185-Aayah Na Mafunzo: Dunia Haina Thamani Kulingana Na Aakhirah

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Dunia Haina Thamani Kulingana Na Aakhirah

 

 

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۖ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿١٨٥﴾

185. Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na uhai wa dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu.

 

Mafunzo:

 

 

Dunia haina thamani kulingana na Aakhirah.

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Sehemu ndogo katika Jannah, kiasi cha ukubwa wa fimbo, ni bora kuliko dunia na yaliyokuwemo ndani yake. Someni mkipenda: “Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu… (3: 185) [Ameinukuu Ibn Abi Haatim, At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Swahiyh].

Anas (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Siku ya Qiyaamah ataletwa mtu wa motoni katika watu wa dunia aliyeneemeshwa neema nyingi mno, ataingizwa motoni kidogo kisha atatolewa: Ataulizwa: Ee mwana wa Aadam!  Je, umeona kheri yoyote? Ushawahi kuneemeka aslani? Atajibu: Hapana Wa-Allaahi Rabb wangu! Na ataletwa mtu aliyekuwa ana shida mno duniani katika watu wa Jannah. Ataingizwa Jannah kidogo kisha atatolewa. Ataulizwa: Ee mwana wa  Aadam! Je, umeona shida yoyote? Ushawahi kutaabika aslani? Atajibu: Hapana Wa-Allaahi Rabb wangu! Haikunipitia shida yoyote abadan, wala sikuona tabu yoyote Abadan.” [Muslim].

Sahl bin Sa'ad (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ingelikuwa (thamani ya) dunia ni sawasawa na bawa la mbu mbele ya Allaah, basi Asingelimnywesha kafiri hata tama moja la maji.” [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh].

Share