029-Aayah Na Mafunzo: Anayejiua Ataingizwa Motoni Kwa Hali Ile Ile Kujiua
Aayah Na Mafunzo
An-Nisaa
Anayejiua Ataingizwa Motoni Kwa Hali Ile Ile Kujiua
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى)
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ مِّنكُمْ ۚ وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٢٩﴾
Enyi walioamini! Msiliane mali zenu kwa ubatilifu, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Allaah daima kwenu ni Mwenye kurehemu.
وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ عُدْوَانًا وَظُلْمًا فَسَوْفَ نُصْلِيهِ نَارًا ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿٣٠﴾
Na atakayefanya hivyo kwa uadui na dhulma, basi Tutamuingiza motoni. Na hilo kwa Allaah ni mepesi. [An-Nisaa: 29 - 30]
Mafunzo:
Haramisho la kujiua na tahadharisho la adhabu yake kwamba afanyae hivyo, atakariri kujiua Siku ya Qiyaamah: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Yeyote atakayejitupa kutoka mlimani na kujiua, atatupwa motoni milele. Atakayekunywa sumu na kujiua, basi atatupwa motoni na huko atakuwa akiinywa hiyo sumu milele. Atakayejiua kwa kipande cha chuma, atatiwa motoni akiwa na kipande hicho cha chuma akijitwanga nacho tumboni kwake humo motoni milele.” [Muslim].