024-Aayah Na Mafunzo: Kulinganisha Jibu Kati Ya Mayahudi Na Maswahaba Kwa Nabii Wao

Aayah Na Mafunzo

Al-Maaidah

Kulinganisha Jibu Kati Ya Mayahudi Na Maswahaba Kwa Nabii Wao

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِنَّا لَن نَّدْخُلَهَا أَبَدًا مَّا دَامُوا فِيهَا ۖ فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ ﴿٢٤﴾

24. Wakasema: “Ee Muwsaa!  Hakika sisi hatutoingia humo abadani madamu watabakia humo, basi nenda wewe na Rabb wako mkapigane, hakika sisi tunakaa hapa hapa.”

 

Mafunzo:

 

Kulinganisha jibu la Mayahudi kwa Nabiy wao Muwsaa (عليه السلام) na jibu la Swahaba kwa Nabiy wao (صلى الله عليه وآله وسلم) katika vita vya Badr: ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Nimeshuhudia kutoka kwa Al-Miqdaad bin Al-Aswad (رضي الله عنه) tukio ambalo laiti ningelikuwa mimi ndio muhusika wa tukio hilo ingependeza mno kwangu kuliko kulikosa. Miqdaad bin Al-Aswad alimwendea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamkuta akiwaombea washirikina du’aa ya maangamizi. Miqdaad akasema kumwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “Wa-Allaahi Ee Rasuli wa Allaah, hatutosema sisi kama walivyosema baniy Israaiyl kumwambia Muwsaa:

 

فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ ﴿٢٤﴾

“basi nenda wewe na Rabb wako mkapigane, hakika sisi tunakaa hapa hapa”, lakini sisi tutapigana jihaad kuliani mwako na kushotoni mwako na mbele yako na nyuma yako.”  Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) akasema: Nikaona uso wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) umejawa na bashasha na akiwa amefurahishwa na hayo maneno. [Al-Bukhaariy].

 

 

Share