253-Aayah Na Mafunzo: Aina Mbali Mbali Za Kufadhilishwa Manabii
Aayah Na Mafunzo
Al-Baqarah
Aina Mbali Mbali Za Kufadhilishwa Manabii
تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـٰكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ ﴿٢٥٣﴾
253. Hao ni Rusuli, Tumewafadhilisha baadhi yao juu ya baadhi. Miongoni mwao kuna aliyesemeshwa na Allaah, na Akawapandisha baadhi yao vyeo. Na Tukampa ‘Iysaa mwana wa Maryam hoja bayana na Tukamtia nguvu kwa Ruwhil-Qudus (Jibriyl (عليه السلام. Na lau Angelitaka Allaah wasingelipigana wale wa baada yao, baada ya kuwajia hoja bayana. Lakini walikhitalifiana, basi miongoni mwao ambao walioamini na miongoni mwao waliokufuru. Na lau Angelitaka Allaah wasingelipigana lakini Allaah Anafanya Ayatakayo.
Mafunzo:
Maana inayokusudiwa katika Aayah hii ni Hadiyth ambayo Swahiyh mbili ziliikusanya kutoka kwa Abuu Hurayrah ambaye amehadithia: Wakati fulani Muislamu na Yahudi walikuwa wakibishana. Yahudi akaapa: “Hapana! Naapa kwa (Allaah) Ambaye Alimteua Muwsaa (عليه السلام) kuwa mbora kwa walimwengu wote.” Muislamu aliinua mkono wake akampiga Yahudi kibao usoni, kisha akasema: “Amemzidi Muhammad pia ewe khabithi!” Yahudi akaenda kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumlalamikia. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Msinifidhalishe zaidi juu ya Manabii kwani watu watapoteza fahamu Siku ya kufufuliwa (Qiyaamah) na nitakuwa wa kwanza kuzindukana na nitamkuta Muwsaa ameshika nguzo ya ‘Arsh. Sitojua kama Muwsaa (عليه السلام) alizindukana kabla yangu ama kulimtosha kupoteza kwake fahamu kulikompata mlimani. Hivyo misnitukuze juu ya Manabii.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]