255-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Aayatul-Kursiyy Na Kuweko Jina Tukufu Kabisa La Allaah

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Fadhila Za Aayatul-Kursiyy Na Kuweko Jina Tukufu Kabisa La Allaah

 

 

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾

255. Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Aliyehai daima, Msimamia kila kitu. Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake. Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye Uluwa, Ametukuka, Adhimu; Mkuu kabisa.

 

Mafunzo:

 

Aayah hii ndiyo Aayah adhimu kabisa katika Qur-aan kwa dalili ya Hadiyth ya Muslim (810) kutoka kwa ‘Abdullaahi bin Rabaah Al-Answaariy kutoka kwa ‘Ubayy bin Ka’ab ambaye amehadithia: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Yaa Abal-Mundhir! Hivi unajua ni Aayah gani ndani ya Kitabu cha Allaah kuwa ni adhimu kabisa?” Akasema: Nikasema: Allaah na Rasuli Wake ni wajuzi zaidi. “Yaa Abal-Mundhir! Hivi unajua ni Aayah gani ndani ya Kitabu cha Allaah kuwa ni adhimu kabisa?” Akasema: Nikasema: Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Aliyehai daima, Msimamia kila kitu” (mpaka mwisho wa Aayah). Akasema Ubayy: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akanipiga kifuani kisha akasema: “Wa-Allaahi upongezwe kwa ‘ilmu yako yaa Abal-Mundhir.” [Muslim] na katika mapokezi ya Ahmad imeendelea: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, Aayah hii ina ulimi na midomo miwili ambao inamtukuza Mfalme (Allaah) katika mguu wa Arsh.”  [Swahiyh At-Targhiyb (1471)]

 

Pia, zimetajwa katika Sunnah, fadhila zake kadhaa, zifutazo ni baadhi yake:

 

“Atakayeisoma anapoamka asubuhi itamkinga na majini mpaka itakapofika jioni. Na atakayeisoma jioni atakingwa nao mpaka asubuhi.” [Al-Haakim (1/562) Taz. Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/273)]

 

”Atakayezisoma mara tatu asubuhi na jioni  zitamtosheleza kwa kila kitu.” [Abuu Daawuwd (4/322) [5082], At-Tirmidhiy (5/567) [3575], Taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/182)]

 

Pia, Aayah hii ina Jina tukufu kabisa la Allaah katika kauli Yake (تعالى): ”Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Aliyehai daima, Msimamia kila kitu” na  dalili ni:

 

Abuu Umaamah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  ”Jina Tukufu  kabisa la Allaah  Ambalo likiombewa kwalo Anaitikia limo katika Suwrah tatu; Al-Baqarah, Aal-‘Imraan, na Twaahaa’. [At-Tirmdhiy, Silsilah Asw-Swahiyhah (746)] Na mapokezi mengineyo yaliyothibitisha kuhusu Ismul-A’dhwam (Jina tukufu kabisa).

 

Kuhusu kauli ya Allaah (تعالى): ((Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi)) Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: “Iwapo mbingu saba na ardhi saba zingekunjuliwa na kulazwa sambamba, basi zingefikia kipimo cha (udogo wa) pete katika jangwa, kulinganisha na ‘Arsh.” [Ibn Abiy Haatim (3/981)]

 

 

Share