26-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa Uradi "Swalaatun-Naariyah"
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah
26-Kutawassal Kwa Uradi Unaoitwa "Swalaatun-Naariyah"
Swalaatun-Naariyah – صلاة النارية
Uradi wa Swalaatun-Naariyah ni uradi wa shirki kwa sababu anaombwa humo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa fadhila zake badala ya kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Hata kama Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angekuwa hai basi uradi huu ungebakia kuwa ni shirki kwa sababu ya kumuomba jambo ambalo hakuna mwenye uwezo nalo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee Naye Amemuamrisha Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴿١٨٨﴾
188. Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa Apendavyo Allaah. Na lau ningekuwa najua ya ghayb, bila shaka ningelijikithirishia ya kheri, na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini.” [Al-A’raaf: 188]
Na pia Anasema Allaah ('Azza wa Jalla) kumwambia Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا﴿٢١﴾
Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.” [Al-Jinn: 21]
Asili ya uradi huo ni kutoka Bara Hindi ukafika Afrika Mashariki. Husomwa pale mtu anapofikwa na matatizo, janga, dhiki au mtu anapotaka haja yake ikidhiwe. Husomwa mara elfu nne, mia nne na arubaini na nne (4444) kama ifuatavyo:
أللهم صلي صلاةً كاملة وسلم سلاما تاما على سيدنا محمد الذي تنحل به العقد، وتتفرج به الكرب، وتقضى به الحوائج ، وتنال به الرغائب، وحسن الخواتيم ويستسقى الغمام بوجهه الكريم وعلى آله وصحبه في كل لمحة ونفس بعدد معلوم لك
‘Allaahumma Swalli Swalaatan kaamilatan wa-sallim salaaman taamaa, ‘alaa Sayyidinaa Muhammad alladhiy tan-hallu bihil-‘uqadi, wa-tanfariju bihil-kurab, wa-tuqdhwaa bihil-hawaaij, wa-tunaalu bihir-raghaaib, wa-husnul-khawaatim, wa yustasqal-ghamaamu bi-wajhil-kariym, wa ‘alaa aalihi wa-swahbihi fiy kulli lamhatin wa nafsin, bi’adadi kulli ma’aluumin Lak’
(Ee Allaah, Mswalie Swalaah iliyotimu bwana wetu Muhammad ambayo kwa fadhila zake, vizuizi vyote vinaondoka, mazonge (misukosuko) yanapoa, shida zote zinafarijika, na mahitaji yanakidhika, na inafikisha kwa yanayotamaniwa, na mwisho mwema wapatikana, na kwa fadhila zake yule mwenye uso mtukufu mawingu (mvua) huombwa kunyesha, na Swalah na Salaam ziwe juu ahli zake na Maswahaba wake kwa kila muda na kila pumzi kwa idadi ya kadiri ya Ujuzi Wako)
Sababu nyinginezo za kutokujuzu Uradi huo wa Swalaatun-Naariyah:
1. Nyiradi au du’aa za kuondosha matatizo, shida, dhiki zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah zimejaa tele, kwa hiyo kutafuta nyiradi za uzushi ni kujiingiza katika dhambi na upotofu.
2. Uradi huo husomwa idadi maalum, (mara 4444); ni uzushi kutaja idadi kadhaa katika aina yoyote ya ‘ibaadah bila ya dalili.
3. Husomwa kwa kukusanyana watu, nalo hili ni jambo la uzushi katika Dini. Na baya zaidi baadhi ya watu huusoma pale wanapokusanyika katika makhema Minaa katika katika kutekeleza 'ibaadah ya Hajj; wanaharibu Hajj zao kwa uzushi kama huu!
4. Uradi huo umekusanya maneno ambayo yanavuka mpaka katika kumtukuza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumpachika Sifa ambazo zinamstahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee. Mfano wa sifa zilizohusishwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) uradi huu ni:
“Kwa fadhila zake shida za watu kufarijiwa, vizuizi kuondolewa, mazonge kupoozwa, mahitaji kukidhiwa, na mwisho mwema wupatikana, na kwa fadhila zake yule mwenye uso mtukufu mawingu (mvua) huombwa kunyesha.”
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuweza kujinufaisha nafsi yake wala mtu yeyote jambo ambalo hakuwa na uwezo nalo kama alivyoambiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) aseme:
قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي ضَرًّا وَلَا نَفْعًا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ
Sema: “Siimilikii nafsi yangu dhara wala manufaa isipokuwa Aliyotaka Allaah. [Yuwnus: 49]
5. Kuusoma uradi huo ni kuufadhilisha uradi huo badala ya nyiradi au du’aa zilizothibiti katika Sunnah na hivyo kudharau mafundisho ya Sunnah na kumtuhumu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amekasiri katika kuwafundisha yale wanayohitajia Waislamu katika hali za shida na dhiki; ilhali yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((مَا تَرَكْتُ شَيْئًا يُقَرِّبُكُمْ إِلى اللهِ إِلاَّ وَأَمَرْتُكُمْ بِهِ، وَمَا تَرَكْتُ شَيْئًا يُبْعِدُكُمْ عَنِ اللهِ إِلاَّ وَقَدْ نَهَيْتُكُمْ عَنْهُ))
“Sikuacha jambo lolote linalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimeshakuamrisheni nalo. Na sikuacha jambo lolote linalokubaidisheni na Allaah ila nimeshakukatazeni nalo.” [Atw-Twabaraaniy Isnaad yake ni Swahiyh. Rejea Swiffatu-Swalatin-Nabiy (3/942) ya Imaam Al-Albaaniy].
Kwa hiyo, uradi huo unapelekea katika ushirikina na kuacha mafundisho ya Sunnah na badala yake kupelekea kwenye uzushi. Basi haifai kabisa kwa Muislam kuusoma wala kushiriki ndani yake.