Uuzaji Wa Pesa (Swarf) Ni Halal?

SWALI :

Assalaam Alaykum!

Natumai muwazima mukiendelea na kutupa mambo matamu matamu kuhusu dini yetu.

Leo hii nimetatizika na biashara ya kuuza na kununua pesa (bureau de change).

Naomba maelezo kuhusu biashara hii, Dini yetu ya Uislamu yalizungumzaje swala la kuuza pesa kwa pesa.

Wakati huo huo kuna namna nyingine ambapo katika sehemu hizo hizo za kubadilishia pesa, watu huzitumia kupokea na kutuma pesa kwenda nchi mbali mbali. Mfano wanaoishi Uingereza na Omani huwambia tu ndugu zao waishio Zanzibar waende sehemu fulani kuchukua pesa kiasi fulani.

Naomba maelezo sheikh mana hapa nimetatizika kidogo.

Maassalaam!

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Suala la Bureau de change

Uuzaji wa pesa (fedha) katika Fiqh waitwa swarf

Hii biashara ya ubadilishaji wa pesa toka kwa pesa (‘umlah) za nchi moja kwa pesa au za nchi nyengine yajuzu kwa msingi wa haja.

Allaah Ameihalalisha biashara hii kwa kuwa binadamu wanahitajia kubadilishana sarafu.

Swarf yajuzu kwa mujibu wa Hadiyth iliyopokelewa na ‘Umar bin Al-khatwaab na Abu Sa’iyd al-Khudry, na ‘Ubaadah bin Swaamit (Riwaya tofauti tofauti) [Radhiya Allaahu ‘anhum] “Msiuze dhahabu kwa dhahabu isipokuwa kiasi kile kile, wala fedha kwa fedha ila kiasi kile kile, na uzeni dhahabu kwa fedha au fedha kwa dhahabu mpendavyo” [Al-Bukhaariy na Muslim].

Pesa (‘umlah) zinashirikiana na fedha na dhahabu na mali nyengineyo kwa kuwa ni thamani na kuna aina nyengine ambayo ya mali ambayo ni  Muthman (kinacho nunuliwa).

Mali ambayo ni aina ya thamani: yabadilishwa kwa shuruti zifuatazo:

a-  Ikiwa ni aina moja ya mali mfano dhahabu kwa dhahabu lazima iwe kiwango/gramu sawa baina zote mbili;

b-  Ikiwa ni mali tofauti hakuna neno ikiwa kuna tofauti baina kiwango mfano dhahabu gramu tano kwa fedha gramu kumi.

c-  Ikiwa ni aina moja lazima sarfu iwe papo hapo. Mfano, Ikiwa utapokea dola malipo yake lazima yawe papo hapo, na haikubaliki kuchelewesha japo kwa lisaa.

Ama mas-alah ya kutuma pesa toka nchi mmoja hadi nyengine mji kwa mji haina neno kwa sababu aliyetuma ananunua/kulipia huduma za kutuma fedha zake nchi moja hadi nyengine. Na hapa hayaingii mas-ala ya riba.

Wakati mtu anakwenda kutuma pesa kwa za nchi za nje hufanya swarf kwa shillingi za Tanzania au nchi nyingine. Hii inachukuliwa kuwa amefanya swarf na qabdh (kuzimiliki) fedha kumepatikana.

Kisha sasa analipia khidmah (huduma) za kutuma pesa na hili si jambo lenye kuingia ndani yake riba. Ni mfano wa mtu aje kwako akupe paundi mia akwambie wewe waenda likizo bara Afrika nifikishie kwa mzee wangu mfano kisha akulipishe kwa huduma hii, haya ni mas-alah ya ijara na si ya uuzaji.

Na kwa msingi huu hakuna suala la kupokea zile fedha siku ile au wakati ule ule.

 

 Wa Allaahu A’alam

 

 

Share