159-Aayah Na Mafunzo: Unyenyekevu Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kutaka Ushauri Kwa Swahaba
Aayah Na Mafunzo
Aal-‘Imraan
Unyenyekevu Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kutaka Ushauri Kwa Swahaba
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚإِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَوكِّلِينَ ﴿١٥٩﴾
Basi ni kwa rahmah kutoka kwa Allaah umekuwa mpole kwao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelitawanyika mbali nawe. Basi wasamehe na waombee maghfirah na washauri katika mambo. Na unapoazimia basi tawakali kwa Allaah. Hakika Allaah Anapenda wanaotawakali. [Aal-'Imraan: 159]
Mafunzo:
Upole na unyenyekevu wa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) umetajwa mare tele katika Qur-aan na Sunnah, na rejea Aayah (9: 128).
Amri na pendekezo la kutafuta ushauri: Allaah (سبحانه وتعالى) Amemuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) atake ushauri kwa Swahaba zake, naye (صلى الله عليه وآله وسلم) akawataka wamshauri katika hali kadhaa ili awatulize nyoyo zao. Na hili ni funzo kwamba ushauri ni jambo muhimu na pia mkubwa au mwenye cheo anaweza kutafuta ushauri kwa wadogo wake au walio duni yake.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwataka ushauri Swahaba zake katika mambo mbali mbali, mfano;
- Aliwataka ushauri katika vita vya Badr kama kuteka msafara wa Abuu Sufyaan au kupigana vita wakamshauri kupigana vita.
- Aliwataka pia ushauri katika vita vya Uhud alipowauliza kama wanaona bora kuweka boma Madiynah au waende kupigana vita, basi wengi wao wakashauri kwenda vitani.
- Alichukua ushauri wao katika vita vya Khandaq kuhusu kufanya sulhu na makabila ya Al-Ahzaab (makundi ya washirikina wa Makkah), ili badala yake wawape thuluthi moja ya mazao ya Madiynah, lakini Sa’d bin ‘Ubaadah na Sa’d bin Mu’aadh (رضي الله عنهما) wakakataa bali wakakhitari na wakashauri vita.
- Aliwataka ushauri kama wawahujumu washirikina siku ya Hudaybiyah, lakini Abuu Bakr alikataa akasema: “Hatukuja kupigana bali tumekuja kutekeleza ‘Umrah.”
- Aliwataka ushauri katika tukio la Ifk (kusingiziwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها).
- Pia alimtaka ushauri Mama wa Waumini Ummu Salamah (رضي الله عنها) walipokuwa Hudaybiyah pindi makafiri wa Quraysh walipowazuia kuingia Makkah. Ummu Salamah (رضي الله عنها) Akamshauri Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wajivue Ihraam; wakachinja na wakanyoa nywele zao.
Na katika hali nyinginezo mbalimbali alikuwa akiwataka ushauri Swahaba zake (رضي الله عنهم).
Kwa faida ziyada tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho: