23-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Haijuzu Kutawassal Kwa Jaha Ya Nabiy
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
Tawassul Za Shirki, Kufru Na Bid-'ah
23-Haijuzu Kutawassal Kwa Jaha Ya
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
Haijuzu kutawassal kwa jaha ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kufariki kwake. Dalili ni Hadiyth ifuatayo ambayo Maswahaba hawakutawassal kwa jaha ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kufariki kwake:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) أَنَّ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) كَانَ إِذَا قَحَطُوا اسْتَسْقَى بِالْعَبَّاسِ بْنِ عَبْدِ الْمُطَّلِبِ فَقَالَ: "اللَّهُمَّ إِنَّا كُنَّا نَتَوَسَّلُ إِلَيْكَ بِنَبِيِّنَا فَتَسْقِينَا وَإِنَّا نَتَوَسَّلُ إِلَيْكَ بِعَمِّ نَبِيِّنَا فَاسْقِنَا" قَالَ" فَيُسْقَوْنَ.
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliomba mvua kulipokuwa na ukame kwa kutawassal kwa ‘Abbaas bin ‘Abdil-Muttwalib akisema: “Ee Allaah, tulikuwa tunatawassal Kwako kupitia Nabiy wako, Ukatunyeshea mvua, na sasa tunatawassal Kwako kupitia ‘ami wa Nabiy Wako, basi tunyweshee mvua”. Akasema: Wakanyweshewa mvua. [Al-Bukhaariy Kitaab Al-Istisqaa, na Kitaabu Fadhwaail Aswhaab An-Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam]
Baadhi ya Waislamu hukosea kwa kutawassal kwa jaha ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kufariki kwake.
Mfano kusema: “Ee Allaah, hakika mimi nakuomba kwa jaha ya Nabiy Wako Unikidhie haja zangu kadhaa” au “Uniokoe na janga au balaa fulani” au “Unighufurie dhambi zangu n.k.”
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
“… Basi tunasema tawassul kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) imegawanyika sehemu tatu:
Kwanza: Atawassal mtu kwa iymaan yake kwake, na kwa kumfuata (Sunnah zake), na hii inakubalika katika uhai wake na baada ya kufariki kwake.
Pili: Atawassal kwa du’aa yake, yaani amwombe Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili amwombee mtu. Na hii inakubalika katika uhai wake wala si baada ya kufariki kwake, kwani baada ya kufariki kwake yeye ni mwenye udhuru (hayuko tena).
Tatu: Kutawassal kwa jaha yake na utukufu wake mbele ya Allaah. Hii haijuzu katika uhai wake wala si baada ya kufariki kwake, kwa sababu yeye siye wasiylah, hivyo hawezi kufikisha mtu katika lengo kwani si kazi yake.
Kwa hiyo akiuliza mtu: “Nimefika katika kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuomba anighufurie au anipe shifaa (aniombeleze) mbele ya Allaah; je, inajuzu au haijuzu? Tunasema: Haijuzu.”
[Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn - Hukmu At-Tawassul Wa Ahkaamuhu (2/25 -380)]