275-Aayah Na Mafunzo: Adhabu Za Anayekula Ribaa Kurushiwa Mawe Mdomoni

 

Al-Baqarah

Adhabu Za Anayekula Ribaa Kurushiwa Mawe Mdomoni

 

www.alhidaaya.com

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا ۗ وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ فَمَن جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَانتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَمَنْ عَادَ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٧٥﴾

275. Wale wanaokula ribaa hawatosimama (Siku ya Qiyaamah) ila kama anavyosimama yule aliyezugwa na shaytwaan kwa kuguswa na kupatwa. Hivyo kwa sababu wao wamesema: “Hakika biashara ni kama ribaa.” Na Allaah Amehalalisha biashara na Ameharamisha ribaa. Basi atakayefikiwa na mawaidha kutoka kwa Rabb wake akakoma (kula ribaa); basi ni yake yale yaliyopita, na hukumu yake iko kwa Allaah. Na atakayerudia basi hao ni watu wa motoni, wao humo ni wenye kudumu.

 

Mafunzo:

 

Samurah bin Jundub (رضي الله عنه) amehadithia Hadiyth ndefu kuhusu ndoto ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) (katika msafara wake wa Israa wal-Mi’raaj pamoja na Jibriyl ((عليه السلام “Tukafika kwenye mto. Nilidhani alisema: Mto ulikuwa mwekundu kama damu, na tukamuona mtu akiogelea mtoni, na kwenye kingo zake alikuwepo mtu mwengine aliyejikusanyia mawe mengi. Mtu ndani ya mto aliogelea kisha akaja kwa mtu aliyekusanya mawe na kufungua kinywa chake, na yule mtu mwengine akitupa mawe kinywani mwake.” Tafsiri yake kwamba huyo ni mla ribaa. [Fat-h Al-Baariy (3295)]

 

 

Share