama Anavyosema:
الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ﴿٧﴾
(Malaika) Ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih kwa Himidi za Rabb wao, na wanamwamini; na wanawaombea maghfirah wale walioamini: “Rabb wetu! Umekienea kila kitu kwa rahmah na ujuzi, basi waghufurie wale waliotubu, na wakafuata njia Yako, na wakinge na adhabu ya moto uwakao vikali mno.”
رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدتَّهُمْ وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٨﴾
“Rabb wetu! Waingize Jannaat za kudumu milele ambazo Umewaahidi, pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao, na wake zao, na dhuria wao. Hakika Wewe Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.
وَقِهِمُ السَّيِّئَاتِ ۚ وَمَن تَقِ السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٩﴾
“Na wakinge maovu, kwani Unayemkinga na maovu Siku hiyo, basi kwa yakini Umemrehemu. Na huko ndiko kufuzu adhimu. [Ghaafir: 7-9]
Mifano mingi mengineyo imo katika Qur-aan. Na hii ni fursa mojawapo kubwa kutawassal kwa neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa sababu neema Zake (Tabaaraka wa Ta’aalaa) ni nyingi mno hakuna awezaye kuzihesabu. Kwa hiyo Muislamu afuate kielekezo hiki cha kutafakari maajabu ya Allaah ('Azza wa Jalla), na Rahma Zake, na kukumbuka neema za Rabb wake na amshukuru kisha aombe anachotaka katika mas-alah ya dunia na Aakhirah.