095-Asbaabun-Nuzuwl: An-Nisaa Aayah 095: لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
An-Nisaa 095-Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani)…
لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ وَالْمُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ ۚ فَضَّلَ اللَّـهُ الْمُجَاهِدِينَ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ عَلَى الْقَاعِدِينَ دَرَجَةً ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَفَضَّلَ اللَّـهُ الْمُجَاهِدِينَ عَلَى الْقَاعِدِينَ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٩٥﴾
Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani), isipokuwa wale wenye udhuru, na kati ya wenye kupigana Jihaad katika Njia ya Allaah kwa mali zao na nafsi zao. Allaah Amewafadhilisha kwa cheo wenye kupigana Jihaad kwa mali zao na nafsi zao kuliko waliokaa nyuma. Na wote Allaah Amewaahidi Al-Husnaa (Jannah). Na Allaah Amewafadhilisha wenye kupigana Jihaad kwa ujira mkubwa mno kuliko wanaokaa (nyuma) (4:95).
Sababun-Nuzuwl:
Ilipoteremka Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ
Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani). (4:95)
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwamrisha Zayd bin Thaabit (رضي الله عنه) aiandike, na mara hapo akaja ‘Abdullaah bin Ummi Maktuwm(رضي الله عنه) akilalamika kuhusu upofu wa macho yake. Na hapo ikateremka Kauli ya Allaah kwa kuongezeka:
غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ
Isipokuwa wale wenye udhuru (4:95).
[Amehadithia Al-Baraa bin ‘Aazib na Zayd bin Thaabit(رضي الله عنهما) na imepokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Sababun-Nuzuwl: Katika riwaayah nyingine ya Al-Bukhaariy, Sahl bin Sa’d As-Saa’idiy amehadithia kwamba: Nilimuona Marwaan bin Al-Hakam amekaa kitako Masjid. Nikamkabili na nikaketi karibu naye. Akatujulisha kwamba Zayd bin Thaabit amemwambia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesomea imla Aayah hii:
لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ
Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani). (4:95)
Kisha Ibn Ummi Maktuwm akaja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati akinisomea Aayah ili niiandike. Ibn Ummi Maktuwm akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ningekuwa na uwezo bila shaka ningeshiriki katika Jihaad. Alikuwa ni kipofu, basi hapo Allaah Akamteremshia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati mapaja yake yakiwa juu yangu na yakawa mazito mno kwangu (kutokana na Wahyi kuteremka) mpaka nikakhofia kuwa mapaja yangu yatavunjika. Kisha Allaah Akateremsha:
غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ
Isipokuwa wale wenye udhuru
Pia Sababun-Nuzuwl: At-Tirmidhiy amerekodi kwamba Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba:
لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ
Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani). (4:95)
Inahusiana na wale wasiotoka kwenda kupigana vita vya Badr na wale waliokwenda Badr. Wakati vita vya Badr vilipokaribia kuanza, Abuu Ahmad bin Jahsh na Ibn Maktuwm walisema: Ee Rasuli wa Allaah! Sisi ni vipofu, je, tuna udhuru? Hapo ikateremshwa:
لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ
Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani), isipokuwa wale wenye udhuru (4:95).