169-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Mashuhadaa

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Fadhila Za Mashuhadaa

Alhidaaya.com

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ﴿١٦٩﴾ 

Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa.

 

فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُوا بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿١٧٠﴾ 

Wanafurahia kwa Aliyowapa Allaah kwa fadhila Zake na wanawashangilia ambao hawajaungana nao, walio nyuma yao, kwamba: “Hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.”

يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٧١﴾

Wanashangilia kwa neema za Allaah na fadhila na kwamba Allaah Hapotezi ujira wa Waumini. [Aal-'Imraan: 169-171]

 

 

Mafunzo:

 

Fadhila za kufa shahidi: Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Pale walipopatwa msiba (walipofariki) ndugu zenu wa Uhud, Allaah Alijaalie roho zao kuwa katika maumbile ya ndege wa kijani ambao wanakunywa katika mito ya Jannah na wanakula katika matunda ya Jannah na hurukia na hustarehe kwenye kandili ya dhahabu chini ya kivuli cha ‘Arshi ya Allaah. Kisha roho hizo zilipopatwa na utamu wa kunywa na kula katika neema za humo ndani ya Jannah na uzuri wa makazi na marejeo yao wakasema: Laiti wangelifahamu ndugu zetu yale Allaah Aliyotufanyia sisi ili wasipuuze jambo la jihaad na wala wasirejee na kuogopa vita. Basi hapo Allaah Akasema: “Mimi ninayafikisha hayo kutoka kwenu!” Ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa… (mpaka Aayah (3: 169-171[Imaam Ahmad].

 

Pia ...

 

Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikutana nami siku moja akaniambia: “Ee Jaabir! Unanini nakuona una huzuni?” Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Baba yangu amekufa shahidi na ameacha nyuma madeni na watoto. Akasema: “Je, nikujulishe kuwa Allaah Hajapata kuongea na mtu yeyote sipokuwa nyuma ya pazia? Lakini Amemhuisha baba yako na akazungumza naye moja kwa moja. Akasema: Tamani (lolote) Nikupe!  Akasema: Yaa Rabb! Nihuishe (nirudi duniani) ili niuliwe tena kwa ajili Yako! Akasema Rabb (تبارك وتعالى): Nimeshatanguliza kauli kwamba wao hawatorudi tena (maisha ya dunia). Akasema: Yaa Rabb! Basi nifikishie khabari kwa nilioawaacha nyuma. Kisha Allaah Akateremsha: Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa… (3: 169-171) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Swahiyh At-Targhiyb (2276), Swahiyh At-Targhiyb (1361)].

 

 

Share