000-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Suwratul-Baqarah

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Fadhila Za Suwratul-Baqarah

 

 

 

Zifuatazo ni fadhila za Suwrah Al-Baqarah kama zilivyopokelewa katika Ahaadiyth mbalimbali:

 

Hadiyth Ya Kwanza:

 

عن ‏ ‏أبي هريرة ‏ رضي الله عنه ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال‏: ((لَا تَجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ مَقَابِرَ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنْفِرُ مِنَ الْبَيْتِ الَّذِي تُقْرَأُ فِيهِ سُورَةُ الْبَقَرَةِ)) رواه مسلم  

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Msifanye nyumba zenu makaburi. Kwa hakika shaytwaan haingii nyumba ambayo husomwa humo Suwratul-Baqarah)). [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Swahiyh] na katika Riwaayah ya Muslim, Hadiyth (780):  ((Shaytwaan anakimbia nyumba inayosomwa ndani yake Suwratul-Baqarah)).

 

 

 

Hadiyth Ya Pili:

 

عَنْ سَهْل بْن سَعْد قَالَ قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((إِنَّ لِكُلِّ شَيْء سَنَامًا وَإِنَّ سَنَام الْقُرْآن سُورَة الْبَقَرَة وَمَنْ قَرَأَهَا فِي بَيْته لَيْلًا لَمْ يَدْخُل الشَّيْطَان بَيْته ثَلَاث لَيَالٍ وَمَنْ قَرَأَهَا نَهَارًا لَمْ يَدْخُل الشَّيْطَان بَيْته ثَلَاثَة أَيَّام)) القاسم الطبراني وأبو حاتموابن حبان في صحيحه، وابن مردويه

Sahl bin Sa’d As-Saa’idiy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila kitu kina kipeo cha kudhibiti (na kuangaza yaliyo chini) na Al-Baqarah ndio kipeo cha Qur-aan. Atakayesoma Al-Baqarah usiku nyumbani kwake, shaytwaan hatoingia ndani ya nyumba yake nyusiku tatu. Na atakayesoma mchana ndani ya nyumba yake, shaytwaan hatoingia ndani ya nyumba hiyo kwa siku tatu.” [Atw-Twabaraaniy (6/163), Ibn Hibbaan (2/78) na Ibn Mardawayh, Swahiyh At-Targhiyb (2/314)]

 

 

Hadiyth Ya Tatu:

 

عن النَّوَّاسَ بْنَ سَمْعَانَ قال: سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((يُؤْتَى بِالْقُرْآنِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَأَهْلِهِ الَّذِينَ كَانُوا يَعْمَلُونَ بِهِ تَقْدُمُهُ سُورَةُ الْبَقَرَةِ وَآلُ عِمْرَانَ وَضَرَبَ لَهُمَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ثَلاثَةَ أَمْثَالٍ مَا نَسِيتُهُنَّ بَعْدُ قَالَ كَأَنَّهُمَا غَمَامَتَانِ أَوْ ظُلَّتَانِ سَوْدَاوَانِ بَيْنَهُمَا شَرْقٌ أَوْ كَأَنَّهُمَا حِزْقَانِ مِنْ طَيْرٍ صَوَافَّ تُحَاجَّانِ عَنْ صَاحِبِهِمَا)) 

Amesimulia An-Nawwaas bin Sam-‘aan (رضي الله عنه):  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Siku ya kufufuliwa, Qur-aan na watu waliokuwa wakiisoma na kutekeleza mafunzo yake, wataletwa mbele wakitangulizwa na Suwratul-Baqarah na Aal-‘Imraan.” Akasema An-Nawwaas: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akatoa mifano mitatu kwa Suwrah mbili hizi na sikusahau mifano hiyo tokea wakati huo. Alisema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): “Zitakuja kama mawingu mawili au vivuli viwili vyeusi kati yake kuna nuru, au makundi mawili ya ndege waliotandaza mbawa zao wakiruka. Zitawatetea watu wake (wanaoshikamana nazo).” [Muslim]

 

Hadiyth Ya Nne:

 

عن أبي أمامة رضي الله عنه  قال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((اقْرَءُوا الْقُرْآنَ فَإِنَّهُ يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ شَفِيعًا لِأَصْحَابِهِ ، اقْرَءُوا الزَّهْرَاوَيْنِ، الْبَقَرَةَ وَسُورَةَ آلِ عِمْرَانَ فَإِنَّهُمَا تَأْتِيَانِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كَأَنَّهُمَا غَمَامَتَانِ، أَوْ كَأَنَّهُمَا غَيَايَتَانِ، أَوْ كَأَنَّهُمَا فِرْقَانِ ، مِنْ طَيْرٍ صَوَافَّ، تُحَاجَّانِ عَنْ أَصْحَابِهِمَا، اقْرَءُوا سُورَةَ الْبَقَرَةِ فَإِنَّ أَخْذَهَا بَرَكَةٌ وَتَرْكَهَا حَسْرَةٌ وَلَا تَسْتَطِيعُهَا الْبَطَلَةُ)) مسلم

Amesimulia Abuu Umaamah Al-Baahiliy (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Someni Qur-aan kwani itakuja Siku ya Qiyaamah ikiwa ni shafaa’ah (kiombezi) kwa watu wake wanaoisoma na kutekeleza (amri zake). Someni taa mbili: Al-Baqarah na Aal-‘Imraan kwani zitakuja Siku ya Qiyaamah kama kwamba ni maumbile ya mawingu, au sehemu mbili za mawingu, au makundi mawili ya ndege waliotandaza mbawa zao wakiruka. Zitawatetea watu wake (walioshikamana nazo) siku hiyo. Someni Suwratul-Baqarah, kwani kushikamana nayo ni baraka, na kuiacha kwake ni khasara na majuto, na wachawi hawawezi kuihifadhi kwa moyo.” [Muslim (804)] 

 

 

 

 

 

  

 

Share